Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Bhagwanji Maganlal Meisuria

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chwaka

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja hii ya Serikali inayohusu Mpango. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Kamati yake, lakini sana Mheshimiwa Rais wa Muungano pamoja na Rais wa Zanzibar, wamejitahidi kwa kuleta maendeleo katika Taifa letu. Mungu awasaidie na sisi Waheshimiwa Wabunge, Mawaziri pamoja na wananchi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekitik, katika Mpango huu nitazungumzia mambo yetu ya uwanja wa ndege. Terminal three imejengwa kwa awamu ya Mheshimiwa Rais, ni mpya kabisa. Mungu akipenda, kesho kutwa naondoka kwa ndege yetu ya Tanzania. Naomba Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Dkt. Mpango ziongezwe ndege nyingi katika nchi yetu, kwa sababu sisi hatushindwi, tunakwenda mbele na hiyo mbele, ndiyo kazi yetu. Hapa ni Kazi Tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ndege inatoka Dar es Salaam moja kwa moja inakwenda India. Sasa wafanyabiashara, wagonjwa na wengine wanataka kitu kama hicho, nami nimekata tiketi, basi ndege zote ziko full kwenda na kurudi. Tutapata utalii na mambo mbalimbali. Naomba Serikali yetu ya Muungano ndege ndogo ndogo ziongezwe kwa sababu mpaka Zanzibar tunahitaji ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Zanzibar tuboreshe katika uwanja wetu wandege kwa sababu watalii wengi wanakuja kama Bara. Tutafaidika na mambo mbalimbali tutafaidika. Tukiondoka hapa bandari yetu; Mheshimiwa Rais katika awamu yake, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu. Kuhusu bandari tumekubaliana ndani ya Kamati na inafanyiwa kazi. Tunakwenda mbele. Bandari yetu sasa hivi tunapanua, ili hata zikija meli kubwa ziweze kwenza mbili kwa pamoja. Tunatakiwa katika bandari yetu tuongeze mapato kutokana na makontena na mambo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Rais, kwa uwezo wa Mungu, sisi wote ni ndugu moja, ni Muungano; kwa hiyo hata Bandari ya Zanzibar, kule Mpigaduri tuwasaidie. Kwa sababu tulikuwa nyuma, sasa hivi tuko mbele. Zamani haikuwa namna hiyo, sasa hivi imekuwa. Kontena nyingi zinaletwa na biashara nyingi zinaletwa mpaka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Zanzibar anajitahidi katika mambo mbalimbali ya barabara, bandari, maji na umeme. Vile vile nampongeza Rais wa Muungano kwamba bandari yetu itaboreshwa. Siyo bandari hiyo tu, bandari ya Tanga na Mtwara. Nilikwenda katika Bandari ya Mtwara kutembelea, nimeona maendeleo yake. Bandari ya Mtwara siyo kama zamani, sasa hivi bandari ni kubwa, imepanuka na yataletwa mambo mbalimbali, kontena zote zitafika kule na kusafirisha korosho na mambo mengine.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maendeleo yetu vilevile, katika mipango ya reli pamoja na barabara (Standard Gauge), katika Kamati yangu nimeona, nimetembelea na karibu tutafika Dodoma. Standard Gauge hii, siyo Dodoma tu, tufike katika mipaka ya wenzetu; Mwanza na kwingine mpaka iende Zambia mpaka iende Burundi. Kwa hiyo, Standard Gauge inatakiwa iende katika mipaka ya nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe barabara vilevile, kwa sababu tunaongeza mapato vilevile. Standard Gauge zitapakia hizi kontena pamoja na barabara kwa biashara mbalimbali za kilimo, watasafirisha nchi za nje nasi tutafaidika. Naomba Mheshimiwa Rais aendelee mbele na anaendelea mbele kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kilimo. Sasa hivi haturudi nyuma, tunakwenda mbele; tunazalisha pamba, alizeti, tumbaku pamoja na korosho na mambo mengine. Zanzibar tunazalisha karafuu. Kwa hiyo, tunataka hizi pamba na mazao mengine tunao uwezo wa kusafirisha India, China pamoja na hizi mazao mengine na kupata mapato katika nchi yetu na kuondosha umasikini wetu. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri, tumsaidie na tumpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaondoka hapo, tunakuja katika viwanda. Viwanda ni lazima visaidiwe. Mheshimiwa Rais wetu tumpe nguvu; viwanda vya Serikali na viwanda vya watu binafsi, kwa mfano, kiwanda chetu cha sukari, alizeti pamoja na korosho, tufanye hapa tuboreshe. Maana yake, viwanda hivi ni uhai wa uchumi wa nchi yetu na uhai wa uchumi wa Taifa letu. Kiwanda cha Sukari vilevile sisi tunao uwezo. Tukisimamia, nashukuru Mawaziri wanasimamia viwanda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango viwanda vyetu ni lazima tusimamie kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende katika elimu na hospitali. Elimu yetu inatakiwa kuboreshwa zaidi. Watoto wa leo wakisoma, kesho wanakuwa Mawaziri, Rais na elimu yetu inasongea mbele. Kwa sababu elimu inatoa faida nyingi sana kwa watoto. Kama umewakosa kusomesha watoto, namshukuru Mheshimiwa Rais, elimu yetu katika Skuli zote za Sekondari pamoja na Skuli ndogo zote wanafanya vizuri sana, wanaboresha halafu hata katika mitihani anasimamia Mheshimiwa Waziri na Serikali, watafaulu na watakwenda mpaka nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali, nashukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali ilikuwa zamani hakuna kitu. Leo sasa hivi katika zetu, Zanzibar na Bara kila kitu Kituo cha Afya, yaani kote na madawa yanapatikana. Kituo cha Wilaya vilevile na Mkoa, namshukuru Mheshimiwa Rais, tuko mbele. Hakuna mtu hapa katika Tanzania yetu… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina lake nani?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Bhagwanji. Nilikuwa nimekuongezea muda kwa sababu unatelemka leo vizuri sana. (Makofi)

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anaitwa John Joseph Magufuli…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Bhagwanji.

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay naunga mkono hoja hii. (Makofi/Makofi)