Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia siku ya leo. Nafikiri leo tunajadili Mapendekezo ya Mpango wa Taifa. Nina mambo matatu ambayo nataka kujadili siku ya leo. Jambo la kwanza kabisa, nataka kuanza na Utawala Bora. Tunavyojadili Mpango, tunajadili mambo muhimu sana kwa ajili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli tu ni kwamba utawala bora ndiyo itakuwa dira na itakuwa mwongozo mzuri sana kuhakikisha kwamba tunatekeleza Mapendekezo ya Mpango huu ambao tunaujadili siku ya leo. Kama hatutaweza kulinda utawala bora katika Taifa hili, tutakuwa tunafanya mchezo ambao hautaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa sababu, ili wawekezaji waweze kufika katika nchi, hii ni lazima kuhakikisha kwamba utawala bora unakuwa ni kipaumbele, pia utulivu na amani katika nchi yetu lazima viwe kipaumbele zaidi. Ninazungumzia utawala bora kwa sababu ni lazima tuhakikishe kwamba sheria zinasimamiwa vizuri na zinafuatwa katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kuzungumzia tu kuhusiana na suala la mchakato wa uchaguzi ambao ulikuwa unaendelea kwenye nchi yetu na ambao unaendelea mpaka sasa hivi. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI akizungumzia hali halisi ya kwamba wale wote waliojaza fomu na kurudisha na wale ambao hawakuteuliwa lakini walijaza fomu na kurudisha, waendelee na uchaguzi. Yako matatizo mengi sana yaliyojitokeza kwenye mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa, kwa mfano ukifika kwenye Mji wangu wa Tunduma na Wilaya ya Mbozi, kuna baadhi ya Kata kama sita Watendaji hawakuonekana kabisa na hakuna aliyechukua fomu katika maeneo hayo. Kwa hiyo, fomu hazikuchukuliwa kwa sababu milango ilikuwa imefungwa na hakuna mtu yeyote aliyepata fomu. Watu walishinda pale kuanzia asubuhi mpaka jioni na maeneo mengine ambamo Watendaji walikutwa, waliwaita Polisi wakawakamata na wananchi sasa hivi wanasota wako rumande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna matatizo makubwa sana. Tulikuwa tunataka tupate ufafanuzi, kwa mfano yale maeneo ambayo watu hawakupewa ruhusa kabisa ya kwenda kuchukua fomu, namna gani watakwenda kushiriki uchaguzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia maeneo mengine, ni wale watu ambao walikataliwa kabisa wasirudishe fomu hizo, ni namna gani wangeweza kushiriki uchaguzi huo. Kwa hiyo, wakati unazungumza maneno haya, tumekwenda kwa Mheshimiwa Jafo zaidi ya mara tatu, tumemkuta Mheshimiwa Waziri, lakini pia tumemkuta Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tumemweleza matatizo haya tukiongozana na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, lakini hakuna kilichoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulistaajabu sana, wasimamizi wa uchaguzi ambao wamepewa fursa ya kusimamia uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wamepewa kazi na Ofisi ya TAMISEMI, lakini cha kushazangaza maelekezo ambayo Mheshimiwa Waziri alikuwa anasema anawalekeza, hawakuweza kutekeleza hata moja. Sasa tunakwendaje kwenye uchaguzi wa namna hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli utaratibu uliokuwa ukiendelea ni utaratibu wa kihuni ambao kwa kweli haustahili kabisa. Ninashangaa kwamba mpaka sasa hivi Serikali haijachukua hatua kwa hao watu ambao wamekwenda kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo naomba sana, kwenye suala la utawala bora ni muhimu tukaeshimu sheria tunazo zitunga wenyewe, lakini pia na kanuni na taratibu mbalimbali ambazo tunakuwa nazo ili kujenga imani pamoja na kujenga umoja na mshikamano ulio katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka pia kuzungumzia kuhusiana na suala la uchumi. Nimesikia mara nyingi sana Mheshimiwa Rais anazungumzia kuhusiana na vita ya uchumi. Vita ya uchumi tunayoizungumzia ni kuhakikisha kwamba fursa yoyote inayopatikana kwenye nchi ni lazima tuitumie kwa muda mwafaka; tumekuwa tunachelewa sana kufanya maamuzi katika taifa hili. Mara nyingi mipango mingi; na nimepata taarifa mbalimbali ambazo si rasmi; wanasema mipango tunayoipanga katika taifa hili inakwenda kutumika kwenye nchi nyingine na wanafanya vizuri, lakini sisi tumekuwa ni wazito na wagumu wa kuamua ni namna gani tunaweza tukatekeleza fursa na mipango mbalimbali ambayo inapatikana na ambayo tunaipanga katika taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kidogo, na wewe mwenyewe umekuwa unasisitiza sana; kwa mfano kama Bandari ya Bagamoyo, tumekuwa na hofu na tunapiga kampeni ya hofu badala ya kuingia. Tuna wataalamu wengi na tuna wasomi wengi. Hivi kweli wameshindwa kupata ukweli? Wameshindwa kupata uhakika wa namna gani tunaweza tukahakikisha kwamba fursa ya Bandari ya Bagamoyo tukatekeleza, na tusifikiri kwamba tuko peke yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Beira kule Mozambique wana nafasi wanaweza wakafanya hayo tukienda Mombasa wanaweza wakafanya hayo hasa ni lazima twende na wakati tunashindwaje kujadili na watu tunawasomi wengi wa kutosha tumeshindwaje kujadili na watu ili miradi hii ambayo inaweza ikainua uchumi wa taifa iweze kutekelezwa katika taifa letu tunaona haya mambo hayatekelezeki na kila wakati tunaona kimya.

Mheshimwa Mwenyekiti, lakini yapo mambo mengine ambayo tunaona kabisa kwamba yanasababisha uchumi wetu usisonge mbele. Kwa mfano sasa kuna tume/ kamati uliiunda kwa ajili ya kuchunguza masuala ya madini, wakaenda Mererani wakaangalia mambo mabaya yaliyokuwepo kule na wakasema wanaweza wakafika mahala wakasitisha ule mgodi ili kujadili kwa manufaa ya taifa hii. Hata hivyo ni miaka mitatu leo au mwaka wa nne leo hakuna kinachoendelea; mgodi umesimama, wafanyakazi zaidi ya 400 wamefukuzwa kazi na hawajapewa hata mafao yao mpaka sasa hivi lakini kazi aiendelei na migodi ile imesimama na hakuna kinachozalishwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tufike mahala kama taifa tujuwe kwamba tunapokuwa tunahitaji uchumi upande ni lazima tuhakikishe kwamba tuna fanya haraka kwenye fursa ambazo tunazo. Leo tuna mgodi lakini hamna kinachoendelea; tanzanite imekaa pale inaoza watu wanaochimba pale hawaeleweki wanasema tunajadili, miaka mitatu mnajadili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na huo mgodi si kwamba labda anamiliki mbia peke yake, ni sisi nay eye; sisi tuna asilimia 50 na yeye anaasilimia 50, lakini tunashindwa kujadili kitu kama hicho kitu kidogo tunakaa miaka 3. Wananchi wetu ambao ni Watanzania waliokuwa wanafanya kazi pale zaidi ya 400 wameshindwa kulea familia zao na kupeleka watoto wao shuleni kwa sababu ya majadiliano, ni siri ambayo mpaka leo hatuelewi. Kwahiyo tunaomba sana Wizara ya fedha pamoja na Serikali watuambie ni kwanini mpaka leo hawajafikia makubaliano kwenye majadiliano ya Mgodi wa Tanzanite ili uweze kuzalisha na kuhakikisha kwamba unachangia Pato la Taifa kwa kipindi ambacho tumekuwa nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine; tumeshangaa sana, tunasema kwamba tuna madini na tunataka madini yachangie Pato la Taifa; na kila mwaka tunapanga bajeti humu ndani lakini fedha hazijawahi kwenda. Waziri wa fedha pia atuambie ni kwanini hapeleki fedha ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kuinua uchumi kwa kutumia madini? miaka yote mwaka wa kwanza mpaka wa tatu mpaka miaka minne hakuna kilichoendelea. Mwaka jana tulitenga takriban bilioni sita ili waweze kufanya shughuli za maendeleo katika migodi yetu lakini haikwenda hata shilingi; na hata mwaka juzi pia. Sasa maaana yake ni nini? Kama kweli tukaanzisha shirika la kusimamia madini katika nchi kuhakikisha migodi yetu inafanya kazi na tunapata pato kubwa la taifa kutokana na madini lakini hatupeleki fedha. Kwahiyo mambo haya ni lazima tuyatazame sana, na kama Watanzania tuchangamkie fursa; tunapokuwa na mradi wowote ni lazima kuhakikisha kwamba twende na muda. Tunavyozidi kuchelewa ndivyo ambavyo tunachelewa kufanya maendeleo katika taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kuhusiana na kilimo. Asilimia 65 ya Watanzania ni wakulima, wafugaji na wavuvi; fedha zimekuwa zinatengwa kila mwaka; nitoe mfano wa miaka mitatu tu. Mwaka wa 2016/ 2017 tulitenga ndani ya Bunge hapa bilioni 101 lakini fedha iliyokwenda kwenye shughuli za maendeleo bilioni tatu peke yake. Mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi bilioni 150, fedha iliyokwenda kwenye kilimo ilikwenda bilioni 16 peke yake. Pia mwaka 2018/2019 tulitenga fedha hapa bilioni 95 lakini fedha iliyokwenda ni takriban bilioni 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 65 ya Watanzania ambao ni kundi kubwa kuliko kundi lolote katika nchi hii hawapelekewi fedha; sasa leo tunasema tunakwenda kwenye uchumi wa kati; tunawezaje kwenda kwenye uchumi wa kati kama wananchi hawa ambao ni kundi kubwa wangeweza kuzalisha lakini pia wangeweza kuchangia Pato la Taifa hawapelekewi fedha. Kwahiyo tunaomba sana; tunapozungumzia uchumi ni lazima tuhakikishe kwamba tunalenga maeneo muhimu ambayo yanaweza yakainua uchumi wa taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni lazima tukubaliane, leo katika takwimu za Serikali vijana wetu wanaomaliza kwenye vyuo mbalimbali hapa nchini ni takriban 800,000, lakini watu wanaoingia kwenye ajira rasmi ni takriban watu 40,000 watu takriban 760,000 hawana kazi; hawa watu wanakwenda kwenye kilimo na uvuvi lakini fedha haziendi kule tunasema tunataka kujenga taifa linaweza likatusaidia kuinua wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo mapendekezo ya mpango tunayoyaangalia leo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa, hauoneshi ni namna gani tunakwenda kwenye uchumi wa kati, inaonekana tunazungumza ndani ya Bunge lakini utekelezaji kwakweli hauko sawa sawa. Tunaomba uwe mkali lakini uendelee kutoa maagizo tukishirikiana na sisi Waheshimiwa Wabunge ili tuhakikishe kwamba Serikali hii inafanya yale tunayoyapitisha ndani ya Bunge hili. Ahsante.