Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii adhimu kwa Wizara yetu na sisi kuweza kuchangia kuhusu hoja iliyowasilishwa Mezani na Waheshimiwa Wenyeviti. Na nitajikita zaidi kwenye hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Mheshimiwa Kaboyoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyekiti yeye pamoja Kamati yake kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuleta taarifa hii muhimu sana ndani ya Bunge letu Tukufu. Niseme tu kama ambavyo wamekiri ndani ya taarifa yao hoja zote ambazo ziliwasilishwa mwezi Februari mwaka 2019 tunazifanyia kazi kama ambavyo wamekiri, zimebaki chache sana ambazo tunaendelea kuzishughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye hoja ambayo imeonekana imevuta hisia kubwa ya Waheshimiwa Wabunge, nayo ni kuhusu Uchambuzi wa Taarifa ya CAG kwa Hesabu za Serikali kwa Mafungu ya Serikali Kuu na Mashirika ya Umma, hasa hali halisi ya ufanisi katika utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kamati ilipendekeza, kama tulivyosikia na kuona wote kwa pamoja kwamba, Serikali iziboreshe na kuziongezea uwezo Bodi za Rufaa za Kodi na Baraza za Rufaa za Kodi kwa kuteuwa Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wa kutosha, ili kuziwezesha taasisi hizi kufanya vikao vyake vya kusikiliza na kuhitimisha kesi za kodi kwa wakati, lakini pia kamati ikapendekeza Serikali iweze kutoa bajeti ya kutosha kwa ajili ya taasisi hizi, ili zifanye kazi zake kwa wakati na kwa ufanisi:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Bodi hizi za Rufaa za Kodi Mheshimiwa Rais ameweza kuteuwa Mwenyekiti na Makamu Wenyeviti pamoja na wajumbe wote wa bodi hizi mbili. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kwanza kabisa ambalo kama Wizara tulikuwa tunaliomba na ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji kazi wa taasisi hizi mbili muhimu sana katika ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, sasahivi bodi hizi zina wajumbe wake wote pamoja na Wenyeviti na Makamu Wenyeviti kama ambavyo sheria ilivyopitishwa na Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata wajumbe hawa bodi hizi zimeanza kufanya kazi vizuri kabisa na tumeweza kwa mwaka 2019 bodi imeweza kushughulikia jumla ya kesi 652 zenye thamani ya shilingi trilioni 2.073 na Dola za Kimarekani 81,644,013. Tuishukuru pia Ofisi ya CAG kwa kuweza kuyasema haya kwenye taarifa yake ya mwaka 2017/2018; imetusaidia na tumeanza kufanyia kazi yote haya na sasa tunaendelea kumalizia machache yaliyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliambie pia Bunge lako Tukufu kwa kesi za mwaka 2017 zote zimeshashughulikiwa na taasisi zetu hizi mbili, hatuna kesi hata moja ambayo imebaki ya mwaka 2017. Kesi za mwaka 2018 zimebaki kesi 13 tu na sasa hivi bodi hizi zinashughulikia kesi zilizofunguliwa mwaka 2019. Kwa hiyo, tumefuta kabisa baklog ambayo taasisi hizi mbili ziliikuta na sasa tunafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niweze kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, bajeti pia, taasisi hizi zinapatiwa bajeti ya kutosha na kwa kesho tu, kesho siku ya Alhamisi zitatolewa hukumu kwa kesi zaidi ya 10. Kuna Makamu Wenyeviti wako Arusha na baadhi ya wajumbe wanaendelea kuendesha kesi hizi. Mwenyekiti yuko Dar es Salaam anaendelea na kesi na baadhi ya wajumbe na Makamu Mwenyekiti wa pili yuko Mwanza na baadhi ya wajumbe wote wanaendelea kuzishughulikia kesi hizi. Ni dhamira ya Serikali yetu kwamba, mpaka kufikia mwezi Juni, 2020 kesi zote za mwaka 2019 ziwe zimekwisha, ili tuanze kushughulika na kesi za mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi nayo ilikuwa ni mapendekezo ya Kamati kwamba, Serikali iongeze wataalamu, lakini pia wataalamu waongezewe uwezo wa kufanya kazi katika maeneo yao husika:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, Serikali yetu kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa kodi ikiwa ni pamoja na weledi katika sheria za kodi, ukaguzi na ukadiriaji kupitia mafunzo ya ndani na mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu pia. Mafunzo haya hutolewa na chuo chetu cha kodi (Institute of Tax Administration) ambacho kinafanya kazi kubwa sana katika eneo hili kutuandalia wataalam wetu, ili waweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii tunaiona kwa pamoja kama Taifa. Ni kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwezi Juni, kuanzia mwezi Julai, 2019 hadi mwezi Disemba, 2019 Mamlaka ya Mapato walitarajiwa kukusanya shilingi trilioni
9.45 na kwa sababu sasa tunawawezesha wataalam wetu kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa Mamlaka ya Mapato kwa miezi hii sita imeweza kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 9.1 ambayo ni sawasawa na 96.3%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ufanisi wa hali ya juu, tuendelee kuwapa moyo wataalam wetu, lakini pia Watanzania kwa ujumla tuendelee kulipa kodi kwa hiyari tusisubiri kulazimishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana tukafahamu mengi makubwa yanayotendwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli yanatendwa kwa sababu ya makusanyo mazuri ya mapato. Kwa hiyo, niwaombe Watanzania kwa pamoja tujitolee kwa hiyari yetu kila mmoja kulipa kodi yake ile anayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishukuru pia Bunge lako Tukufu walipotupitishia sheria yetu ya fedha ya mwaka jana na mwaka huu tunayoitekeleza pale tulipoleta hoja ya Tax Amnest, imetusaidia sana pia kuweza kukusanya kodi. Hii yote ni mikakati mbalimbali ambayo Serikali inakaa na kutafakari na kuona ni jinsi gani ya kupeleka unafuu kwa walipa kodi, lakini pia Serikali yetu iweze kupata kodi yake inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya naomba niwapongeze tena Wenyeviti na wajumbe wa kamati zote mbili ambazo zimewasilisha taarifa zao mbele ya Bunge lako Tukufu. Kama Wizara tunasema kwa niaba ya Serikali tutaendelea kuyafanyia kazi yote yaliyopendekezwa na Kamati kwa sababu, tayari tumeshayaanza na ufanisi wake tunauona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii ya kutoa mchango wangu kwenye hoja hizi. Ahsante sana. (Makofi)