Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niweze kuchangia kidogo Mpango. Nitachangia katika maeneo mawili au matatu, lakini jambo la kwanza nilitaka kuzungumzia kupitia hiki kitabu cha Mpango; ukisoma ukurasa wa 10 wameelezea maendeleo ya miundombinu katika Taifa letu. Nami niseme, Mheshimiwa Waziri ameainishaa baadhi ya mikoa ambayo mpaka sasa hakuna muunganiko wa lami kwa maana ya mikoa, hasa ukiangalia Mkoa wa Tabora, Ruvuma, Lindi, Mtwara pamoja na Tabora, Katavi, Kigoma na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kupitia huu Mpango, kwa sababu katika mikoa hii bado kuna changamoto ya miunganiko hii ya barabara; na jambo hili la suala la miundombinu katika hii mikoa ambayo imebaki nyuma, inaleta ukakasi na inaendelea kuwatesa wananchi kwa maana ya kwamba wanashindwa kufanya biashara na ukizingatia katika kanda hizi, asilimia kubwa ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia Mpango huu, kwa sababu umeainisha kabisa kwamba katika mikoa hii imebaki nyuma ili sasa wakazi hawa wa mikoa hii nao wapate ahueni ya maisha kupitia masuala ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masuala ya fidia, miundombinu ya barabara nilitamani sana iendane na masuala ya kufungamanisha uchumi wao na wananchi, kwa maana tunaposema maendeleo ya vitu, iendane sambamba na maendeleo ya uchumi wa wananchi, kwa maana ya personal development.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika maeneo mengi ambayo yanahusiana na masuala ya fidia kwa maana ya wananchi ambao walikumbwa na bomoa bomoa katika mikoa mbalimbali, kwa mfano Mkoa wa Mwanza, Dar es Salaam, Katavi na mikoa mingine ambayo bomoa bomoa imepita; ni kweli wananchi wanazihitaji barabara lakini katika mikoa ambayo bomoa bomoa imepita wananchi wengi wamebaki ni masikini. Sasa lengo la Serikali ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uchumi mnaosema umekua kwa asilimia 7.0 ni uchumi wa aina gani? Tunahitaji kuona mafanikio au uchumi wa wananchi unakwenda moja kwa moja kwa wananchi kwa maana ya kwamba msivunjie nyumba wananchi ambao wamejenga kwa gharama kubwa, leo wanaishi katika nyumba za kupanga. Katika jambo hili mnapokuwa mnafanya tathmini na hata wananchi ambao wanakuwa wameachwa, wameshindwa kufanyiwa tathimini, mweze kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jambo hili limekuwa ni changamoto na mpaka sasa kuna taharuki kwa wananchi ambao waliingia kwenye mchakato huo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa sbabu mnatangaza amani ambapo mnatumia nguvu kubwa kuwaaminisha watu kwamba katika uchaguzi huu kila kitu kiko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makovu na majeraha ya watu ambao wameumia kwenye uchaguzi huu especially katika Mkoa wangu wa Katavi, tarehe 5 Novemba, 2019 Mtendaji aliagiza watu wakawavamie vijana wa CHADEMA; na mpaka sasa kuna kijana ambaye anaitwa Dominic Bazilio Mwila alipigwa na Mgambo mpaka akafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme katika hayo marekebisho mnayoyatoa, kwamba tunahitaji kufanya maridhiano ya pamoja, naomba kabisa, kama kweli mnahitaji kuwa na maridhiano ya pamoja na kuwe na amani katika Taifa hili, mwache kuumiza watu na majeraha ambayo wanayapata. Leo hii tutarudi kwenye uchaguzi, lakini watu wana majeraha, watu wameumizwa, watu wako ndani na siyo katika Mkoa wa Katavi tu peke yake…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rhoda, mtu alipigwa na mgambo huko kwa mambo yao huko. Sasa ukituambia au ukiwaambia waache, sasa kweli unaamini hawa wamemtuma huyo mgambo amuue huyo ndugu yetu! Endelea tu kuchangia.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaendana sambamba kabisa na masuala ya uchaguzi, ndiyo maana nikasema, kama mnahitaji amani mnayoitangaza, wasimamizi na wahusika waliotumia mamlaka yao kufanya majanga haya kwenye maeneo mbalimbali, siyo mkoa wa Katavi peke yake, mpaka na mikoa mingine, naomba kabisa katika masuala ya maridhiano kwenye mambo haya ya suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tupunguze majeraha na kutumia nguvu ambayo Serikali inatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika maeneo ambayo kuna upungufu, hawa Watendaji au Makatibu Tarafa, Wasimamizi Uchaguzi...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Rhoda, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Mheshimiwa Rhoda taarifa kwamba kwanza tuwe wakweli kwenye Bunge hili, suala la kusema kwamba watu wanauawa, kulikuwa hakuna uchaguzi sehemu yoyote unaofanyika, kulikuwa kilichofanyika ni ujazaji wa fomu sasa huyo mtu aliyeenda kuuawa kwa kujaza fomu, kulikuwa kumetokea nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine hapa jamani tuwe tunasema ukweli. Haya mambo, vitu vinaenda kwenye nchi za watu. Tanzania inachafuka kwa mambo ya uongo. Hakuna uchaguzi uliofanyika, ni ujazaji wa fomu. Huyu mtu aliuawa wapi? (Makofi)

MWENYEKITI: inawezekana walikuwa wanagombea mpango kando au nini, ndiyo anachosema Mheshimiwa Rhoda. Malizia, bado dakika moja tu.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu. Ninachokiongelea hapa, kifo cha mtu huyu kinahusishwa na masuala ya uchaguzi kwa sababu kama nilivyosema mwamzo, Katibu Tarafa pamoja na Watendaji walitoa magizo kwenda kuwashughulikia wagombea CHADEMA. Kwa hiyo, kesi ipo, Ndiyo maana nasema katika maridhiano haya, katika mipango ya Serikali kuhakikisha mnatuliza uchafuzi uliotokea, naomba kabisa m-deal katika maeneo ambayo kweli hali siyo shwari na Serikali ione haja ya kuweza kutatua migogoro ambayao ipo na inaendelea. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Nakushukuru sana.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.