Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni hii kuchangia na kuweza kushauri mambo mbalimbali kuhusu Wizara ya ELimu. Na-declare interest kwamba mimi ni Mwalimu by profession lakini vile vile ni mmiliki wa shule binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutalaumu sana, tutaongea sana mambo ya Wizara ya Elimu lakini kidogo kuna mambo ya mkanganyiko wa sheria, sera, kanuni na nyaraka mbalimbali. Mambo yanaweza yasiende tukamlaumu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, mambo yanaweza yasiende tukamlaumu Mheshimiwa Simbachawene, mambo yanaweza yasiende kumbe yako Wizara ya Utumishi kwa dada yangu pale; na mambo mengine mengi, lakini mengine yako Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mdogo tu, anayelipa mishahara ya Walimu, ni Wizara ya Fedha; anayepandisha Walimu madaraja katika nafasi mbalimbali ni Utumishi; anayesimamia elimu mashuleni ni TAMISEMI, ndiye anayeangalia kama madawati yapo, kama Walimu wamefika tayari wanafundisha, nyumba za walimu na kujenga madarasa; na usimamizi wote wa elimu kule Shule za Msingi na Sekodari. Ni TAMISEMI wala siyo Wizara ya Elimu. Anayetengeneza Sera ya Elimu ni Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona wenzangu hapa wanachangia na kila kitu wanapiga madongo kwa Wizara ya Elimu. Well and good kwa sababu yote ni Serikali kwa ujumla. Nataka vile vile Serikali mjue hilo kwamba lipo jambo moja na lingine linaweza likasababisha huku kukawa kuzuri ama kukawa kubaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kushauri hilo, naomba niingie kwenye hoja zangu. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako kwa kuteuliwa kuwa Waziri katika Wizara hii. Namfahamu vizuri sana, tumefanya naye kazi vizuri sana. Ni mama mwenye msimamo, lakini mimi huwa namwita ni mama wa quality of education. Namfahamu toka akiwa pale Baraza la Mitihani la Taifa. Huwa hapendi mchezo na hataki mambo holela holela! Nadhani mtakuwa mmeona anavyoendelea hata kutumbua baadhi ya majipu fulani fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima mama huyu tumshauri; na kwa hii miezi sita aliyokaa Wizarani yapo baadhi ya mambo yanaonekana, lakini akikaa miaka mitano, tunaweza tukaanza kuona impact ya baadhi ya mambo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri. Suala la kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Elimu Nchini ni suala muhimu sana. Nami kwa sababu ni mzoefu wa mambo haya, Waheshimiwa Wabunge naomba nitoe hili jambo mlione jinsi lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu wa Wizara ya ELimu, kama nilivyosema, anatunga sera, lakini Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI ndiye mwenye Shule za Sekondari na Msingi kama Serikali. Vile vile kuna shule za private upande mwingine, hawa watu wa TAMONGSCO na TAPIE, kwa wamiliki wa shule. Sasa inakuwaje tena pale pale kwenye Wizara ya Elimu kwa Mheshimiwa Profesa Ndalichako pana watu wanaitwa Wakaguzi wa shule ambao watakapokwenda kukagua shule, wakakuta kwenye Shule ya Msingi matundu ya vyoo ni machache, ama Walimu darasani hawapo, ama shule haina madawati, ama kuna mlundikano wa wanafunzi, wanaandika ripoti, wanampelekea mwajiri. Unategemea mwajiri atafanya nini? Naomba niseme, mwajiri atafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukipata kitu ambacho kinajitegemea, kama ilivyo EWURA, au kama zilivyo bodi nyingine na mambo mengine ambapo labda tumeanzisha Wakala wa Serikali ama mamlaka ambazo ni independent zinajitegemea, ni autonomous, agency, ili ikague shule zote kwa usawa. Ikienda kwenye private wasema bwana shule yako haina ubora, haina fence, haina vyoo, haina Walimu wenye vyeti vizuri, haina madirisha fulani, haina vitabu na kadhalika, iandike kwamba shule hii imepata asilimia 70. Ikienda na kwenye shule za Umma iandike vile vile, shule hii haina vyoo, ifanye hivi; imwandikie TAMISEMI arekebishe na itoe siku 60 shule irekebishwe; mambo yatakwenda vizuri sana, kuliko tunavyofanya sasa. Kwa sababu sasa hivi anayeandika ripoti anampelekea mwajiri wake ambaye akiandika vibaya anaweza hata akamfukuza kazi. (Makofi)
Kwa hiyo, ni suala ambalo kidogo naomba mlifikirie, mimi nina udhoefu nalo. Naomba tuanzishe mamlaka huru ya udhibiti wa shule. Leo tunasema ada elekezi; tukipata hicho kitu kitaangalia kila kitu kwenye shule zetu. Mfano mdogo, unaposajili shule ya private, sekondari ama primary kuna vigezo vingi sana pale Idara ya Udhibiti ambapo zamani ilikuwa Idara ya ukaguzi. Unakuta mwenye shule anajenga kila kitu, anakamilisha madarasa nane, anaweka miundombinu ya shule, walimu vizuri halafu ndipo Serikali inasajili shule maana ina vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwenye shule za Umma, shule inaanzishwa hata kama ina madarasa mawili. Tukimpata huyo ambaye atakuwa ana-regulate, shule ya Umma haiwezi kunzishwa kwenye madarasa matatu; Haiwezi kuanzishwa haina madawati; haiwezi kuanzishwa hawana vyoo; haiwezi kuanzishwa watoto wakakaa 80 darasani. Kwa sababu yule mtu atakuwa ni independent, atatoa ripoti ambayo haina upendeleo. Naomba niishauri Serikali na Mheshimiwa Waziri naomba a-take care jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba sana nimshauri dada yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Wizara hii umepewa utakaa miaka mitano hapo, lakini naomba ufanye mambo mengine tutakayoweza kukukumbuka. Katika nchi hii hatuna Chuo cha Ualimu kinachofundisha Walimu kwenda kufundisha English Medium. Nani aseme ni chuo gani kipo hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imekataza shule za binafsi kuchukua Walimu kutoka nchi ya Rwanda, Uganda, Kenya ama mataifa mengine, tunataka tujiweke sisi kama ni kisiwa, tumepandisha kodi mbalimbali ili shule hizi zibanwe, zianze kuchukua Walimu wa ndani ambao hawana hiyo taaluma. Tunaua elimu sisi wenyewe, kwa nini? Kwa nini tuue elimu sisi wenyewe wakati tunajua hatuna Chuo cha namna hiyo? Vyuo vyetu vya elimu vinafundisha certificate ya kwenda kufundisha masomo yanayofundishika kwa Kiswahili japo content ni ile ile na syllabus ni ile ile, wanatafsiri tu mtihani.
Leo ukienda wanapotunga mtihani wa Darasa la Nne kwenye English Medium wanachukua maswali kwa Kiswahili halafu wanatafsiri. Kuna ada tunalipa shule za binafsi kwa sababu unasema eti katafsiri mtihani wa Darasa la Nne. Jamani! Tafadhali, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie hili kwa makini sana. Mimi ni Mwalimu, naliona, ni hatari kubwa! Kwa nini tuweke wigo kwa shule za binafsi zisiajiri Walimu kutoka nchi za nje? Tujue Tanzania hii siyo kisiwa, kuna Mabalozi wapo hapa, kuna wafanyakazi mbalimbali kutoka nchi za nje wapo hapa, wawapeleke wapi watoto wakasome shule? Naomba hili nalo lifanyiwe kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba lingine niishauri Serikali; yapo mambo jamani kwa kweli niseme kama ni kero hivi; ama yupo mtu mmoja Wizarani pale akilala akiamka anasema ngoja leo niandike hivi. Hivi unawezaje ukaandika kwamba shule za private hakuna kukaririsha wanafunzi? Mzazi anaamua kumpeleka mtoto kwenye shule ya private; kwanza naomba nitoe elimu hii. Serikali inachukua wanafunzi waliofaulu, the best students, wanawachagua kuwapeleka Shule za Serikali mwezi Januari. Baada ya hapo, wanaokuwa wamebaki, maana yake ni slow learners; hujawachagua wewe kuwapeleka kwenye shule zako za Serikali. Shule za private zinaokoa jahazi, zinawachukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwatambue kwamba wale ni slow learners. Slow learner huyo unamwingiza darasani, wengine ndiyo kama hivyo, hawajui hata kusoma na kuandika; unamwingiza darasani, ni lazima umfundishe pole pole. Inafika mwisho wa mwaka ili afanye mtihani wa Form Two, hajui chochote, mzazi anakwambia mimi hapa nalipa ada shilingi milioni mbili kwa mwaka, mtoto wangu bado ana umri mdogo, nataka arudie shule. Serikali inasema aah, aendelee. Jamani! Ulishawahi kuona wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe huru, waachieni wazazi wa nchi hii wawe huru. Unaandika barua kwa Afisa Elimu wa Mkoa, wanasema Serikali imesema hakuna kukaririsha. Si ulimwacha mwenyewe huyu motto, ni slow learner, sasa amekwenda kwa watu wengine wamfundishe. Kama wanamfundisha na mtu analipa, anafundishika pole pole huyo! Mwache asome. Ruhusuni shule za binafsi zianze kukaririsha. Hata shule za Serikali vile vile zikaririshe kama zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wengine tulisoma, tusingekariri tusingekuwa hapa! Tulirudia shule tukasoma, ndiyo maana kuna private schools, ndiyo maana kule kwenye mitihani ya Form Two kuna kitu kinaitwa Qualifying Test, wanasoma hata Elimu ya Watu Wazima. Nini maana ya kuweka kwamba elimu ni free? Jamani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, lingine, naomba niishauri Serikali. Tunataka kuua Elimu ya Ualimu nchini. Tumevichukua Vyuo vya Ualimu kuvipeleka NACTE. Mungu wangu! Hebu naomba nifafanue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NACTE maana yake ni National Council of Technical Education, yaani Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Sasa unamchukua Mwalimu anayesoma education in general unampeleka akasomee huko. Hakuna utaalam wa kuwalea walimu kule! Turudishe Walimu kwenye Wizara ya Elimu kama ilivyokuwa zamani.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.