Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na kuweza kuwepo hapa tukaendelea na shughuli zetu za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia niwapongeze wananchi kwa namna walivyojitokeza kujiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kwamba baadaye hili zoezi lilikuja kuvurugwa, nitazungumza hapo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wizara ya Kilimo. Mara nyingi Watazania tumekuwa tukisema kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu lakini tumekuwa tunasema kwa nadharia siyo kwa vitendo. Kwa nini nasema hivyo? Kilimo cha Tanzania kimekuwa katika misamiati ya kisiasa, tumeanza na Kilimo cha Ushirika, Kilimo cha Bega kwa Bega, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo Kwanza na kadhalika lakini ukikitazama kilimo chenyewe kimekuwa kila siku kinarudi chini badala ya kwenda juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na nini? Kwenye bajeti ya kilimo fedha zilizotengwa, kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 zilitengwa shilingi bilioni 100.52 lakini mpaka Machi 2017, fedha iliyotolewa ilikuwa ni bilioni 2.25 tu ambayo ni sawasawa na asilimia 2.2 kwa maana ya kwamba asilimia 98 haikutekelezwa. Je, hapo tunaweza kusema kwamba tuko serious na kilimo kweli! Jibu ni kwamba hatuko serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia kwenye mwaka 2017/2018, tulitenga shilingi bilioni 150.235 lakini mpaka mwezi Machi, 2018, fedha iliyotoka ni shilingi bilioni 16.52, ambayo ni sawasawa na asilimia 11, ina maana asilimia 89 haikutekelezwa. Hatuishii hapa, hata kwenye mwaka 2018/ 2019, tulitenga shilingi bilioni 98.119 lakini mpaka mwezi Machi ikapokelewa shilingi bilioni 41.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa napata tabu kidogo kuona kwa nini tunatenga bajeti ambazo hatuwezi kuzitekeleza. Badala ya kuweka shilingi bilioni 100 basi angalau tungeweka shilingi bilioni 50 halafu tukipeleka shilingi bilioni 39 au 40 tunakuwa tumeweza kufikia angalau asilimia 50 lakini hili jambo limekuwa ni la kila mwaka. Wakati mwingine ndiyo tutazidi kusema bajeti zetu zinakuwa ni kama vile za copy and paste kwamba tunapeleka hivyo hivyo tu. Yanatokea matatizo lakini haturudi nyuma kujiuliza kwa nini hatukufikia asilimia hii ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mwaka 2016/2017 ilitengwa bajeti ya shilingi bilioni 4, lakini mpaka mwezi Machi, 2017 zilimepelekwa Wizarani shilingi milioni 130 ambayo ni sawasawa na asilimia 3.25. Mwaka uliofuata 2017/2018, bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 4 kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi lakini mpaka mwezi Machi, 2018 haijapelekwa hata senti 10! Sasa hapa tunakwendaje? Hii mipango tunayoipanga halafu haitekelezeki inakuwaje? Ndiyo ile if you fail to plan, you plan to fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niseme tu tutayarishe au tuandae mipango ambayo inatekelezeka. Wananchi wetu sasa hivi wanafuatilia na wanaona katika nchi za wenzetu mipango wanavyoipanga na wanaona na sisi jinsi tunavyopanga mipango yetu ambayo haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wa Tanzania wanajitahidi sana kwenye kilimo. Pamoja na hiyo misamiati inayosemwa kuna kama asilimia 10 ambao wanalima kilimo cha kisasa kutumia matrekta na dawa na kadhalika. Kuna kama asilimia 30 wanaolima kutumia wanyama kazi kwa maana ya mifugo hii na plau lakini asilimia 60 ni wakulima wa jembe la mkono ambao hawa ndiyo haohao wakulima wanaolima mbaazi, korosho, njugumawe na mhogo ambapo mwisho wake kwenye mavuno wananchi wanakuwa hawana masoko, tunawakatisha tamaa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuelewe kwamba tunapopanga hii mipango tujue kwamba tunawapaingia mipango wananchi ambao wanasikiliza Serikali yao inawapangia nini ili waweze kutekeleza. Tukumbuke kwamba hawahawa wakulima ambao tunawakwamisha kwenye masoko ndiyo hawahawa ambao wanasomesha watoto vyuo vikuu na English Medium Schools, tunapowakwamisha kwenye masoko ndiyo hapohapo sasa wanafunzi wanapobaki nyumbani kwa sababu wazazi wanakuwa hawakuuza mazao, hawana fedha, hawawezi kulipa ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mwishoni mwa wiki nilirudi Tanga, amekuja kijana na mzazi wake ananiambia Mheshimiwa sisi tuna shamba letu la mihogo Kirare, Kirare ni Kata moja Tanga ambayo ni mashuhuri kwa kilimo cha mhogo, wanasema lakini mhogo kawaida miezi sita unavuna kama kuna soko, sasa tuna mhogo una miezi nane haujavunwa, hatuna soko, carry nzima ya mhogo unauza Sh.60,000. Matokeo yake mzazi yule ana watoto wawili wamefaulu, mmoja anatakiwa aende chuo Mbeya mwingine Iringa, mzazi hana fedha, mazao ambayo ni mhogo yako shambani, afanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tuhangaike sasa kutafuta wafadhili, mfadhili wa kumsaidia mtoto kusoma itategemea na anavyojisikia na anavyojua umuhimu wa elimu. Je, kama mhogo ungekuwa na soko la uhakika kwa nini mzazi yule asingeenda kukopa hata benki kwa dharura halafu akatumia fedha ile kuwalipia watoto wake ada? Huu ni ushahidi kwamba Serikali tunasema maneno mengi sana, tunaandika sana, lakini ukirudi kwa wananchi hali zao ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, hii mipango ambayo kila mwaka tunaitayarisha, tunaitangaza, tunaipitisha halafu haitekelezeki, inawakatisha tamaa wananchi. Matokeo yake sasa wakati mwingine mtu anaona bora aachane na shughuli za kilimo. Akienda kwenye biashara nako anakutana na kodi kubwa huko biashara inamshinda, duka anafunga, hajui afanye nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine wengine wanafikia hata kujinyonga, maana yake mtu anadaiwa school fees za watoto, ana biashara kwenye frame anadaiwa, ana gari huku labda bovu, huku ana watoto wengine wanasoma shule za msingi, huku anadaiwa bili za umeme na maji, afanye nini? Inafika mtu anachukua maamuzi magumu ya kufikia kujinyonga, maisha yamekuwa magumu kila kukicha. Waheshimiwa Wabunge wenzangu ukitaka kujua kama maisha magumu turudini mitaani hali ni mbaya sana, milo mitatu tuliyoizoea hailiki sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu sasa hivi wanakunywa cha saa tano asubuhi, chakula cha mchana kinaliwa saa kumi na moja, ndiyo imetoka watu wameua winga mpaka siku ya pili. Kwa nini Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi, Mwenyezi Mungu ametujalia bahari, madini ya aina zote (tanzanite, almasi, dhahabu mpaka uranium), kwa nini Watanzania washindwe hata kula milo mitatu kwa siku? Ni kwa sababu mipango yetu tunaipanga vizuri kwenye makaratasi lakini kwenye utekelezaji inakuwa ni asilimia chache sana. Kwa hiyo, naomba tubadilike Mheshimiwa Waziri tunapopanga mipango basi mipango hiyo itekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nije kwenye masuala ya mipango ya uchukuzi, nagusa Kitengo cha Bandari. Watanzania tuna Bandari kubwa ya Dar es Salaam lakini tusisahau tuna bandari nyingine kama Tanga, Mtwara na Zanzibar. Mimi nitazngumzia huu upande wa Bara kwa sababu Zanzibar angalau inafanya kazi vizuri inachukua mizigo yote ya Unguja na Pemba lakini Tanzania Bara mizigo yote tunaisukumiza Dar es Salaam, matokeo yake sasa Bandari ya Dar Salaam imezidiwa, makontena na meli ni nyingi, zinashindwa kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nishukuru baadhi ya kilio changu kusikilizwa na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Bandari ya Tanga sasa ipo meli pale inayoongeza kina (inachimba) na vilevile pia tumepata vifaa vipya, kama ile crane ya forty, fifty containers imepatikana na nyingine ndogondogo lakini kama cranes zile tumepeleka na kina kinaongezwa halafu hakuna meli za mizigo zinazokwenda, faida ya kutumia fedha zote hizo takribani shilingi bilioni tatu na milioni mia saba Mheshimiwa Waziri umetenga kwa mwaka huu wa fedha itakuwa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ni lango kuu la biashara duniani. Nashauri tufanye categories za mizigo, bandari ya Dar es Salaam ichukue mizigo ya Dar es Salaam yenyewe, Pwani na Morogoro lakini Bandari ya Tanga ichukue mizigo ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Msoma na Bukoba na nchi za jirani kama vile Rwanda na Burundi mizigo yao ipitie kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Bandari ya Mtwara, tunayo Mtwara Corridor, kwa nini Bandari ya Mtwara basi isichukue mizigo ya Mtwara yenyewe, Lindi, Mbeya, Sumbawanga, Katavi, Kigoma, Zambia na Malawi. Hapo tutakuwa tumezitendea haki bandari zetu lakini Bandari ya Dar es Salaam tumeibebesha mizigo yote, bandari nyingine kama Tanga ukienda sasa hivi watu wanacheza draft. Hivi kweli bandarini unaweza ukacheza draft au karata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tunaambiwa na wazee wetu linapitishwa tangazo kwamba jamani vijana wa mjini kuna kazi bandarini, meli ya Spain, Ujerumani, China na German zote zimekuja kwa wakati mmoja zinahitaji vibarua wakafanye kazi lakini leo unaweza ukakaa kwa mwezi zinakuja meli mbili au moja, matokeo yake tunawekeza fedha nyingi kwenye bandari zetu lakini mizigo inayoingia na kutoka haipiti katika bandari zetu. Kwa hiyo, nashauri Serikali tufanye categories za mizigo, bandari zetu zote ziwe zinafanya kazi, tushindane na nchi jirani ya Kenya ambayo imekuwa kimbilio la wafanyabiashara wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kuzungumzia suala la demokrasia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante lakini ujumbe umefika.