Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mwanakwerekwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia leo kuweza kuwasilisha ripoti zetu mbili hizi, lakini pia nikushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Spika kunipa fursa hii na nitangulie kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati kwa kazi nzuri ambayo wamefanya na leo wameweza kuwasilisha taarifa hizi hapa kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina mambo mawili tu ya kuchangia kwenye Kamati zetu mbili hizi na la kwanza ni suala la bandari. Suala la bandari tukichukua kumbukumbu nyingi ambazo zimepita huko nyuma ni jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Rais alitilia mkazo na nguvu nyingi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba bandari inafanya kazi zake kwa weledi. Pia Mheshimiwa Waziri Mkuu na yeye alichukua jitihada hizo ili pia kuhakikisha kwamba bandari inafanya kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari ni uchumi wa nchi katika Taifa letu ama Taifa lingine lolote lile duniani. Leo ukiangalia Dubai ukiacha masuala ya mafuta jambo kubwa ambalo wanalitegemea katika kuendesha nchi yao ni bandari na wanapokea mizigo mingi kutoka sehemu mbalimbali na kusafirisha mizigo mingi na kuongezea pato lao la Taifa kwa nchi yao. Kwa hiyo ni muhimu na sisi sasa kuona kwamba bandari ni sehemu ya kuweza kukuza uchumi wa nchi yetu na kuonekana kwamba ni mahali pazuri pa kuweza kukusanya mapato ili kuleta ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu kwa mujibu wa taarifa yetu ambao tumewasilisha hapa toka mwaka 2010 mpaka mwaka 2019 bandari inahangaika kuweka mifumo ya kieletroniki kwa ajili ya kukusanya mapato na kupatikana uhalisia ni mapato kiasi gani ambayo yanapatikana. Gharama kubwa ambayo imetumika zaidi ni kwamba zaidi ya bilioni 57 zimeshatumika kwa ajili ya kuweka hiyo mifumo lakini bila mafanikio. Sasa tuombe kwamba Serikali kama nilivyotangulia kusema Mheshimiwa Rais alifanya juhudi kubwa, lakini katika eneo hili la bandari mpaka leo kwenye masuala haya ambayo ni muhimu ya ukusanyaji wa mapato hayajakamilika ili kupata ufumbuzi wa mfumo sahihi wa kuweza kutoa takwimu sahihi na mapato sahihi ambayo yanakusanywa kwenye bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama ambavyo Kamati imeshauri naona sasa ifike mahali kwamba bandari iweze kufikia mwisho kwa ajili ya kuweza kuokoa fedha za walipa kodi ili kuweza kuweka mifumo sahihi na ambayo itaweza kutoa takwimu sahihi za mapato yanayopatikana katika bandari yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nimekusudia kuchangia leo na nilimwona Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa muda si mrefu na nina imani yupo na Naibu Waziri yupo. Kuna jambo ambalo ni muhimu kulielekeza kwake Mheshimiwa Waziri wa Fedha na jambo hili linahusiana na Shirika letu la Ndege ambalo mara ya mwisho katika ukaguzi wa mwisho ambao umefanyika 2018/2019, Mkaguzi ameonesha tahadhari ya Shirika letu la Ndege kwenda kwenye hatari ya kufilisika kama madeni ambayo yapo hayatalipwa. Sasa Serikali imechukua jukumu la kwamba watalipa hayo madeni ili kuhakikisha kwamba Shirika linafanya kazi zake upya na kutengeneza faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye yupo hapa kwamba hii commitment ambayo Serikali imekubali kuchukua juu ya Shirika la Ndege basi itekelezwe kwa wakati ili shirika lisije likapata matatizo kama yale ambayo yametokea huko awali na ukizingatia sasa hivi uwekezaji ambao umeshafanyika ni zaidi ya trilioni moja na nusu kwa ajili ya kulirudisha shirika hili ili liweze kufanya kazi kwa mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mwaka 2016/2017 na 2017/2018 nilitoa ushauri hapa kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye alileta hoja mezani na nikasema kwamba kuanzishwa shirika ni jambo jema na tukakubali kwamba shirika hili litasaidia nchi, lakini tukatoa mawazo kwamba tunahitaji uweledi kwenye hili shirika. Najua kwamba wapo wataalam kwenye hili Shirika la Ndege Tanzania wanafanya kazi vizuri lakini utaalam wao una kikomo yaani unafika mahali lazima upate usaidizi kutoka kwa wataalam ambao wamebobea katika biashara hizi za ndege ili kulinyanyua shirika liweze kufanya kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, leo ukiangalia shirika letu la ndege la Air Tanzania limeshindwa hata kuanzisha safari za kutoka aidha, Dar es Salaam- Nairobi au Dar es Salaam – Zanzibar – Nairobi mpaka huu muda ambao tunazungumza. Leo Jomo Kenyata Airport ni hub katika Afrika Mashariki katika masuala ya kibiashara iwe ya ndege na mambo mengine, lakini hadi leo shirika letu halijaweza kwenda Nairobi, lakini ukiangalia Kenya Airways wanakuja mara saba kwa siku Dar es Salaam pamoja na Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba sasa tunahitaji wataalam waliobobea zaidi katika masuala haya ili kulifanya shirika liweze kufanya kazi zake kibiashara zaidi na kuweza kuleta faida katika shirika hilo na hasa ukizingatia kwamba mwaka 2017/2018 shirika limepata hasara ya bilioni 10 baada ya tax, lakini 2018/2019 limepata hasara ya bilioni 16. Kwa hiyo badala ya hii hasara kupungua inaongezeka sasa na nature ya biashara hii maana yake leo ukipata hasara bilioni 10, mwakani ipungue ili mwisho wa siku iweze ku-recover ile loss na iweze kutengeneza faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu yeye ndio ambaye alileta hoja ya kulisimamia shirika hili na nina imani kwamba commitment ya Serikali kwamba wamekubali kulisimamia na ili shirika liweze kuendelea vizuri basi, sasa wakati umefika kwa Serikali kufikiria kutafuta mtaalam mbobezi katika masuala haya ya biashara ya ndege ili aweze kulisaidia Shirika la Air Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano wa pili mdogo tu, Air Tanzania imeanza kuja Dodoma na inakuja mara mbili kwa siku, lakini baada ya kuanzishwa hii route ya kuja Dodoma kwa sababu ya potentially ya biashara ya ndege utakuwa leo Precision Air anakuja mara tatu kwa siku wakati mwingine mara nne Dodoma na ndege zinajaa. Sasa wapi tunafeli tuna matatizo wapi ili tuone kwamba shirika tunalisaidia liweze kujiendesha kibiashara zaidi na liweze kwenda kwenye ushindani wa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa badala ya kwamba sisi tulianzisha shirika ili tuweze kupata faida matokeo yake tunatengenezea watu njia kuwafanya watajirike zaidi katika hii biashara na sisi tunabaki kuwa tunawafuata wao nyuma. Kwa hiyo haya ni mambo ambayo yanaonesha kwamba pamoja na kazi nzuri ambayo wanafanya wataalam wetu lakini wanahitaji utaalam wa ubobezi ili kuwatoa hapa waliko kwenda kwenye stage nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru kwa kunipa fursa. (Makofi)