Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi na mimi nichangie Azimio hili la kumpongeza Mheshimiwa Rais. Kwa vile tumeamua kwenda na utamaduni huu wa kumpongeza Mheshimiwa Rais, basi niombe hasa Baraza la Mawaziri wamshauri mambo ambayo yeye mwenyewe moja kwa moja yuko responsible kuyatekeleza, wamshauri hilo ili isije ikatia doa hizo sifa nyingi ambazo wanampatia.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI na mpaka leo tunavyozungumza pamoja na joto kali la matatizo makubwa yanayojitokeza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mpaka leo Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hatujasikia kauli yake juu ya Uchaguzi wa Serikali za uchaguzi wa Mitaa. Kwa hiyo mumshauri kwa sababu mwisho wa siku Wizara zenu ninyi Mawaziri zinakwenda vizuri lakini yeye Wizara yake imesua sua na kuna doa kubwa la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikukumbushe tu...

SPIKA: Mheshimiwa Salome kuna taarifa Chief Whip amesimama hapa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
naomba kumpa taarifa mchangiaji wa Azimio hili zuri sana la kumpongeza Rais wetu Dkt. John Magufuli kwamba Ibara ya 34 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa madaraka Mheshimiwa Rais kukasimu majukumu yake kwa Baraza lake la Mawaziri na watendaji wengine ambao watamsaidia kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hilo limefanywa vizuri sana na Waziri aliyekasimiwa madaraka hayo, Waziri wa TAMISEMI, ndugu yetu Mheshimiwa Selemani Jafo na hivi tunavyoongea Watanzania wote ni mashahidi, Mheshimiwa Selemani Jafo ameshafanya kazi yake ya kueleza kila kilichojiri katika uchaguzi huu, taratibu zilizotakiwa kufuatwa na maamuzi ya Serikali katika jambo hilo. Kwa hiyo kuendelea hapa kumng’ang’ania Mheshimiwa Rais, kwanza pia ni kuvunja kanuni ya kiutaratibu, kanuni 64(1)(c) kinachotupa mwongozo wa kuzungumza masuala na mwenendo wa Rais katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba unapokea taarifa hiyo?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei amesema mwenyewe kwamba amekasimu madaraka kwa Mheshimiwa Jafo na sisi Vyama vya Upinzani Tanzania nzima hatujaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na Serikali kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa hiyo tunahitaji Waziri mwenye dhamana atoke atoe kauli juu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa Baraza la Mawaziri wamkumbushe Mheshimiwa Rais, hivi tunavyoongea tangu 2015 tumekuwa tukijadili bajeti humu ndani na kupitisha, Wizara karibu zote hazijapelekewa angalau asilimia hamsini ya bajeti yake, hiyo inamaanisha kuna mdodoro mkubwa wa uchumi…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …na maendeleo kwenye nchi yetu. Mumkumbushe Mheshimiwa Mheshimiwa Rais kwamba tunahitaji…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …sisi Wabunge ni wawakilishi wa wananchi tunayoyaleta ni mapendekezo ya wananchi…

SPIKA: Mheshimiwa Salome…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …pesa zipelekwe kwenye hayo maeneo ili wananchi waweze kupata maendeleo.

SPIKA: Mheshimiwa Salome kuna taarifa uipokee.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Getere nimekuona.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Salome anayeongea unajua kuna vitu vingine unaongea kwa kukariri makaratasi. Hivi kama kweli hela haziendi majimboni, haziendi kwenye halmashauri kwenye mikoa, hivi haya mambo yote ambayo yanayotajwa barabara za lami, hospitali, shule, na vitu vingine, vitu vyote vinavyotajwa hapa vinafanya biashara gani? Hivi labda kuna hela zinatoka mbinguni zinaenda kufanya kazi ya maendeleo kwenye maeneo hayo au zinatoka wapi?

SPIKA: Taarifa inakwambia Mheshimiwa Salome tangu uwe Mbunge kuna mshahara unaodai, mbona Magufuli amelipa mishahara yako yote. (Makofi/Vigelegele)

Ndiyo taarifa anayoitoa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Baraza la Mawaziri na Wabunge wa CCM wamkumbushe Mheshimiwa Rais, kuna mambo yanaendelea ndani ya nchi hii ambayo ni very serious, kuna watu wanauawa kwenye nchi hii, kuna watu wamepotea kwenye nchi hii, mpaka leo Mheshimiwa Tundu Lissu alipigwa risasi, hatujasikia kauli yake juu ya matatizo yanayoendelea kwenye nchi hii, mnapompongeza inamtia doa Mheshimiwa Rais Mwenyewe, wamkumbushe tunahitaji kusikia kama Rais…

SPIKA: Mheshimiwa Salome umetumia neno…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba tusikilizane. Mheshimiwa Salome umetumia neno kuna watu wanauawa, kidogo ni neno hatari katika nchi hii, Watanzania wakisikia maneno kama hayo basi ni vizuri uka-qualify kidogo.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima kuna Diwani wetu anaitwa Lenwa anaishi kule Morogoro, iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba ameuawa na watu wasiojulikana. Kwa heshima na taadhima, Mheshimiwa Mawazo aliuawa na kesi yake mpaka leo ipo mahakamani, hatujapata hatima ya kesi yake na watu hao…

SPIKA: Mheshimiwa Salome unajua kabisa jambo ambalo lipo mahakamani haliruhusiwi kujadiliwa hapa.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Ndiyo nasema Mheshimiwa…

SPIKA: Tuongee mengine siyo ya Mahakamani.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, sawa. Naomba niendelee; katika nchi hii kuliwahi kutokea saga la makinikia na Mheshimiwa Rais alikuwa mbele sana kusimamia saga hii na sheria zililetwa tukapitisha hapa Bungeni kwamba hakuna jambo lolote litafanyika mpaka Bunge hili lipate habari. Tumesubiri kwa muda mrefu wananchi wangu wa Shinyanga wanasubiri Noah, tulichokipata leo ni kauli ya Mheshimiwa…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …amekuja na kampuni yake ya Twiga, tunataka kujua mustakabadhi ya kesi ya makinikia…

SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, Mheshimiwa Salome, kuna taarifa. Mheshimiwa Mlinga.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …imefikia wapi ili tumpongeze Mheshimiwa Rais.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Naomba tusikilizane, Mheshimiwa taarifa yako iwe kwa kifupi.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza, suala la makinikia siyo dogo kama anavyolifikiria yeye. Katika chama chao michango tu ya Wabunge zaidi ya milioni 300 mpaka leo vikao vinakalika usiku na mchana bado haijapata jawabu, michango ya Wabunge imeenda wapi? Kwa hiyo suala la makinikia siyo dogo kama anavyolifikiria yeye, waanze kwanza na michango ya Wabunge.

SPIKA: Mheshimiwa Salome, bado muda uko kwako, malizia tu maana naona kuna nusu sekunde tu hapo.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie Mheshimiwa Mlinga kwa taarifa yake siipokei na mwisho kabisa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …wakati mnaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, naomba mumkumbushe nchi hii ni nchi ya vyama vingi na kila chama kina haki ya kufanya siasa ili kiweze kujiendeleza na kukua.

SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshalia.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa muhimu sana.

SPIKA: Tunahitaji kufanya mikutano ya hadhara ili tushindane kwa hoja na siyo kushindana kwa…

SPIKA: Kengele imeshalia Mheshimiwa Salome.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Mwenyezi Mungu akubariki. (Makofi)