Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya PAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kama Mjumbe wa Kamati ya PAC ambayo kwa takribani kwa miaka minne nimekuwa kwenye Kamati hii. ni lazima niseme wazi kabisa kwamba mabadiliko makubwa yapo katika uandaaji wa hesabu na hoja nyingi zimepungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, na yasema hayo kwa sababu ukipitia hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya umma. Pale mwanzoni kulikuwa na hoja za ukaguzi nyingi sana. Sasa ukiangalia kwa taarifa hii tunayopitia hapa tunazungumzia taarifa ya Mwaka 2017/2018 na msingi wa taarifa hii ni taarifa ambayo inaandaliwa na Kamati ikishirikisha wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa namsikia mzungumzaji mmoja hapa anaanza kuhoji kwamba jambo fulani halipo, jambo fulani halipo. Msingi wa Kamati ni kwamba ni maoni ya washiriki wote na ukitaka kuona hilo limefanyika ni kwamba hata Mwenyekiti ambaye anatoka upande mwingine ndiye ambaye ameongoza vikao hivyo. Kwa hiyo, nataka kutoa wasiwasi kwamba haya ambayo yameingia kwenye taarifa hii ya Kamati ya PAC ni maoni ya Kamati ya PAC na wala siyo maoni ya mtu mmoja kwa sababu msingi wa hoja za Kamati ni hoja za CAG na kama CAG ameleta hoja anaitwa accounting officer au Katibu Mkuu, anapoleta majibu lazima yapelekwe kwa CAG ayaptie apate majibu sasa inawezekana haya unayoyauliza sasa hivi ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanyiwa kazi na CAG ili yarudi tena katika Kamati. Hilo nilitaka kuliweka sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo lingependa kulzingumzia ni juu ya mambo mbalimbali ambayo Kamati yetu imeiona na ambayo kwa kiasi kikubwa Kamati ya PAC imetoa maoni yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite eneo ambalo ni eneo muhimu sana kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA); tumegundua changamoto nyingi sana, Kamati imegundua changamoto nyingi sana sasa hizi kwa kiasi fulani zinaonekana ni changamoto ambazo inaonekana kwamba Serikali haijakusanya mapato kwa kiasi kikubwa sana lakini ukitazama hoja za CAG utaona kwamba kile kinachoonekana katika hesabu za Mamlaka ya Mapato (TRA) ni mambo ambayo yemafanyika kitaalam ambayo pengine yamefanyika kwa makusudi au yemefanywa na watu ambao hawana utaalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja, ni juu ya kodi la zuio (withholding tax); utaona kwamba maeneo mengi inaonekana mapato hayajakusanywa kwenye eneo hilo. Lakini pia yapo maeneo mbalimbali ambayo mamlaka ya mapato yanaonekana hayajafanya vizuri. Mfano, kuna kesi takribani 417 ambazo zilipaswa ziwe tayari zimetolewa maamuzi hazijafanyika mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini ushauri wangu? Najua Ofisi ya Mamlaka ya Mapato (TRA) wanafanyakazi nzuri sana kupitia kwa Kamishina wa TRA na watu lakini naona sasa umefika umuhimu sasa wa kuhakikisha kwamba hoja hizi ambazo zinaonekana Serikali haijakusanya mapato wakati hakuna uhalisia wa mapato basi ziweze kutafutiwa majibu na namna gani wanaweza wakafika hapo ni kuhakikisha kwamba wanakuwa na wataalam wa kutosha ambao wanafanya assessment ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaweza ukamkadiria mtu kwamba kwa mwaka anaweza kukusanya milioni 800 kumbe pato lake ni milioni 200. Hesabu zile zitaingia kwenye Ofisi ya Mamlaka ya Mapato CAG akipitia ataona kwamba TRA hawajakusanya mapato kumbe ni makadirio mabaya ambayo yamefanyika. Mimi nimuombe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha yuko hapa alione hilo wakae na watu wa TRA waone namna ambavyo ukadiriaji ufanywe na watu sahihi kwa wakati sahihi na watu ambao wana taaluma ya kutosha vinginevyo itaoneonekana siku zote kwamba hesabu hizi haziko sawa, Serikali haijakusanya mapato kumbe siyo mapato sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningepanda kulitolea maelezo au kulichangia ni hija ambayo imeonekana kwamba watu wa mfuko wa Bima walitoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Benjamin. Sasa ukiangalia hapa utaona kwamba hapa hakuna hoja ya matumizi mabaya ila no hoja ya kuweka hesabu vizuri kwa maana kwamba hesabu za watu wa National health Insurance hazionyeshi kwamba wamewekeza kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali sasa hivi kuangalia watu wa National Health Insurance wakae na watu wa Wizara ya Elimu kupitia Benjamin pale kuona kwamba hesabu hizi, uwekezaji huu wa National health Insurance utaweza kuwekwa kwenyte vitabu kiasi gani. hilo ndilo ambalo linesemekana ndiyo maana hoja ya CAG imeonyesha kwamba uwekezaji ule hauonekani kwenye vitabu vya wenzetu wa National Insurance kwa sababu wanaonekana mfuko wa Bima ya afya wao mfuko ule hauendi vizuri lakini kama hesabu hizi, kama uwekezaji huu wa ujenzi wa hospitali ya Benjamin ungeweza kuonekana katika hesabu zao pengine wangeonekana wanafanya vizuri sana. Naomba wahusika walisikie hili na waweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kuchangia ni juu ya Shirika letu ya Nyumba; sisi Wajumbe wa Kamati ya PAC tulifanya ziara kutembelea miradi mbalimbali. Tulipata fursa ya kwenda pale Morocco kuangalia ujenzi wa majengo makubwa lakini tulienda Kawe. Sasa kinachoonekana pale ni kwamba watu wa National Housing miradi ile imesimama. Mkandarasi yupo pale site na kila siku analipwa takribani milioni 20, uwekezaji ule umesimama lakini unajiuliza kwanini umesimama? Ndiyo tunaamini na Kamati inaamini kabisa kwamba uwekezaji ule haukuwa mzuri, sasa nii kifanyike?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauari wangu kama Mbunge; kwa sababu ukiangalia kama Serikali itasitisha miradi ile maana yake yule Mkandarasi tutamlipa bilioni 99.99 ni takribani bilioni 100 lakini tayari watu wa Shirika na Nyumba wameshapokea kodi ya bilioni 2.6 sasa nini kifanyike hapa? Waziri wa Ardhi yupo hapa ambae Shirika la Nyumba liko chini yake; hebu wakae chini waangalie namna gani wanaweza kutoka kwa sababu kuendelea kutokuendeleza ile miradi maana yake ni kuipelekea Serikali kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri sana tuangalie waliofanya makosa hawapo sasa hivi, menejimenti iliyopo ni mpya sasa tuangalie kwamba Serikali isiendelee kupata hasara. Miradi ile iko pazuri ukichukulia mfano mradi wa Kawe uko karibia na bahari pale kwa maana tukimalizia majengo pale Serikali inaweza ikapata kiasi kikubwa sana cha pesa na ukianglia unapofanya investment lazima return yake ile ionekane. Sasa pesa ile tumeiweka chini tunatarajia nini maana Mkandarasi yule hawezi kuondoka, ukiondoka maana yake utalipa bilioni 100. Hebu tuangalie namba ya kutafuta pesa miradi ile tuyikwamue itoke hapo ilipo iende mbele zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni juu ya Bodi hizi za kusuluhisha kwa sbabau mwaka jana hapa tulipitisha Sheria kwamba tunaanzisha kitengo pale Wizara ya Fedha kwamba kama umekadiriwa vibaya basi unahakikisha unapeleka malalamiko yako Wizara ya Fedha pale. Ninaushauri mmoja; kuna Bodi hizi ambazo ndizo zinazotatua kesi, naona Bodi hizi hazifanyikazi sawasawa na ndiyo maana bado kuna kesi nyingi sana zinazohusu ukadiriwaji wa mapato. Namuomba Waziri wa Fedha aliangalie hili pengine kama hawana wataalam wa kutosha ili kesi ziendelee na hoja hizi ambazo zimekwama ziweze kuondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni juu ya Kamati ya LAAC; yupo Mheshimiwa mmoja amezungumza hapa kwamba mfumo wa Force account ni mfumo ambao una tija. Ni kweli una tija kwa sababu kwa kiasi kikubwa umeweza kuokoa fedha lakini kitu ambacho nimekiona na ambacho hata halmashauri yangu ya Wilaya ya Kilindi inacho ni kwamba hatuna wataalam, hatuna Mainjinia wa Civil engineering ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni kwamba kama hatuna wataalam, imefika wakati Waziri wa TAMISEMI yupo hapa naomba anisikilize; hakikisha unapeleka wataalam, fundisha wataalam, wapeleke katika halmashauri. Miradi hii lazima iwe na wataalam wa kusimamia vinginevyo thamani ya pesa haitapatikana hata kidogo. Tutasimama hapa, tutasema Force account ni nzuri lakini bila wasimamizi wenye taaluma ya kutosha hatuwezi kufika mbele na wala hatuwezi kufanikiwa. Naomba Serikali ione kwamba ni eneo lenye changamoto kubwa sana ambalo lazima lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia juu ya TBA, mimi ushauri wangu kama Mbunge, naamini kabisa TBA wamefanya kazi nzuri lakini walikuwa wameelemewa na mzigo, nadhani kama Serikali inaweza ikachukua njia iliyo sahihi, wachukue miradi hii ya ujenzi wawapelekee watu wa National Housing waweze kufanya kazi hizo kwa sababu wao wameonekana baadhi ya miradi wanafanya kazi vizuri sana, vinginevyo tutapelekea kuwalaumu, tutawalaumu lakini kumbe wamezidiwa. TBA wamezidiwa kwa sababu walipewa kazi nyingi sana na hili linaonesha wazi kwamba wakiendelea kutopewa kazi hizi basi watafeli hawataweza kufanikiwa kwa sababu Kamati yetu sisi imepitia miradi mingi ikaona kwamba TBA wameshindwa kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kurudia kusema tena kwamba tulipoanza na tulipo ndio ni vitu viwili tofauti, Serikali inakusanya mapato ya kutosha, TRA wanafanya kazi vizuri, lakini waangalie mapengo, waangalie namna ya kuimarisha utendaji wa TRA hususani kwa wataalam wanaofanya makadirio kwa sababu malalamiko ni mengi sana ili tuweze kutengeneza hesabu ambazo ni hesabu sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)