Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hoja kwanza hii ya kutotekeleza bajeti ya miradi ya maendeleo. Ni kwa muda mrefu sasa Serikali imekuwa haitekelezi ipasavyo bajeti ya miradi ya maendeleo kama ambavyo tunaidhinisha hapa Bungeni. Kama Wabunge tutakuja hapa Bungeni, tutapitisha bajeti, tutapitisha Mipango ya Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka Mmoja au Miaka Mitano, halafu ile bajeti kama haiwezi kutekelezwa, maana yake mwisho wa siku ni kuendelea kumpigia mbuzi gitaa ambapo kwa namna yoyote ile hawezi kucheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano mdogo. Kwa mfano, bajeti ya kilimo ya mwaka 2017/2018, fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa au zilizoidhinishwa hapa Bungeni, ni shilingi bilioni 150.253 lakini zilizotolewa ni shilingi bilioni 16.5 sawa na asilimia 11 tu. Kutekeleza bajeti kwa asilimia 11 hii kwa kweli siyo sahihi na hatuwatendei haki Watanzania kabisa. Kwa hiyo, ukienda mwaka mwingine 2018/2019 tulitenga shilingi bilioni 98.119 lakini fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 41.22 ambapo ni sawa na asilimia 42. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 fedha za maendeleo zilizoidhinishwa hapa Bungeni na Bunge hili Tukufu ni shilingi bilioni 100.527, lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 2.25 sawa na asilimia 2.2. Kwa kweli miaka yote mitatu hii niliyotoa mifano kwenye kilimo hatujawahi kufikisha asilimia 50. Sasa sijui tunafanya nini!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama hatuwezi kuweka kilimo kama ndiyo kipaumbele namba moja ambapo tunajua wote kwamba ndiko Watanzania wengi wamejiajiri, zaidi ya asilimia 70, tunajua kabisa huko ndiko ambako hata pato la Taifa mchango ni mkubwa, lakini inaonekana kilimo siyo kipaumbele tena katika Taifa hili. Bajeti zenyewe ndiyo hizo tunatenga, lakini pesa za maendeleo hazipelekwi. Kwa kweli jambo hili linasikitisha sana na hatuwatendei haki Watanzania ambao kwa kweli wengi wapo katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunafahamu wote kwamba Watumishi wa Umma kwa muda mrefu sasa hawajaongezwa mishahara. Serikali ya Awamu ya Tano haijawahi kupandisha mshahara kwa Watumishi wa Umma. Mheshimiwa Dkt. Mpango anafahamu unapozungumzia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, watekelezaji wa Mpango huu ni Watumishi wa Umma. Kwa mfano, unapozungumza leo watu wanaofanya kazi TARURA, au wanaofanya kazi TANROADs au wanaofanya kazi ya kufundisha Walimu au TRA na kwingineko, hawa watu ndiyo wataenda kuteleleza Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wamekata tamaa, kwa sababu gharama za maisha zinazidi kuongezeka, hawajawahi kuongezwa mshahara hata shilingi 100/=, hali ni mbaya, halafu tunataka wakatekeleze Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Hili jambo Serikali lazima itafakari vizuri. Haiwezekani! Kuna muda fulani kiongozi anasema kwamba kupanga ni kuchagua, tumeamua kuanza na SGR, tumeamua kuanza sijui na kununua ndege na vitu vingine, sasa hivi vitu hata wewe kwenye nyumba yako, unapojenga nyumba, huwezi ukaacha kuwanunulia watoto chakula eti kwa sababu unajenga, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi wa Umma wamekata tamaa na hawa ndio watekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Sasa hawa wameshakata tamaa, mwisho wa siku tutakachopanga hapa Bungeni hakitatekelezeka kwa sababu watu wamekata tamaa na hili jambo Serikali lazima ijitafakari vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Awamu ya Tano, ndiyo muda sasa, bado mwaka mmoja. Sasa sijui hili jambo Serikali inaonaje, lakini kwa kweli jambo hili lazima atakapokuja ku- wind up Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie Serikali inafikiria nini kuhusu Watumishi wa Umma ambao hawajapandishwa mishahara kwa muda mrefu na ndio watekelezaji wa Mpango? Kwa kweli wanachozungumza kitu kibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu au Watumishi wengine wa Umma wana maandamano au mgomo wa chini chini. Huu mgomo hawawezi kusema hadharani. Siyo rahisi, hawawezi kusema hadharani, lakini mwisho wa siku matokeo yake tunaweza tukayaona miaka inayokuja huko baadaye ambayo siyo mazuri hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimejaribu kuangalia, ni kweli kupanga ni kuchagua, siyo jambo baya. Alipokuja Mheshimiwa Rais Mkoa wa Songwe, alikuja pale kwangu Mbozi, ameenda pale Jimbo la Vwawa, ameenda Tunduma, ameenda Momba, kote alikopita kero namba moja ilikuwa ni maji; kero ilikuwa ni barabara pamoja na mambo mengine. Wananchi wale hamna hata mmoja aliyesema Mheshimiwa Rais sisi tunafurahishwa sana na ununuzi wa ndege. Hamna aliyesema tunafurahishwa sana na ununuzi wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za wananchi ni maji na ndiyo kipaumbele namba moja ambacho ukienda huko kwa wananchi wanalia. Hata wewe mwenye ni Mbunge, ukienda kule kwako, wananchi wanalia na maji; wanauliza kuhusu Vituo vya Afya, kuhusu Zahanati, kuhusu barabara. Sasa Serikali inaweza ikawa imeamua yenyewe kufanya kitu ambacho hawajafanya tathmini vizuri kwamba je, ndiyo mahitaji halisi ya wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri jambo moja. Nimeona kwenye Mpango hapa, nimesoma, Serikali inasema kwamba imenunua ndege nane na ndege nyingine kabla ya mwaka kwisha...

MHE. RICHARD P. MBOGO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, hebu sikiliza taarifa. Mheshimiwa Richard Mbogo.

T A A R I F A

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Haonga. Ununuzi wa ndege ni moja ya mikakati ya kuweza kuongeza mapato ambayo yataenda kutekeleza miradi mbalimbali ya huduma za jamii ikiwepo maji ambayo ameyasema. Katika Mpango huu, maji yametengewa shilingi bilioni 686 ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali na Halmashauri yake inapokea zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya miradi ya maji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, unasemaje kuhusiana na taarifa hiyo?

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Taarifa yake naona siyo msaada kwenye ninachotaka kuzungumza. Kwa hiyo, sijaipokea kwa sababu hajui hata Halmashauri yangu napokea shilingi ngapi, anabumbabumba maneno tu. Ni vizuri akafanya utafiti kabla ya kuzungumza. Namheshimu sana, lakini ajaribu kuangalia namna tunavyopoteza muda Watanzania. Huu muda siyo wa Haonga, ni muda wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani hapa niseme tu kwamba ni kweli Serikali imesema inataka kununua ndege 11 na imetumia zaidi ya shilingi bilioni 700 na kitu. Kwa hiyo, maana yake ndege 11 zitakapokuja, kwa taarifa ni kwamba itakuwa ni zaidi ya trilioni moja na kitu. Hizi fedha zingeweza kupelekwa kwenye miradi ya maji, kwenye miundombinu ya barabara au kwenye vitu vyote vinavyowagusa wananchi, tungekuwa mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, kwa mfano, kwenye Jimbo langu, hata wananchi wa Mkoa wa Songwe wanafahamu, wananchi wa Rukwa wanafahamu, wananchi wa Mkoa wa Katavi wanafahamu…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka pale Mbozi eneo linaitwa Mloo, Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe, kuna barabara kutoka pale kwenda Kamsamba inayoenda…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: …Rukwa hadi kwenda Kibaoni. Hii barabara Serikali iliahidi kwamba ingeweza kuItengeneza kwa kiwango cha lami. Sasa daraja wanasema imeKwisha lakini ile barabara haijatengenezwa kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, tunaamini fedha nyingi zingekuwa zinapelekwa kwenye maeneo kama haya, lile eneo ni eneo la mkakati.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa rafiki yangu Mheshimiwa Haong kwamba tunavyoongea sasa hivi tunatoka naye kwenye kikao kule Ashera, tumeitwa na Wizara ya Kilimo kusikia maoni ya wadau mbalimbali. Yeye mwenyewe kwa kinywa chake amemshauri Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Serikali inunue ndege ya mizigo (cargo) kwa ajili ya kusafirisha mazao ya horticulture. Sasa namshangaa anafika hapa tena, anageuka. (Makofi)

Mheshimiwa Haonga, si tulikuwa na wewe pale, umesahau tena!

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Haonga.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wote duniani wanaoyumba kwanza kwa mitazamo ya vyama, wanahamahama hawawezi kuwa na akili sawasawa.

MWENYEKITI: Hapana.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu tumsamehe tu, tumeshamsamehe, hajui alitendalo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Haonga, nakusihi sana, tutumie lugha ya kibunge. Huyu ni Mbunge kama wewe, amechaguliwa na wananchi wa Tanzania kwa eneo lake. Wewe sema tu, unaikubali taarifa hiyo au unaikataa?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikataa taarifa yake na asiwe anahama hama vyama, maana yake Watanzania hawatamwamini tena.

MWENYEKITI: Haya endelea kuchangia.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MBUNGE FULANI: Kigeugeu! (KIcheko)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii barabara ya kutoka Mloo, Mbozi pale, Mkoa wa Songwe kwenda Kamsamba, nadhani wewe unaifahamu hii, kwenda Kamsamba, kwenda Kinyamatundu kule Rukwa kwenda Kibaoni, Katavi, hii barabara…

MWENYEKITI: Sawa, lakini daraja je? Sema na daraja basi.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumzia barabara, kama wewe umeliona daraja, nakushukuru, mimi nazungumzia barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni muhimu sana ambapo kule wanalima ufuta, mpunga, kahawa, mahindi, maharage, alizeti na wanalima mazao mengi sana. Barabara hii ingeweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami uchumi wa Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi ungeweza kupaa. Sasa leo barabara hii imeachwa, tunafanya vitu vingine ambavyo kwa kweli kwa Watanzania wala siyo kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani hii barabara ni vizuri Waziri Mpango utu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako. Ahsante sana, lakini na daraja ni muhimu sana na ndiyo maana Serikali imeona ianze na daraja hilo na baadaye ina mpango wa lami, utafika tu.

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia ambacho hakipo. Huwezi ukazungumzia kitu ambacho kipo.

MWENYEKITI: Ahsante sana.