Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye Mpamgo wa Taifa wa mwaka 2020/2021. Kwanza naomba nimpongeze Waziri wa Fedha kwa kuja na mpango mzuri, leo nitatoa ushauri kwa badhi ya mambo. Nimeusoma mpango wetu, nashauri sasa nadhani umefika wakati kwenye mpango ningetamani tuoneshe mwaka kesho baada ya mwaka mmoja kama ambavyo tumesema tutajenga barabara, tunajenga madaraja, lakini nataka tuoneshe production, kwa sababu ili tuweze kupata fedha nyingi tuweze kuendelea cha kwanza lazima tuhakikishe production yetu kwenye mpango wetu ionekane na hapa nitatoa mfano kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunakaa hapa tunapitisha Bajeti ya Kilimo, nadhani umefika wakati kwenye mpango basi tuseme kwa mfano kwenye kahawa; kwenye kahawa tunataka tuafanye kazi ili mwaka kesho tutoke kwenye tani 50,000 twende kwenye tani 200,000, lakini hili kwenye mipango yote haionekani na ndiyo maana kwa miaka yote minne kahawa haijawahi kuzidi tani 60,000, lakini wenzetu Uganda ni tani 2,88,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende kwenye chai; tunazalisha chai tani 19,000, tani 20,000 au 25,000; wenzetu Kenya hapa ambao sisi tuna ardhi zaidi, wanazalisha tani 350,000. Sasa lazima na sisi tunapokuwa tunapanga, tupange kwa kuweka matarajio, haiwezekani tunajadili tu kilimo, lakini tuweke deliverables ili tuweze kuwapima hawa wenzetu. Tukifanya vizuri kwenye kilimo nina hakika tutapata export nyingi, tutapata fedha za kigeni na kwa sababu hiyo balance of payment itaondoka kwenye negative. Tanzania kama nchi katika vitu ambavyo ni advantage kwetu cha kwanza tuna ardhi kubwa sana, Tanzania tuna maji mengi sana, Tanzania tuna mifugo, sasa kama tuna vitu vikubwa hivi vitatu, lakini zaidi ya hapo tuna jiografia ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tunapopanga tupange kuona ambavyo vitu hivi vitatu kwenye mifugo, itatuletea nini baada ya mwaka mmoja, bada ya miaka mitano, hatuwezi kuwa tunasema kuwa ni wa pili Afrika tuna mifugo lakini ukienda kwenye mchango kwenye GDP, ukienda kwenye mchango wa pesa ya mmoja mmoja siyo kubwa. Tuna uvuvi, wenzetu tukienda kujifunza hata pale Namibia, wanafanya uvuvi mkubwa sana kwenye bahari kuu, sisi tuna eneo kubwa la bahari kuu lakini tujiulize maswali, mwaka huu tulivua kiasi gani mwaka kesho tutavua kiasi gani. Kama hatujiwekei namna ya kwamba mwaka huu tutoke hapa kwenda pale, tutakuwa kila siku tunajadiri tunamaliza mpango tunakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuja na mawazo kwamba umefika wakati Wizara ya Fedha inapokuwa inapanga mpango tuwekeane, wakae na Mawaziri wasainiane mikataba kwamba tunataka kwenye kilimo, kwenye kahawa iwe hivi, kwenye katani iwe hivi, kwenye mkonge iwe hivi. Kwa mfano mkonge sasa hivi, una bei kubwa sana kwenye soko la dunia, lakini unajua tunazalisha tani ngapi? Tunazalisha tani 34.6 kwa mwaka, wakati ardhi tuliyonayo tunaweza tukazalisha tani milioni moja na hela hii ikaingia kwenye economy. Ardhi tuliyonayo tunaweza tukatoka, leo korosho inaleta fedha nyingi sana, lakini korosho ni tani ngapi, laki mbili, laki tatu, lakini uwezo tulionao tunaweza tukaenda tani milioni moja. Sielewe watu wanaopanga mipango yetu kwa nini hatujiwekei target, tukiweka target nina hakika tutafanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania haikuwa bahati mbaya kuwepo hapa ilipo, jiografia yetu lazima tuitumie kukuza uchumi; hatuwezi kuwa tunasema tuna amani, nchi imetulia, tuna jiografia nzuri, lakini inaleta nini, tuangalie tunafanye biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimelisema kila nilipoingia kwenye Bunge hili, ni suala la miradi ya PPP. Kwenye miradi ya PPP sielewi kuna ukakasi gani Serikalini, kwa sababu PPP wako watu wanasema tumeshajaribu PPP ukisikia inatajwa wanataja TANESCO, haikuwa PPP ilikuwa ni management, wanataja RITES, RITES haikuwa PPP ilikuwa ni management, wanataja maji ya Dar es Salam City Water, hiyo haikuwa PPP, it was a management. PPP ni lazima mtu alete fedha, awekeze, azalishe, mgawane na mfano thabiti wa PPP ni daraja la Kigamboni, tumefanya, Serikali na NSSF na watu wanalipa pale, lakini wananchi hawajazuiliwa kwenda kupanda pantone, mwenye haraka ataenda kwenye daraja. Tukifanya hivi tuta-leverage haya tunayofanya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano, leo Mheshimiwa Rais anafanya miradi mikubwa sana mmoja ukiwepo mradi wa maji wa Nyerere wa Rufiji, jambo jema, jambo nzuri sana. Hata hivyo, lakini ukisoma sera ya Tanzania ya mwaka 2003 sera ya energy inasema energy mix maana yake nini? Tuna geothermal, tuna upepo, tuna gesi, tuna makaa ya mawe, mpango wetu unasemaje? Kama hatuna fedha kwa sababu tunafanya kwenye maji tutafute watu wafanye, wakifanya tutagawana zile fedha na Tanzania tutapata umeme mwingi. Nataka niwaambie leo wenzangu umeme ni bidhaa, umeme ni biashara, nina hakika tukizalisha umeme mwingi tutauza Kenya, tutauza Uganda, tutauza Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia na Malawi, tunaweza, lakini hatuwezi kuyafanya yote kwa wakati mmoja lazima mengine yafanywe na PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo barabara, tumekalia tunataka kila kitu kijengwe na Serikali, wewe umetembea duniani barabara za express way zipo; hivi tunaona tabu gani kujenga express way ya Dodoma Dar es Salam halafu hii barabara ya zamani iendelee kuwepo mwenye haraka atakwenda kwenye kulipia, wako watu wanakuja na hoja kwamba tunajenga SGR hakuna ya barabara siyo kweli hata kidogo, nenda China bigger as it is population one point four billion people wanajenga mabarabara, wanajenga reli yanaenda kwa kasi, reli haiwezi kuchukua nafasi ya barabara, wala haiwezi kuchukua nafasi ya ndege, vyote tunavihitaji kama Taifa. Ili mtu akitoka hapa aende Mwanza haraka, akitaka aende taratibu kuna barabara hii atakutana na ma Traffic, hii ya haraka atalipa, shida iko wapi? Leo wenzetu Uganda kutoka Entebbe kuja Kampala wamejenga express way, maana yake kule watu watalipia, lakini ile barabara ya zamani itaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe wenzangu PPP ni lazima, ndiyo way to go kama nchi. Kama na kwa sababu PPP itatusaidia, leo Serikali inajenga sana hospitali kila mkoa, kila wilaya, hivi tunaona tabu gani kuingia PPP mtu akaleta vifaa; kwamba vifaa vile yeye ndiyo anahangaika na vifaa, teknolojia ikibalika atalipisha yeye, kinachotokea yeye anaweka hela zake. Kwa hiyo maana yake tunaweza tukajenga hospitali nyingi zaidi kwa sababu vifaa ni gharama, lakini somebody yes will do it for us. Kwa nini wenzetu hawataki kuhangaika na PPP? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee miradi mitatu, ukisoma kwenye Mpango haitajwi sawasawa. Mradi wa kwanza ni wa LNG plant wa gesi kule Lindi, Mradi wa pili ni Mchuchuma na Mradi wa tatu ni Engaruka. Nataka wenzangu tuelewane miradi hii mitatu leo ingekuwa inatekelezwa ni zaidi ya bilioni 40 zingekuwa kwenye economy yetu. Leo Tanzania kila mtu angekuwa ana kazi, leo Tanzania shilingi yetu ingekuwa na thamani kwa sababu kuna dola nyingi zingekuja in our economy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Msumbiji muuza hata toilet paper ni tajiri pale Msumbiji kwa sababu ya Mradi wa LNG, watu watasema tatizo ni mikitaba, mimi nasema mikataba kwa Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Magufuli itakuwa mizuri tu, kwa nini tusi-negotiate, hatuwezi kuwa tunakaa tunasema tatizo letu ni mikataba mibaya, hapana, mikataba tuisahihishe mbona mkataba wa Barrick tumeubadilisha. Tunaogopa nini ku-negotiate vizuri na haraka kwenye LNG, huku kwenye Mchuchuma huku kwenye Engaruka, tunaogopa nini? Tatizo ni nini na hatutumii fedha zetu somebody yeye si analeta pesa. Pia kinachotokea tukitekeleza hii miradi, mradi wa PPP wa reli kutoka Mtwara kwenda huku Liganga utawezekana, lakini kama Liganga haiwezekani hiyo reli haitokuwepo. Hata Mradi wa Bagamoyo tukiamua kufanya hii miradi tuka-renegotiate upya, tuwaondoe wale wezi tulete watu wazuri, hii miradi tunaihitaji kwenye hii economy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mambo mawili makubwa; naomba sana wenzetu mpango wetu lazima uje na mambo makubwa mawili, lazima mpango uwe clearly kwenye job creation, mpango lazima uwe clearly kwenye foreign currency tunazipata wapi, kwa maana exports, kwa sababu kama hatutengenezi jobs, tunasomesha kila siku hizo kazi zitatoka wapi? Lazima PPP ndiyo ije na ili PPP ije mambo mawili yafanyike; moja, lazima tuangalie sheria zetu upya, tuweke legal framework yenye clarity, pia tuhangaike na education kwa maana kuandaa skills zitazofanya kazi kwenye hivyo viwanda vipya, kwenye hiyo miradi mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale mnaojua trend ya dunia, trend ya duni sasa hivi kule China gharama za kazi zimeanza kupanda kwa sababu wanakwenda first world; Asia, India gharama za kazi zinapanda maana yake ni nini? Wanakuja Afrika lakini watakakokuwa wamejiandaa, ndiyo maana leo unaanza kuona viwanda vikubwa vinatoka China vinakuja Ethiopia kwa sababu wamejiandaa, wameweka mazingira wezeshi na kwa kufanya vile wanapata jobs, wanapata technological transfer, pia above all wanaweza kupata hela za exports. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanawezekana, naamini tukiamua haya yanawezekana, naomba mpango wetu uhangaike na haya mambo, kwangu mimi ni makubwa sana. Niseme, umefika wakati siyo vibaya ku- copy vitu vizuri, ukisoma historia nchi zote zilizoendelea miaka ya 60; China, India, Singapore, Malaysia, South Korea, vitu vitatu vimewapeleka haraka sana. Cha kwanza wame-embrace free market na free trade, wameweka tu governance ya kuhakikisha inafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili ni pragmatism, hii means yake what? Maana yake ni kwamba, hutojali kama huyo paka ni mweusi ama ni mweupe, cha msingi akamate panya tu. Kama mtu anaweza akaja akajenga barabara, express way kwa hela zake, shida yetu nini? Mtu akishajenga barabara hawezi kuibeba akaondoka nayo, mtu akija akawekeza LNG plant hawezi ku-assemble akaondoka nayo haiwezekani, lakini pia lazima tuanze ku- impress meritocracy, tuanze kuhangaika na watu wenye maarifa, tutengeneze Taifa ili lihangaike na watu wenye maarifa, tuweze kwenda haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kama Tanzania kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Magufuli, ni Rais anayefanya maamuzi, ni Rais mwenye nia ya kutaka kuleta maendeleo kwa kasi, ni jukumu letu sisi Wabunge na watu wa Serikali, tumsaidie aende kwa haraka. Haya anayoyafanya lazima yawe leveraged na kitu kingine na kwa sababu anafanya maamuzi haraka, naombeni Serikalini na ninyi mfanye maamuzi haraka. Nchi hii itaenda kwa kasi sana kwa sababu tuna kila kitu unachoweza kusema hapa duniani, tuna madini, tuna gesi, tuna everything, kwa hiyo mipango yetu iwe ya kusaidia kwenda haraka kwenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la, kuna kitu kimeletwa Serikalini Mheshimiwa Waziri Mkuu amekianzisha kinaitwa MTAKUWA. MTAKUWA ni utaratibu wa kuhangaika na kuondoa unyanyasaji wa akinamama na watoto ni initiative kama ilivyo initiative ya UKIMWI, lakini nimesoma mpango wote hawaongei chochote kuhusu MTAKUWA. Taifa lolote lenye heshima ni Taifa ambalo linajali haki za watoto, haki za akinamama na haki za jinsia yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kwenye Mpango na bajeti ijayo kila Wizara ije na gender budget statement, tuoneshe tunavyojiandaa kuhangaika na mambo haya, huu ndio ustaarabu, hamwezi kuwa na Taifa la watu kila siku akinamama wananyanyaswa; watoto wananyanyaswa; ukiyasikiliza yanayotokea huko ndani, sio Taifa la Tanzania. Naombeni tukusanye nguvu za kifedha, za mikakati, za kisheria, kuhangaika na unyanyasaji wa akinamama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)