Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.Napenda nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia mpango wa maendeleo kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa mpango ambao unaendelea. Tumeona upanuzi waBandari zetu zote kuanzia Mtwara, Dar es salaam na hata Tanga. Nina imani kabisa upanuzi wa bandari hizi utawezesha kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Serikali ya viwanda, kwasababu matarajio yetu bandari hizi zitaweza kubeba malighafi na pia kubeba bidhaa ambazo zinazalishwa katika maeneo yetu.Sasa hivi Bandari yetu ya Mtwara inatumika kusafirisha saruji kupeleka Comoro, kupeleka Zanzibar lakini ni imani yangu kwamba Bandari yetu ya Mtwara itakapokamilika, upanuzi ule ambao unaendelea utawezesha ubebaji wa korosho kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tulikuwa na korosho ambayo ilikuwa haijapata wanunuzi. Baada ya kupata wanunuzi, meli zinazokuja sasa hivi za kizazi cha nne(fourth generation), meli moja tu ikija ku-park basi nyingine zinasubiri kwa muda mrefu. Ndiyo kusema ule muda ambao meli inachukua kusubiria ili nyingine itoke ili nyingine ije i-park pia inaathari katika bei ya korosho kwasababu mnunuzi anawekewa na ile gharama ya kusubiria. Ni imani yetu kwamba mara baada ya upanuzi wa Bandari ya Mtwara utakapokamilika meli nyingi zaidi zitaweza ku-park kwa wakati mmoja na kuweza kuchukua korosho kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji na faida ile itakwenda moja kwa moja kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuiomba Serikali yetu; upanuzi waBandari ya Mtwara uende sambamba na ujenzi wa reli ambao umeshafikia hatua nzuri kwa maana ya upembuzi yakinifu umekamilika, tathmini ya gharama za fidia nao umekamilika. Kwahiyo, tulikuwa tunaomba ili Bandari ile ya Mtwara iweze kufanyakazi vizuri, basi ule ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbambabay na matawi yake ambayo yanakwenda Liganga na Mchuchuma sambamba na miradi ya Liganga na Mchuchuma kwa maana ya chuma na makaa ya mawe na yenyewe sasa ianze kutekelezwa ili bandari pamoja na reli viweze kufanyakazi kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Mpango wetu tunaonesha tuna nguvukazi ya kutosha yaani watoto wenye umri wa miaka 0-14 lakini pia hata kwenda kwenye miaka 45 ambayo ndiyo nguvukazi kubwa tunayoitegemea ni zaidi ya asimilia 50. Nguvukazi ile kwa maana ya watoto wenye umri ule wa miaka 15, 14 mpaka miaka 30 ili tuweze kunufaika nayo na iweze kutumika vizuri katika kukuza uchumi ni vizuri tukawekeza katika rasilimali watu na uwekezaji wa rasilimali watu ili uweze kuwa na manufaa zaidi ni lazima tuanze kuwekeza katika mwaka sifuri mpaka siku zile1,000za mwanzo nikimaanisha lishe kwa watoto wetu. Kama tutawekeza kwa maana ya lishe ya watoto kuanzia siku sifuri kwa maana ya ujauzito mpaka anafikia siku 1,000 zile ndipo hapo tutakapowapeleka shuleni na hata kwenye vyuo tutaweza kupata matunda mazuri sana na yataweza kusaidia katika kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia lishe watu wengine wanakuwa hawaelewi, lakini zile siku 1,000 tangu mtoto akiwa kwenye tumbo la mama yake mpaka anazaliwa na siku zile 1,000 ndizo zinazojenga ubongo wa mtoto na ndizo zinazoweza kumfanya aweze kujadiliana vizuri, aweze kushika vizuri masomo darasani na hivyo hivyo aje kuchangia katika uchumi wa nchi. Nchi kama Japan hazina rasilimali kama ambazo sisi tunazo, lakini wenzetu wamewekeza katika rasilimali watu, wamewekeza katika vichwa vya vijana wao, ndiyo maana wanaweza kutengeneza magari, wanatengeneza computer na wameweza kuendeleza nchi zao kwasababu wamewekeza katika rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo nataka pia nilisisitize; tuache mtazamo wa kuwekeza zaidi kwenye vyuo vikuu na tukaacha hizi taaluma za kati kwa maana mafundi Mchundo, kwa maana vyuo vyetu vile ambavyo vinawajengea uwezo zaidi kuliko vyuo vikuu.Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana atakuwa shahidi, sasa hivi wanaomba vibali vya kufanyakazi katika nchi yetu ni katika nafasi za fundi mchundo zaidi kuliko hata wahandisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mkutano wa wadau wiki iliyopita kule Mtwara, mkutano wa uwekezaji na katika makundi yaliyopangwa kwenda kutembelea mimi nilikwenda kutembelea kiwanda cha Dangote. Tumekuta pale wanajenga mtambo ambao utazalisha umeme kwa kutumia makaaya mawe, kutumia gesi, kutumia mafuta yaani mtambo uko combined kwa pamoja yaani mafundi mchundo waliojazana pale ni shemeji zangu kutoka India ndiyo waliojazana kwa maana kwamba sisi hatuna, tuna wahandisi lakini hatuna ma-technician kwahiyo tunalazimika sasa kuagiza kutoka nje. Kwahiyo, naomba tuwekeze katika vyuo vyetu vya ufundi, tuwekeze katika VETA zetu,kwasababu kama tunavyofahamu Injinia mmoja anahitaji zaidi mafundi mchundo zaidi ya watano na kuendelea. Baadhi ya vyuo vyetu vyote ambavyo vilikuwa vinatoa mafunzo hayo sasa hivi vyote tumevigeuza kuwa vyuo vikuu. Sasa hii rasilimali watu tuliyonayo ambayo ni mtaji mkubwa sana katika ukuzaji wa uchumi. Ni lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa ili tuweze kuitumia inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunaweza tukalitumia katika kukuza uchumi wetu ni katika eneo la uvuvi; niiombe sana Serikali yangu iwekeze kwenye uvuvi. Iwasaidie wavuvi kupata zana bora za kisasa ambazo wanaweza wakazitumia. Kwenye uvuvi tofauti na kilimo unahitaji kulima, unahitaji pembejeo, unahitaji mbolea; kule baharini ni kwenda kuvuna tu. Tunachotakiwa kupata ni zana za kisasa ambazo zitatuwezesha kwenda katika bahari kuu na kuweza kuvuna rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujaalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wavuvi wetu ni kama aneo ambalo limesahauliwa. Ukienda Msimbati, nenda Nalingu, nenda Msanga Mkuu tunachokifahamu Serikali ni kwenda kufanya operation lakini zile operation zinatokana na kwamba hawana hizo zana bora. Hatujawapa kama ambavyo wakulima au wafugaji tunawapa pembejeo, tunawasaidia kuwajengea majosho, tunawasaidia kuwaunganisha katika vikundi na kuwawezesha.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hawa malizia.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kuomba wenzetu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wawawezeshe zana na ujuzi wavuvi katika eneo hilo tunaweza kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)