Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa ujumla, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa maandalizi ya Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwanza kwa pongezi. Nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watoto wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nawapongeza watoto? Wakati Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani alikuwa anapenda kutueleza Watanzania kwamba iko siku mtanielewa. Msemo huo aliupenda kuusema mara kwa mara, “iko siku mtanielewa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza watoto kwa sababu gani? kati ya watu wa kwanza kumwelewa Mheshimiwa Rais, walikuwa ni watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Mheshimiwa Rais alipoingia alisisitiza sana umuhimu wa kulipa kodi lakini pia kudai risiti. Sisi Watanzania hatukuwa na huo utamaduni. Ukinunua bidhaa, ilikuwa ukipewa risiti unaona kama usumbufu, unamwambia mwenye duka, kaa na makaratasi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto walimwelewa na hapa nitatoa mfano. Mimi nikiwa na wanangu, nimeenda Petrol Station, nikijaza mafuta nikitaka kuondoka, wanangu wananiambia Baba risiti, risiti! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba watoto wa Taifa hili walikuwa wa kwanza kumwelewa Mheshimiwa Rais, lakini baadaye with time Watanzania tumeendelea kumwelewa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema sisi tufanye kazi. Watanzania wanachotaka ni kazi na mambo yanayoonekana, maana wanasema acha kupiga mayowe, wacha wayaone wenyewe na Watanzania wanayaona wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huu, nina hii karatasi. Nimesoma Mpango kwa utulivu na ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Spika na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kutuletea hivi vitendea kazi. Maana yake hapa nabofya tu, nasukuma tu maandishi yanashuka yanapanda, nachangia kwa wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachotaka nikiseme katika sura ya 4 ya Mpango ambapo umeeleza mipango ambayo tutaielekeza kwa nguvu kubwa kuifanyia kazi. Yapo mambo mengi, nami nataka niseme jambo moja; namwomba Mheshimiwa Waziri kama kuna Msaidizi katika Bunge aje achukue hii document ambayo inaeleza small and medium scale sugar plant. Hii nyaraka kila mwaka nimekuwa nikichangia kwa maandishi na kuiwasilisha kwenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunapozungumza hapa, India sasa hivi wanazalisha sukari tani milioni 35, wamewapita Brazil ambao walikuwa wanazalisha tani milioni 32. Ukitaja mahitaji ya sukari kwa mwaka katika dunia hii, yanaingiza kiasi cha dola bilioni 22 za Kimarekani. Maana yake kwanza uhitaji wa sukari ni mkubwa, lakini hata sisi katika Taifa letu sukari ni kitu ambacho uhitaji wake ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu Brazil wamefanikiwa vipi? Pamoja na Miradi kama hii ya Mkulazi ambayo ni Miradi mikubwa, bado Mheshimiwa Waziri tunaweza tukawekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha sukari ambavyo kwanza moja, havihitaji mtaji mkubwa, lakini pili, havichukui muda mrefu kuweza kujengwa na tatu, vinaweza vikawa viwanda shirikishi. Viwanda shirikishi kwa namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano. Tuna maeneo katika nchi yetu yana mabonde ambayo tungeweza kuzalisha sukari. Kwa mfano, maeneo potential, kuna Bagamoyo, kuna hiyo Mkulazi ambayo tunaenda nayo, kuna Lwipa Ifakara, Rufiji Pwani, Mkongo Mara na Kasulu Kigoma, kote huku tunaweza tukajihakikishia kuzalisha sukari ambayo itatosheleza Taifa letu, lakini kwa sababu pia sukari inahitajika kwa wingi katika dunia tukapata fedha za Kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kufupisha tu katika hili, naomba nimkabidhi Mheshimiwa Waziri hii nyaraka kwa sababu nimeichangia kwa maandishi kwa muda wa miaka mitatu, huu ni mwaka wa nne, pengine ikija kwa maandishi haipati. Sasa niikabidhi kabisa mkononi mwake nikimaliza hapa nitaenda kumpelekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo ambalo msisitizo wake kwanza tuzalishe sukari ya kutosha, tujitosheleze kwenye soko la ndani lakini tuuze nje kwa sababu itatuletea fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ningependa kuzungumza kuhusu utalii. Napongeza kuhusu ununuzi wa ndege ambao unaendelea. Watu wengi, nikienda kule kwetu Bumilayinga, Matanana, Ndolezi kuna watu wanapita wanawaambia wananchi wewe utapanda lini hiyo ndege? Nawaelimisha wananchi kwamba kwa uwepo wa ndege, maana yake tunarahisisha suala zima la utalii ambapo tutapata fedha za kigeni, kesho tutapata umeme, maji, Vituo vya Afya na dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina ushauri katika ndege. La kwanza, mimi siyo mtaalam wa mambo hayo, lakini ukweli usemwe na tuambizane humu ndani. Kumekuwa na delays kwenye Shirika la Ndege zisizoelezeka. Mbaya zaidi handling yake imekuwa siyo nzuri. Siku moja mimi nasafiri kuja Dodoma, nimekutana na mzee pale Airport Dar es Salaam anaenda Mwanza, ndege yake ilikuwa ya saa kumi 12.00, anafika kwenye ku-check in, ndipo anapoambiwa bwana ndege itakuwa ina-delay mpaka saa 3.00.
Mheshimiwa Mwenyekiti, worse enough mtu huyu hata hakuna namna ya kumjali. Utaratibu wa Mashirika mengi ya Ndege unaweza ukampa voucher hata ya thamani ya shilingi 10,000/= kwamba bwana nenda pale Canteen kwamba nenda upate japo kikombe cha kahawa. Kwa hiyo, nawaomba tusijisahau kwa sababu demand iko kubwa. Tuwajali abiria wetu na kadri tunavyoweza hizi delays inawezekana ni mambo technical, lakini tujitahidi kuzipunguza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nashauri, baada ya kuwa na hizi ndege, sasa tu-focus kwenye ndege za kubeba capacity ya abiria 14 labda mpaka 32. Hizi sasa zitatusaidia kuwa-fetch abiria kwa mfano katika utalii. Kama tunavyosema, nia ni kupanua wigo katika utalii. Inaweza kubeba abiria kutoka Dar es Salaam ikawamwaga Mikumi, ikaenda ikawamwaga Ruaha National Park, ikaenda ikawamwaga Selou, Manyara na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ilivyo, kutoka Dar es Salaam kwenda Ruaha kwa mfano, gharama yake kwa hizi ndege za private tulizonazo, unaweza kukuta ni sawa sawa na kutoka Dar es Salaam kwenda Johanesburg au kwenda Dubai. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali ione uwezekano wa kupata ndege ndogo ambazo zitakuwa zina-shuttle hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia mazingira ya wezeshi katika suala zima la Uwekezaji. TIC na Waziri katika Uwekezaji wanafanya kazi nzuri, lakini jamani lazima tuseme ukweli, tutoke kwenye digit tatu. Sasa hivi tuko 141, hebu twende tukawe hata 99. Sasa kuwa hivyo maana yake nini? Tumeona miundombinu inajengwa, umeme shughuli inafanyika, barabara zinajengwa, lakini Mheshimiwa Waziri bado kuna mambo yanatakiwa yaendelee kufanyika katika kupunguza ule urasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kuna blueprint, operational itakuwa lini? Hii blue print iwe operational. Pamoja na hayo, napenda kusema baadhi ya maeneo naomba yatazamwe kwa macho mawili. Kwa mfano, mimi natoka Mafinga, nimeona Mheshimiwa Waziri hapa kuna zile Kanda maalum za Kiuwekezaji, nashauri tuwe na Kanda maalum ya Kiuwekezaji kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini maalum kwa ajili ya mazao ya misitu. Huu nao ni uchumi ambao ni mkubwa sana, (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nafahamu suala la umeme ni huduma, lakini ni biashara, lakini kuna maeneo yatizamwe kwamacho mawili. Katika Wilaya Mufindi tuna-consume Megawatt 14, kuna maeneo Mkoa una-consume Megawatt 4. Sasa maeneo kama sisi ambao demand ni kubwa, tuna Viwanda vya Mbao, tunaomba tutazamwe kwa sababu tutazalisha, tutalipa bili kubwa ambazo zitasaidia TANESCO na REA kupanua umeme katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Matanana, Mwongozo Mafinga na Ifingo watu wana viwanda, wana mashine lakini umeme haujafika. Kwa hiyo, naomba hata kama tunapeleka katika nchi nzima, yale maeneo ambayo kuna uzalishaji, tuyatizame kwa macho mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niseme kuhusu TARURA. Tunajenga kweli barabara za kuunganisha Mikoa, lakini kwa mfano, mimi pale Mafinga, Mtula tuna scheme ya umwagiliaji, tutafikishaje bidhaa sokoni ikiwa TARURA wanapewa fedha ndogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea kusisitiza, kwa sababu TARURA ndiyo inatuhudumia kwa kiwango kikubwa, natoa ushauri kwa Serikali, tutafute chanzo maalum ambacho kitaiwezesha TARURA ili iweze kuzihudumia barabara ambazo ndiyo backbone ya nchi kwa maana ya kwamba, mbali ya kubeba mazao, lakini pia zinabeba bidhaa, wakati mwingine zinabeba mbolea kuwafikishia wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumejenga Kituo cha Afya, Ihongole, lakini barabara haipitiki kwa mwaka mzima. Sisi Mafinga tunahitaji shilingi bilioni 4.8 kwa mwaka, tunapata shilingi bilioni moja, tunajua ni kwa sababu ya ukomo wa Bajeti. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali, tuone pia TARURA tutaijengea vipi uwezo ili kusudi tuimarishe barabara zetu kwa ajili ya kusafirisha mazao, bidhaa na mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)