Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa uhai huu. Kwanza niseme kwamba, naona fahari kubwa sana kuwa Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Kamati ambayo kwa kushirikiana na Serikali imefanya mambo makubwa, ime-improve vitu vingi sana kwenye mashirika ya umma. Pia nimpongeze Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuwasilisha vizuri taarifa yetu na nimpongeze pia kwa namna ambavyo anaendelea kuendesha Kamati hii kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe kwa kuamua kushirikiana na Mawaziri kuhakikisha kwamba, anasimamia mashirika ya umma kwa ukaribu mkubwa, lakini na weledi wa hali ya juu sana. Usimamizi huu na umakini ambao Rais ameuonesha umeleta mafanikio makubwa sana kwenye mashirika ya umma, ziko chagamoto ndiyo, lakini mafanikio ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano taarifa imeonesha hapa na imesema kwamba, Shirika kama TANESCO kwa zaidi ya miaka 20 shirika limekuwa linapata hasara zaidi ya miaka 20 wanatengeneza hasara tupu. Na wamekuwa wanatumia fedha za umma kwa ajili ya kujiendesha, yaani wamekuwa wanapokea ruzuku, lakini kwa mara ya kwanza imetoka kwenye shirika linalotengeneza hasara na kuanza kutoa gawio, limetoa zaidi ya bilioni 1.4 mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi Shirika la Madini la STAMICO. Hili nalo tangu lmeanzishwa mwaka 1970 halijawahi kutoa gawio lolote Serikalini, lakini chini ya jembe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli sasa STAMICO imetoa gawio la shilingi bilioni moja. Kama hiyo haitoshi tumeona uundwaji wa kampuni ya Twiga Minerals, hii sasa ndio baba lao, shirika ambalo limeenda kufanya mabadiliko makubwa sana. Tumeibiwa sana, tumenyonywa sana na vijana wote wa nchi hii, wasomi, wazee, hata ambao hawajasoma kila mtu alikuwa anajua kwamba, nchi hii ilikuwa inaibiwa kwenye upande wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapata mwanga mweupe kwamba, kwa mara ya kwanza imeundwa kampuni ambayo tutakuwa tunagawana fifty fifty yaani 50 wao 50 sisi, jambo ambalo ni maajabu kabisa kwenye nchi yetu kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Wabezaji watakuwepo tu watabeza, acha wabeze, lakini Watanzania wenye akili timamu wanaona na wanaona kazi kubwa ambayo anaifanya na wako pamoja na yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye mambo machache. Jambo la kwanza nataka kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo na mabadiliko ya sheria ili tuweze haya mambo ambayo Rais mheshimiwa Dkt. Magufuli anayafanya kwenye mashirika mbalimbali yaweze kuwa sheria. Kwa sababu, leo yuko Rais Magufuli na leo amesema, kesho akinyamaza asiposema au kesho akitoka, tuna uhakika gani kama atakayekuja naye atakuja kusema kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Magufuli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wakati anapokea mwaka jana gawio, Mheshimiwa Rais akasema mashirika yote ya umma ambayo hayajatoa gawio leo, akawapa siku 30 nadhani ilikuwa, siku 60, akasema ambao hawajatoa gawio basi bodi za mashirika hayo zimejifuta rasmi. Baada ya kutoa kauli ile ziliongezeka bilioni 20 zaidi, hizi bilioni 20, Mheshimiwa Waziri, Mama Ndalichako anajua, ndizo fedha ambazo zinzenda kutumika kugharamia elimu bila malipo nadhani kwa mwezi ni bilioni 19. Yaani kauli moja tu ya Rais imeenda kugharamikia elimu mwezi mzima nchi nzima. Kwa hiyo, haya mambo tuyafanye sasa kuwa ni sheria kwamba, tufanye mabadiliko ya sheria, sheria isitamke tu kwamba, mashirika yalete gawio, lakini bodi ambazo zitashindwa kuongoza mashirika kuleta gawio ziwe zimejivunja kwa mujibu wa sheria, iwe sheria kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale ambao watafanya matumizi ambayo hatuyaelewi kwa sababu, matumizi nayo yamekuwa regulated na sheria. Kama wataenda kinyume na sheria kwa sababu yako makampuni mengi na mashirika mengi ambayo wanatumia hela hovyo hovyo tu, sasa lazima tuweke kisheria hii kwamba, wakienda nje ya mfumo wa sheria bodi zenyewe zijivunje na kama haitoshi hata kwenye uwekezaji usio na tija, tumeona NSSF, watu wanaenda kujenga majumba porini huko ambayo hayauziki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme haya tuyaweke kwenye sheria kwa sababu, hawa watu najua wanaenda kufanya uwekezaji mbovu wana akili, kwa nini nyumba zao wanajenga mjini, lakini uwekezaji wanaenda kupeleka maporini? Wanajua, washapiga percent zao halafu wanafanya vitu vya hovyo. Sasa lazima Sheria itamke kwamba itoe kwamba mtu anapofanya uwekezaji ambao hauna tija ambao kwa wazi wazi unaonekana kabisa kwamba huu ni utapeli, na zenyewe wawajibishwe, Bodi kuvunjwa na kuchukuliwa hatua za Kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Hazina TR, kwanza nimpongeze Msajili wa Hazina Bwana Mbuttuka amekuwa ni msaada mkubwa sana kwenye Kamati yetu, ametuongoza vizuri sana na kwa sababu amepewa jukumu la kusimamia Mashirika zaidi ya 200 kwenye nchi hii, mimi nadhani anapaswa kuongezewa raslimali watu lakini pia na raslimali fedha, mashirika zaidi ya 200 ya nchi hii huyu Msajili wa Hazina ndiye anayeangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashirika 256 kwa hiyo lazima aongewe fedha sisi tunajua kazi ambayo anaifanya kule tunajua kwa hiyo aongezewe pesa na raslimali watu ili aende kuyasimamia vizuri mashirika haya ninaamini akiongezewa fedha na raslimali watu tutajua mengi zaidi kwenye Mashirika huko tukishirikiana na Kamati yetu ambayo iko chini ya Jemedari Mheshimiwa Chegeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba suala la sukari, tumekutana na watu wa Kilombero tukaenda mpaka Kiwandani kwao kutembelea. Suala la sukari nchi hii bado kuna jambo la ziada na nimuombe Mheshimiwa Rais, jambo hili aliingilie kati mwenyewe, ukweli ni kwamba nchi hii ya Tanzania ina ardhi kubwa sana ya kuweza kuzalisha miwa ya kutosha, lakini ukweli ni kwamba tunayo nafasi kubwa sana ya kuongeza uzalishaji wa sukari kinachotakiwa hapa ni utashi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wapo, kama tukipunguza bureaucracy kwenye Uwekezaji lakini pia kukatokea msukumo mkubwa wako watu wengi ambao wanaweza wakawekeza kwenye sukari na tukapata sukari ya kutosha kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo tu-burn importation of sugar, kuagiza sukari nje ya nchi ndiyo kunaleta sukari isiyo na viwango, sukari ya bei ndogo ambayo inakuja kuathiri uzalishaji wa sukari nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nimekuwa naona kwenye maduka wanauza, juzi nimeshangaa kweli, kwenye maduka tunauziwa sukari hii nyeupe hii, kwa ajili ya matumizi, juzi wamekuja wataalamu wanatuambia sukari nyeupe ni sukari ya viwandani, siyo nzuri kwa afya mtu kuunga kwenye chai, lakini tunakula sisi, na wengine wanakula wakidhani sukari nyeupe ndiyo sukari tamu, ndiyo sukari ya premium kumbe wanakula uchafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo yote kama tunakuwa tuna uzalishaji mkubwa wa sukari kwenye nchi yetu maana yake tunaweza kupunguza uingizaji wa sukari isiyo na viwango lakini pia tunaamini tutakuwa tunalinda Viwanda vyetu katika nchi, na tutaongeza uchumi kimsingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ninalisema kwa uchungu mkubwa kwa sababu ninaamini tunao uwezo wa kuzalisha sukari kwa kiwango ambacho Taifa hili linahitaji na wakati mwingine mpaka tukafanya exportation kwa sababu ardhi tunayo, Wawekezaji wapo, kinachotakiwa ni utashi na kuweka mazingira mazuri ya Uwekezaji ili watu waje kulima na kuzalisha sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kabisa ni kuhusu hawa watu ambao wanakaimu Ofisi, ooohh! muda umeisha nadhani…

MBUNGE FULANI: Bado! Bado! bado.

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako ya mwisho….

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Makaimu hawa ufanisi wao wa kufanya kazi ni mdogo kwa sababu mtu anapokuwa anakaimu nafasi yake confidence ya kufanya kazi inakuwa ni ndogo sana. Kwa hiyo, Mashirika mengi yana watu ambao wana Kaimu tunaomba Mamlaka ili jambo kama tumeweza kuchomoa Wafanyakazi hewa tukafanya hiyo, hili linashindikana vipi kwenye Mashirika haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye uchunguzi mzuri wa ambao wanafaa wapewe nafasi zao na ambao hawafai basi waondolewe wapewe watu wengine ili kuondoa suala la kukaimu kuongeza ufanisi kwenye Mashirika ya Umma. Nakushukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)