Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema kwamba tunachangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa ambao fedha zake zinatokana na kodi za wananchi bila kujali hao wananchi wapo kwenye vyama gani vya kisiasa ama wao ni wafuasi wa kundi lolote lakini wote ili mradi ni Watanzania tunchangia kodi na ndiyo fedha hizi ambazo zinatumika kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yako maelezo yanasemwa na wako watu wanzunguka kwenye majimbo yetu kwenda kusema maendeleo hayapatikani kwa sababu kuna Mbunge wa Upinzani kwamba Seriakli ya Rais Magufuli haipeleki miradi ya Maendeleo kwenye Majimbo ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linapaswa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ulikemee kwa sababu ni kinyume kabisa na Katiba na Sheria lakini pia nadhani ni kinyuma hata na matakwa na Rais Magufuli kwamba yeye siye aliyeagiza watu wapite kwenye majimbo yetu waseme kwamba maendeleo hayaji kwa sababu mechagua Wapinzani. Ni jambo ambalo kidogo ukilisikiliza linaleta fadhaa kuona watu wenye uelewa wa kiwango hicho wanasema maneno hayo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bobali upokee taarifa!
T A A R I F A
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa Taarifa mzungumzaji. Anachokisema si sahihi. Kuna vituo vya afya viwili vimejengwa Mchinga na Mchinga ni Jimbo la Upinzani.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bobali unasema maendeleo hayapelekwi, anasema kuna vituo vya afya viwili. Karibu bilioni moja imeletwa kwako.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuelewa na nadhani kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka hakunielea nilichokisema. Kwanza, tumepata kituo kimoja cha afya sio viwili lakini hakunielewa. Nilichosema ni, wako watu wanazunguka na tukisema hivi wengine tunawaweka bracket, wengine tunawaheshimu sana. Inawezekana wengine wako ndani humu wanasema kwamba hapa hayaji maendeleo, Rais hapeleki maendeleo kwenye Jimbo la Upinzani ndiyo maana sisi tumeishia hapo hapo tu kwa hiyo hili Waziri wa Fedha alitolee ufafanuzi. Aliseme kwamba jambo hili si mkakati wa Rais na ni kwa sababu yako mambo yamefanywa ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano yamefanywa ndani ya Jimbo la Mchinga. Yanapaswa hayo, wanaokwenda huko waseme kwamba pale limefanyika, kituo cha afya milioni 420 zimepelekwa.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bobali taarifa pokea.
T A A R I F A
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka nimpe kaka yangu ambaye ni mstaarabu sana na ninamuheshimu mno lakini nilitaka tu nikupe taarifa kwamba wakati nikiwa CHADEMA nilipata bilioni 52.3 kwa ajili ya lami. Nimepata bilioni 1.8 kwa ajili ya maji, nimepata milioni 250 kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, nimepata milioni 751 kwa ajili ya maji sehemu nyingine na zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya elimu. Kwa hiyo, nikupe tu taarifa kwamba hilo sio suala la Waziri wa Fedha, ni suala lako na watu wanaofanya siasa ndani ya eneo ako. Ahsante sana.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba niendelee. Nimepokea Taarifa yake nadhani ameongezea tu kile nilichokuwa nakisema…
Mheshimiwa Mwenyekiti…
MWENYEKITI: Anamaanisha ni vigumu sana kwa Waziri wa Fedha kuzungumzia hilo jambo. Hajui nani aliyesema, wapi, ilikuwakuwaje sasa yeye atoe statement yaani ataanzia wapi? Lakini endelea tu kutoa mchango.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru, nianze na mradi wa LNG mradi. Mradi wa kufua umeme na nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha ukurasa wa 20. Amezungumzia ni sehemu ya Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatoka Lindi. Lindi kwa sasa nafikiri ndiyo Mkoa maskini zaidi kuliko yote Tanzania kwa mujibu wa taarifa zilizopo. Kipato chetu ni kidogo, hali ya udumavu umekuwa ni mkubwa sana na hata matokeo yetu ya shule yamekuwa mabaya sana, bahati mbaya sana miaka mitano tunaburuza mkia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha inapaswa ifanye affirmative action kwa maeneo kama haya ili kutusaidia ili na sisi vijana wa Lindi wapate ajira kwenye miradi ambayo itakuwa inatekelezwa na Serikali kwenye maeneo yetu na hakuna mradi mkubwa ambao ungetekelezwa ungesaidia sana kama mradi wa LNG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri anasema suala la kufanya tathmini ya malipo ya watu wanaopaswa kuondoka pale limekamilika lakini shida iliyopo ni suala la kimkataba kati ya wawekezaji na Serikali. Wakati nachangia bajeti ya Wizara ya Nishati wakati wa Bajeti nilishauri kitu. Hii mikataba hizi negotiations zimechukua muda mrefu sana. Kama inawezekana kwanini Wizara ya Fedha isitume wataalam kwenda kujifunza kwenye maeneo ya nchi za kiafrika am bapo miradi kama hii inatekelezwa ili i-fast track hiyo negotiation inayofanyika baina ya Serikali na wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sasa mashamba ya watu hayaendelezwi. wananchi wanshindwa kuziendeleza nyumba zao wakisubiri mradi uweze kuja ku- take off lakini mpaka sasa zaidi ya miaka sita au saba mradi haufanyi kazi. Sasa nilikuwa napendekeza Waziri Mheshimiwa Dkt Mpango tunaomba jambo hili mli-fast track kwa sababu kwanza litaleta kodi kubwa kwa Serikali, litatuletea mapato ndani ya nchi lakini pia ni mradi mkubwa wa kielelezo. Leo tukisoma hapa Taarifa ya Mpango, miradi yote ile mikubwa ya kielelezo tunaona inaelekezwa kwenye mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Mikoa ya Kati hakuna mradi mkubwa wa kielelezo unaokwenda kusini zaidi ya huu mradi wa umeme wa Nyerere na ambao utatekelezwa katika nchi yote sio kwamba utakwenda moja kwa moja Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango ni kweli, naona unasikitika. Ukiangalia kitabu hiki, mradi mkubwa ambao unakwenda direct Kusini ni mradi wa LNG pamoja na mradi wa kiwanda cha gesi cha Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sisi ni maskini ndiyo maana nilizungumza kwamba…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bobali, maneno yako haya yana ukweli wowote?
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, yana ukweli.
MWENYEKITI: Haya sema, hebu toa mifano kwamba miradi sijui inaelekea wapi, inaelekea wapi haielekei huko kwenu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia miradi ya kielelezo ambayo imezungumzwa kwenye hotuba.
MWENYEKITI: Si useme mradi fulani na fulani.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mradi wa reli ya kisasa ambao unatumia pesa nyingi, ukiangalia miradi ukifanya calculation…
MWENNYEKITI: Kwa hiyo ukichukulia mradi kwa mfano wa reli ya kati kukata nchi wewe unaona kama ni ubaguzi dhidi ya Kusini?
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana! Nilikuwa naendelea, kwa mfano, kuna mradi umesemwa humu wa reli…
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Samahani kuna taarifa Mheshimiwa Waziri tafadhali.
T A A R I F A
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba tunajenga Bandari Mtwara kwa bilioni 147, tunajenga uwanja wa ndege mpya pale Mtwara, tunajenga barabara ya Mtara – Mivata na karibu tutajenga barabara kutoka pale Mivata kwenda mpaka Masasi kwa zaidi ya kilometa 160. Niliona nikupe taarifa hiyo hayo maneno unayoongea sio kweli.
MWENYEKITI: Ndiyo maana nikakustua kidogo. Unajua kuwa na concept za kama vile kuna ubaguzi baguzi hivi wakati hakuna na haya ni maendeleo ya nchi, maana reli haiwezi kupita angani, lazima ipite mahali fulani. Endelea tu Mheshimiwa.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru. Naomba niendelee na uzuri taarifa niliyopewa imezungumza kabisa ni Mtwara, nami nimesema natoka Lindi na Lindi ni Mkoa masikini katika orodha Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango anajua ni Mkoa wa mwisho kabisa. Mradi mkubwa uliotajwa kwa Lindi ni mradi huu wa LNG ndiyo maana nimeusisitiza. Mwishoni nilikuwa nataka niseme kwamba kuna mradi hata wa reli umetajwa kwenye Mpango kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. Nilikuwa nataka niseme mwishoni, lakini ameniwahi Mheshimiwa Waziri. Sasa labda nikumbushe kwamba upo kwenye Mpango, lakini yote inazungumzia Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukizungumza Mkoa wa Lindi specifically, hakuna mradi mkubwa uliotajwa zaidi ya mradi LNG na ndiyo maana naomba ufanyiwe fast tracking. Naomba sana mradi huu kwa sababu ungegusa direct kabisa maisha ya watu wa Mkoa wa Lindi.
MHE. JOSEPH KASHEKU MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Musukuma nilikuona.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Kiti chako kilinde hizi kauli zinazozungumzwa na mchangiaji. Tukianza kuzungumza watu masikini; moja ya Jimbo masikini ni Jimbo langu la Geita ambalo miaka yote Serikali imekuwa ikikusanya pato kubwa sana kwenye dhahabu inayotoka Geita, lakini ukienda Geita leo hakuna lami hata robo, hatuna maji ya bomba hata theluthi kwenye Jimbo langu. Juzi tu tumemwona Mheshimiwa Rais anazunguka Mkoa wa Lindi akiporomosha maahadi na kufungua miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya maneno anayoyazungumza Mheshimiwa, naomba Kiti chako kimwambie ayaondoe kwa sababu yanatugawa sisi ambao wengine tumechangia mapato makubwa kwenye Taifa hili lakini hatujawahi kuwa na hiyo hata miradi ambayo Mheshimiwa Rais kafungua juzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Serikali ya Awamu ya Tano, Lindi haiwezi kuwa masikini tena kwa ahadi tulizozisikia na ziara iliyofanywa pale; iko ni Mikoa ambayo ni masikini. Sisi Geita ni masikini lakini kwao Mwalongo ni Mkoa wa tatu na hauna dhahabu na hauna kitu chochote. Tukianza kutajana hapa tunajenga chuki na tutaligawa Bunge kwa watu ambao hatujafaidika na hiyo miradi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bobali, labla uliona kidogo nilijaribu kuingia ingia, anachokisema Mheshimiwa ni kitu cha msingi. Sisi ni viongozi wa Kitaifa, kwamba kuchaguliwa kwangu Kongwa kuja hapa au ninyi kwa madirisha mliyoingia nayo, ni namna ya kupatika kwenu. Katika nchi yetu tumeamua kwamba tupatikane kwa taratibu hizi tulizopatikana, wengine Viti Maalum, wengine Jimbo hili, zile categories zetu za kupatikana kwetu.
Tukishafika hapa, sisi ni viongozi wa Kitaifa. Haisadii sana kama kila anayesimama atakuwa anapanda mbegu za kibaguzi kuonesha kwake ni masikini, kwake ni nini; factors za umasikini ni nyingi, hazitokani na Serikali peke yake. Tusingekuwa Bungeni huko, tungekaa nje tungeanza kuambiana. Mimi mwenyewe nimeishi Lindi, ningeweza kukwambia baadhi ya mambo ya umasikini, hili nalo Serikali! Kwani watu wa Kongwa ni tajiri? Ni masikini, na kadhalika.
Kwa hiyo, concepts hizi za kwamba kuna ubaguzi na nini, hizi fikra siyo sahihi. Kama ndiyo mnawahutubia watu wenu namna hiyo, mtazidi kuwachelewesha. Tusonge mbele, twende mbele kama nchi. Wewe jenga hoja yako ya mradi wa LNG, nasi tunaunga mkono wote. Tutapinga kwa sababu gani? LNG ina faida kubwa katika uchumi wa nchi. Sasa LNG utaiweka Kongwa? Si lazima iwekwe Mtwara bwana au Lindi ambako na gesi iko huko huko na kadhalika! (Makofi)
Kwa hiyo, tuisaidie Serikali katika namna ya kuweka mambo vizuri kwenda mbele, lakini hii ya ubaguzi baguzi kila wakati kwamba kuna hiki, kuna kile unless kweli unaona kuna ubaguzi hatukatai, lakini kama haupo haisaidii sana kupanda mbegu za kibaguzi. Inaleta tu sentiments, hata kwa wengine unaona watu wanaanza kuwaza kwamba dhahabu yetu na kadhalika. Kweli raslimali za Taifa siku zote sera yetu ni kwamba zinakuwa katika chungu kimoja, tuna-share wote, hata korosho ile nasi tunapatapata mnyepe mnyepe huko kidogo, na kadhalika.
Mheshimiwa Bobali, endelea tu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima yako nimeamua niifute kabisa ile, naona iondolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia jambo la pili ambalo ni Sekta ya Uvuvi. Tuna eneo kubwa la bahari ambalo kama wavuvi wangekuwa wanawezeshwa na ni Mheshimiwa Ghasia amezungumzia hapa, tungeweza kuongeza kipato cha wananchi kwa kutumia Sekta hii ya Uvuvi. Niseme, wakati Waziri wa Uvuvi akiwa Mheshimiwa Dkt. Magufuli ambaye sasa hivi ni Rais wa nchi, wavuvi waliwezeshwa kwa kupewa boti, mashine na vifaa; vyavu za kuvulia. Ulikuwa ni mpango madhubuti wa kuwawezesha wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nahoji leo, ule mpango uko wapi sasa hivi? Watu walihamasishwa waache kutumia uvuvi wa mabomu; na kwa kiwango kikubwa kabisa watu wameacha sasa hivi utumiaji wa mabomu, umekufa kabisa, haupo. Bahati mbaya sasa mabomu hayatumiki, lakini leo ukienda kijijini kule huli samaki, kwa sababu hawana alternative. Nyavu tunajua namna ilivyo. Nyavu ambazo wanaweza kuzinunua na kuzifikia ni hizi za bei ya chini ambazo nyingi zimekatazwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mpango hebu tengenezeni mfumo maalum wa kusaidia wavuvi; na siyo wavuvi wa ukanda wa bahari tu, hata wavuvi waliopo kwenye maeneo ya mito, ziwa na wenyewe pia. Kwa mfano, kwenye Sekta ya Kilimo kuna Taasisi nyingi sana zinazosaidia kilimo, ukianza kuzihesabu hapa, zaidi ya tano, sita, zote zina-deal na wakulima; lakini kwenye uvuvi huoni hizo Taasisi ambazo zimeanzishwa na Serikali. Zinasaidia moja kwa moja wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiulizia hizi boti ambazo zimepewa ruzuku ya Serikali tunazipataje? Ukimwuliza hapa ndugu yangu Mheshimiwa Ulega atakwambia fuata utaratibu huu, mimi nilishawahi kuzungumza nao, utaratibu wake ni mrefu mno, mlolongo wake ambao kwa mwananchi wa kawaida, aliyeko Mchinga, Ruvu, Lushungi na kwingineko hawezi kufikia; na tumejaribu mara kadhaa, imeshindikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kwenye Sekta ya Uvuvi kiwekwe kitengo maalum ambacho kitakuwa kinasaidia wavuvi hata kwa kutoa subsidiaries kwa wavuvi ambao watakuwa wanataka kununua aidha boti, ama injini za boti ama nyavu zile kubwa za kuvua baharini. Vinginevyo samaki wapo baharini kule, wamebakia wengi, watakuja wavuvi kutoka nje na meli zao, watapata vibali, watakwenda kuwavua, wataondoka. Sisi hapa hatutakula samaki wazuri kwa sababu wavuvi wetu hawana capacity ya kuweza kuvua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilitaka nilichangie ni suala la fedha za TARURA. Miradi ya maendeleo ya TARURA na Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia hapa, kwamba kweli inapatikana asilimia 30 ni ndogo; na kwa bahati mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI na Utawala ya Bunge ambayo inasimamia hiyo TARURA. Shida kubwa, ukikutana na watu wa TARURA, ni kwamba siyo kutengwa tu ile asilimia 30, shida nyingine ni kwamba hiyo asilimia 30 yenyewe haipelekwi. Yaani utakuta barabara imetengewa shilingi milioni 100 au milioni 150 ambayo inapaswa ipelekwe, lakini mpaka mwaka wa fedha unamalizika, fedha ile haikupelekwa, labda imepelekwa asilimia 40 au asilimia 50. Kwa hiyo, jambo hili na lenyewe ni la muhimu sana. Ufuta, korosho, zabibu na vitu vingine vinalimwa huko vijiji ambako vinahitaji usafiri wa uhakika. Sasa kama TARURA ingekuwa inawezeshwa, yule sungura mdogo wa asilimia 30 ambaye amepangiwa kwa mujibu wa sheria, wangekuwa wanapata kwa uhakika. Nadhani barabara nyingi za vijijini zingekuwa zimetatuliwa ile changamo ambazo zipo kwa sasa hivi ambayo nyingi hazipitiki zingekuwa zimeweza kuondolewa changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)