Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya PAC.Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nafasi ili kuweza kusimama kwa ajili ya kuchangia. Pili, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mingi katika Halmashauri zetu. Miundombinu katika Sekta ya Afya na Sekta ya Elimu tumeona kazi iliyofanyika, tunaipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ambayo nitapenda kusisitiza kama ambavyo tumeweza kuyaeleza katika taarifa yetu, baadhi ya Halmashauri na niseme kwa wingi zaidi ya asilimia 50 kuna maeneo ambayo yamepelekea kuweza kupata hoja za ukaguzi kwa mfano eneo la ku-dispose mali za Serikali kwenye Halmashauri zetu hususan magari chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi hoja zimekuwa zikijirudia mara kwa mara na hazipatiwi ufumbuzi, lakini katika kutafakari kwa kina tumekuja kugundua kwamba yawezekana kuna changamoto hususan katika suala zima la sheria ya ku-dispose mali hizi, kwa sababu inachukua muda mrefu kwanza kukamilisha mchakato huu wa ku-dispose na hata Halmashauri wanapoanza initiative za kuandika barua kwa ajili ya kuomba kibali, kibali kinachelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika,vile vile tumekuja kugundua kwamba pengine Halmashauri kwa sababu wao ndio wanapaswa kumgharamia Mhakikimali Mkuu wa Serikali au timu yake inayokuja kufanya assessment, basi Halmashauri wanaona hakuna sababu kwa sababu wanagharamikia baada ya kuuza fedha zinaenda Hazina na sio lazima kwamba zirudi kwa ajili ya kusaidia ama kununua gari nyingine kwa ajili ya ku-replace kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipendekeze kwamba katika kipengele hiki ni vizuri tukaangalia kama kikwazo ni sharia, basi tuone namna gani ambavyo unaweza ukaletwa Muswada kwa ajili ya kurekebisha sheria hii ili kuwaondolea mzigo mkubwa Halmashauri ambao wanaamua sasa kuacha magari yanakuwa grounded na Serikali inaendelea kupata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ya pili ni kuhusu miradi hii inayotekelezwa na force account na hii inatokana na upungufu wa watumishi ambao wapo katika Halmashauri zetu. Serikali naipongeza kwamba wanaonesha jitihada za kuongeza watumishi hususan kwenye Sekta ya Elimu na Afya lakini kwenye upande wa uhandisi bado kasi ya kupeleka/kuajiri watumishi hao ni ndogo kiasi kwamba sasa usimamizi wa miradi hii ambayo inakuwa ikitekelezwa kwenye Halmashauri zetu inakuwa ni shida. Wapo ma-engineer natechnicians ambao wapo mitaani hebu na wenyewe sasa kutokana na umuhimu kwamba Serikali inapeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii basi tuongeze pia idadi ya kuajili wataalam katika maeneo haya ili kusudi tuweze kupima ile value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ukijaribu kuangalia wakati tunatekeleza miradi ya MMEM mwaka 2000/2001, tulikuja kukutana na changamoto hii kwamba tulianza kujenga madarasa kwa wingi maeneo yote nchi nzima lakini kwa sababu usimamizi ulikuwa ni mdogo tumejikuta kwamba madarasa mengi yaliyojengwa leo hayatamaniki wakati ni muda mfupi. Kwa hiyo, ili tusiendelee kufanya makosa yaleyale ndio maana nashauri kwamba Serikali tuongeze idadi ya kuajiri hususan wataalam katika sekta hii ya uhandisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikielekea kwenye upande wa makusanyo, niipongeze Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI kwamba kwa sehemu kubwa kwa kweli wamefanya kazi kubwa baada ya kupeleka POS 7,227 kwenye Halmashauri zetu. Kupeleka POSni jambo moja lakini pia kukusanya mapato inavyotakiwa ni jambo lingine kwa sababu unaweza ukapeleka POS lakini POS zile wakazi-locate kwenye vyanzo ambavyo sio reliable yaani vyanzo ambavyo havina mapato ya kutosha na zile POS zingine ambazo zimekuwepo na zimekuwa zikifanya udanganyifu zinapelekwa kwenye vyanzo vile ambavyo ndio kuna makusanyo makubwa na kukawepo na leakage kama ambavyo tumefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kama ambavyo Mbunge aliyechangia Mheshimiwa Komanya alisema kwamba ni afadhali zile POS ambazo zilikuwa zikitumika ambazo udhibiti wake sio rahisi basi zitolewe na Halmashauri hizi kwa sababu bei ya kununua POS hizi ambazo sasa zimedhibitiwa na kisasa bei imeshuka karibu kwa asilimia 75, basi walazimishwe kununua hizi POS mpya ambazo ni rahisi kuzidhibiti na hatimaye iwe rahisi sasa kuweza kuzungumza mfumo mzima wa makusanyo ili Halmashauri ziweze kuongezewa makusanyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusisitiza kwenye upande wa stahiki za Madiwani. Tunamalizia muda lakini wapo Madiwani katika maeneo mengi wanadai Halmashauri zao posho zao lakini pia hata makato ambayo yamekuwa yakikatwa kwenye mikopo yao haipelekwi kwenye mabenki lakini pia hata huduma ya bima wamekuwa wakikatwa lakini hazipelekwi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda uliobaki ni mdogo, tuombe kwamba Waziri mwenye dhamana na Serikali waweze kufuatilia kuhakikisha kwamba kwenye Halmashauri Madiwani hawa wasiondoke na madeni, wakati mwingine inakuwa ni ngumu kuweza kuja kudai baada ya kuwa wamemaliza muda wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo ya kuchangia na naunga mkono taarifa hizi za Kamati ya LAAC na Kamati ya PAC. Ahsante sana. (Makofi)