Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nami napenda nitoe shukrani kwako mwenyewe pamoja na Makatibu wanaokusaidia katika meza wakati wa kuliongoza Bunge hili Tukufu wakati wa mawasilisho Azimio hili muhimu. Niendelee kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge na kwa kuanzia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati ya Madini kwa wasilisho lake nzuri ambalo kimsingi limeunga mkono karibu kwa asilimia mia moja. Pia niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia na kwa kiasi kikubwa wametoa mapendekezo lakini kimsingi wameridhia kwamba Azimio hili liungwe mkono.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, yako mambo mahususi ambayo yamejitokeza ambayo Waheshimiwa Wabunge wangependa kupata uhakika wa ufafanuzi wa kina. Baadhi ya mambo ambayo ni ya msingi sana ambayo wananchi wangependa kusikia kutoka kwenye Bunge letu Tukufu ni utashi wa Serikali. Napenda niliambie Bunge lako Tukufu kwamba utashi wa Serikali wa kutekeleza Azimio hili ni mkubwa sana na ndiyo maana mmeridhia katika kikao chako hivi leo na sisi kama Serikali baada ya Azimio kuridhiwa na Bunge sisi ni kwenda kutekeleza mara moja. Kwa hiyo utashi wa kiserikali upo, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wanaotusikiliza.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na matumizi ya solar, baadhi ya vyanzo vya nishati hapa nchini ni pamoja na rasilimali ya solar. Tunavyo vyanzo vingi sana vya kuzalisha umeme, kama ambavyo mnafahamu tuna vyanzo vya rasilimali gesi, tuna vyanzo vya rasilimali maji, makaa ya mawe, upepo na kadhalika, lakini pia solar.

Mheshimiwa Spika, kulingana na tafiti ambazo zimeshafanywa, na nimeshukuru sana baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutaka kujua mikakati. Mkakati wa kwanza uliokwishafanyika ni kufanya utafiti wa kina na kubaini uwezo uliopo wa kuzalisha nishati ya solar. Tafiti zilizofanywa mpaka kuishia mwaka 2015 zinaonesha Tanzania tunaweza tukazalisha umeme wa solar kufikia mpaka megawati 1,000.

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sana, Tanzania tuna potential kubwa ya mionzi ya jua. Potential tuliyonayo sisi ni kilowatt-hours 4 mpaka 7 kwa mita za mraba kwa siku ambapo kipimo cha kimataifa ni kilowatt-hours 3.97, kwa hiyo tuko juu sana kwa maana ya rasilimali ya jua tuliyonayo. Lakini katika mwaka pia Tanzania tunaweza tukapata mionzi ya jua mpaka takribani ya saa 2800 mpaka saa 3500 kwa mwaka kwa hiyo vyanzo vya kuzalisha umeme wa solar ni vingi.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kutoa taarifa hiyo ili kuwapa uhakika kwamba baada ya azimio hili kupita na matarajio tuliyonayo ni kwamba Serikali tunakwenda kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwepo na umeme wa solar hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine limeelezwa kwamba pengine ni muhimu kutekeleza mradi huu kuliko Bwawa la Julius Nyerere. Nataka niseme mkakati wa Serikali ni kuzalisha umeme mchanganyiko kwa kutumia rasilimali zote tulizonazo. Ni kweli zipo tofauti kutoka chanzo kimoja kwenda kingine lakini nataka niseme, chanzo cha kwanza kabisa kwa unafuu katika kuzalisha umeme ni umeme wa maji ambao unatumia shilingi 36 kuzalisha uniti moja ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na umeme wa pili unaofuata kwa unafuu ni huu umeme wa solar ambao wenyewe utazalisha uniti moja kwa Shilingi ya Tanzania 103.28, kwa hiyo bado nao ni wa nafuu. Lakini pamoja na hayo bado tunaona ni jambo la busara kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mchanganyiko ndiyo maana tunaendelea kuzalisha pia vyanzo vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunasema, pamoja na mambo mengine, unapotumia umeme wa solar unakabiliana kwa hatua ya juu sana na uharibifu wa mazingira, lakini pia usimamizi wake nao ni mwepesi na kwa sababu vyanzo tunavyo, rasilimali ya kutosha, na tumejipanga kwa ajili ya kutekeleza jambo hilo tunadhani azimio hili likipitia itachangia kwa kiwango kikubwa sana kuzalisha umeme wa solar na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kwa sasa katika Gridi ya Taifa hatujaweza kuunganisha umeme wa solar ingawa tunao umeme wa off-grid katika maeneo mtambuka nje na Gridi ya Taifa chini ya megawatt tano. Kwa hiyo mkakati wetu ni kuzalisha walau megawatt 1,000 za umeme wa solar nazo ziingie kwenye Gridi ya Taifa, na ni kupitia azimio hili likipitishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo ni muda mwafaka sana sasa kukubali azimio hili ili tuingize umeme wa solar katika Gridi ya Taifa na kuchangia ipasavyo katika kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge Ruth alisema tulisaini mwaka 2015, ninapenda niweke sahisho dogo tu; sisi tulisaini mwezi Novemba, 2016. Hata hivyo, mikakati ambayo Mheshimiwa Mbunge alipenda kuona tumechukua ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza ni kuweka mpango wa kuzalisha umeme wa solar kwa miaka 30 ijayo ambao tumeweka walau zaidi ya megawati 1,000. Lakini mkakati wa pili ni kuendelea kutafuta fedha; napenda kuishukuru sana Serikali, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 kupitia Mpango wa Umeme Vijijini, Serikali ilitenga shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kuwawezesha wazalishaji wadogowadogo kuzalisha umeme wa solar kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini. Hii ni hatua kubwa sana kwa Serikali ilichofanya katika hatua za kwanza za mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba rasilimali ya jua nayo inatumika kwenye kuunganishia umeme wananchi.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ni kwamba bado tunaendelea kupata fedha kwenye makampuni na mashirika ya kimataifa. Benki ya Dunia katika mwaka huu wa fedha pia imetoa dola milioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini. Na hii ni hatua kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wadogowadogo kuweza kuzalisha umeme huu wa solar ili nao uweze kutumika katika maeneo ambako Gridi ya Taifa haijafanikiwa kupita; hii ni mikakati ambayo Serikali inaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ambayo Serikali inafanya katika eneo hili ni kuhakikisha kwamba wazalishaji wadogowadogo wa Tanzania, hasa binafsi nao wanashiriki katika kuzalisha umeme wa aina hii. Mwaka jana mwezi Oktoba tulitangaza kwa wazalishaji wadogowadogo, na hasa Watanzania, ili waanze nao kuzalisha umeme huu wa solar walau kuanzia megawati 50 mpaka megawati 250. Taratibu zinazofanyika sasa ni kukamilisha uchambuzi ili kuwapata wakandarasi wa ndani ili nao waweze kuzalisha umeme huu. Huu ni mkakati muhimu sana shirikishi ambao Watanzania pia tunawashirikisha.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine mahususi katika eneo hili, kama ambavyo nimeeleza, ni kuhakikisha makampuni ya Kitanzania yanashiriki. Hivi sasa – kwa kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Tibaijuka – yako makampuni zaidi ya saba ya Watanzania; yupo Lex Energy, yupo Enzora, yupo Baraka, yupo ITOZ, yupo ZOTI, yote hayo ni makampuni ya Watanzania wadogowadogo na wanashiriki katika kuzalisha umeme mdogomdogo na kusambaza kwa Watanzania. Kwa hiyo, ushirikishwaji wa Watanzania uko palepale.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bado kama Serikali tunawahamasisha Watanzania waendelee kushiriki kwa kiwango kikubwa sana katika kuzalisha umeme huu wa solar ili kuweka mchango mkubwa kwa ajili ya matumizi, lakini kujenga sustainability kwa Watanzania hata kwa miaka mingi ijayo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo niliyosema katika eneo hili, lakini ningependa tu kusema kwamba mkakati mwingine tumetenga maeneo. Yapo maeneo mahususi sana ambayo ni muhimu na yanaweza kuzalisha umeme wa jua. Baadhi ya maeneo tunayo hata hapa Dodoma, eneo la Zuzu linaweza kuzalisha megawati 50 mpaka 100; eneo la Kishapu kule Shinyanga, megawati 150 mpaka 250; eneo la Mkwese kule Manyoni, Singida megawati 100 mpaka 250 na eneo la Same kule Kilimanjaro nayo yanaweza kuzalisha umeme. Haya maeneo tumeyaainisha na kuyatenga kwa ajili ya kuzalisha umeme wa solar.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, hii ni baadhi ya mikakati tu tuliyochukua kuhakikisha kwamba umeme huu unanufaisha hasa rasilimali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa manufaa; pamoja na kwamba kwa sasa tunaomba kuridhiwa, lakini kwa vile tulishasaini mkataba huu yapo manufaa ambayo Serikali ilishaanza kuyapata. Hivi sasa ninapongea wapo Watanzania ambao wameshaenda kupata ufadhili wa ISA ambao wanakwenda kusoma kwa level ya PhD kwa ajili ya masuala hayahaya ya solar ili waweze kutoa mafunzo kwa Watanzania wengine. Na bado kuna nafasi ambazo tutaendelea kuzipata kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa levels za chini, kati na juu ili Watanzania wengi waweze kupata elimu hii na kuweza kuwafundisha Watanzania wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaposema tutakuwa na umeme mwingi hapa nchini, umeme mwingine unatakiwa utokanae na huu utaratibu wa solar. Na tuna mpango huo kwa sababu unapokuwa na umeme wa kutosha na mchanganyiko, hata inapotokea dharura katika vyanzo vingine bado unaweza kuendesha nchi bila kuwa na mashaka yoyote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utaratibu huu wa ISA hadi sasa mwaka jana tulishiriki kwenye mkutano na ISA ime- commit kwa mwaka wa fedha ujao kutoa takribani Dola za Marekani milioni 385 kwa nchi yetu, na nchi yetu imekuwa- committed pesa nyingi kuliko nchi zote duniani ambazo zimeshiriki kwenye hii ISA, kwa hiyo ni mafanikio makubwa endapo Serikali yetu itaridhia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu yaliyosemwa ni mengi, itoshe tu nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kweli kwa michango yenu mizuri, lakini Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda kwa kutumia umeme mchanganyiko. Na mikakati na malengo yetu ni kufikisha megawatt 10,000 mwaka 2025 na kuwapelekea Watanzania umeme pote wanapokaa mijini na vijijini kwa zaidi ya asilimia 85 na kupeleka Gridi ya Taifa maeneo yote ya pembe nne za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.