Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Maana naona Walimu tuko wengi sana, nami nimefundisha zaidi ya miaka 15, ni muhimu sana kutoacha bajeti hii ipite hivi hivi bila ya kuwasemea Walimu na elimu kwa ujumla. Kwa nini? Kwa sababu, kimsingi elimu ndiyo injini ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la kwanza ni kuzungumzia maslahi na madai ya Walimu. Tulitoa ahadi na tunaendelea kuitoa ahadi hiyo kwamba tutawatetea Watumishi wa Umma na hili ni jambo la msingi ambalo ni lazima tulifanye. Tumewaahidi tutawatetea na sisi tutafanya kazi hiyo, ila Serikali nayo itimize wajibu wake katika kuhakikisha inatimiza ahadi inazozitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wana changamoto kubwa. Wapo Walimu ambao wanadai kupandishwa mishahara katika maeneo mbalimbali nchi nzima. Kwa mfano, tu katika Jimbo langu la Masasi Walimu zaidi ya 50 bado wanadai kupandishwa mishahara. Hili ni jambo la msingi na ni lazima Serikali iwajibike kuhakikisha kwamba watu hawa wanapata fursa ya kulipwa mahitaji yao ili waweze kufundisha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jambo hilo, kimekuwa kilio cha Walimu cha muda mrefu cha kupata posho ya madaraka (responsibility allowances). Tunao waraka ambao umetolewa na utumishi, Waraka Na. 3 wa mwaka 2014, unaotoa maelekezo, toka mwaka 2015/2016 maelekezo hayo yalipaswa kutimizwa kwa bajeti iliyopita, kwamba Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi alipaswa kulipwa shilingi 200,000/= kila mwezi kama posho ya madaraka; Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari shilingi 250,000/=, Mkaguzi wa Elimu Kata ni shilingi 250,000/= lakini Mkuu wa Chuo cha Ualimu ni shilingi 300,000/= kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mazuri tu, tumwambie Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atupe mkakati ukoje katika kutekeleza mahitaji ya waraka huu unaotaka Walimu walipwe responsibility allowances.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ni muhimu tuliweke wazi suala ambalo kimsingi nchi yetu imepita katika mtikisiko wa kutoka kufanya mabadiliko makubwa ya namna ya kutoa vyeti vyetu kwa wanafunzi wetu wa Kidato cha Nne. Hili ni jambo la msingi sana! Sasa hivi tunao vijana wetu ambao tumeshatikisa standard ya vyeti vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali, sasa iandae utaratibu na Waziri atuambie utaratibu anaokuja nao, tufute vyeti vyote vyenye GPA, badala yake watoto hawa wapewe vyeti ambavyo vina division.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tumeamua kufanya mabadiliko, tumetoka tena kwenye GPA tunakwenda kwenye division, tayari tumeshaathiri watu katika kundi kubwa sana ambao mpaka sasa hivi wanashindwa kutambulika wana standard gani ya elimu katika vyeti vyao. Naomba tuliangalie sana hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusu Elimu Maalum. Kama kuna eneo ambalo limesahaulika katika nchi hii, ni Elimu Maalum. Ninajua tukisema Shule za Sekondari na Shule za Msingi tutasema ziko katika eneo la TAMISEMI, lakini acha tu tuseme, nami ninaishauri Serikali, iangalie uwezekano wa kuchukua shule hizi za Elimu Maalum na kuzipeleka kwenye Wizara badala ya TAMISEMI ili ziweze kupata jicho maalum la kuziangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika katika hizi Shule za Msingi na Shule za Sekondari ambazo zinawasaidia vijana wetu wenye mahitaji maalum, unaweza ukatokwa na machozi. Vijana hawa wanasoma katika mazingira magumu sana. Nadhani hata kama tukienda kwenye theories of learning tunajua kabisa miongoni mwa shule ambazo zilitakiwa ziwe na mazingira rafiki na ya kuvutia ni hizi zenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna shule mbili za msingi; Shule ya Msingi Masasi na Shule ya Msingi Migongo. Watoto hawa wamesahaulika! Naomba Serikali iangalie namna invyoweza kuziboresha shule hili ili na hawa wenye mahitaji maalum wajione ni sehemu ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mambo hayo, napenda tu kuelezea jambo la msingi kwamba tunaposhughulikia elimu katika nchi yetu, hatuwezi kuweka mkazo moja kwa moja kwenye formal education pekee, yaani kwenye elimu ndani ya mfumo rasmi. Hili nimekuwa nikilisema na leo nalirudia tena. Ninaposoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri sioni inapojitokeza non formal education.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo takwimu kwamba kama asilimia 50 ya Watanzania ni watoto; na kama asilimia 50 ni watoto, maana yake ni takriban milioni ishirini na kitu. Kama waliopo katika mfumo rasmi wa elimu ni milioni 12 tu, ni wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu ambalo haliwezi kufikiwa bila ya kushiriki nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie, hatuwezi kutumia madarasa yetu pekee kutoa elimu ya sekondari. Naiomba Wizara iangalie namna ambavyo inaweza ikazitumia taasisi zake kama vile Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha kwamba watoto wengi ambao wanakosa kuingia katika elimu rasmi, waende nje ya mfumo rasmi wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ya kuyaangalia katika hilo. Nimekuwa nikisema, Waziri naye sasa hivi atakuwa na dhamana kubwa ya kuhakikisha tunakuja na mikakati ya kupunguza kiwango cha watu ambao wako nje ya mfumo wa elimu, wasiojua kusoma wala kuandika, wengine ni watu wazima; nao pia tuwaelimishe, tusizingatie tu elimu rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya kuzungumza, lakini niseme tu kwamba hali ya elimu tunaendelea kujikokota, tunakwenda, lakini yako mambo ambayo bado ni changamoto. Katika Jimbo la Masasi tuna tatizo kubwa la Walimu wa Shule za Msingi. Tunahitaji Walimu takriban 252; hatuna hata Mwalimu mmoja wa kufundisha Shule ya Awali, katika Walimu wa sayansi kiwango cha sekondari tuna matatizo makubwa. Tunapungukiwa Walimu zaidi ya 60, haya ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto tulizonazo, pamoja na juhudi kubwa tunazofanya za kutoa elimu bila malipo, lakini pia tuongeze nguvu katika kutatua changamoto zinazotukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi, huo ndiyo mchango wangu. Naunga mkono hoja. Naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ambayo yatatupa imani. Ahsante sana.