Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kutoa shukurani za dhati, kwako wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vema mjadala wa hoja iliyowasilishwa mnamo tarehe 5/11/2019 na Waziri wa Fedha na Mipango ambayo ni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia ama kwa maandishi au kwa kuzungumza. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 111 wamechangia katika mjadala huu, ambapo Wabunge 95 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 16 kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyotangulia kusema, lengo la wasilisho la Waziri wa Fedha na Mipango mbele ya Bunge lako Tukufu lilikuwa ni kuomba maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wakiwasilisha mawazo na maoni ya wananchi kuhusu maendeleo ya nchi yao na mgawanyo wa rasilimali fedha ili yazingatiwe katika hatua inayofuata ya kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka ujao wa Fedha, mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali nakiri kuwa lengo hili limefanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu sana na narudia kusema, ahsanteni sana kwa michango yenu Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kutoa maoni na ushauri kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2020/2021, Waheshimiwa Wabunge wametoa pia pongezi nyingi sana kwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kufanikisha kwa kiwango cha juu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti tangu Serikali yetu ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba, 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo mkunjufu na kwa unyenyekevu mkubwa sana, napenda kupokea pongezi hizi za Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima napenda kuwashukuru kwa moyo wa dhati kabisa Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutuamini katika kusimamia majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika pongezi hizi zilizotolewa na Kamati yako ya Mipango ni matokeo ya miongozo na maelekezo yao ambayo wamekuwa wakitupatia kwa lengo la kuliletea Taifa letu maendeleo. Kwa niaba ya Waziri wangu, pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango, napenda kuwaahidi kwamba hatutawaangusha, kwani heshima na dhamana mliyotukabidhi kwa niaba ya Watanzania ni kubwa sana na yenye utukufu ndani yake nasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa kuniamini na kunipa jukumu la kutoa ufafanuzi kwa niaba yake, wa hoja za Waheshimiwa Wabunge siku hii ya leo. Nitumie pia fursa hii kuwashukuru kwa dhati watendaji na watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bwana Doto Mgosha James, kwa kuchambua na kutafuta takwimu na taarifa zilizohitajika kutolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kutambua mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi. Kamati ilitupatia ushauri wa msingi na wa mwanzo ambao Waziri wa Fedha na Mipango alieleza kwa ufupi wakati akiwasilisha hoja hii mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, tumepokea mchango uliotolewa na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kwa niaba ya msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja iliyombele yetu. Aidha, nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wewe binafsi kwa mchango wako kama Spika na miongozo yako ambayo umetupatia ndani ya kipindi hiki cha siku tano, lakini pia mchango wako kama Mbunge unayewakilisha wananchi wa Jimbo la Kongwa nasema ahsante sana tumepokea mchango wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majadiliano ya hoja iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu, Serikali imepokea maoni mengi sana kwa uchache tumejitahidi kuyachambua na kuyaweka katika makundi yafuatayo:-

(i) Kundi la kwanza ambapo mchango umewekwa nguvu na Waheshimiwa Wabunge ni kuweka msukumo thabiti kwenye sekta ya kilimo, hususan kuwa na uhakika wa upatikanaji wa pembejeo, mbegu na zana bora, huduma za ugani, mikopo na mitaji, miundombinu ya umwagiliaji na utafiti ili kuongeza uzalishaji, tija, ubora na uhakika wa masoko na bei ya masoko ya wakulima wetu; (Makofi)

(ii) Eneo la pili ni kwamba Serikali ichukue hatua ya kuboresha uratibu na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maji ili thamani halisi ya fedha inayopelekwa kwenye miradi ya maji iweze kuonekana na hatimaye kufikia malengo ya kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wetu;

(iii) Kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya kimkakati kama vile umeme, reli na barabara ili kuvutia uwekezaji mahiri na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii ndani ya Taifa letu;

(iv) Kuwekeza na kutumia kikamilifu rasilimali za bahari na maziwa (the blue economy), hususan uvuvi wa bahari kuu;

(v) Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ndani ya Taifa letu; na

(vi) Kuimarisha mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali, naahidi kuwa, wakati wa kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/ 2021 tutazingatia ipasavyo maoni na ushauri uliotolewa na Bunge lako Tukufu lilipokaa kama Kamati ya Mipango kwa sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kazi ya Wizara yetu ya Fedha katika siku hizi tano ilikuwa ni kupokea maoni na ushauri, ambao sasa tunakwenda kuutafakari kama serikali nzima na kuufanyia kazi hatimaye kuja na mpango wetu wa maendeleo na bajeti kwa mwaka ujao wa fedha naomba nisiseme mengi sana. Hata hivyo, kama ilivyo ada naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi kwa baadhi tu ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza na naamini wengi watashangaa nisipoongelea kuhusu Serikali yetu kuwekeza katika kilimo ili sekta ya kilimo ambayo imepewa msukumo mkubwa na hoja ya kwanza ni Serikali iwekeze zaidi katika sekta ya kilimo ikiwezekana kutenga 10% ya bajeti kama Azimio la Maputo na Azimo la Malabo linavyotuelekeza ili kuiwezesha kukua kwa 6% kama Azimio la Malabo pia linavyotuelekeza na hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunafahamu umuhimu wa sekta ya kilimo na mchango wake mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wetu na pato la Taifa. Lakini ni vizuri kama watanzania tukafahamu kuwa ili sekta ya kilimo iweze kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa ni muhimu sana serikali yetu kuwekeza kimkakati katika maeneo makuu yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni mafunzo, utafiti pamoja na ugavi. Eneo la pili ni usalama wa chakula, uhifadhi na lishe. Eneo la tatu masoko kwa ajili mazao kwenye soko letu la kilimo. Eneo la nne upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, eneo la tano miundombinu na elimu ya kuongeza thamani ya mazao yetu. Eneo la sita upatikanaji na usambazaji wa pembejeo na zana za kilimo, na eneo la saba ni kuwa na miundombinu wezeshi kama vile umeme, maji na umwagiliaji, barabara, reli, madaraja, vivuko na meli pamoja na mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu inatambua sana na imekuwa ikitenda mengi katika maeneo haya na ninaomba niseme machache ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Tano imekuwa ikiyatekeleza ili kuhakikisha ukuaji wetu wa sekta ya kilimo unakua kama tulivyosaini maazimio mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza Serikali yetu imeanza utekelezaji wa Programu ya ASDP II ambapo shilingi bilioni 25.19 ambazo ni fedha za ndani na shilingi trilioni 1.37 fedha za nje zimetumika kati ya mwaka wa fedha 2016/ 2017 na robo ya kwanza ya mwaka 2019/2020 katika kutekeleza kazi zifuatazo;-

(i) Serikali imefadhili jumla ya wanafunzi 3,897 kama yalivyo malengo yetu kwenye program hii ASDP II katika ngazi ya Astashahada na Stashahada ili kuhakikisha tunakuwa na maafisa ugani wa kutosha;

(ii) Tumewekeza pia kwenye Utafiti ambapo tumefanikiwa jumla ya miche 37,816 ya korosho kuzalishwa na kusambazwa nchini katika mikoa ile ambayo ina potential kubwa ya uzalishaji wa korosho. Lakini pia mbegu bora 14 zimegunduliwa na TARI na aina 11 ya mbegu mpya za mpunga zimegunduliwa na kutambulishwa katika skimu 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema akiba ya chakula ni jambo la muhimu sana taifa letu limeona na sisi ni mashahidi tunaona Taifa letu limekuwa na akiba ya chakula ya kutosha kwa sababu ya uwekezaji ambayo serikali ina wekeza. Tumeweza kufikia tani 68,124.69 na ukarabati wa maghala 105 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 31,500 umekamilika ili kuhakikisha chakula chetu kinakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumefanyika ukarabati na ujenzi wa skimu za umwagiliaji. Ambapo skimu 5 zimekamilika ikiwa ni pamoja na barabara za kuingia na kutoka zenye urefu wa kilomita 15 na mafunzo kwa wajumbe 311 wa umoja wa umwagiliaji katika Wilaya za Mvomero, Kilosa na Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo ya kina niwaombe Waheshimiwa Wabunge wa utekelezaji wa ASDP II yanapatikana katika ukurasa wa 65 - 66 wa Mapendekezo ya Mpango wa 2020/2021 na ukurasa wa 259 – 277 wa Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi robo ya kwanza ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu haikuishia hapo kwenye utekelezaji wa ASDP II peke yake, tumekuwa pia na utekelezaji wa mpango wa kuendeleza wa kuendeleza kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania. Baadhi ya kazi zilizotekelezwa kati ya 2016/2017 na 2019/2020 kwa fedha za ndani ni pamoja na kuendeleza kongano sita zakuongeza tija katika uzalishaji, thamani ya mazao, usambazaji wa mbolea, masoko na watoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hekta 38,477 za mazao zimelimwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Tumeendelea kutenda mambo mengi ambapo pia tumeweza kufufua vinu vya kusaga nafaka NMC Dodoma na Mwanza. Ambapo kwa kinu cha Dodoma kimekamilika na kinu cha Mwanza kimefikia 80% ili kuhakikisha sasa tunaweza kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu na tumetumia shilingi bilioni 15.53 katika kufufua vinu hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu pia imetoa jumla ya shilingi bilioni 9.92 kwa ajili ya kufufua kiwanda cha Ngozi Karanga – Moshi. Kazi ya kutengeneza na kusimika mashine inaendelea hii yote ni katika kuhakikisha mipango yetu ya kuinua kilimo chetu mazao yetu ya kilimo inafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu pia imetekeleza programu ya uendelezaji wa mifumo ya masoko na Huduma za Fedha Vijijini ambapo tumetumia shilingi bilioni 114.28 fedha za nje zimetumika kuboresha miundombinu ya masoko vijijini, kuwajengea uwezo wakulima wapato 83,988 katika vikundi 2,408, taasisi 10 za fedha na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo 720 pia vimefikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulieleza Bunge lako Tukufu yameelezwa mengi kwamba Serikali yetu haitoi kipaumbele kwenye kilimo chetu haya nayaeleza na yameandikwa kwenye document ambazo tayari tunazo tuweze kuzipitia ili tuwafikishie watanzania ujumbe kwamba nini kinafanyika na Serikali yetu ya Awamu wa Tano kuhakikisha kilimo chetu kinakuwa imara na kinatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii iliunganishwa na ukuaji wa sekta hii ya kilimo. Lakini Waheshimiwa Wabunge naomba kwa unyenyekevu mkubwa tupitie vitabu yetu. Kitabu chetu cha Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2017, ukurasa 20. lakini pia taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2018 ukurasa 20 pia utaona kwamba, sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 5.6 kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2018 tofauti na ambavyo Waheshimiwa wabunge wengi wamesema sekta hii imekuwa kwa chini ya asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango hiki kinakaribiana na lengo la Malabo ambapo nilisema tulisaini azimio hili la Malabo la kuhakiksha sekta yetu ya kilimo inakuwa kwa angalau la asilimia 6 sisi tupo asilimia 5.6 na taarifa zetu mbalimbali tunazozisambasa na ambazo watanzania wanatakiwa kufikishishwa na kuzisoma zinaeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jitihada nilizozieleza tunaendelea kupiga hatua katika nyanja ya uwekezaji, kaika sekta ya kilimo na sekta wezeshi, hususan katika Awamu ya Tano ya uongozi wa Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Hivyo basi, ni matarajio yetu kuwa, tutavuka lengo hili la Malabo la asilimia sita ndani ya muda mfupi ujao tunachohitajika ni kuisapoti serikali yetu kuongea na watanzania kuongea na wakulima na wafugaji wetu ili wazione fursa zinaletwa mbele yao na serikali yao tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja namba mbili, hoja na mbili ambayo ningependa kuitolea maelezo kidogo ni ile ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi pia wamesema Serikali iangalie uwezekano wa kukopa kupitia export credit ili kukamilisha Mradi wa Reli ya Kisasa kwa pamoja badala ya kujenga kidogo kidogo ili kuona matokeo chanya na yenye tija ya uwekezaji huu. Hoja hii ni muhimu sana na kama Serikali tunaipokea lakin lazima tufahamu dhamira njema ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ya kutekeleza mradi huu wa Reli yetu ya Kisasa kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu Awamu ya kwanza ya ujenzi inafanyika kwa kutumia mapato ya ndani na Awamu ya pili inagharimia kwa fedha za mkopo utakaopatikana kwa utaratibu wa Export Credit Agency ambao masharti yake ni nafuu tofauti na ilivyodaiwa na Waheshimwa wabunge kwamba tunakopa kwa masharti ya kibiashara hapana tunakopa mikopo naafuu ili tuweze kutekeleza mradi wetu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kutekeleza mradi huu kwa awamu unatokana na tathmini ya kitaalam iliyofanyika kuhusu upatikanaji na gharama za mikopo, uwezo wa Serikali wa kuhudumia deni bila kuathiri utekelezaji wa bajeti ya maeneo ya kipaumbele pamoja na uhimilivu wa deni la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakisisitiza sana kuhusu uhimilivu wa deni la Serikali na katika hili naomba niliombe Bunge lako Tukufu lifahamu kwamba kwa mujibu wa sheria ya mikopo, dhamana na misaada sura 134, tunatakiwa kukopa kwa kuzingatia tathimini ya uhimilivu wa deni yaani debt sustainability analysis na ukomo wa kawaida ni kati ya dola za kimarekani milioni 800 hadi dola Kimarekani 1,000 kwa mwaka. Hivyo basi, uamuzi wa kukopa fedha za mradi mzima kwa wakati moja tutakwenda kuvunja sheria tuliyoitunga wenyewe lakini pia tutakwenda kupata usumbufu kwenye kuli-manage deni letu la Taifa. Naomba tuendelee kuiamini serikali yetu dhamira yake ni njema katika kuhakikisha mradi wetu unakamilika kwa wakati lakini utekelezwe kwa awamu kama ambavyo Bunge lako tukufu limeletewa mbele yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tatu ambayo ningependa kuisemea kwa ufupi ni hoja iliyosemwa kwamba utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu ya kimkakati ambayo ni mradi wa wa reli ya standard gauge, kufua Umeme katika Mto Rufiji na ununuzi wa Ndege za Serikali imechukua shilingi trilioni 4.42 ambayo ni sawa na asilimia 36 ya fedha zote za miradi ya maendeleo. Lakini hoja hii ikasemwa zaidi kwamba miradi hii haina faida za moja kwa moja katika uchumi wa nchi yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba malighafi inayotumika kujenga reli yetu ya kisasa ambayo ni chuma na cement karibu zote zinatoka nje ya nchi na hivyo fedha zinaondoka katika mzunguko wa ndani na kupelekwa nje kwa ajili ya ununuzi wa malighafi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa watanzania wafahamu ukweli kuhusu miradi hii na faida ambayo inapatikana wakati wa utekelezaji wa miradi hii na baada ya kukamilika kwa miradi hii. Ni vizuri watanzania wasipotoshwe ukiaacha faida za moja kwa moja kwenye uchumi wetu zitakazopatikana baada ya miradi hii kukamilika, zipo faida ambazo zimeshaonekana tayari kwenye Taifa letu tangu kuanza kwa utekelezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache na ufupi, naomba niseme kwa kila mradi nini Taifa letu limepata? Nianze na mradi wa reli yetu ya kisasa (Standard Gauge Railway). Hadi Septemba, 2019 Serikali yetu tunafahamu kwenye mradi huu imetoa shilingi trilioni 2.52 lakini mradi huu umezalisha ajira kwa Watanzania takribani 13,117. Hawa ni Watanzania ambao hawakuwa na ajira. Wamepata ajira kwenye mradi huu na wanaendelea kulipwa kutokana na utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu pia umefungua fursa kwa Wakandarasi na Wazabuni wa ndani zaidi ya 640. Hawa walikuwa hawana kazi. Kupitia mradi huu Wakandarasi hawa wamepata kazi kupitia mradi huu na fedha wanazolipwa zinabaki ndani ya Taifa letu tofauti na ambavyo imesemwa fedha nyingi inaondoka kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni za Wakandarasi hawa 640 zina thamani ya shilingi bilioni 664.7. Tunaweza kuangalia kwa asilimia, ni kiwango kikubwa cha pesa kinachobaki ndani ya Taifa letu kutokana na utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi huu pia unakadiriwa kutumia cement mifuko milioni tisa na nondo za madaraja kilogramu milioni 115 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Makutupora tu. Malighafi hizi zinatoka ndani ya Taifa letu. Hakuna cement inayonunuliwa nje ya nchi kuja kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, viwanda vyetu vinaendelea kuzalisha cement kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji na fedha hizi zinaendelea kubaki ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mradi huu utaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia masharti ya mkataba ambapo asilimia 30 ya gharama za mradi itatumika katika ununuzi wa huduma na bidhaa kutoka nchini. Kwa hiyo, Serikali yetu chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, iko makini katika kila mradi unaotekelezwa kuhakikisha Taifa letu linafaidika na utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa mradi huu, tunafahamu ni mengi tutafaidika nayo, lakini dogo tu ambalo Taifa hili limekuwa likiumia kwa muda mrefu ni gharama za matengenezo ya barabra zetu, tutaokoa takribani kwa mwaka mmoja zaidi ya shilingi bilioni 6.7. Ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, ndiyo dhamira ya Chama cha Mapinduzi, ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa wakati, fedha zake zinatafutwa kwa wakati na ndiyo maana tulijibana na kuhakikisha awamu ya kwanza ya mradi huu inatekelezwa na fedha za Watanzania wenyewe, fedha za walipakodi wa Tanzania wenyewe. Nawashukuru sana Watanzania kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari, kwa kuendelea kujitolea kusimamia miradi yao ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye mradi wa pili ambao nao tumeambia kwamba fedha zote zinaondoka hazibaki nchini. Ni mradi wa uzalishaji wa umeme kwa nguvu za maji wa Julius Nyerere. Mradi huu hadi Oktoba, 2019, nao pia umetusaidia kuzalisha ajira za Watanzania ambao walikuwa hawana ajira zaidi ya 1,456. Mradi huu pia umeongeza fursa kwa Wakandarasi wa Kampuni zetu za ndani. Kampuni 10 za Kitanzania hadi Oktoba 2019, zimepata kazi kwenye mradi huu wa uzalishaji umeme kwa nguvu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mradi huu tumeona kuna ongezeko la ununuzi wa bidhaa za ndani, mfano, cement, nondo, kokoto, mchanga pamoja na vyakula vya aina mbalimbali ambavyo vinatusaidia kuchochea ukuaji wa sekta yetu ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, Tanzania tunayoiendea na Tanzania tuliyopo ni Tanzania ya viwanda. Hakuna Tanzania ya viwanda bila ya kuwa na umeme wa uhakika, hakuna Tanzania ya viwanda bila ya kuwa na umeme wa bei nafuu. Tunatarajia tutakapokamilisha mradi huu, bei ya umeme itashuka na kwa uhakika tutaweza kuiona Tanzania ya Viwanda ambayo Watanzania wameisubiri kwa muda mrefu. Nitoe tu rai yangu kwa Waheshimiwa Wabunge, tuendelee ku- support miradi hii kwa dhamira njema kabisa ili kuwapa fursa Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa Shirika la Ndege; mradi huu pia umesaidia sana katika kuzalisha ajira za Watanzania zaidi ya 436 hadi kufikia Septemba 2019. Mradi huu pia umerahisisha huduma ya usafiri ambapo njia 11 za ndani ya nchi; na sita nje ya nchi zimeanzishwa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2019. Tunaona mapato yetu yakiongezeka tukiweza kukusanya kutokana na utekelezaji wa uboreshaji huu wa Shirika letu la Ndege, lakini pia kuongezeka kwa idadi ya watalii ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilikuwa no hoja ya pili ambayo ningependa kuitolea maelezo kidogo ili tuondoke tukiwa na ufahamu. Yote ambayo yamependekezwa na Kamati yako ya Mipango juu ya miradi hii tutakwenda kuitekeleza tunapoanza kuandaa Mpango wetu wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021 lakini tukizingatia pia hatuvunji sheria tunapotekeleza miradi yetu hii ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya nne ambayo ningependa kuisemea kidogo ni fedha za kutosha kwa ajili ya TARURA. Hili limesemwa karibu na Wabunge wote ndani ya Kamati yako ya Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu inatambua sana umuhimu wa kuboresha barabara za mijini na vijijini ili kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji hususan katika maeneo ya vijijini. Katika kutekeleza azma hii, Serikali yetu imeongeza bajeti ya TARURA kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 kutoka shilingi bilioni 272.6 mwaka 2018/2019 hadi Shilingi bilioni 285.2 mwaka 2019/2020 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 12.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inafanya mapitio ya mtandao wa barabara nchini ili kubaini mtandao wa barabara za TANROADS na zile za TARURA na hatimaye kufanya maamuzi juu ya mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Barabara. Tunatambua uhitaji huu na tunakwenda kushughulika nalo tunapokwenda kuanda Mpango wetu wa Maendeleo wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tano ambayo ningependa pia kuitolea maelezo kidogo ni hoja ambayo pia imesemwa na angalau na Wabunge zaidi ya asilimia 80, nayo ni kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa njia ya ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ina dhamira njema sana ya kuona Sekta Binafsi inashiriki katika utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya maendeleo na ndiyo maana tulileta sheria hapa, tukafanya marekebisho ya Sheria yetu ya Ubia, Sura 103 na kwa mujibu wa Kanuni ya 29(1) ya Sheria ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kama ilivyorekebishwa mwaka 2018 kwa dhamira njema kabisa, miradi yote inayoibuliwa inatakiwa kutangazwa inapofikia hatua ya ununuzi kwa kumpata mbia wa kuwekeza. Kanuni hii imeainisha kuwa miradi hiyo itatangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpendekezo ya Mpango wetu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/ 2021 ukurasa wa 74, tumeainishwa jumla ya miradi nane ya ubia. Kati ya miradi hiyo ambayo inatarajiwa kutangazwa kwa mwaka 2019/2020 na utekelezaji wake kuanza 2020/ 2021:-

(i) Mradi wa uendeshaji wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam awamu ya kwanza;

(ii) Mradi wa Kuzalisha Dawa za Binadamu (General Pharmaceuticals), kiwanda tunachotarajia kitajengwa Pwani;

(iii) Mradi wa Kuzalisha Bidhaa za Pamba za Hospitali (Medical Cotton Products) ambacho kinatarajiwa kujengwa Mwanza; na

(iv) Mradi wa Kuzalisha Maji Tiba (IV fluids) kinachotarajiwa kujengwa kule Jijini Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi huu, siyo kweli kwamba Serikali haitaki kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Serikali ipo tayari kwa kuanza na miradi hii huku tukiendelea kuandaa miradi mingine kama sheria inavyotuelekeza. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla kwamba, yeyote mwenye Mwekezaji mwenye dhamira njema wawalete wawekezaji hao na Serikali yetu ipo tayari kufanyanao kazi kwa mujibu wa Sheria na kanuni zilizopo na kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Tuko tayari kabisa, tuaomba mtuletee wawekezaji na tutafanyanao kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya sita ambayo pia napenda kuitolea maelezo kidogo, ambayo nayo karibu asilimia 98 ya Waheshimiwa Wabunge wameigusia ni hoja ya mapendekezo kwamba Mpango huu tunaoupendekeza unakuja na mkakati gani wa kutatua tatizo la maji ifikapo mwaka 2020/2021?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Mpango wetu huu yanalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, kusimamia vyanzo vya maji, kudhibiti matumizi ya fedha za maji, ikiwa ni pamoja na ubora wa miradi ya maji. Aidha, Mapendekezo ya Mpango wetu yanalenga pia kuongeza kiwango cha upatikanaji maji mijini na vijijini kutoka hali ya sasa ambapo Jiji la Dar es Salaam limefikia asilimia 85, mikoa mingine asilimia 80, Miji Midogo ni asilimia 64 na vijijini ni asilimia 64.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji pamoja na ubora wa miradi ya maji, Mpango tunaoupendekeza mbele ya Bunge lako Tukufu umeainisha kufanya yafuatayo ambapo kama Serikali tumekuwa tukiyarudiarudia na tunakwenda kuyasimamia:-

(i) Tunakwenda kuendelea na usimamizi wa matumizi endelevu ya maji;

(ii) Kuimarisha uratibu, ufuatiliaji na tathmini katika miradi ya maji nchi nzima;

(iii) Kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini na mijini kwa kukamilisha miradi inayoendelea na kuanza miradi mipya ambayo itapendekezwa ndani ya Mpango tunaokuja nao; na

(iv) Tunakwenda kuimarisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini, yaani RUWASA pamoja na shughuli za mfuko wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tumeyaeleza katika mapendekezo ya Mpango na tunapokwenda sasa kuandaa Mpango wetu, tunakwenda kuainisha kazi zote zinazokwenda kutekelezwa ndani ya mwaka ujao wa fedha ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ningependa kuisemea kidogo ni ile ambayo Waheshimiwa Wabunge pia wameiongelea na kuomba Serikali ifanye marejeo ya vipaumbele vya Kitaifa hususan kwa kuzingatia Sekta ya Maji, Sekta ya Afya na miundombinu ya barabara hasa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji, afya na miundombinu kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wetu wamependekeza ni miongoni mwa vipaumbele vya awali kabisa vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano yaani Mwaka 2016/2017 hadi 2020/ 2021 na Serikali yetu imekuwa ikiwezekeza fedha nyingi kwenye sekta hizi. Maeneo hayo kama ilivyopendekezwa na Waheshimiwa Wabunge yataendelea kuwa ya kipaumbele kwa Taifa kutokana na umuhimu wake katika kuboresha maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, maeneo hayo yameainishwa vizuri kabisa pia katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango tunaokwenda kujanao ukurasa wa 69. Kinachokosekana ni kazi zinazokwenda kufanyika ambazo zitakwenda kuainishwa baada ya kuwa tayari tumeshapokea maoni na ushauri wa Kamati yako ya Mipango tunapokwenda kuandaa Mpango wetu wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021, tutauleta mwezi wa Tatu kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameisema kwa nguvu ni ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi; maboma katika Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya. Serikali yetu inatambua nguvu za wananchi zilizowekezwa katika ujenzi wa maboma haya na ndiyo maana kila mwaka tunatenga bajeti na kuitekeleza kwa asilimia kubwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa na wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kati ya Julai, 2018 na Oktoba, 2019, Serikali yetu imetoa jumla ya shilingi bilioni 104 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya huduma za jamii katika Sekta ya elimu na Afya. Kati ya fedha hizi, shilingi bilioni 38.9 zilitolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma 96 ya Vituo vya Afya na shilingi bilioni 29.9 zilitolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya madarasa 2,392 ya shule zetu za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo, katika Sekta ya Elimu ilitoa shilingi bilioni 35.2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya vyumba vya madarasa 2,760 na matundu ya vyoo 670 kwenye shule zetu za msingi. Tunaendelea kutekeleza bajeti hii kwa mwaka huu wa 2019/2020 ili kuhakikisha maboma yote yanafunikwa na wananchi wetu wanaanza kupata huduma kwenye maeneo haya ambapo waliweka nguvu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo napenda kuisemea kwa ufupi sana ni hoja ambayo karibu asilimia 100 ya Waheshimiwa Wabunge wa upande wa Upinzani walisema kuhusu fedha za miradi ya maendeleo katika Sekta ya Kilimo ambazo zimetolewa kwa asilimia mbili na asilimia 98 hazikuweza kutolewa. Hili naomba nilisemee ili Watanzania waelewe uhalisia, nini Serikali yao inafanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema wakati najibu hoja ya kwanza kabisa kazi nyingi ambazo zimefanyika katika Sekta ya Kilimo; ni vizuri tukatambua kwamba, bajeti ya Sekta ya Kilimo inajumuisha fedha zinazotengwa kwenye Fungu 43 - Wizara ya Kilimo, Fungu 64 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Fungu 99 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi, upande wa Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ya mwaka 2018/ 2019, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Sekta ya Kilimo ilikuwa shilingi bilioni 108.4 na kiasi kilichotolewa siyo shilingi bilioni mbili kama ilivyosemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi wa upande wa Upinzani. Kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni 66.2 ambayo ni sawa na zaidi ya asilimia 61 ya fedha yote ambayo ilitengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusisitiza kwamba ni muhimu tukawa na takwimu sahihi ili tunaposimama kwenye Bunge lako Tukufu tuweze kuwaleleza Watanzania dhamira njema ya Serikali yao ya kuweza kukiinua kilimo chetu ili kiendelee kuchangia katika ukuaji wa pato letu la Taifa. Tunatambua sana umuhimu wa Sekta ya Kilimo na kama Serikali tutaendelea kuweka nguvu yetu kubwa huko.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia kengele imegonga lakini niseme pia hoja ya mwisho ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamesema ni vizuri tukafanya tathmini, yaani tufanye tathmini tunapokwenda kukamilisha utekelezaji wa Mpango wetu wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Tayari Serikali yetu imeanza zoezi hili la kufanya tathmini ya utekelezaji ya Mpango wetu wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wakati tunaanza kuandaa Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo katika utekelezaji wa Dira yetu ya Taifa mwaka 2020/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna tunaloliogopa kwa sababu tunajua tumetekeleza mengi katika sekta zote na tuko tayari kama Taifa kuwaeleza Watanzania, dhamira yetu ilikuwa ni kuiondoa Tanzania kutoka kwenye Taifa la kipato cha chini kwenda kwenye Taifa la kipato cha kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Watanzania wakajua kwamba katika taarifa iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika Juni, 2019 inaainisha nchi nne ambazo zimechangia kukua kwa uchumi wa Bara la Afrika. Naomba nizitaje hizo nchi nne mbele ya Bunge lako Tukufu. Nchi ya kwanza ni Djibouti, nchi ya pili ni Ethiopia, nchi ya tatu ni ya Rwanda na ya nne ni taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenda mengi makubwa, wananchi wanajua, Watanzania wanaelewa na walioko nje ya taifa letu wanaona mengi makubwa yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, na tumekuwa ndani ya nchi nne zilizochangia ukuaji wa asilimia 6.5 wa Pato la Bara letu la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miradi mikubwa tunayotekeleza naomba niwaambie Watanzania wasiwe na wasiwasi, tumejipanga tunaweza kukusanya mapato yetu wenyewe, tu natekeleza miradi mingi. Miradi ya afya tunatekeleza; zaidi ya hospitali 67 tumejenga, hii ni kwa ajili ya wananchi wenyewe. Zaidi ya vituo vya afya 352 tumevijenga. Mwaka huu tunakwenda kujenga zaidi ya hospitali nyingine 19 za halmashauri zetu. Hii yote ni kuwafikia Watanzania, ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanafikiwa na maendeleo kama ambavyo sisi viongozi wao na viongozi wetu wa kitaifa wanavyotuelekeza kuyatenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na jambo moja ambalo tumekuwa tukilisisitiza kwa muda mrefu lakini linarudiwa rudiwa sana kutamkwa katika Bunge lako tukufu. Hoja yenyewe ni pale ambapo Kambi Rasmi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja.

MWENYEKITI: Malizia tu Mheshimiwa, nakuongezea dakika tano.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni pale ambapo Kambi Rasmi ya Upinzani inaposema Seriakli yetu inavunja Katiba kwa kutokuleta sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango. Leo nimeongea taratibu sana na nimekuwa mpole sana ili niweze kueleweka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba niseme, Serikali yetu imekuwa ikiheshimu Ibara inayotajwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyoweka sharti ya kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa kufanya yafuatayo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tunalishukuru Bunge lako Tukufu, mwaka 2015 Bunge letu lilipitisha Sheria ya Bajeti Sura 439 ambayo inasimamia uandaaji, uidhinishaji, utekelezaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali. Kwa hiyo, hiyo ni sheria ya kwanza inayosimamia utekelezaji wa Mipango ya muda mrefu na Mipango ya muda mfupi inayopangwa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kila mwaka Serikai yetu huwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu Muswada wa Sheria ya Fedha unaobainisha vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyotumika kugharamia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka husika. Naomba tutambue mpango wa maendeleo unatafsiriwa kwenye bajeti ya mwaka husika. Kwahiyo sheria zinazoletwa kwenye kutekeleza bajeti ya mwaka husika ndiyo sheria zinazosimamia utekelezaji wa mpango ule wa mwaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kila mwaka Serikali yetu bila kukaidi tumekuwa tukiwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Muswada wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali kwa Mwaka Unaofuata kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Kwahiyo naomba niseme nikisimama kwa nguvu zote kifua mbele kwamba hatujavunja Katiba wala sheria yoyote ndani ya nchi yetu kwa sababu tunasema yale yote tuliyoelekezwa na taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwa Waheshimiwa Wabunge waliotueleza kwamba mpango wetu mapendekezo haya hayakuainisha deliverables au outcomes. Haya ni mapendekezo, tumechukua maoni, tunakwenda kuyafanyia kazi, tutakapokuja na Mpango wetu tutaeleza. Nitoe mfano ambao ulitolewa wakati wa kuchangia kwamba Sekta ya kilimo na likatajwa zao la pamba kwamba hatuna deliverables kama Serikali yaani tunakwenda tu hatujui tunaelekea wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua Mpango wa Maendeleo wa mwaka huu tunaoutekeleza ukienda ukurasa wa 86 kwenye kilimo cha kahawa na pamba imeainishwa wazi wazi wapi tupo na wapi tunaelekea. Kwahiyo naomba niseme tumejipanga vizuri, Serikali ya Awamu ya Tano inaongozwa kiuadilifu kabisa na tunaandaa mipango yetu inayotakiwa kwa ajili ya utekelzaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe tena kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/2021 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. Aidha nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wetu tusisite kuendelea kutoa maoni na ushauri wa kuboresha Mpango wetu huu kwani sasa kazi ndiyo imeanza; tunaenda kutekeleza yale yote ambayo mmetuelekeza. Siku zote kama Wizara/ Serikali tunathamini sana maoni, ushauri na mapendekezo yenu. Tuko tayari kuyapokea muda wowote. Kama nilivyoainisha hapo awali, Serikali itazingatia maoni na ushauri wenu wote lakini bila kuvunja sheria na kanuni za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika dhamira yake ya kujenga Tanzania mpya, Tanzania ya kipato cha Kati, Tanzania ya viwanda. Yanawezekana, tumeanza kuyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuwahimiza wananchi wetu kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kujiletea mabadiliko chanya katika maisha yao na Taifa letu kwa ujumla lakini bila kusahau kwamba hakuna taifa ambalo liliwahi kuwa huru bila kuwa na mapato yake imara ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Watanzania wanaponunua waombe risiti na wale wanaouza waweze kutoa risiti ili tuendelee kukusanya mapato ya Taifa letu. Aidha, mwisho kabisa natoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kwa amani na salama kabisa katika uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa tarehe 24, Novemba 2019 kwani uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio msingi imara wa uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2020 japo umeshaonesha kuna green light kwa chama kile kile cha kijani kuendelea kufanya vizuri. Tuendelee kusimama imara tunakwenda kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya naomba nikushukuru tena na naomba kuwasilisha. (Makofi)