Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi ya leo. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa kibali cha kuona mwaka huu na niipongeze sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani na kufanya miradi ya maendeleo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze asubuhi hii kwa kunukuu baadhi ya maeneo ya Katiba Ibara ya 3(8), Katiba inasema; Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia, wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii. Lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi, Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenukuu maneno haya ili tukubaliane pasipo shaka kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi ndiyo chama kilichokabidhiwa dhamana ya kuongoza dola na Taifa hili. Tukiacha nchi yetu ikashambuliwa, ikafedheheshwa, ikanyimwa haki yake, ikadhalilishwa na watu wasioitakia mema nchi hii, siku ya siku wananchi hawatawauliza wale ambao wameishambulia nchi yetu, watatushambulia sisi ambao tumepewa dhamana ya kuilinda na kulisimamia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Bunge hili na hasa wanaCCM nataka niwaombe tulinde heshima ya Taifa hili kwa heshima kubwa na kwa wivu unaostahili na kumtunza n kumlinda Rais wetu ambaye ndiye kioo na ndiye msingi wa uadilifu wa Taifa letu ambaye amerudisa nchi yetu katika misingi ya haki na ya kidemokrasia na kusimamia rasilimali ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Bunge au Wabunge wa CCM wakanyamaza wakati Serikali yao inashambuliwa na watu wasioitakia mema nchi hii. Haiwezekani, lazima tuwe na wivu uliopitiliza wa kuilinda Serikali yetu na kumlinda Rais wetu pasipo shaka na bila aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi imezungumzwa hapa habari ya watu wanaoichafua nchi yetu lakini siku ya siku maslahi mapana ya Taifa liko katika Chama Cha Mapinduzi ambao ndiyo wamepewa dhamana na wananchi. Nataka niwaombe wale ambao tumepewa dhamana na wale ambao Rais amewapa nafasi ya kumsaidia Rais, sisi Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi tuko nyuma yenu endeleeni kutekeleza majukumu yenu bila kusita na sisi tunawaunga mkono kwa kile ambacho mnafanya kwa ajili ya kumsaidia Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni la aibu kwa viongozi ambao wamepewa dhamana wanatumia nafasi waliyopewa katika kushambulia Taifa hili na kuinyima haki na kuidhalilisha mbele hata ya Mataifa. Sisi tuko mstari wa mbele kulinda heshima ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mchango wangu katika maeneo mawili na nianze katika kamati ya viwanda na biashara ambayo mmesikia Taarifa yake, tuliletewa Taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Jengo la maabara mradi namba 6260, Fungu namba 60. Wakati tunaletewa mradi huu tuliambiwa jengo hili limetumia bilioni 19 kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeomba kwa miaka karibu miwili, Serikali ilete taarifa ya utekelezaji mradi huo kwa sababu inaonekana kuna ufisadi mkubwa sana lakini mpaka sasa tunavyoongea kwenye Bunge hili, Serikali haikuleta taarifa hiyo. Tunaomba Bunge lako lione namna nzuri ya kusimamia mradi huu wa TBS kwa sababu hata kama sisi sio wataalam wa ujenzi, lakini sehemu ya mkataba ule unakuambia umeme utawekwakwa shilingi bilioni 3.1 na kiyoyozi cha mfumo wa hewa, bilioni 3.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mfumo mzima wa mradi huo, tumeomba sana mkataba huu kwenye Kamati, hatukuletewa. Tunaiomba Serikali na hasa Waziri anayeshughulikia viwanda aone namna ya kulisimamia suala hili ili haki ijulikane kama kuna ufisadi katika mradi huu, uweze kujulikana na wale walioisababishia nchi yetu hasara wachukuliwe hatua. Mradi huu kuna harufu ya rushwa na inaonekana kabisa hata katika tendering documents. Wale waliokuwa juu ndiyo waliopewa mkataba na wale waliokuwa chini wakanyimwa mkataba lakini ukiuliza mfumo uliotumika, hawasemi. Ninaomba muangalie jambo hili ili liweze kushughulikiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili ni mradi wetu wa magadi wa Engaruka ambao wanasema inatoa tani milioni 4 kwa mwaka. Ardhi hii wananchi tumetoa karibu ekari 100,000 kwa ajili ya mradi huu lakini kwa miaka minne sasa hakuna jambo lolote linaloendelea katika eneo la Engaruka kwenye mradi huu. Tunaomba Kamati inayohusika itusaidie Serikali ituambie ina mpango wa kuendelea na mradi huu au haina mkakati wowote wa kuendelea na mradi huu ili kama mradi huu hauendelezwi ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi wafanye maendeleo yao na kuendeleza eneo lile kwa sababu tumezuiwa kuendeleza ile ardhi lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote ambazo Serikali imechukua katika kuhakikisha wawekezaji katika eneo lile la magadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atuambie baadaye vilevile kama Serikali inahitaji kuendeleza eneo hili na hata kama haiendelezi kwa leo, ile fidia ambayo wananchi wetu walipaswa kupewa, wapewe ili ardhi ile ibaki kwenye mikono ya wananchi la sivyo wananchi wapewe nafasi ya kuiendeleza na Serikali itakapokuwa tayari kuendeleza mradi huo italipa fidia kwa wakati maendeleo yaliyokuwa yamefanyika wakati huo kuliko kuacha ardhi ya wananchi wa Monduli heka 100,000 bila kufanya maendeleo yoyote. Naomba nipate Mwenyekiti wa Kamati atusaidie katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ni suala la miundombinu katika nchi yetu, ukiangalia Wabunge wengi humu tunalalamika uharibifu wa miundombinu iliyosababishwa na mvua, Lakini ukienda kwa wataalam hasa TARURA na hata TANROADS unaambiwa hakuna bajeti ya dharura katika kutatua matatizo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tunapoelekea katika bajeti na Mwenyekiti wa miundombinu atusikilize vizuri, hatuwezi tena kupitisha bajeti bila kuonekana kama kuna kipengele cha bajeti ya dharura katika utekelezaji wa miradi ya TARURA pamoja na TANROADS kwa sababu tunasema tu watu wakaribishe miundombinu lakini uhalisia hakuna fedha iliyotengwa kama dharura kwa ajili ya miundombinu pale ambapo mvua imeharibu miundombinu na siku ya siku barabara hizo na maeneo yale hayarekebishwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kadiri tunavyoelekea katika bajeti, hili eneo la dharura kwa ajili ya barabara zetu zitakapokuwa zimeharibiwa na mvua ziwekwe aidha katika kila Mkoa au katika ngazi ya hamashauri ili watu wa TARURA waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi na waweze kusaidia pale ambapo kuna uhitaji kwa sababu nao wanaenda kuangalia tu lakini hakuna ambacho wanaweza wakafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru lakini la mwisho kabisa ni suala hili la blue print, suala la blue print inaonekana kwamba Serikali imekubali kwamba tuwe na mfumo utakaosimamia biashara nchini lakini mifumo hii na wewe ni mwanasheria haijatungiwa sheria kwa hiyo kila mmoja anapotaka kutengeneza inaonekana kuna vikwazo vya kisheria ambavyo vinasababisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kama Serikali itakubali katika Mwaka huu wa Fedha kabla hatujamaliza Bunge hili, tume ilete usheria hapa hata kama ni kwa dharura ili baadhi ya sheria ambazo zinakwaza biashara nchini ziondolewe na wafanyabiashara wetu waweze kufanya biashara zao katika hali ya utulivu na kwa amani kwa ajili ya usalama na utukufu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea kuunga mkono hoja. (Makofi)