Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nitaanzia kuchangia kamati ya PIC, ukurasa wa 25 ambao unazungumizia mashirika ambayo yanafanya matumizi kuliko uwezo wake wa kukusanya na vilevile uwezo ama faida ya shirika kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye Shirika la Nyumba hasa ukizingatia kwamba mimi ni Mbunge wa Jimbo la Kawe na katika kipindi cha mwaka 2000 – 2015, kulikuwa kuna miradi mingi sana ya ujenzi ambayo ilikuwa inasimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na kama miradi husika ingefanikiwa Serikali ingeweza kupata mapato mengi; mosi kwa kutumia property tax, lakini pili kwa kutumia uuzaji wa nyumba ama kupangisha nyumba na shughuli zozote za kijamii zilizokuwa zikiendelea ama ambazo zingeendelea katika eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia taarifa ya PIC inaonesha kwamba Shirika la Nyumba la Taifa mwaka 2016/2017, mapato yalikuwa bilioni 154 matumizi 122; mwaka 2017/2018 mapato milioni 116, matumizi bilioni 83.2. Hata hivyo, ukiangalia taarifa ya Kamati inaonyesha kwamba ina dhamira ya kulaumu shirika zaidi pasipo kuangalia shirika limefikaje hapo. Sote tunajua kwamba mpango wa ujenzi wa nyumba Regent, ujenzi wa nyumba Morocco, ujenzi wa nyumba 711 (I) Kawe na ujenzi wa nyumba 711 (II) Kawe zimekwama kwa sababu Waziri wa Fedha amegoma kutoa kibali cha Shirika la Nyumba kuweza kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Waziri wa Fedha atujibu hili kwa sababu jana wakati Mwenyekiti wa PAC alipokuwa akizungumza na hili Bunge alisema, kutokana na miradi kukwama miradi yote mwaka 2017 Serikali inalazimika kumlipa mkandarasi kila siku ya Mungu shilingi milioni 20, kila siku ya Mungu. Hapa tunapozungumza project hizi nne tofauti kuna wakandarasi wanne tofauti. Sasa hii milioni 20 inalipwa kwa mkandarasi mmoja ambaye yupo kwenye project moja ama inalipwa kwa wakandarasi wanne, ama kila mkandarasi kati ya hawa wanne analipwa hiyo hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana huu mradi tunaelezwa mimi ni jimboni kwangu 711(I) ulianza kufanyiwa kazi kwa 20% imewekezwa pale milioni 26.3, mradi ambao umekwama. Kwa hesabu ambazo Mwenyekiti ametuambia jana, kama kwa siku wanalipwa milioni 20 kwa project kwa mkandarasi. Tafsiri yake kwa mwaka wanaojua mahesabu zinakaribia bilioni saba kwa mwaka. Kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2017 mpaka sasa hivi tafsiri yake kuna bilioni karibu 21 ama 26, mimi nimesoma sheria mambo ya hesabu hesabu siyajui 21.6 nimeambiwa hapa na wachumi, zinadondoka chini kwa sababu tu kuna Waziri wa Fedha mmoja ambaye hata kama shirika limefikia ukomo lakini lilikuwa lina business mind, fedha ingeweza ikarudi zaidi ya kile ambacho kimekopwa na faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu mfululizo, mradi umekwama, juzi kama miezi kadhaa iliyopita niliuliza swali hapa Wizara ya Ardhi akajibu Naibu Waziri wa Ardhi, nikauliza ni kwa nini Mradi wa Kawe, Kawe 711 (I) 711 (II) Morocco na Regent imekwamba; akaniambia eti ni kwa sababu Serikali imehamia Dodoma, kwa hiyo nguvu zote zilizokuwa zifanyike kwenye zile project zimehamia Dodoma. Serikali isiyokuwa na vision, Serikali isiyokuwa na mipango, anayeibuka anaibuka na jambo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Mradi wa phase II ambao ulikuwa unagharimu bilioni 103 na wenyewe, ile ni phase I, umefanywa kwa 30% tu, umetumia bilioni 34.8 mradi umelala. Kwa hiyo tafsiri nyingine na huyu mkandarasi wa pili na yeye analipwa milioni 20 yake kwa siku amekaa tu anakula bata halafu leo wanasema wana uchungu wa Watanzania, wana uchungu na matumizi ya fedha, we can‟t allow this. Nina ripoti ya CAG hapa, naomba ninukuu CAG amesema nini kuhusiana na hayo mamlaka ambayo Mheshimiwa Waziri anayo lakini ameamua kuyakalia. Anasema hivi

“Ikiwa NHC haitapata kibali cha kukopa na kushindwa kukamilisha miradi yake itapaswa iwalipe wakandarasi jumla ya shilingi bilioni 99.99 kutokana na uvunjaji wa mkataba.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii fedha ni extra ya zile bilioni 21 ambazo tunazimwaga chini kwa sababu tu ya maamuzi ya kisera ya kukurupuka. Pia anasema:

“Pia itawapasa kufanya marejesho ya shilingi bilioni 2.6 kwa wateja walioanza kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa nyumba hizo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kawe ama lile eneo ni very strategic yaani NHC walikuwa wanapata wateja kabla hata hawajamaliza ujenzi. Kwa hiyo kulikuwa kuna uhakika wa fedha upo hapa mkononi, kulikuwa kuna uhakika wa kodi za majengo, Mheshimiwa Mpango aliamua kutunyang’anya halmashauri property tax ili lile kapu lake linenepe. Kwa akili yangu iliniambia kama kweli yeye ni Mchumi maana sisi wengine ni Wanasheria makanjanja, uchumi hatujui, uchumi wake ungemwelekeza kwamba kuwekeza kwenye zile nyumba kungeweza kulisaidia hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba nipate majibu ya uhakika kutoka Serikalini project za Shirika la Nyumba, nimeamua nisimame nizungumze nyumbani kawe na nilizungumze shirika letu ambalo chini ya akina Mchechu tulikuwa tunaliangalia kama shirika la mfano. Halafu wanakuja watu wanasema, hatuwezi kukulipa milioni kadhaa. Lazima awalipe watu mamilioni kutokana na brain, kama brain yao inaleta trillions wawalipe kwa thamani hiyo. Wanakaa wanawaza kimaskini halafu wanataka productivity, hakuna vitu kama hivyo. Hata wenzetu waliotangulia huko brain yako ndio inaangalia kipimo chako cha mshahara. Kama wewe ni kilaza utapata hivi, kama Mungu amekujaalia kuwa hivi utapata hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri tupate majibu ya haya mashirika na waache kusakizia ama kutupa mzigo kwa wetendaji wetu, wakati kinyumenyume wao ndio wanaovuruga na kuyanyonya mashirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana na natarajia Mwenyekiti anatanipa majibu. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati msilembelembe hizi taarifa. Nimeaangalia jana taarifa ya PAC, ukiangalia CAG ana hoji mambo mengi ya muhimu, wanakuja hapa wanachagua vieneo vichache ili kuonyesha Serikali imefanya wonders kumbe kwenye hizi taarifa kuna mambo ya ajabu, mambo ya hovyo ambayo Bunge tunatakiwa tusimamie kwa maslahi mapana ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, Mheshimiwa ndio nimerejea kama hivyo, msiyempenda amekuja. Ahsante sana.(Makofi)