Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu wa mapendekezo ya Mpango kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na jambo moja ambalo ni la msingi sana, kutoa pongezi kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa maelekezo kwa zile Halmashauri mpya kuhamia kwa wananchi ili kutoa huduma kwa wananchi kwa ujirani sana na hatua hizo zimeshaanza kutekelezwa. Nampngeza sana, nami Halmashauri yangu imeshahama tayari na wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nawapongeza wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwa kujiandikisha kupiga kura. Wananchi wamejiandikisha vizuri kabisa na uchaguzi ambao wenzangu wanaongelea wa kidemokrasia, nadhani kwenye Jimbo langu hakuna tatizo na tunakwenda vizuri kabisa. Nawapongeza sana wananchi wa Jimbo langu la Mufindi Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ni mapendekezo ya Mpango, nami napenda nitoe mapendekezo yangu. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri sana. Wameandaa Mpango sana. Nimesoma Mpango wiki nzima na bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Bajeti, tulikuwa tunajadili pamoja, hakuna kitu walichoacha, kila kitu kimeandikwa vizuri na ukisoma vizuri, maana kuna utekelezaji wa miaka mitatu iliyopita na kuna mapendekezo ya Mpango kwa miaka inayokuja, wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mapendekezo kwa TARURA. TARURA wanafanya kazi vizuri na ukiangalia tafsri ya TARURA ni Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini; na ukiangalia kazi zao wanavyofanya, kwa upande wa mijini na wenyewe wanajenga hata barabara za lami. Ukienda vijijini wanajenga barabara zile za kokoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ile bajeti, tukisema tunawapa asilimia 30, fedha ile haitoshi. Sasa hivi nchi nzima barabara zinazoangaliwa ni zile ambazo ziko chini ya TARURA. Wenzetu wa TANROADS walifanya kazi vizuri, kutekeleza ile sera ya kuungalisha barabara za mikoa na mikoa na wilaya na wilaya. Walifanya kazi nzuri sana na barabara nyingi sana zimejengwa. Ukiangalia Tanzania nzima sasa hivi barabara za mikoa na wilaya zinapitika vizuri, lakini tuna tatizo kubwa kwa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye Mpango huu mpya, naiomba Serikali ijielekeze sana kuiangalia TARURA kuweza kuiongezea uwezo ili wafanye kazi vizuri sana na tuhakikishe kwamba barabara za vijijini zile zinapitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa hospitali katika wilaya 67. Ni jambo jema sana. Hizi hospitali zitasaidia sana wananchi na zimeenda kasi. Sasa zile hospitali ambazo Serikali ilitoa fedha, naweza nikasema kwamba wameshafikia asilimia kuanzia 80 mpaka 90 kwa kujenga, lakini wakimaliza tu kujenga, naiomba Serikali itazame, zile hospitali zianze kutumika mara moja haraka sana ili value for money ionekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijenga hospitali zikakaa muda mrefu bila kutumika, itakuwa ni kazi bure. Kwa speed hiyo tuliyojenga, iende sambamba sasa na ununuzi wa vifaa vya hospitali, kuwaandaa watumishi ili waweze kufanya kazi katika hospitali zile. Kuna hospitali nyingi sana tuna tatizo la vifaa vya hospitali. Kwa mfano, hata pale Mjini Mafinga, tuna tatizo moja la X-Ray, hospitali haina X-Ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hospitali mpya hizi maandalizi ya vifaa yawepo ili kuhakikisha tunapomaliza majengo yote, watumishi na vifaa viwepo ili hospitali ianze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Serikali mwaka huu mmefanya vizuri sana. Kila ukimwuliza mwanafunzi anasema nimepata asilimia 100, asilimia 80, asilimia 90, Serikali imefanya vizuri, mikopo imeongezeka sana kwa wanafunzi. Nilikuwa nasoma hapa, hao wanafunzi wa mwaka wa kwanza karibu 41,000 wameshapata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe pendekezo moja, kuna wanafunzi ambao wako mwaka wa pili na wa tatu, kuna wengi walikosa mikopa na mwaka huu hawajaomba; sasa wameona wenzao wamepata mikopo ambao wamekuja kwa mwaka huu na wale wa mwaka wa pili na wa tatu wana vigezo vya kupata mkopo; sasa kufuatana na bajeti ilikuwa kidogo, hawakupata mikopo. Naiomba Serikali, basi wale wa mwaka wa pili na wa tatu waruhusiwe sasa, wafungue dirisha ili waombe na wenyewe ili wale ambao walikopa waweze kukopeshwa tena. Kuna wanafunzi wanapata taabu sana wa mwaka wa pili na wa tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni changamoto hasa na tumejadili sana hata kwenye Kamati ni kumiliki akaunti za benki. Wananchi, hasa kwenye vikundi, imetuletea shida sana kwenye vikundi. Unaweza ukaona kikundi kina akaunti au kijiji kina akaunti, sasa kwa sababu wanaweka fedha kwa msimu, akiwa na fedha ndiyo anakwenda kuweka, kama hawana fedha wanaweza wakakaa hata miezi sita hawajaweka fedha. Kwa hiyo, akaunti yao inaonekana iko dormant. Sasa ikiwa dormant, wakipata fedha, wakitaka kwenda kuweka tena kwa mara ya pili (hata kwenye Vyama vya Ushirika hili tumeliona), wanasema akaunti yako imefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tatizo kubwa sana, naomba, Waziri wa Fedha, awaambie mabenki, mtu akiweka akaunti yake, kwa nini ifungwe? Kwa sababu akianza process upya, anasema nenda kachukue barua kwa Mwenyekiti, nenda sijui kwa Mtendaji, anaanza process upya. Hiyo inawakatika tamaa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi Wabunge kwa mfano hata kwenye Mfuko wetu wa Jimbo ukitaka kupeleka fedha kijijini kwa ajili ya maandalizi ya kununua vifaa kule kijijini, utasikia akaunti imefungwa. Kwa hiyo, unashindwa kupeleka fedha. Wananchi kule kuji-organize kuanza upya process inachukua muda mrefu na vijiji vyetu viko mbali sana na benki. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atoe tamko kwamba benki vile kusema kwamba akaunti ziko dormant, hilo neno lisiwepo. Mtu ameonyesha ID number tu, akaunti inakuwa active; akiweka hata shilingi 10,000/= au shilingi 20,000/=, akaunti inakuwa active kwa sababu details zote zinakuwepo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, Benki Kuu walifanya kitu kizuri sana katika kupunguza riba kwa mabenki. Ile ilikuwa kwamba, wanapunguza riba kwa mabenki ili mabenki yale yaweze kukopesha wananchi. Tunajua kule kwa wananchi kuna wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wakubwa na wafanyabiashara mtu mmoja mmoja. Sasa impact kwa wananchi bado haijaonekana, yaani ile juhudi ya Serikali kuwaambia kwamba wapunguze riba kwa mabeki ili ilete impact kwa wananchi na wenyewe wale mabenki ya biashara yapunguze kwa wananchi, hayajafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi bado wanalalamika, riba ni kubwa sana, kubwa sana. Sasa na hilo naomba Serikali ifuatilie ili kuondoa malalamiko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine, nimeona kwenye Mpango, umekaa vizuri kuhusu masuala ya umeme vijijini. Serikali imefanya kazi vizuri sana. Hata kwenye vijiji vyangu vyote, upimaji, survey imeshafanyika, ingawa kuna vijiji vingine bado kupeleka nguzo. Kuna sehemu nyingine nguzo zimelala tu chini, wananchi wanalalamika. Naomba twende speed. Tumesema mwaka 2021 vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme, vitongoji vyote vitakuwa vimepata umeme. Sasa ile kasi tuliyokuwa tumeanza nayo mwanzo iendelee, maana tunaona sasa Makandarasi kama wanafifia hivi, wananchi wanashindwa kuelewa vizuri. Tuwahamasishe wafanye kazi vizuri, kwa sababu Serikali ina lengo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema kwamba, kuna vijiji wanapita bila kupingwa kwenye uchaguzi. Kwa nini wasipite bila kupingwa kama wanaona umeme uko tayari pale? Wananchi wanachotaka ni huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaona mtandao wana maji, wako wako site. Ingawa kuna chagamoto ya maji, lakini watu wako site, sasa mtu atapinga nini? Wanaona majengo ya shule ambayo yalikuwa hayajaisha yanamalizika, wanaona Vituo vya Afya vinajengwa, Hospitali za Wilaya zipo; sasa mtu atalalamika nini? Barabara zinajengwa, sasa utalalamika kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa, tuishauri Serikali kuongeza speed ya kuhakikisha kwamba mazingira bora kwa wananchi yanakuwepo kujenga hospitali, kujenga Vitu vya Afya, kujenga Zahanati, barabara, umeme; tukiimarisha haya, ndiyo maisha bora kwa jamii tunayoyataka. Tukisema kupunguza umasikini, maana yake tunaangalia vitu kwa jamii vipo? Hospitali zipo? Madawa yapo? Hivi vitu vinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni process, usije ukasema utafika siku moja, ukasema sasa tumetosheka kila kitu tunacho. Hata ukienda nchi za wenzetu zilizoendelea, barabara wanajenga mpaka leo. Hata ukienda pale Uingereza, London penyewe pale mjini, barabara mpaka leo hii wanajenga. Ukienda hata Marekani, barabara mpaka leo hii wanajenga. Kwa hiyo, hii ni process ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda wangu umeisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)