Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. ESTER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naenda kuchangia kwenye taarifa ya PIC na nikipata muda na Bajeti kidogo, lakini kwanza niwapongeze Wenyeviti wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza na hoja ya kutokukamilika kwa miradi, tutaona kwenye Shirika la NSSF kuna Mradi wa Holiday Inn na ule wa Dege kule Kigamboni, mpaka leo haujakamilika hatujui hatima yake na zile fedha ni za wanachama ambazo zinatakiwa ziweze kuwekeza kwa tija zaidi ili ziweze kuzalisha na kuweza kuwalipa wanachama ambao wamechangia kwenye huo Mfuko.

Mheshimiwa Mwenyeki, kingine nitagusia pia kwenye Shirika la Nyumba la Taifa, kwenye miradi mitatu kama ilivyoainishwa kwenye taarifa yetu ya PIC. Kwenye Mradi wa Mji wa Kawe tulitembelea pale Kamati yetu ya PIC mwaka juzi tukaelezwa na by then tukaambiwa kuna Watanzania ambao tayari walikuwa wameshatoa deposit kwa ajili ya kupanga na wengine kununua nyumba, kuanzia 2016 walikuwa wameshatoa deposit. Sasa tujiulize leo hao Watanzania ambao walitoa zile deposit zao, mradi haujakamilika that means hawajaweza kuhamia kwenye huo mradi. Sababu ambazo Serikali inatoa ni zile ambazo hazina tija kwa kweli na Serikali lazima iwe responsible kwa maamuzi ambayo imeyafanya ambayo yanaathiri miradi kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imesemwa hapa na jana imesemwa kweli, hivi kwa mtu gani ambaye anaweza akaona kwamba ni sawa kutoa bilioni 21kuliko kutoa kibali kuweza kukamilishwa kwa ule mradi ambao tunajua kabisa Shirika la NHC ni shirika ambalo linajiendesha kibiashara, wala Serikali haitakiwi kutoa dhamana ila inatakiwa itoe kibali na benki ndiyo wanatakiwa ku-assess business plan ya shirika husika kuona kwamba ni viable apewe mkopo, wakitoa mkopo for a certain period inaweza ikarejesha na wala siyo Serikali kuendelea kukatalia kibali, just kutoa tu kibali shirika likakope, hiyo haikubaliki na sisi kama Wabunge lazima tuazime sasa Serikali iweze kutoa kibali ili NHC iweze kukopa, iweze kumalizia ule mradi na Watanzania ambao wamesha-deposit waweze kuhamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tutaonekana wendawazimu sana, kwa yeyote yule ambaye anaweza kupata hata ile view tu ya ule Mji wa Kawe ulikuwa si tu unaenda kukuza uchumi wa Tanzania, lakini unaenda kubadilisha taswira ya Tanzania kabisa kwa Jiji la Dar es Salaam. Sasa ukisema umeutelekeza kwa sababu mnahamia Dodoma, ni mambo ya ajabu sana, hata mwendawazimu hawezi kuyakubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Morocco square ulikuwa umeshakamilika kwa asilimia 90 mwaka juzi, imebaki asilimia 10 nao umeachwa hizi asilimia kumi kwa miaka mitatu, unaachwa kukamilishwa. Hii siyo haki kabisa, mkandarasi anaendelea kulipwa asilimia 10 tu kukamilika kwa mradi, lazima Serikali iwajibike na ijue kabisa kwamba hii sekta ya ujenzi ndiyo sekta ya pili ambayo inachangia katika kutoa ajira Tanzania ukiacha ile ya kilimo, kwa hiyo ni lazima tujitoe zaidi kuhakikisha mambo yanasonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kupungua kwa mitaji kwenye mashirika yetu, taarifa imefafanua vizuri sana. Hapa nitaenda kugusia Shirika la STAMICO, shirika hili tumelitwisha jukumu kubwa sana la kusimamia miradi mikubwa na ya kimkakati, linasimamia Stami Gold, Buhemba kule, inasimamia Kiwira, inasimamia utafiti wa madini, ununuzi wa madini bati, lakini shirika hili limeendelea kujiendesha kwa hasara, mtaji unapungua kila mwaka, matumizi ya shirika hili tumeona na kwenye ripoti ni zaidi on average 134 percent ya pato ghafi, ina maana linajiendesha kihasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiuliza kama Serikali imeamua kuwekeza kwa baadhi ya mashirika kama ambavyo wamewekeza kununua ndege nyingi tena kwa mabilioni mengi ya fedha, wamewekeza kwenye SGR trillions of money. Shirika la STAMICO ambalo ni muhimu sana na miradi ambayo wameipa Tanzanite One ipo STAMICO kwa nini wasitenge mtaji wake mpaka juzi ilikuwa bilioni 33. Kwa nini hata tusi-invest pale hata bilioni 200 tu tuone ijiendeshe sasa hivi na iweze kuendeleza hiyo miradi ya kimkakati, we have to start a balance, huwezi kupeleka materials kwenye SGR, sijui wanataka popularity ili Watanzania waone, unaacha shirika ambalo ni la muhimu sana ambalo umelipa majukumu makubwa sana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuipa hela STAMICO ili iweze kuendesha vizuri hiyo miradi yote ambayo imeelekezwa STAMICO. Tunaona STAMICO imerithi madeni ambayo yametoka kwenye baadhi ya hayo mashirika mengine ambayo yamehamia STAMICO, lakini Serikali haionyeshi njia ya ku- clear hayo madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni ukosekanaji wa uwekezaji wa tija kutoka kwenye makampuni ya ubia tuliyonayo na hapa na-cite mfano wa TBC na Star Media, hii Star Media imekuwa ikijiendesha kwa hasara tangu ianze 2009 hapa Tanzania. Nakumbuka nilivyokuwa PIC Bunge la kumi tulihoji sana juu ya hii Star Media, lakini ukiangalia na ripoti yetu leo inaonyesha Star Media ilianza kwa mtaji wa milioni 238 ambayo ni takribani bilioni 547 za Kitanzania mwaka 2009. Walisema kwa business plan yao ikifika, ile business plan 2009 - 2014 wangeanza kutoa gawio kwa wanahisa lakini imekuwa kinyume ina-operate under loss, ripoti imeainisha kabisa, 2014 walipata loss ya bilioni 6.8; mwaka 2018 ilipata loss ya bilioni 19. Cha kushangaza mtaji mwaka 2009 ulikuwa bilioni 547, 2018 mtaji ni half wa bilioni 119, lakini bado tunaendelea kukumbatia Star Media kwamba ni shirika mbia na cha kushangaza hii Star Media ukitaka kuundwa hata Kamati Teule kufuatilia, unazuiliwa kwamba sijui kuna mambo nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaita Kamati ya PAC hawakutokeza, tunataka tujue kuna nini nyuma ya Star Media, fedha za Watanzania asilimia 35 tumewekeza pale kama wabia, tunataka kueleza Watanzania ni kwa nini huu mkataba hausitishwi ili tuweze kujua tuanze upya au tuachane nao? Huwezi kuwa na mbia ambaye ana-operate under loss. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine na mbaya zaidi Star Media, CAG walifanya ukaguzi 2014/2015; 2015 walivyotaka kufanya ukaguzi wakakataa kutoa nyaraka, lakini CAG aliainisha madudu zaidi ya 34 kwenye Star Media. Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali kama hamna kitu nyuma ya pazia ambacho mnakijua, tunaomba huu mkataba uwe reviewed na uvunjwe kwa sababu tayari wameshavunja makubaliano kwenye MoU kwa kutoweza kutoa hiyo faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni hoja ya kuhusiana na kukaimu tumeona na tumeshuhudia watendaji wanakosa mamlaka kamili ya kufanya decision kwa sababu unamkuta mtendaji anakaimu zaidi ya miezi 30, sheria inasema miezi sita kama umemkaimisha miezi 30 ina maana huyu mtendaji anafaa kuidhinishwa ili aweze kufanya maamuzi kamili akijua yeye ni CEO wa kampuni fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kuna madeni mengi sana Serikali inadaiwa na hayo mashirika au taasisi. Kwa mfano tumeona ALAF wanadai bilioni 3.94 kutoka TBA kuanzia 2017, TRA wanadaiwa VAT fund na ALAF ambayo ni mbia mwenza wa Serikali bilioni 15. Sasa nyie mnadaiwa VAT fund bilioni 15 na siyo ALAF tu hawa ata ma development partners nao wengi wanadai kwamba wanadai billions of money kutoka Serikalini. Halafu mkija hapa mnasema makubwa, rudisheni kwanza hiyo VAT fund kwa wanaohusika halafu ndiyo mje mtupe tathmini halali ya makusanyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anadai bilioni 15 mnategemea ata-operate vipi hii kampuni.

MHE. HALIMA MDEE: Wapigaji!

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ni kampuni moja tu, Serikali jamani tuache upigaji watu wanajua kwa sababu hamrudishi VAT funds.

MHE. HALIMA MDEE: Wanapiga kwa staha.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo AICC nayo inadai zaidi ya bilioni tatu kutoka Serikalini na mashirika lakini na taasisi nyingi sana zinadai wanapotoa huduma Serikalini hawalipwi. Msipowalipa hawa wanashindwa kujiendesha na kukosa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napongeza kabisa mashirika yanapotoa gawio lakini nasikitika kwa mashirika ambayo yanakuta yanaomba mitaji lakini na yenyewe yanatoa gawio kama STAMICO. STAMICO anajiendesha kwa hasara lakini tulishughudia ikitoa bilioni moja Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther malizia.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vyuo vikuu na wengine eti wanatoa michango kama UDSM, UDOM, UCLAS, VETA ni kama vile tunaweka kahela halafu baadae tunakazungusha kwa mgongo wa nyuma kanarudi tena. Siyo sahihi ni kama unakunywa uji wa mgonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pamoja na kwamba tuna-encourage watu watoe ile asilimia 15 ya michango na gawio lakini tuangalie zile ambazo zinatoa huduma per se. Kwa mfano UDSM au vyuo vikuu vingine ambavyo ndiyo vinatutolea, tunazalisha pale watu ambao wanakuja wataalam kwenye nchi yetu tena wenyewe wanataka tena waje pale watoe 15 percent na unajua Serikali ndiyo wanaleta hapa ndiyo tunawapitishia votes zao. Siyo haki ni kama vile tunacheza viini macho mbele ya macho ya watanzania, ahsante sana. (Makofi)