Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kuchangia mpango wetu huu wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa mpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyosimamia Wizara hii, Wizara nyeti na Wizara ambayo ndiyo inatupa mustakabali wa Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko Kamati ya Bajeti, Kamati ya Bajeti wasiwasi wetu mkubwa ilikuwa ni kuona utekelezaji wa mipango tunayoipanga. Mfano nizungumzie ile miradi ya vielelezo, mradi kama ule wa SGR, mradi kama huu wa Liganga na Mchuchuma, mradi wa uwekezaji Bagamoyo lakini pia mradi wa maeneo ya uwekezaji kama vile Kurasini. Tunachokiona hapa kwa mfano kwenye SGR Serikali inatumia pesa zake za ndani, kwa kutumia pesa zake za ndani mradi huu utachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuko kutokea Morogoro kwenda Makutupora, tutoke Makutupora tuje mpaka Dodoma, tuendelee mpaka Isaka, Isaka – Mwanza, Mwanza – Isaka – Tabora na Tabora – Kigoma. Sasa mimi nikawa nafikiri dhamira ya Serikali ni mradi huu wa SGR ukamilike ili Serikali ianze kukusanya mapato. Sasa nikawa najiuliza kwa nini Serikali kama inakopesheka isione namna ya kukopa pesa ili huu mradi wa SGR uweze kukamilika kwa muda mfupi na tuweze kuona matunda yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie kuhusiana na mabehewa reli ya kati. Serikali imeweka mkakati wa kununua mabehewa 200 na wanasema hadi sasa wamenunua mabehewa 70. Nilifikiri kwamba tungejikita kununua haya mabehewa yote 200 ili tuanze kuchukua mizigo inayotoka Dar-es-Salaam badala ya kusafirishwa na magari isafirishwe na treni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza sasa hivi tunakuwa tumejihakikishia kwamba SGR itakapokamilika tutakuwa na mzigo wa kutosha ili wafanyabiashara waanze kuona sasa kumbe badala ya kutumia magari tuna uwezo wa kutumia reli kupeleka mizigo yetu Mwanza, Isaka, Tabora na Kigoma. Ukiangalia tayari Serikali ina mkakati maalum wa kuweka bandari ya nchi kavu pale Kibaha lakini pia ina mkakati maalum kuweka bandari ya nchi kavu pale Kigoma. Sasa tukiboresha reli ya kati pamoja na mabehewa nadhani tunaweza tukafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilitaka nizumgumzie hii miradi ya elimu. Miradi ya elimu Serikali imefanya vizuri lakini bado kuna changamoto kwenye maboma. Ukisoma kwenye Mpango wanasema wananchi wahamasishwe kuchangia maendeleo yao. Wananchi wamehamasishwa, wamechangia madarasa, vyoo na nyumba za walimu, tatizo kubwa ni katika umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie hilo, lakini dada yangu Mheshimiwa Joyce Ndalichako kazi nzuri anayoifanya na yeye aangalie ni mkakati upi ndani ya hii miezi sita iliyobaki tunaweza tukamalizia maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano pale kwangu Nguruka ninayo shule mpya imejengwa, mkandarasi anadai kama shilingi milioni 76. Serikali inaweza ikafumba macho ikatuletea hela hizo, tumeshajenga vyumba sita, tunataka kama shilingi milioni 76 ili vile vyumba vikamilike na shule iweze kuanza. Watoto wanasoma kwenye maabara za Shule ya Sekondari ya Nguruka. Kwa hiyo, mnaweza mkaona mnafanyaje kutupa pesa ili tuweze kukamilisha ujenzi wa shule ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie hali ya miradi ya maji. Tunayo miradi mingi ya maji ambayo haijakamilika. Mfano pale kwangu tunao Mradi wa Rukoma. Serikali katika miradi hii mikubwa ya vielelezo, sawa mmeweka kujenga Mradi ule wa Ziwa Viktoria, lakini hata hii miradi ambayo ilishaanzishwa kwa sababu ipo ndani ya mpango ni vema tukajipanga namna ya kuimalizia ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii miradi mikubwa ya vielelezo, hivi tumewezaje kuanzisha Mradi wa Ziwa Victoria unaotoka Mwanza unaenda Tabora, Igunga, Uyui mpaka Nzega, kwa nini hatuweki mkakati wa makusudi wa kutoa pia mradi wa maji kutoka Ziwa Tanganyika. Maji ya Ziwa Tanganyika ni baridi unaweza tu ukachota ukayanywa, kwa hiyo nafikiri katika mpango ujao wa miaka mitano tunaweza pia tukaanza kuweka maandalizi ya kuweka huu Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika ambao utasaidia karibu mikoa mitatu Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili nimpongeze Mheshimiwa Rais juzi na mimi nilipata fursa ya kupokea ile Dreamliner ya pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais amejiwekea mipango yake na ameweza kuitekeleza. Hii ni changamoto kwa Waheshimiwa Mawaziri kwamba Rais amesema lazima ninunue ndege, lazima nifufue ATCL na amefanya hivyo, sasa haya mambo na Mawaziri kila mmoja aangalie kwenye Wizara yake na yeye anatimizaje ahadi ambazo ameziweka katika huu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri huku tunanunua ndege, tuweke pia na mkakati madhubuti wa kuboresha viwanja vyetu vya ndege. Kiwanja cha Kigoma, Kiwanja cha Tabora, Kiwanja cha Mwanza, Kiwanja cha Mbeya, hii mikoa mikubwa mikubwa kiwanja cha Arusha pale Mjini tunao Kilimanjaro lakini tunayo Arusha Airport, hebu tuboreshe. Hapa nataka nitanie kidogo tu, hizi ndege zetu ni nzuri na zinafanya vizuri, lakini mle ndani nako tunaowaajiri wale ma- air hostess hebu tuangalie ambao hata wakiitwa mle kwenye ndege unamwita air hostess akigeuka hivi abiria anaona kweli tuna ma-air hostess humu ndani, lakini naangalia kama vile, mtanisamehe ndiyo maana nimesema hili nilizungumze jamani, unakuta air hostess, sijui mnatumia vigezo gani, mfupi hana mvuto wa kuifanya ndege yetu ya Air Tanzania ionekane. Leo mimi Hasna hapa nimezeeka nina miaka hamsini na kitu, lakini ukiniweka..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasna, kuna taarifa ya Musukuma tusikilize

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Musukuma ananiharibia.

T A A R I F A

MHE. KASHEKU J. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa kuhusu utaratibu Mheshimiwa Hasna kwamba huu ubaguzi anaoutaka sisi binadamu tunatofautiana, wengine tunazaa watoto hawana hizo shepu ambazo anazitaka, lakini tunazaa wafupi, tunazaa weusi, sasa tutakuwa na mizigo ambayo tumeisomesha halafu kwenye ajira kunakuwa na ubaguzi. Ni hayo tu.

MWENYEKITI: Ahsante. Hiyo taarifa nzuri wafupi pia wazuri Mheshimiwa Hasna.

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya air hostess lazima awe mrefu aliyenyooka, akiwa mvulana, akiwa msichana, awe mrefu aliyenyooka. Tunaomba hilo lizingatiwe, ndege zetu zinafanya kazi nzuri, tunataka na ma- air hostess pale wawe na mvuto ili abiria wanaposafiri waweze kuona tofauti na ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie na bandari, naomba katika mpango Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuendeleza Bandari ya Kigoma, Bandari ya Kalema, kwa ajili ya kuteka soko la Kalemi lakini vis-a-vis na ununuzi wa meli ya mizigo na meli ya abiria. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mpango hebu tujitahidi kuhakikisha kwamba meli ya mizigo inanunuliwa katika Ziwa Tanganyika, meli ya abiria inanunuliwa katika ziwa Tanganyika, lakini sambamba na kuitengeneza meli ya Mv Lihemba, watu wa Kigoma wanauliza Mv Lihemba itakamilika lini? Sasa hivi hakuna usafiri wowote ule wa meli kubwa ndani ya Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono Mpango, ni mzuri na nampongeza sana Mheshimiwa Rais na niwaombe Watanzania wote, tunapoenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa jamani Rais kafanyakazi Chama cha Mapinduzi kimefanya kazi, twendeni tukaonyeshe mfano, tarehe 24 Novemba tupige kura kumwonyesha Rais kweli Chama cha Mapinduzi kimefanya kazi katika miaka yake hii minne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)