Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia tena kusimama tena katika Bunge lako hili Tukufu, naamini hili ni Bunge la pili kutoka mwisho, lakini namwomba Mwenyezi Mungu anijalie ili nirudi tena katika Bunge lijalo. Pia nawaombea na Waheshimiwa Wabunge wenzangu warudi tena maana si vizuri kujiombea mwenyewe peke yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze taarifa ambazo zimewasilishwa siku ya leo, lakini naomba pia nipongeze michango mizuri ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na hasa Wajumbe wa Kamati ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na hizi Wizara ambazo zimewasilisha leo taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo machache ambayo naomba pia niseme, niweke nyongeza katika maeneo ambayo wenzangu wameyazungumza. Naomba nizungumzie suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri zetu. Nafahamu kwamba Serikali inapeleka pesa katika halmashauri zetu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kupitia force account, hiyo ni hatua nzuri na kwa kweli naomba niipongeze Serikali kwamba ilikuwa na lengo zuri sana kupitia force account.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize suala la uhakiki wa miradi, tunaenda tunatekeleza hii miradi, lakini wakati mwingine pengine miradi inatekeleza kwa haraka sana inakuwa inakosa ubora. Unaweza ukakuta jengo limekabidhiwa kwamba limekamilika, lakini baada ya mwezi mmoja ukienda kuhakiki unakuta tayari lina ufa. Sasa kwa namna nyingine inaonekana kama pesa yetu imekwenda lakini haijafanya kazi kadri inavyokusudiwa. Kwa hiyo naomba sana nisisitize uhakiki wa miradi ambayo inatekelezwa katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusisitiza kwamba mfumo huu ni mfumo mzuri kupitia force account lakini tuwe imara katika kuhakikisha miradi hii inayojengwa, basi hiyo ni miradi yenye ubora. Kama jengo linajengwa basi liwe jengo bora, kama ni kituo cha afya, kama ni madaraja na miradi mingine yote ambayo inatekelezwa katika halmashauri zetu iwe na ubora unaohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze suala la vyanzo vya mapato. Katika halmashauri zetu sasa ni kama vyanzo vinaenda kwa kusuasua, naomba niseme kwamba Serikali ilikuwa na dhamira nzuri sana ya kufuta vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa vinakusanywa na halmashauri na kuleta kwenye Serikali Kuu, lakini kwa lengo la kurudisha pesa kwenye halmashauri ili ziendelee kufanya kazi ilivyokusudiwa. Naomba niseme na jambo hili nimekuwa nikisema lakini hata Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamelisema, kwamba pesa haziendi kwa wakati. Kutopeleka pesa kwa wakati ni kuifanya ile miradi isikamilike na tunapochelewa kupeleka pesa miradi ile inaongezeka gharama za uendeshaji. Kwa hiyo, naomba sana kupitia Bunge lako hili, ni vizuri tupeleke pesa kwa wakati ili halmashauri ifanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna suala la miradi viporo, kwenye halmashauri zetu tuna majengo mengi, majengo mengine nguvu za wananchi wanakuwa wamefyatua tofali kwa lengo la kuanzisha miradi na wakati mwingine ni maagizo ya Serikali kwamba lazima mradi unapokwenda kuwepo na nguvu za wananchi. Hivyo wananchi wanafyatua tofali kwa maana ya nguvu zao, maeneo mengine wanakusanya mawe, wanapeleka mchanga, lakini kukiwa kuna jengo limejengwa jengo halikamiliki kwa ajili ya kukosa pesa ambapo ndio mchango wa Serikali kwenye lile jengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana kupitia Serikali tuhakiki miradi yetu viporo, vinginevyo unaweza ukakuta majengo mengi saa hizi badala ya kufanya kazi iliyokusudiwa wanakaa popo au mengine wanalala mbuzi na mengine yanafanyika mambo ambayo hayakukusudiwa. Kwa hiyo naomba sana niisisitize Serikali yangu na sina shaka kwa kweli na Serikali yangu naamini ni Serikali sikivu, isikie iufanye uhakiki, vile ambavyo tunahakiki watumishi hewa, turudi sasa tuhakiki hata miradi viporo ili tupeleke pesa ile miradi ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba nilizungumze, ni suala la posho za Madiwani, wenzangu wamesema na mimi nafahamu ukiachia kwamba ukiwa Mbunge pia ni Diwani, lakini mimi pia nimekuwa Diwani toka huko nyuma, sasa nafahamu mazingira ambayo wanaishi Madiwani wetu kwenye halmashauri. Hili jambo limesemwa sana na linaposemwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi inaonesha kwamba jambo hili ni la halmashauri zote, Madiwani wetu hali zao sio nzuri, posho zenyewe hawapati kwa wakati, lakini mwingine amesema, Diwani anaweza akaenda amefanya kikao anapomaliza kikao hakuna anachosaini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naanza kujiombea hapa ili nishinde tena niliwaombea na wenzangu, lakini hata wale Madiwani kule pia tunawaombea, sisi hapa tumejaza, tukishajaza per diem, ukijaza Jumatatu per diem mpaka siku ya pili ya tatu hujaona mnaanza kuulizana, hapa nilikuwa nateta na jirani yangu vipi kuhusu utaratibu na naamini jambo hili ni kwa wote tunaulizana. Sasa vile tuone nafsi, lile ambalo sisi tunaliona sio jambo jema hata wenzetu kule haliwapendezi. Kwa hiyo, tuhakikishe Madiwani wetu wanapata pesa zao kwa wakati, wanadai na inaonekana wengine mpaka tutamaliza Mabaraza hata haki yao hawataipata. Sasa jukumu la kuhakikisha wanapata haki zao ni sisi tuliomo humu ndani, tuhakikishe wale wanapata haki zao kama vile ambavyo sisi leo tunaanza kuuliza utaratibu utakuwaje na ndio maana nimesema hili ni Bunge la pili kutoka mwisho, kwa hiyo…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sikudhani Chikambo kuna taarifa Mheshimiwa John Heche.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa kwamba ni kweli kwamba Madiwani hawana pesa na hawalipwi, lakini kuna baadhi ya Ma-DC wanaona kwamba Madiwani wakilipwa ni fever na sio haki yao, mfano mzuri ni DC wa Gairo anaona kwamba Madiwani wakilipwa sio haki yao na wanafanya kazi. Kwa hiyo anachozungumza ni sahihi Madiwani wanahitaji kulipwa pesa zao.(Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sikudhani unapokea taarifa hiyo.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia. Kama nilivyosisitiza upande wa Madiwani, lakini pia tunapozungumza halmashauri tunaanzia ngazi ya kijiji hata Wenyeviti wetu wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji tumekuwa tukiyazungumza sana. Hii miradi tunayoizungumza hapa inaenda kutekelezwa kwenye vijiji, lakini unamkuta Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji hapati chochote, hawezi kufanya kazi kwa sababu hakuna motisha yoyote. Kwa hiyo, niombe sana tunapowafikiria Madiwani lakini pia hata viongozi wetu wa ngazi zile ambazo ndiko tunakoenda kufanya kazi ni lazima tuwafikirie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niyaseme hayo, lakini kwenye suala hili la posho nimalizie kwenye matatizo ambayo yanajitokeza kwenye halmashauri. Tunafahamu kwamba miradi yote ambayo tunapeleka kwenye halmashauri wahakiki wa miradi ni Kamati ya Fedha, ndio inatakiwa ikahakiki miradi kwa niaba ya Baraza zima, lakini inasikitisha Kamati ya Fedha mnaweza mkakaa hata miezi mitatu haijaenda kwenda kuhakiki miradi, sasa nani atajua ubora, nani ataleta changamoto kwenye halmashauri, hiyo inaleta tabu. Wakati mwingine inaonekana halmashauri zingine wanapeleka Madiwani au Kamati ya Fedha kwenda kuhakiki ni kama funika kombe mwanaharamu apite, kuna utaratibu wa kutaka ile Kamati ikahakiki, lakini unaiambia Kamati ya Fedha iende ikahakiki siku moja, hivi kweli itapitia miradi yote ikamaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara itoe tamko kwa ngazi ya halmashauri, ni vizuri kama haya mambo yako kwa mujibu wa Katiba au kwa mujibu wa sharia, basi tuagize halmashauri wahakikishe wanatekeleza kwa mujibu wa utaratibu kwa sababu kupeleka pesa ni hatua nyingine, lakini pia hata kuhakiki ubora wa miradi yetu ni jambo lingine. Nimeona niliseme sana kwa sababu mimi ni sehemu ya Madiwani, naona madhara yanayojitokeza kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo hata wenzangu wamelizungumza ni suala la TARURA. Naomba niipongeze Serikali wazo lilikuwa zuri la kuweka TARURA, inawezekana kukawa na wazo zuri lakini katika utekelezaji tukabaini changamoto. Mimi binafsi changamoto mojawapo ambayo naiona ni watu wa TARURA kutokuwa sehemu ya halmashauri, wanaenda kwenye halmashauri pale wanapoalikwa, si kama vile ilivyokuwa nyuma, kwa sababu mimi kama Diwani kuna shida mradi unategemea ninavyokwenda kwenye Baraza la Madiwani ndipo ambapo nitaenda kusema kulingana na barabara yangu, kulingana na zahanati yangu lakini ukija kwenye masuala ya barabara wale watu wa TARURA sio sehemu ya halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba sana Serikali yangu narudia kusema ni Serikali tukufu na Serikali sikivu ni vizuri sasa ione uwezekano watu wa TARURA wawe sehemu ya Wakuu wa Idara katika halmashauri zetu ili wa-report taarifa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)