Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia ripoti ya LAAC na mimi pia ni mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 1998 na mwaka 2008 ilifanyika reforms kubwa sana kwenye Local Government na ilitumia fedha nyingi. Reforms hizo zilielekeza kuwajengea uwezo watumishi kwa maana ya Mkurugenzi na timu yake na menejimenti kwa ujumla lakini pia reformshizo ziliwajengea uwezo Madiwani katika kusimamia fedha za Halmashauri zinazoletwa katika Halmashauri zao na reforms hizi zilitumia fedha nyingi kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani kwa kweli imeonesha kabisa kutokuzithamini Local Government kwanza kwa uteuzi tu uliofanyika wa ma- DED tumeona ma-DED walioteuliwa kwa kiwango kikubwa wengi hawana uwezo, hawakutoka kwenye mfumo wa Local Government. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma utaratibu uliokuwa unatumika kutokana na hizo reformszilizofanyika, Mkurugenzi alikuwa anateuliwa ni mtumishi wa Serikali za Mitaa ambaye amehudumu kwa kipindi kisichozidi miaka mitano anaenda kuteuliwa kushika hiyo nafasi. Hii maana yake ni kwamba alitakiwa awe anazielewa Serikali za Mitaa, ajue kusimamia fedha vizuri, aielewe Serikali za Mitaa kwa ufanisi zaidi, lakini sasa hivi watendaji walioteuliwa kwa kweli hawana uwezo wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo yanayosababisha tunaona Local Government leo hata miradi kwanza miradi yenyewe inayotekelezwa vipaumbele vinavyowekwa havifikiwi na wala havifanyiki kwa sababu ya upungufu huo. Pia reforms zile zilijenga uwezo kwa Madiwani, leo Madiwani wetu kwanza hata baadhi ya Halmashauri vikao havikai, hakuna fedha. vikao havifanyiki, Kamati za Fedha hazisimamii ipasavyo hata hizo fedha kidogo zinazopelekwa kwenye Local Government. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tufike mahali kama nchi kama utawala wa awamu fulani unafanya mambo wa kadha wa kadha. Mfano, kama tulifanya reforms kwenye tawala zilizopita huko nyuma, utawala unaokuja hauna budi kurithi na kuhakikisha inaendeleza yale ambayo yaliendelezwa na utawala uliopita na sio kupindisha. Nadhani uzalendo wa nchi hii ni pamoja na kuyaenzi na kuyatekeleza yalifanyika kwenye awamu zilizopita na kuendeleza na si kuharibu ama kufanya ambavyo haitakiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea toka tunaanza Bunge hili na sasa tunaelekea ukomo wa Bunge hili. Tumeeleza jinsi ambavyo Serikali za Mitaa zimenyang’anywa mapato ya uhakika ambayo kwa kiwango kikubwa ndio yalikuwa yanasaidia kuwepo na uhai wa Serikali za Mitaa.

Leo wamenyang’anya vyanzo vya uhakika, mambo hayaendi kwenye Serikali za Mitaa, tutaendelea kuwataka Serikali kuhakikisha kwanza vyanzo vya uhakika kwenye Local Government vinarudishwa, waziachie Halmashauri zikusanye mapato/hizo fedha ili iweze kuendeleza miradi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hiki kitu kinachoitwa force account; Serikali inaisemea sana na kuipigia chapuo, lakini mimi naona kutakuwa kuna shida kubwa sana mbeleni. Hizi force account miradi inayotekelezwa kwaforce account inaenda kutekelezwa kwa kiwango kikubwa na hao mafundi ambao watateuliwa kwa utaratibu unaokuwepo lakini hatuangalii ubora wa majengo yanayojengwa kwa force account. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawataka wasimamizi kwa maana ya Mainjinia wa Wilaya wakasimamie lakini tuna mainjinia wangapi kwenye wilaya moja wakasimamie miradi hii kuangalia ubora wa majengo yanayojengwa? Mainjinia wenyewe hawatoshi, utakuta kwenye wilaya moja labda kuna miradi minne ama mitano inayojengwa kwa force account halafu unataka injinia mmoja kwenye Halmashauri kwa sababu pia tuna upungufu mkubwa sana kwenye Halmashauri, unataka injinia huyohuyo mmoja akasimamie, hivi ufanisi wa miradi hii uko wapi?.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokwenda mbele watakuja kuona miradi ya force account majengo yanaanguka tu hovyo hovyo kwa sababu hayajajengwa kitaalam, hayana usimamizi wa kila siku, tunawaachia hao mafundi sanifu ambao kwa kweli hawakidhi vigezo wanaenda wanazitazama hatuwaachii mainjinia, kwanza hatuna lakini haipati usimamizi wa kutosha kuhakikisha kwamba miradi hii kwa kweli inasimamiwa inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la miradi ya mikakati. Kuna fedha nyingi sana zinakopwa kwa ajili ya miradi ya mkakati. Mfano hapa Dodoma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, zilikuwa dakika tano, ahsante sana.