Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nakumbuka kuna Bunge lililopita ambalo tulifanya kazi kubwa sana ya kutunga Sheria ambayo ingesaidia kuboresha, kulinda demokrasia, lakini kuhakikisha vyama vyetu vya siasa vinaendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu, lakini leo tumekuwa na vyama ambavyo vimegeuka ni SACCOSS ya kikundi cha watu wachache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wenzetu wa CHADEMA wamekuwa na kikao chao cha Kamati kuu lakini maswali ya msingi yaliyoibuka kwa Wabunge wa CHADEMA na baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu ni kwamba walimtaka Mwenyekiti wao aweze kuwasaidia moja michango yao ambayo wamekuwa akiwachangisha ili iweze kusaidia chama kujipanga kwenye uchaguzi ambao unakuja.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakawa wanamuomba kwamba kuna ruzuku ambayo imekwisha ingizwa na Serikali huko nyuma na ile michango ambayo tayari kama milioni 600 na mingine ambayo Wabunge, mwenyewe nadai milioni 18 kule! Nadai milioni 18 kwa hiyo, naomba hapa ile sheria itumike ili hata na mimi tutakaporudishiwa hela na mimi 18 zangu zirudi huku na Watara apate ya kwake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Wabunge wakumwambia Mheshimiwa wao kwamba kama sisi tusisusie huu uchaguzi, twendeni kwa sababu ni fursa ya sisi kufanya siasa lakini tuchukue pesa ambazo tumepata za ruzuku lakini michango ya Wabunge ambao tumekuwa tukisema inakusanywa inawekwa akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi. Wakasema uchaguzi huu ndiyo wenyewe sasa, twendeni tukafanye siasa hata kama kuna maeneo wenyeviti wameweka mpira kwapani hawajajiweka, lakini tutapita kufanya siasa. Wabunge wameomba hilo ili wazunguke hii nchi nzima kila kijiji wapate pesa waende huko, pesa hamna! Sasa wamekimbilia kwenye siasa rahisi za kusema kwamba uchaguzi sio huru na haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakawa wanazungumzia suala la watendaji na wakurugenzi kufoji sijui kufanya nini. Wao waliwaambia watu wao na walipita kwa semina zao na kuwaambia hakikisheni hamfanyi hivyo halafu wao wanafanya siasa rahisi huku juu kuonesha kwamba hakuna uhuru wa kufanya uchaguzi. Haya nilitaka kuomba kwenye hiki kipengele kwamba kama tulitunga sheria na kama kweli tunataka tupate vyama ambavyo maana yake uwepo wa vyama vya upinzani vinasaidia sana kwenye maendeleo kwa sababu vinajenga amsha amsha na vinaamsha chama ambacho kinatawala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaruhusu watu wachache watuulie vyama hivi vya upinzani maana yake siasa na maendeleo yetu yataenda kupata shida. Tunataka tumuombe Msajili wa Vyama vya Siasa sasa aanze kuitisha kufuatilia hivi vitu kwa makini na kama nitakuwa nimesema uwongo, niko tayari na mimi kuitwa pale juu na kwenda kujieleza kama nitakuwa nimesema uongo kwamba hawa ndugu zangu hawaibiwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondokane kwa sababu wanasema mambo yanavyokwenda usalama unapata matatizo, nchi hii haitakuwa salama. Kuliko watu watengeneze mambo halafu wahatarishe usalama wa nchi yetu, ili kunusuru hilo twendeni tukaone ukweli, Watanzania wajue ukweli, watu waache kuchonganisha wananchi na Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimewashauri huko nyuma wakati CUF wanagombana nikawaambia mbona hii game rahisi wakati nikiwa kule. Mchukueni Sharif pale anakuja anakuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA mambo mengine yanaenda, siasa inakuwa bora kwa sababu ni kijiwe na mtu mmoja, walimkataa ameenda ACT wanaanza kupiga kelele.
Mimi nimeamua niseme hilo kabla sijaingia masuala ya maendeleo kwa sababu hili ni muhimu sana kwa usalama na heshima ya nchi yetu Kimataifa, hao watu wanachafua nchi yetu sana. Naomba tufanye hilo na Msajili afanye hiyo kazi lakini kama Serikali ina n amna ya kufuatilia ruzuku yake, ifuatilie niko pole pole naenda Mahakamani kudai milioni 18 zangua mbazo hazijafanya kazi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wabunge wetu wamechangia kwenye…
MWENYEKITI: Sijakuelewa, Mheshimiwa Mollel kuna hela zinatolewa kwa Waheshimiwa Wabunge na Spika sijui, hela za namna gani?
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimechangia 500,000 kwa miaka mitatu kila mwezi na niliandika mwenyewe barua kweli, sipingi! Lakini ukweli ni kwamba haijatumika kwenye lengo tulilopanga. Sasa hivi watu wamepiga kitu kwapani, wamekula hela, wamejenga mahoteli wenzao wanatesema hapo, ukiwaona wamechoka hapo Mheshimiwa Silinde hapo usimuone ndugu yangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Viti Maalum wamedaiwa 1,500,000.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Nina uhakika hiyo Taarifa ni muhimu sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara nimekuona, kuhusu taarifa.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru. Waheshimiwa Wabunge naomba nimpe Mheshimiwa Mbunge anaendelea kuchangia Godwin Mollel Mbunge wa Siha Taarifa kwamba na mimi ni miongoni wa wanaodai Chama hicho za zamani shilingi milioni 18 kwa sababu tulikuwa miaka mitatu pale kwa hiyo Mheshimiwa kwenye kesi ambayo utafungua na mimi nitaku-join ili tukadai hizi hela Mahakamani. (Makofi/Kicheko)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo na namkumbusha
Mheshimiwa Waitara yeye ni milioni 19 na pesa kwa sababu yeye alichelewa kidogo kurudi huku. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye eneo la kilimo. Viti Maalum ni 1,500,000 na bado wanachangishwa 2,000,000 na wengine wamechelewa kikao fulani wakapigwa faini 2,000,000 na watu wakapiga kwapani wala haikuifanya kazi ya chama. Hiyo ndiyo CHADEMA halafu inasema tuna taka uadilifu katika nchi, uongozi wenye maslahi, sijui vitu gani! Hapa tunataka kujenga nchi, tuko serious, hatutaki vijiwe na CHADEMA wale wanaotaka kuiua CHADEMA hatutakubali. CCM itatetea CHADEMA isimame CHADEMA kama chama. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaenda kwenye eneo la kilimo. Wabunge wengi wamechangia na wakaonesha kwamba kilimo kinachangia asilimia 28 ya pato la Taifa lakini kwa mwaka huu ukuaji wake ni asilimia 5.3. ni ukweli kwamba kilimo ni sehemu nyeti sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Nilitaka kuomba Wizara ambazo zinahusika ukitaka kumsaidia mkulima sio kumpa pembejeo, ukitaka kumsaidia mkulima ni kumtafutia masoko ya mazao yake, sio kutenga, ni kutafuta masoko ya mazao yake. Kutembea kwenda sehemu mbalimbali na kutafuta masoko kwa ajili ya mazao husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kumsaidia mkulima inawezekana kweli wakati mwingine tunajaribu kudhibiti mazao kutoka nje ili kudhibiti mfumuko, lakini hasara yake nini? Unaweza ukawa undhibiti mazao kutoka nje kwa ajili, najua sasa hivi limeondolewa lakini hasara yake inawezekana ndiyo iliyotuathiri mwaka huu tukashuka madhara yake ni kwamba wananchi wanaweza wakaachana na hayo mazao ambayo walikuwa wanayazalisha mahindi wakaachana nayo wakaenda kwenye mazao mbadala halafu mwisho wa siku ukajikuta unatumia fedha za kigeni kununua mahindi na mwisho wa siku ukapandisha bei ya shilingi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuuachie uhuru wa watu kuuza popote na Serikali ifanye juhudi ya nguvu sana kutafuta masoko sehemu mbalimbali kahawa na mazao mengine yote ambayo wananchi wetu wanayalima kwa namna hiyo hatutakuwa na haja ya kuuza pembejeo kufanya nini, wananchi wenyewe watatafuta vitu vyao na Serikali itaachana na mizigo ya kutaka kupeleka pembejeo na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili nilitaka tujikite zaidi kutoa elimu kwa sababu Serikali imefanya kazi kubwa mno. Leo tukizungumzia vile vile kilimo kushuka katika Taifa letu maana yake ni kwa sababu hatuna viwanda, kwa sbabau tukiwa na viwanda ambavyo vinachakata aina ya mazao tunayozalisha maana yake ni kwamba wananchi wetu watapata masoko ya kuuza mazao yao na hata kilimo na uzalishaji utapanda ndiyo maana tuna bwawa la Nyerere ambalo tunatengeneza umeme. Ukiwekeza kwenye eneo la umeme ukazalisha umeme wa kutosha maana yake kutakuwepo na viwanda huku Tanzania kwa sababu umeme tulionao leo hata tukisema tutaweka viwanda, hatutakuwa na umeme wa kutosha na tutakapokuwa na umeme wa kutosha hata ujenzi wa viwanda na bei ya umeme itashuka na viwanda vingi vitatengenezwa na mwisho wa siku tutamnyanyua mkulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaposema kwamba uwekezaji kwenye kilimo ni mgumu, ninachokiona kuna umuhimu wa kuelimisha watu kwamba uwekezaji unaofanyika kwenye barabara, umeme, treni na ndege mwisho wa siku uwekezaji huo wote unakuja kumsaida mkulima wetu kwa sababu atasafirisha mazao kwa urahisi, mkulima wetu atapata umeme wa bei rahisi, mkulima wetu akipata umeme wa bei rahisi na kiwanda kinapata umeme wa bei rahisi maana yake viwanda vitafunguliwa vingi. Wakulima wetu, Kenya ndege zinapishana kupeleka mazao yanayozalishwa na wakulima wa Kenya kupeleka huko nje na sisi maana yake ndiyo maana tunasema na ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachosema unapotazama kilimo usitazame kilimo kama ni shilingi ngapi inailetea kilimo moja kwa moja. Tazama ni vitu gani ambavyo vinaweza vikasaidia kilimo na ni vitu gani ambavyo ukiviunganisha mwisho wa siku input yake inaenda kuingia kwenye kilimo. Ndiyo namna hiyo tun apotaka kutazama bajeti ya kilimo ni shilingi ngapi na tukaona. Inawezekana unaona hela iliyopelekwa kwenye kilimo ni kidogo lakini hali halisi hela ni nyingi sana kwa sababu input zote hizo zinakuja kusaidia malighafi ambazo zinazalishwa ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la maji, niseme kuna hela nyingi sana zinapelekwa kwenye maji na watu wengi wamekua wakichangia kuhusu hilo. Nafikiri kuna umuhimu sana nisiongee sana kwa sababu imeshasemekana. Kuna umuhimu wa kutumia force account nayo kwenye eneo la maji kwa sababu tunaibiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Siha tu coverage yetu ya maji ni asilimia 87 lakini…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Malizia.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba tu Naibu Waziri au Waziri wa Maji hapa twende tena Siha, kile kikundi cha mafisadi wa maji waliokwenda Mkoani na sehemu zingine kumzuia asifanye utekelezaji wa mambo ambayo yatasaidia wananchi wa Siha kufanya bill ndogo ya uuzaji wa maji bado kinatusumbua kule. Twende halafu tushushe bei ya maji kwa ajili ya wananchi wa Siha. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa mchango wako. Dah! Kumbe watu wanazoa mahela hapa, hatari kubwa! Na nyie mnatoa tu, nyie vipi? Hatari kubwa! Inahitaji tuwasaidie kwakweli. Waheshimiwa Wabunge, lakini ofisi yangu haihusiki kukata hela ya mtu yeyote. Hatufanyi hiyo biashara sasa hivi.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeibiwa sana tusaidie ndugu yangu.