Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja iliyopo, hoja ya Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Kwanza niwashukuru sana vingozi wote wa Wizara ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuleta mpango huu wa kujivunia, Mpango ambao unasomeka na kueleweka vizuri, lakini Mpango ambao umebeba matakwa yetu Wabunge kama ambavyo tulipendekeza kwenye pendekezo la awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango umegusa maeneo mbalimbali na miradi ya kimkakati. Miradi ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa mradi wa umeme, mradi wa Mwalimu Julius Nyerere huko Rufiji utakaozalisha umeme wa megawati 2015. Pia ufufuzi wa ndege za Shirika la Ndege, ununuzi wa ndege mpya, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ambao limepitia kwetu likitokea Uganda na vilevile kuendelea na kutoa elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo pia ujenzi wa barabara na miradi ambayo imekusudiwa kumaliziwa katika mpango huu. Sisi Tabora tunajivunia Mradi wanaomalizia sasa wa Maji ya Ziwa Victoria, maji yanayochukuliwa kutoka Ziwa Victoria kuja Tabora imekuwa jambo kubwa sana kwetu na ningependa sana kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mpango huu umelenga kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi yetu na kuwa kinara katika Afrika Mashariki na kwa kweli katika Afrika kwa kukuza uchumi wa asilimia 7.1, jambo hili sio rahisi na lilikuwa kama njozi tulipolifikiria hapo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imefanya mengi katika mpango huu uwezo wa kiuchumi na mimi nasema anayemulika nyoka anaanza miguuni mwake, sisi tumeguswa sana katika ukuzaji wa uchumi katika jimbo letu. Jimbo la Tabora Kaskazini limepata moja ya vituo vya afya na pia tumepata hospitali ya wilaya, vilevile hivi karibuni naipongezza Serikali kwa kunipa Chuo cha VETA na hili ni muhimu sana kwetu sisi kwa sababu jimboni kwangu kuna shule za sekondari nyingi na kuna shule za msingi nyingi lakini kuna high school moja tu ya Ndono, kwa hiyo vijana hawa watakaosoma VETA watatusaidia sana kukuza uchumi katika maeneo ya vijijini ambako ningependa pia kuipongeza Serikali kuleta mpango wa umeme wa REA. Umeme wa REA, ambao utakuza uchumi katika vijiji vyetu na wale vijana ambao tutawaandaa katika vituo vya VETA wanaweza kusaidia kukuza uchumi vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 16 naipongeza Serikali kupanga kipaumbele cha hela za maendeleo na hela zimepangwa katika miradi ambayo itakuza uchumi. Katika ukurasa huu wameelezea vizuri sana jinsi ambavyo hela zitapelekwa kwenye miradi ya kimkakati kama reli, barabara, viwanja vya ndege na hivi karibuni tumemalizia terminal III. Naipongeza Serikali kwa sababu katika mradi huo walifikiriwa pia makandarasi wa nchini hapa, naomba ku-declare interest kwamba nilikuwa mmoja wa makandarasi waliojenga terminal III Kiwanja cha Ndege Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii inatoa ajira kwa wananchi Watanzania vilevile inaweka miundombinu ambayo itadumu pia inakuwa chanzo cha mapato ya Serikali. Kumekuwa na maneno kuhusu ilipotolewa taarifa kwamba kwa kipindi fulani Shirika la Ndege uwekezaji mkubwa ule tulipata bilioni chache, lakini napenda kusema kwamba aliyetoa maneno hayo kwamba ndege imeingiza hela kidogo hakuwa na uga mpana wa busara yake kwa sababu ndege inafikiriwa yenyewe, sisi tulipokuwa tunawekeza kwenye ndege ilikuwa na maana ya ndege iwe chanzo cha mapato mengine. Kwa mfano kuleta watalii, kubeba mizigo vilevile kuonyesha kwamba sisi Tanzania tuna uwezo, wanasema watu the bigger the castle the stronger the can, kuonekana kwamba tuna ndege zetu pia thamani yake ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali katika Mpango huu imeelezea kuendelea kujenga na kumalizia hospitali za wilaya na vituo vya afya. Pia ukurasa wa 74, Mpango huu umeeleza jinsi ya kushirikisha sekta binafsi na hapo ndipo nami na-declare interest kwamba mimi pia ni mwajiri na katika Mpango huu Serikali imesema itawahusisha sekta binafsi katika kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba jambo kubwa linalotusumbua Mheshimiwa Waziri afikirie jinsi ya kurahisisha ufanyaji wa kazi yaani easy of doing business. Hii itatusaidia sana sisi waajiri wa Tanzania, tunalo tatizo kubwa la SDL kwamba kila mwajiri anamlipia kila mfanyakazi kiwango cha asilimia 4.5 cha mshahara wake kama tozo ya ujuzi na hii inatusumbua sana kwa sababu ni moja ya mambo yanayofanya sisi Tanzania tusiwe na ile fursa ya easy of doing business na kila mwaka tunaporomoka, kwa hiyo hatuwezi kushindanishwa katika ajira za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunaomba sisi waajiri kwamba ni bora SDL hii, tozo hii ya ujuzi ipunguzwe kutoka asilimia 4.5 ikaribie asilimia 2.0 na hii itatusaidia sisi kupata kazi katika maeneo mengine, lakini ni vigumu kupeleka wafanyakazi wako kutoka hapa kwenda kufanya kazi Uganda au kufanya kazi Kenya kwa sababu wage bill yako itakuwa kubwa kuliko wenzetu kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumelilalamikia sisi waajiri ni Worker’s Compensation Fund. Tungependa tozo hii ya malipo ya mfanyakazi kuumia kazini ikadiriwe au ifikiriwe kutoka na uwezo wa shirika au mwajiri kwa mfano kama mwajiri anafanya kazi za hatari na likely hood uwezekano wa mfanyakazi kuathirika atozwe tozo kubwa kwa sababu ya kuweka akiba baadaye. Pia kuna kazi za salama kabisa na hazina tatizo na kwa kweli historia ya kazi hizo haijapata kuleta matatizo kwa wafanyakazi wake, kwa nini atozwe sawasawa tozo ya worker’s compensation. Wakati Mfuko huu umeanzishwa kulikuwa na utafiti unaofanywa ili kuweza kugawa madaraja ya Worker’s Compensation Fund, tozo ile ya asilimia 1.0 mpaka asilimia 2.0 kutegemea shughuli na utendaji wa mwajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mpango huu umeendelea kufikiria kukuza kuendelea kulipia shule bure, elimu bure ya msingi yaani darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hili ni jambo muhimu, lilipoanzishwa lilionekana kama haliwezekani, lakini Mpango huu unathibitisha kwamba jambo hili litaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia hayo tu. Ahsante sana. (Makofi)