Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii ya uhai na pumzi na leo tumeweza kukutana hapa kuweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru kwa namna ya kipekee sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jemedari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalazimika kuyasema haya mapema kwa sababu kwa namna ya kipekee sisi wananchi tunaotokea Mafia Kisiwani tumepata Ghati la Nyamisati ambalo limeshakamilika na Serikali hivi sasa inakamilisha Kivuko kwa ajili ya wananchi wa Mafia ambacho kitakuwa tayari nadhani kama siyo mwezi ujao basi utakuwa ni mwezi wa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nije kwenye mada husika, nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa namna ambavyo wamewasilisha taarifa zao hapa za mwaka. Nitajadili zote kwa pamoja, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma pamoja na Kamati ambayo pia ninaihudumu Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ya Bajeti inasema TRA wamefanya vizuri sana katika ukusanyaji wa mapato na tunawapongeza sana na uwepo wa Kamishna Jenerari Mpya pale naamini umekuwa ni chachu wa kila siku tunayoiona TRA inavunja rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika sasa mpaka trilioni 1.5 kwa kweli ni mafanikio makubwa sana. Nasahihishwa hapa trilioni 1.9 ni mafanikio makubwa sana kwa kweli na tunawashukuru sana tunampongeza sana Kamishna Jenerari na tunaamini kwamba wataendelea kuvunje rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taarifa inasema mapato yanayotokana na vyanzo ambavyo si vya kikodi hayajafanya vizuri sana. Sasa eneo hilo nafikiri ipo haja ya kuhakikishwa kwamba tuna improve, mwaka jana hapa tulipitisha Sheria hapa kuhusu masuala ya Bandari kwa sababu maeneo ambayo vyanzo vingi sana maeneo ambayo kule mapato yanakopotea sana ni kwenye hizi zinaitwa bandari bubu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipitisha Sheria hapa ambayo tumempa Mamlaka Waziri Mwenye dhamana ya masuala ya Bandari aweze kurasimisha Bandari ambazo anaona inafaa. Sasa nafikiri labda kama wenyewe wapo hapa watakapokuja na wao kuchangia watuambie watu wa Bandari, wanaohusika na dhamana ya Bandari, hivi mpaka sasa wamerasimisha Bandari ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano sisi tunaotoka kule kwetu kule Bandari zimekuwa nyingi sana na mapato ndiko yanakovuja vuja kule ili twende vizuri, lakini eneo jingine ni eneo ambalo ya mapato ambayo pia si ya kodi, mwaka jana na mwaka huu pia nilizungumza hapa kuhusu namna gani sasa kwa sababu tunaiona TRA inaweza kukusanya kwa asilimia nyingi sana na wako vizuri, lakini sasa inaonekana kwamba tunamkamua yule ng’ombe sasa anakaribia kumaliza maziwa yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ipo haja ya kuongeza tax base na kuangalia maeneo mengine ambapo Serikali sasa inaweza ikapata mapato ambayo pia mengine wala si mapato ya Kikodi na tulizungumza hapa mwaka jana na ninashukuru sana nimemuona Waziri Mwenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba yapo maeneo ambayo Serikali ikiwekeza kwa mfano kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, kwenye Uvuvi wa Bahari kuu, bado hatujafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imebahatika kuwa na Mawaziri ambao ni very aggressive na mimi ninawashukuru na ninawapongeza sana, wanafanya kazi nzuri sana. Lakini tunahitaji tuongeze nguvu zaidi kwa sababu mapato haya ambayo ninaamini tunayakosa kule kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni mapato makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeiangalia taarifa hii, pia tulitenga na fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi sijui tunakwenda vipi? Na nimeona pia kwamba Serikali ina Mpango wa kununua meli yake yenyewe ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nitoe angalizo kidogo hapa, isije ikawa ile hadithi ya Kuku na yai, kipi kianze, unaweza ukawa na Bandari ya Uvuvi pamoja ukanunua na Meli lakini kinachotakiwa kuanza hapa tuanze kwanza na ujenzi Bandari halafu meli ije, kwa sababu tutakuwa tunanunua kutokana na gharama kubwa za ununuzi wa Meli hizi za Uvuvi ambayo gharama zake ni kubwa naona. Serikali tungewekeza kwanza kwenye Miundombinu ya Kibandari ambayo multiply effect yake ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi kutakuwa na Viwanda mule vya kuchakata mazao mbalimbali ya samaki, ambayo yatafanya biashara ya minofu kama ile ambayo iliyokuwa ina-boom miaka ile ya 90 kule Mwanza na sisi tukaweza kuitumia Bahari Kuu yetu iweze kutu-feed na minofu ya samaki aina ya tuner ambao wanapatikana zaidi sana katika Pwani yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri na Mheshimiwa Waziri unanisikia ni vizuri sana tukaharakisha mchakato ule wa kuwa na Bandari na Uvuvi tukishakuwa na Bandari ya Uvuvi baadaye meli, hata meli za wageni sasa tukazikaribisha zikaja alimradi kwamba wanapovuna mazao yetu kule Bahari Kuu wasiende nayo nje yarudi ndani ili yaweze kutoa ajira pamoja na mapato mengine zaidi ya Kiserikali ambayo yatasaidia katika kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala tulilizungumza kwenye Kamati suala la namna gani TRA inaweza ikakusanya Kodi ya Majengo, Kodi ya Majengo ni ushauri ambao ulitolewa na sikuiona kwenye taarifa lakini naomba niusisitize hapo, kwamba Kamati ilishauri katika mjadala badala ya kuanza kuhangaika na Wafanyakazi wa TRA wakaingia mitaani kwa wingi kwenda kufuata nyumba hadi nyumba. Inawezekana workforce hiyo tukawa hatuna na moja ya principle nzuri za ukusanyaji wa kodi, lazima Kodi iwe convenient, lazima kodi iwe economical huwezi ukatumia gharama nyingi sana kukusanya Kodi ambayo mwisho wake ile Kodi inakuwa ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, likaja wazo na naomba sana wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mipango waliangalie pamoja na TRA likaja wazo kwamba hii kodi ya majengo kwa nini isiingizwe katika bili ya luku? Bili ya luku halafu ikawa spread kwa muda wa miezi kumi na mbili ili mtu anaponunua luku basi anakuwa ameshalipa Kodi yake ya Majengo, lakini na kubwa zaidi ni kwa sababu sasa hivi umeme umesambaa karibu nchi nzima, na kwa taarifa tulizo nazo kutoka kwa Wizara husika ni kwamba mpaka kufikia Juni mwakani 2021 tutakuwa tumefikia vijiji vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninaamini kwa kutumia utaratibu huu Serikali inaweza ikakusanya Kodi yake ya Majengo TRA bila ya bughudha bila ya kukimbizana na watu, au kuongeza workforce kubwa zaidi kuanza kuingia ingia kwenye address mbalimbali najua kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine ya kibiashara labda nyumba moja inaweza ikawa na fremu za maduka labda thelathini, arobaini na kila fremu ina mashine yake ya luku lakini haya ni mambo ambayo administratively wanaweza wakaripoti baadaye wataalam au Watendaji wa TRA wakaenda maeneo kama hayo waka-harmonize hayo mambo na Serikali ikaweza ikanufaika zaidi na mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine tumeona ufanisi mzuri wa ile ETS ile stamp ya Kodi kwenye bidhaa ilivyoanza inafanya vizuri na kwa kuwa taarifa zinaonekana kwamba tunakwenda vizuri, nilikuwa nashauri tu na Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Bajeti ambaye ndiye mtoa hoja kama mtaona inafaa basi twende kuishauri Serikali sasa twende ku-extend zaidi bidhaa za aina nyingi zaidi ziingie kwenye utaratibu huu wa ETS kwa sababu umeonekana kwamba ni wenye manufaa makubwa sana na unaleta mapato mengi ya Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie jambo moja dogo kuhusiana na TRA, TRA wanatoa certificate kwa hizi Taasisi NGO‟s ambazo zinakuwa wanapata kama exemption ya kulipa kodi, na kule kwetu sisi tuna shida kidogo, tuna shida, kuna wawekezaji wamewekeza pale wanataka kuja kutupatia sisi kitu kinachoitwa CSR ile Cooperate and Social Responsibility kwa ajili ya kurudisha kwa jamii ya Mafia. Lakini hawa Wawekezaji wanatuambia kwamba wataipatia Halmashauri ya Mafia msaada wa bilioni mbili, lakini ule msaada wa bilioni mbili ukija ukiuchanganua na ninaamini wenzangu wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija ukiuchanganua ni kwamba ni mafunzo, ni semina ni tiketi za ndege za Wawezeshaji kutoka Ulaya kulala katika five star hotel na mambo mengine, lakini kinachokwenda kwa wananchi wa Mafia wenyewe ni almost sifuri kwa sababu wanakuja wao na ma-translators wao kwa ajili ya kutafsiri kwa watoto eti wanasema wanawafundisha namna ya ujasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo limetuletea matatizo sana na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Waziri Jafo kama upo nililileta kwako na ukasema kwamba utachukua hatua, kuna tatizo pale tunarundikiwa jambo, tunaambiwa CSR ya bilion mbili lakini ukweli hasa hakuna kitu kule on the ground na hii nimelisema hapa kwa makusudi, nimelisema hapa kwa makusudi kwa sababu lina tax implication kwa ajili ya TRA tuangalie Taasisi hizi sasa ambazo zinakuja kwa wananchi wetu na inaweza likaja likawa swali kwamba inakuwaje kwamba hayo mambo si mgeweza tu kuyamaliza huko kwenye Baraza lako la Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uendeshaji wa haya mambo kuna kitu kinaitwa technical no how na kuna kitu kinaitwa technical no who, sasa kwenye technical no how, nimejaribu kujenga hoja sana ili jambo liishe kule lakini wenzangu wamenizidi kwenye kitu kinaitwa technical no who, na ninaamini Waziri Mwenye dhamana wa hiyo unanielewa nina maana gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)