Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nitajikita katika maeneo manne na nitachangia ripoti kutoka Kamati ya Bajeti ambayo mimi pia ni Mjumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza nataka niligusie ni juu ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 (Value Added Tax). Naishauri Serikali iliangalie suala hili kwa sababu, kwa hali tuliyonayo sasa Serikali inapopata mikopo mfano kutoka World Bank ile mikopo inakuwa taxed. Sasa mkopo unautozaje kodi, hususan vile vifaa ambavyo vinatumika kama capital inayoenda kutekeleza ile miradi, kwa hiyo, unachukua mkopo, mkopo tena unaukata kodi. Naomba Serikali iangalie hili jambo upya, japokuwa kuna baadhi ya maeneo tumeyafanyia marekebisho kwenye sheria iliyopita. Kwenye sheria iliyopita tulifanyia kwenye baadhi ya maeneo, lakini kwa ujumla wake naomba sheria hii iangaliwe upya Value Added Tax especially katika mikopo tunayoichukua kutoka World Bank ili kutekeleza miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ninalotaka nigusie ni suala la ambalo lina ukakasi kidogo nalo ni katika uchumi wetu, ukuaji wa uchumi. Kumekuwa na sintofahamu kwamba, ukiangalia uchumi wa watu au purchasing power kwenye field tunasema uchumi hauko vizuri, lakini tukija kwenye paper work na taarifa za Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango tunahakikishiwa kwamba, tupo vizuri. Kuna baadhi kweli ya sekta zinafanya vizuri kiuchumi nazo zimetubeba, mfano ni sekta ya madini na ujenzi na sekta hizi zimeweza kufanya vizuri kwa kuwa Serikali imewekeza, ime-feed in funds kwenye hizi Wizara husika na imefanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa kwa nini Serikali isiangalie kwamba, kumbe ukiiwezesha sekta inaweza ikatutoa kama ilivyofanya kwenye madini na ujenzi, basi hivyohivyo ifanye kwenye sekta ambayo ni very sensitive katika uchumi wetu kwa sababu majority ya Watanzania tuko kwenye sekta ya kilimo. Kilimo chenyewe uvuvi au ufugaji au kwenye forestry, basi Serikali iangalie hivyo, ili kututoa kwenye huu mkwamo wa kiuchumi katika level ya watu mmoja-mmoja na purchasing power kwa sababu huku chini hatuko vizuri, lakini ukiliangalia hilo katika micro economy level tunaona kwa ujumla wake iko vizuri, lakini majority ya Watanzania tunalia njaa ndio hali ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu naomba niligusie ni kuhusu Shirika la Taifa la Mawasiliano (TTCL). Suala hili tumeweza kulijadili kwa kina katika Kamati yetu ya Bajeti na hali tumeiona kwamba, shirika hili lina uwezo wa kufanya vizuri na kutukwamua katika hali ya uchumi tulionao kutuwezesha kama shirika la mawasiliano namba moja litawezeshwa. Hili pia, sio suala tu la kukuza uchumi bali pia ni hali ya security ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali liliyonayo sasa hivi shirika hili linamiliki minara 207 tu kati ya minara 14,000 ambayo inamilikiwa na sekta nyingine binafsi. Kwa hiyo, shirika hili likiwezeshwa kama wataenda kwenye teknolojia advanced zaidi kama tuta-invest zaidi labda ni satelite level au kununuliwa telephone towers au watawekeza kwenye mambo ya mawasiliano kwa ujumlka wake au internet basi shirika hili linaweza kutoka, lakini kwa hali iliyopo sasa hivi shirika hili linasuasua na ni vigumu kwake ku-compete na mashirika mengine kwenye masuala ya mawasiliano na pia tuna-risk nchi yetu kwenye masuala ya security, kwa sababu huyo anayemiliki mawasiliano kwa ujumla wake ni muwekezaji kutoka nje, akiamua kuzima mitambo tunaweza tukapata hali ambayo si shwari katika nchi. Kwa hiyo, naomba Shirika la Mawasiliano liangaliwe kwa jicho la ziada kwenye masuala sio tu kukuza uchumi potential yake ila pia katika security ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo naomba niligusie kutoka katika taarifa yetu ya Kamati na naomba nisisitizie kwa Serikali walichukulie jambo hili kwa unyeti wake nalo ni hali ya mfumuko wa bei. Japokuwa hali ya mfumuko wa bei imekuwa ikishuka mfano ukilinganisha mfumuko wa bei umeshuka kutoka 5.5% mwaka 2017 mpaka 3.5% mwaka 2018, lakini hali hii ya mfumuko wa bei inaweza ikabadilika kwa hali tunayoi-experience sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasena hivi? Namba moja, hali ya chakula iko hatarishi kwa sababu ya hali ya hewa tunayoiona. Ni mikoa mingi sana sasa hivi ina-experience hali ya mafuriko sio tu ambayo inaondosha uchumi wa wananchi katika mashamba au makazi yao, hii pia wale ambao wamefanikiwa kulima mazao tayari sasa hivi yana hali mbaya kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha na majira ambayo hayatabiriki; hilo ni katika Mikoa ya Kigoma, Tanga, Dar-es-Salaam, Iringa, Lindi na kadhalika, kwa hiyo, kuna hali mbaya ya viashiria vya kutokuwa na chakula nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia kwa sababu, tuna taasisi yetu ya NFRA na Bodi ya Nafaka ya Mazao Mchanganyiko hatukuwapandishia bajeti, hatukuwawezesha kibajeti. NFRA last time 2019/2020, hatukuwaongezea bajeti na kazi yao hawa vyombo hivi vya NFRA ni kuhakikisha usalama wa chakula nchini, usalama wa chakula nchini ndio usalama wa nchi wenyewe. Tumetoka kuuza mazao yetu nje na sasa tunawa-task tena NFRA kufanya biashara ilhali chombo hiki kazi yake mahususi ni kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kununua chakula. Kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia maoni yetu ya Kamati ya Bajeti ilichukulie suala hili kwa ukubwa wake na unyeti wake, NFRA, Bodi ya Mazao ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko yaangaliwe kwa jicho la kipekee, ilhali tuhakikishe security ya nchi yetu kwa kupitia chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ni kitu ambacho tunakiona na tuna- experience ni hali ya haya majanga yanayotokea aidha ni kwa sababu ya haya mabadiliko ya hali ya tabia-nchi au pia ni miundombinu yetu wenyewe tumeiharibu basi, mvua zinazonyesha zinakuwa zinaharibu miundombinu na kuharibu kile ambacho ni sources za income sisi kama wananchi. Kwa bahati mbaya bajeti iliyopita tuliyoipitisha hatukumpatia Mheshimiwa Waziri Mkuu fedha yoyote katika Mfuko wa Maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui tutafanyaje Mheshimiwa Waziri husika wa Fedha na Mipango tuna dalili mbalimbali za viashiria vya milipuko ya magonjwa, tuna viashiria mbalimbali vya hali ya wadudu wanaoenda kuharibu mazao, sasa tuko kwenye in between tutatokajetokaje. Tunajisifia mfumuko wa bei ndio uko vizuri na unashuka, lakini viashiria vyote vinaonesha kwamba, tunakoenda tutakuwa tuna hali mbaya sana. Kwa hiyo, naomba sana kwenye haya mambo manne Wizara husika naomba ichukulie kwa umakini wake kwa sababu, ni maeneo ambayo ni nyeti sana kama Taifa letu na kuweza kutukwamua katika hali ya uchumi tuliyonayo. Nashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)