Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote mbili pamoja na Wajumbe wa Kamati, hakika wamefanya kazi kubwa. Mimi nikiwa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa hakika naomba niipongeze Kamati ya LAAC ambayo binafsi nasema Wajumbe wa Kamati ya LAAC wamesaidia sana ofisi yangu kufanya kazi vizuri. Ushauri wote uliotolewa kwa kipindi chote umeendelea kuimarisha utendaji wa ofisi yangu lakini na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Tunajua kwamba hatuwezi kuwa correct a hundred percent katika muda mfupi, lakini tumejitahidi kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mbalimbali zilijitokeza hasa katika upande wa suala zima la ukusanyaji wa mapato. Tukumbuke kwamba ukichukua historia tulikotoka nyuma hali ilikuwa mbaya sana na Kamati ya LAAC na Wajumbe huko tulikotoka hali yetu ya mwanzo ilikuwaje. Hata ukifanya reflection ya muda mfupi uliopita wa miaka michache collection yetu ilikuwa haifiki hata 80% kwa mwaka. Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, tulifikia 81%. Katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, tumefikia 90% na haya yote ni mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato. Hata hivyo, ushauri wa Kamati ya LAAC na Wajumbe kwa ujumla wake umesaidia, ndio maana katika utekelezaji huo ofisi yangu mwaka huu iliamua kununua PoS takribani 7,227 ambazo tumezigawa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya hivi kwa sababu halmashauri zingine uwezo wake ni mdogo wa kuweza kununua hizi PoS, kwa hiyo nishukuru sisi kama TAMISEMI tutaendelea kutekeleza maagizo yote yanayotolewa kwa lengo kubwa la kuboresha utendaji wa kazi wa Serikali na nia yetu ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika vizuri katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hakika sasa hivi ukiipima Mamlaka ya Serikali za Mitaa ukusanyaji wa mapato umeongezeka na tutaendelea kuhakikisha kwamba ule upungufu wote uliojitokeza kama tulivyonunua PoS na kuweza kuzigawanya katika halmashauri. Pia tunaenda kuzisimamia kwa kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato ilikuwa inasuasua, ili sasa tuweze kuliondoa tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lingine ni suala zima la matumizi ya force account. Niseme kwamba tulikotoka huko na sasa ni vitu viwili kidogo tofauti, japokuwa inawezekana kuna upungufu wa hapa na pale, lakini matumizi ya force account yamesaidia sana. Majengo yale tuliyokuwa tunajenga kwa wastani wa shilingi bilioni mbili leo hii kujenga kati ya shilingi milioni 400 mpaka milioni 500, ni mafanikio makubwa na katika hili niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu miradi hii haikujengwa hewani imejengwa katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa na timu yangu ya akina Mheshimiwa Waitara tulivyotembelea maeneo mbalimbali, miradi mingi kwa kweli kwa sababu kulikuwa na specification hata za ununuaji wa materials, bati iwe ya gauge namba ngapi, tofali, mfuko mmoja utoe tofali ngapi, kwa kweli kwa kiwango kikubwa pale wananchi na viongozi nyie mmefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kubeza hata kidogo mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya force account, kwa mfano unaenda mpaka kule ndani kabisa Nyasa utakuta hospitali ya Wilaya imejengwa nzuri kwa quality, lazima tuone kwamba tuna kila sababu ya kujisifu kwa matumizi ya force account. Hata hivyo, niishukuru sana Kamati ya PAC pamoja na Kamati ya LAAC, wote walipata fursa ya kutembelea miradi ya afya katika maeneo mbalimbali. Walijionea hali nzuri, japokuwa kunaonekana kuna upungufu wa hapa na pale na kazi ya Serikali yetu ni kuhakikisha kwamba pale kwenye upungufu tunaenda kuuboresha lakini kwa kiwango kikubwa matumizi ya force account yamesaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na Kamati za Fedha, tuhakikishe kwa pamoja licha ya kuwepo wataalam watakuwepo kule lakini sisi tuna jukumu kubwa sana kuhakikisha hii miradi tunaisimamia kwa karibu kwa kupitia Madiwani wetu kwa lengo kwamba tupate miradi iliyokuwa mizuri na naamini miradi mingi tumepata mafanikio makubwa sana kwa kutumia force account.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba Jiji la Dodoma halina barabara kabisa. Mimi nilikuwepo katika Bunge la Kumi na sasa hivi ni Bunge la Kumi na Moja. Nishukuru kwa hoja ya mama yangu inatusaidia kuhakikisha kwamba tuweze kuongeza juhudi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Naomba niwahakikishie kwamba Dodoma katika Miji ukifanya ulinganifu miaka mitano iliyopita na hali ya sasa ni tofauti sana, tunajitahidi kujenga miundombinu katika Jiji la Dodoma na hivi sasa tumekamilisha zaidi ya kilometa 168 ndani ya mtandao wa barabara za lami katika Jiji la Dodoma. Haya ni mafanikio makubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sasa hivi tumeweka vifaa, tumeshasaini kandarasi ya ujenzi wa kilometa takribani 51 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya lami. Leo hii watu wa Ilazo, watu wa Kikuyu na watu wa maeneo mbalimbali mnafahamu maeneo mliyokuwa mnaishi mwanzo hali ilikuwa mbaya, hali ya mwanzo sio hali ya sasa lakini ushauri unachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu kubwa yale mapungufu mengine lazima tutayafanyia kazi kwa sababu, hapa ndio makao makuu ya nchi yetu, lazima tuhakikishe tuna speed, tunaongeza juhudi kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa vizuri. Lakini hata hivyo niwahakikishie Jiji la Dodoma litakuwa ni jiji la pekee lenye miundombinu ya barabara za lami ukilinganisha na maeneo mengine hivi sasa kwa kadiri tunavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, agenda nyingine, kulikuwa na hoja, vituo vya afya vipo, lakini vifo vimeongezeka. Wajumbe naomba niwahakikishie, kwa sasa kwa takwimu zetu na wenzetu, Dada yangu hapa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Wizara ya Afya. Kwa kweli vituo hivi vimesaidia sana kwa kiwango kikubwa, isipokuwa tutaendelea kufanya juhudi kubwa kuviboresha vituo hivi kwa juhudi ya Serikali tuliyofanya kwa ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kuhakikisha vyote vyenye mapungufu hasa ya vifaa tiba na kupeleka wataalam ndio maana hata sasa hivi ninapozungumza kuna watu wengine tayari tunawaajiri kipindi hiki kuhakikisha tunaongeza human resource kule katika maeneo yetu vituo hivi viweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wa wajumbe niseme tunaupokea, lakini hata hivyo Serikali imeshafanya juhudi kubwa na inaendelea kufanya. Lengo letu ni wananchi waendelee kupata huduma nzuri katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja suala zima la mfuko ule wa asilimia 10 ya vijana, akinamama pamoja na walemavu, huko tulikotoka hali ilikuwa mbaya na niishukuru sana Kamati ya LAAC ilipendekeza tufute yale madeni ya nyuma na kweli tulifuta. Na hata hivyo, naomba niwahakikishie kwamba sasa hivi kwa mujibu wa kanuni fedha hizi zinatoka vizuri sana. Kwa mara ya kwanza niliposoma ripoti yangu mwezi Septemba, 2019 zaidi ya shilingi bilioni 47 zilipekekwa katika vikundi hivi ambayo haijawahi kutokea ukilinganisha na miaka yote. Imani yetu ni kwamba, zile halmashauri zenye kulegalega na baadhi ya mapungufu mengine tutaenda kuyafanyia kazi kwa makundi haya yaweze kupata fursa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo, tunashukuru kwa maoni mazuri ya wadau na Wabunge pale wanapotoa maoni, inawezekana kwa mujibu wa kanuni zetu uboreshaje utakuwaje. Tutaendelea kuboresha kanuni ili mradi mifuko hii iweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, agenda ya madai ya Madiwani, wajumbe wa Kamati ya LAAC na Kamati ya TAMISEMI ni mashahidi, juzi nilivyokuwa natoa zile mashine za electronic nilitoa maagizo kwa halmashauri zote zenye madeni wakurugenzi walipe hayo madeni kabla ya Baraza la Madiwani halijavunjwa. Na hata jana nilipokuwa nikizindua Jengo la ALAT nikatoa agizo tena halmashauri zote, wakurugenzi wote wahakikishe madeni ya madiwani wanayodaiwa katika mabenki mbalimbali yaweze kulipwa. Na nimemuagiza Katibu Mkuu wangu TAMISEMI afanye mawasiliano kuona ni akina nani ambao ni changamoto kubwa na jana nilitoa mfano mmojawapo, halmashauri hiyo ni Halmashauri ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaambie jukumu letu kubwa TAMISEMI tutaendelea kusimamia maeneo haya yote kuhakikisha Wananchi, hasa Madiwani wetu ambao wamefanya kazi kubwa na nzuri zaidi hakikisha siku ile ya kupata kiinua mgongo chao wasipate mashaka kwamba, fedha zao zinakatwa kwa ajili ya kupelekwa katika maeneo ya mabenki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini agenda ya ujenzi wa masoko, tumelipokea hili, lakini hata hivyo masoko yote tunayojenga hivi sasa tumetoa maelekezo wale wafanyabiashara wa mwanzo wote, hivi sasa nina orodha katika ofisi yangu kuanzia Soko lile la Kisutu, Soko la magomeni, Soko la Morogoro na masoko yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema wafanyabiashara walikuwepo mwanzo wote nipate orodha yao na hivi sasa orodha nimehifadhi pale TAMISEM. Kwamba, wale wafanyabiashara asilia lazima kila aliyetolewa pale soko linapokamilika aweze kupata nafasi ya kufanya biashara. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba, tume-consider mambo haya yote kwa maslahi mapana ya Wananchi wetu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa na suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara, hili naomba nimelichukua katika upande wa TARURA kwa ujumla wake, ushauri umetolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la michango kwamba, watumishi michango inaonekana deni limeongezeka, tumelichukua kwamba, kila linalotolewa kwa wajumbe hapa twende tukalifanyie kazi kwa maslahi mapana ya kuboresha Serikali yetu kwa maslahi mapana ya kuboresha suala zima la wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, binafsi nikiwa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya TAMISEMI niseme nimechukua maoni yote ya wajumbe na Wabunge wote kwenda kuboresha pale maeneo ambayo yanaonekana yana changamoto kubwa tuyafanye yaende vizuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja zote kwa jumla. (Makofi)