Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja zetu za maazimio mawili. Kwanza, niseme naunga mkono hoja za maazimio yote mawili ambayo ni Azimio la Nishati ya Jua na Azimio la Mkataba wa Kimataifa wa FAO.
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia zaidi Azimio hili la Mkataba wa Kimataifa wa FAO. Nianze tu kwa kusema kwamba, Azimio hili linahusu sana vipengele vitatu, ambapo kimojawapo kinahusu illegal, ambayo ni uvuvi usiozingatia sheria na cha pili ni unreported na cha tatu ni unregulated. Sasa katika hiki cha tatu cha unregulated fishing, niseme tu kwamba, katika suala zima la udhibiti hatuwezi tukaepuka kufanya resource assessment, kama nchi.
Mheshimiwa Spika, huwezi ukadhibiti kama hujui una kiasi gani cha rasilimali au aina gani ya rasilimali ya mazao ya bahari. Kwa hiyo, naomba sana Serikali, katika kutekeleza suala zima la udhibiti, iweke nguvu zake katika utafiti ili kusudi tuweze kujua ni kiasi gani ambacho tunacho katika bahari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo hoja na dhana tofauti tofauti katika suala hili. Kwa sababu kuna wengine ambao wanasema kwamba, aina kubwa ya samaki bahari yetu kuu ni jodari; na hawa jodari wana-move sana, wana-move faster, hawakai katika eneo moja la nchi yetu. kwa hiyo siyo wetu. Pia, wanasema kwamba ufanyaji wa resource assessment ni kitu kigumu sana, lakini mimi niseme tu kwamba hii siyo hoja kubwa sana kwa sababu hata kama tutakuwa tumemsikia vizuri mchangiaji aliyetangulia, ametueleza wazi kwamba asilimia 70 ya jodari inatokea Mafia, katika eneo la Kitutia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kwamba hawa samaki ni wetu na tuna kila sababu ya kufanya resource assessment. Hata ukiangalia katika mbuga yetu ya Serengeti, utaona kwamba wale nyumbu, pundamilia na wanyama mbalimbali huwa wana-move kutoka eneo letu la Tanzania na wanaenda Kenya, lakini resource assessment huwa inafanyika. Tunajua tuna kiasi gani cha nyumbu, tunajua tuna kiasi gani cha pundamilia na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili suala naomba Wizara isilikwepe, itilie maanani, iwezeshe vituo vyetu vya utafiti (TAFIRI) na hata Chuo chetu cha Mbegani ili waweze kushirikiana kufanya resource assessment, ndipo tutakapoweza kudhibiti vizuri.
SPIKA: Mheshimiwa Anastazia, nilitaka kukwambia tu, hawa nyumbu ambao wanazunguka Kenya, Masai Mara kurudi Tanzania na kurudi Kenya tena, zaidi ya 90% wanazaliwa Tanzania. Endelea tu namchango wako. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa taarifa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naependa nizungumzie ni kuhusiana hasa na faida kubwa ambayo tunapewa na huu mkataba. Tunapewa fursa kubwa sana na hasa kupitia ile United Nations Conversions on the Law of the Sea, ambapo kuna kifungu kimoja ambacho kinazitaka hizi nchi wanachama wahakikishe kwamba wanatumia rasilimali hizi za bahari wao wenyewe na ile ziada ndiyo wanawapa nchi nyingine na hasa kipaumbele kiwe kwa zile nchi ambazo hazina bahari.
Mheshimiwa Spika, hapa napenda tu kusisitiza kwamba Serikali yetu sasa inatakiwa iangalie suala zima la ustawi wa wananchi na hasa kwa kuzingatia upatikanaji wa samaki kama lishe kwa wananchi. Kwa kweli hili ni muhimu sana na hasa ukiangalia kwamba katika nchi yetu matumizi ya samaki ni madogo sana, lakini ni muhimu sana kuliko hata nyama na vyakula vingine. Samaki ni muhimu sana kwa afya, lakini tunatumia kilo karibu saba hadi kumi kwa mwaka na wakati mahitaji hasa yanatakiwa tupate takribani kilo 20 kwa mwaka. Kwa hiyo, tunachotakiwa sasa kufanya ni kuwawezesha wavuvi wetu wadogo waweze kupata hawa samaki kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wapate lishe bora.
Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la Sheria ya DSFA pamoja na kanuni zake. Kumekuwepo na malalamiko ambayo tumeyashuhudia hasa kutoka Zanzibar, kwamba, kulikuwa na kanuni ambayo inawataka wale wavuvi waweze kuleta by-catch katika nchi husika. Wanapokuwa wamevua na kupata wale samaki ambao hawakuwa wamepewa ruhusa yake kuwavua, basi wawalete katika nchi husika. Sasa kilichokuwa kinatokea ni kwamba, wanawaleta wale samaki, halafu wanauza. Kwa hiyo, kilio kwa wavuvi ni kwamba bei ya samaki inashuka na wakati wao wametumia gharama kubwa katika kuvua.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kupendekeza hapa ni kwamba, hii Sheria ya DSFA pamoja na kanuni zake, irejewe ili kusudi suala zima la by-catch pale ambapo tutakuwa tumeziruhusu sasa meli nyingine za nchi za nje kuja kuvua samaki, suala la by-catch liwekewe utaratibu maalum ili kusudi wale wavuvi ambao wanavua karibu karibu waweze kuwapata hawa by-catch angalau waweze kushusha bei ya samaki kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, sheria au ule Mkataba wa UNCLOS unasema kwamba hawa by-catch ni mali ya nchi husika, siyo mali ya wale wavuvi wakubwa. Kwa hiyo, ni makosa makubwa sana wanapokuwa wakileta samaki halafu wanawauza wao wenyewe kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa nisemee, unapofanya regulation au udhibiti, huwezi kuepuka suala zima la kuwa na bandari. Bandari ya Uvuvi ni lazima, lakini vilevile dry-dock, sijui inaitwaje kwa Kiswahili. Dry-dock ni muhimu sana ili kusudi kuweza kuzihudumia zile meli ambazo zinakuja pale. Badala ya kusema kwamba wanaenda nchi jirani, waende Mauritius au waende Kenya, basi wafanyie pale pale matengenezo ambapo inaweza ikahakikisha nchi yetu inapata kipato kikubwa ukichanganya pamoja na tozo za leseni na mambo mengine basi hata dry- dock inaweza ikachangia kukuza uchumi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia, ahsante sana.