Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu pamoja na watendaji wote katika Wizara hii ya Fedha kwa kuandaa muelekeo huu ambao ndio dira ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka unaokuja wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyopitia hotuba ya Waziri cha kwanza naomba nianze kugusia changamoto ambazo ameweza kuzielezea, lakini pia niipongeze Serikali kwa kuweza kukusanya mapato haya ya ndani kwa wastani wa asilimia 88.7 ambapo ni muelekeo mzuri sana katika utekelezaji wa bajeti. Ni kweli kabisa moja ya changamoto ambayo Waziri alieleza ni kuhusiana na tozo katika sekta isiyo rasmi imechangia kiasi kiasi fulani kwenye kushusha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tumeiona pia hata katika halmashauri zetu kwamba, kile kiwango ambacho ni fixed wanacholipa ukikilinganisha kwa siku ni kidogo tofauti na hela ambayo imezoeleka. Kwa hiyo, nitoe ushauri kwamba, Serikali ijaribu kuangalia namna bora ambayo itaenda kutumika katika kutoza sekta isiyo rasmi kwa sababu wanatofautiana madaraja kutokana na biashara wanazofanya na faida ambazo wanapata. Kwa hiyo, kuweka rate moja kwa watu wote hii nafikiri tuibadilishe tuangalie aina ya biashara na tuwe na rate tofauti tofauti angalau sasa hii itatusogeza pale ambapo tulikuwepo kuliko tunashuka chini. Niipongeze Serikali kwa kurasimisha bandari bubu, kama ilivyoelezwa na pia kuendelea kudhibiti uvujaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mwelekeo wa huu mpango umezungumzia masuala ya bajeti ambapo ni mapato na matumizi. Kwenye matumizi to matumizi ya maendeleo na ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze na suala la mapato yanayotokana na kodi, tumeona kwamba, Serikali iendelee kudhibiti hasa kwenye ukusanyaji wa kodi upande wa import tax ambapo bado kwa mfano juzijuzi tumeona kwamba, wizi wa bomba la mafuta kwenda kwenye ma-tank unafanyika. Sasa kama hiyo tu wananchi humu mtaani wanafanya wizi kama huo maana yake ni nini? Hiyo hata maeneo mengine Serikali itakuwa bado inaibiwa kwa hiyo, tuisihi sana Serikali iendelee kudhibiti. Na hicho tutaweza kufikia malengo ya mapato yetu ambayo yanatokana na kodi, lakini vilevile tuendelee kutanua tax base, ili tuweze kuongeza wigo huu ambao utasaidia kuongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi nyingine ambazo zinakusanywa na TRA kwa mfano Property Tax. Nikiangalia bado hatukusanyi vile inavyopaswa kwa sababu, tukichukua takwimu za nyumba zote ambazo ziko nchi nzima tulinganishe na mapato ambayo yamekusanywa lazima utaona uwiano hauendani. Niiombe TRA kwa sababu tuna watendaji wa kata, tuna watendaji wa mitaa, hebu tuwatumie katika kupata takwimu na kusaidia kufuatilia ukusanyaji wa mapato angalau kwa-commission ambayo itawa-motivate kuweza kukusanya sehemu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja sambamba na hilo kuna kodi la zuwio kwa wapangaji, withholding Tax on the Rent. Kwa mfano inawezekana hata humu Wabunge wapo ambao wamepangisha watu nyumba, lakini uliza ni nani ambaye amelipa Withholding Tax, hakuna. Kwa hiyo, wengi zaidi wanaolipa ni wa Kariakoo na maeneo ya mijini ambako tu official ndio wanalipa Withholding Tax, lakini huku mitaani hii haikusanywi vile inavyopaswa. Kwa hiyo, niombe tutumie pia watendaji wetu wa mitaa, wa vijiji, wa kata katika kuchukua takwimu ni nyumba ngapi zinapangishwa, zina wapangaji, ili wakati mtu analipa kodi basi tuweze kukata hiyo kodi ya zuwio na TRA iweze kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mapato ambayo hayatokani na kodi. Katika makisio ya mapato haya mwaka wa fedha 2019/2020 makisio yalikuwa ni trilioni tatu bilioni 178 milioni 922. Lakini kilichonishangaza makisio kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa mapato yasiyotokana na kodi yanayokusanywa na mashirika, taasisi na Wizara makisio yametoka kutoka hii trilioni 3.1 kwenda trilioni 2.7; sasa nitaomba waziri atueleze tunajua sawa hatujafikia malengo kamili, lakini kwa nini makisio haya yameshuka wakati Bunge na Serikali tunaendelea kuhimiza kwenye taasisi na mashirika ya Serikali kuendelea kutoa magawio kwa mujibu wa sheria ambayo TR ndizo ambazo anasimamia? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tutaomba uangalie hili na uweze kutupa mrejesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine pia katika kuboresha mapato haya tukiangalia kuna tozo mbalimbali za Serikali nyingine hazijabadilika zina miaka zaidi ya 10 nyingine ni zaidi ya miaka 20. Sasa ni wakati muafaka wa Serikali ku-review hizi rates sambamba na kutengeneza takwimu. Kwa mfano tu tozo ya mtu ambaye anaenda kuchukua Loss Report Police unalipa shilingi 500, hii 500 ina miaka mingapi ipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuangalia, lakini tunajua sambamba Sera ya Mapato ya Ndani inazungumzia suala la kuhuisha na kupunguza tozo na ada, lakini kuna wakati lazima tuangalie kuna nyingine tunashusha, lakini nyingine tuangalie namna bora ya kuweza kuzipandisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye Sera ya Mapato ya ndani; cha kwanza Mheshimiwa Waziri ameeleza ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara, hii ni kusema iende sambamba na uwekezaji. Kwa hiyo, niiombe Serikali iendelee kuhimiza watendaji ndani ya Serikali waendelee kufanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu, ili wafanyabiashara waendelee kufanya biashara kama ipasavyo, kuwa na kauli nzuri pamoja na malengo mahususi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo kuna suala la miradi ya kimkakati. Tuliweza kuboresha sheria ya ubia kati ya sekta za umma pamoja na sekta binafsi – PPP. Hebu Serikali iajaribu kuangalia kutengeneza mfumo mzuri ili twende kwenye PPP baadhi ya miradi na hapo tutaipunguzia mzigo Serikali kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kenye nishati ya gesi asilia kuna mikataba ile ya uwekezaji kwenye gesi imeshatengenezwa modal ambayo ndio inatumika mtu akitaka kuwekeza kwenye gesi asilia (PSA – Production Sharing Agreement). Kwa nini na huku kwenye PPP tusitengeneze modal ambayo itakuwa ina-guide katika kuingia hiyo mikataba ambapo itasababisha sasa watu kutokuingia mikataba ambayo itakuwa ni mibovu na haitanufaisha Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lile suala ambalo Mheshimiwa Rais anahimiza suala la win-win situation tulitengenezee modal ambayo itakuwa ni guidance ambayo itatuongoza kuingia kwenye PPP. Kwa mfano hapa umekusanya asilimia 88 tumekosa asilimia kama 12. Je, hii 12 tungekuwa kwenye PPP maana yake ingeenda kusaida katika hiyo miradi ya kimkakati kwa mfano, kuna hii Liganga na Mchuchuma ambayo tunajua kwamba, ni mradi ambao utanyanyua viwanda vingi sana hapa Tanzania na ujenzi wa reli kutoka Mtwara mpaka huko Ruvuma. Sasa tupitie na tuwe engaged tusiogope, utawala bora umeboreshwa, tumeamka, tumejua kuangalia namna bora ya mikataba mbalimbali ambayo Serikali inaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na suala la kilimo. Kilimo kinachangia asilimia 28 kwenye pato la Taifa, lakini bado tija yake ni ndogo. Tumezalisha tani milioni 16.8 lakini ukiangalia ule wastani kwa hekta uzalishaji bado uko chini sana. Kwanini iko hivyo, hatuna mbegu bora, pembejeo bado ni hafifu, jembe la mkono linaendelea kutumika, tulikuwa na kauli mbiu ya kilimo kwanza, sasa tukiongeza uzalishaji maana yake na Serikali itaongeza mapato kwa sababu, uzalishaji wenye tija ni huu wa kuwa kwamba, unakuwa na yield nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo kuna uvuvi wa bahari kuu. Na wewe umewahi kuwa kwenye kamati ukaandaa ripoti Serikali namna gani itaongeza mapato; tuna Ripoti ile ya Chenge I na Chenge II, angalau tufikie zaidi ya trilioni 1.7 sasa hebu Serikali ijikite kwenye uvuvi wa bahari kuu. Ni kwamba, hawa samaki tunaachia nchi nyingine ndio wanawavuna, wanauza, sisi tunakosa mapato; nimeona kwamba, Serikali imefanya upembuzi yakinifu kwenye ujenzi wa bandari ya uvuvi, lakini sasa tuongeze kasi katika utekelezaji wa mradi huu ambayo itakuwa imewaongezea ma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Asante sana Mheshimiwa Richard Mbogo kwa mchango wako mzuri.