Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo, leo tumeweza kukutana hapa kujadili masuala yanayohusu nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa taarifa nzuri kabisa ambazo zimesheheni ushauri na maazimio mazuri sana. Naamini kama tutayafanyia kazi basi tutaona nchi yetu hii ikisonga mbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia Kamati zote mbili kwa pamoja. Kwanza nitaanza na Kamati ya Miundombinu; umefika wakati sasa namna ambavyo tunaendea ujenzi wa miundombinu yetu ya nchi iwe zaidi ya kimkakati na kwa nini ninasema hivyo?
Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya miundombinu ambayo ukienda kuijenga sio miundombinu ambayo inakuwa ni mzigo sana kwa Serikali bali in the long run miundombinu ile inakuwa na tija na yenye kuleta fedha nyingi na mapato mengi kwa Taifa na nitatolea mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea katika Kisiwa cha Mafia, kisiwa hiki kinapata wastani wa watalii kama 6,000 hivi mpaka 7,000 kwa mwaka mzima, lakini Kisiwa cha Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba kwa umoja wao wanapata watalii mpaka 600,000 kwa mwaka, utaona tofauti hizo. Sasa sizungumzi kwa maana ya ku-compete, nazungumza kwa maana ya ku-complement each other. Kwa nini Mafia inakuwa na watalii wachache, ni kwa sababu miundombinu yake haiingiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo hicho ninachokisema kwamba kama ujenzi wa miundombinu utakwenda kimkakati zaidi kwa maana ya kufungua fursa zaidi za kiutalii kwa maeneo kama haya ya Mafia na maeneo mengine tunaamini kabisa badala ya kuwa ni mzigo kwa Serikali in the long run kutakuwa na mapato mengi sana kwa Serikali na vitu vyenyewe nitavielezea kwa muhtasari tu kwa sababu muda sio rafiki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni namna ya accessibility ya kuingia Mafia. Kwa sasa namna pekee salama na ya uhakika ni usafiri wa ndege ambao gharama yake ni kubwa sana, flight ya nusu saa inagharimu Sh.167,000. Kwa mwananchi wa kawaida ambaye uwezo wake ni mdogo, huo ni mzigo mkubwa sana. Sasa alternative yake ni kupita baharini ambako sasa kule baharini hali ya miundombinu sio nzuri. Vyombo vya usafiri ni vya magogo, havipo salama na kipindi kama hiki cha upepo mkali ambao upepo unaitwa upepo wa kaskazi inakuwa ni shida, inabidi wazuiwe abiria wasisafiri kwa muda wa wiki, wanakaa wanarundikana na inaleta shida kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mafia tumepatiwa gati pale, Gati la Nyamisati, gati la kisasa kabisa, zuri kabisa, kwamba walau sasa hata kama chombo cha usafiri cha kisasa kitakapokuja kinao uwezo sasa wa ku-dock mahali na kupakia na kushusha abiria pamoja na mizigo yao kwa salama kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamilifu wa Gati lile la Nyamisati utakuwa hauna maana sana kama hatutakuwa na usafiri wa boti ya kisasa baina ya Nyamisati na Kilindoni Mafia. Kwa nukta hii pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais; kwenye bajeti ya mwaka huu tumewekewa shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kujenga boti ya kisasa ambayo itakamilika ndani ya muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichanganya haya, ule mzigo ambao pengine wasafiri walikuwa wanaubeba mkubwa sana wa ndege na watalii wengi kwao wao kupanda boti ni sehemu kama ya adventure ya kwenda mahali, tunaamini sana utafungua sasa fursa nyingi zaidi kwa maana ya kwamba watalii watakuja wengi sana kwenda kutembelea Kisiwa cha Mafia baadaye na Serikali nayo itapata mapato mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo, miundombinu ya uwanja wa ndege; pale Mafia kuna uwanja wa ndege ambao runway yake ni urefu wa kilometa 1.6. Kwa urefu wa kilometa 1.6, ndege ambazo zinaweza zikatua na kuruka pale ni aina ya Fokker pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa tunataka utalii na baadhi ya watalii wanapenda zaidi wawe na direct flight kutoka wanakotoka, sasa ndege kubwa kama hizi za Boeing 737 na nyingine haziwezi kuja kutua moja kwa moja mpaka Mafia kwa sababu uwanja wa ndege una urefu wa kilometa 1.6 na unahitaji uwanja wa ndege wenye urefu wa angalau kilometa tatu na kuendelea ili kuweza ku-accommodate ndege kubwa zinazokuja moja kwa moja kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu na ni ushauri kwa Mwenyekiti makini kabisa na ni miongoni mwa the finest brains za Wenyeviti wa Kamati, Mheshimiwa Kakoso; atusaidie pale Mafia sasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iweze ku-extend ile runway kutoka kilometa 1.6 kwenda kilometa 3.0 ili kuweza kuruhusu ndege kubwa kutua pale na kuruka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litakwenda sambamba na ujenzi wa terminal building; tuna ka-terminal building pale kadogo sana ambako hata ndege aina hizi za caravan ambazo zinachukua abiria 12 na 13 zikitua mbili tu mnakuwa mmesharundikana pale passenger’s lounge. Kwa hiyo tunaomba sana upanuzi wa uwanja wa ndege huu uende sambamba na ongezeko la ujenzi wa terminal building.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Mafia kama nilivyotangulia kusema ni Kisiwa cha kitalii na utalii kwa sasa, kwa sababu kisiwa kimegawanyika katika maeneo makubwa mawili; eneo la kaskazini na eneo la kusini. Hili eneo la kusini ambapo ndipo kiwanja cha ndege kipo na shughuli za kiutawala kwa maana ya halmashauri na ofisi nyingine za Kiserikali zipo, pale miundombinu iko sawa kwa sababu watalii wakitua wanakwenda kwenye mahoteli moja kwa moja. Hata hivyo, kutoka pale Makao Makuu ya Wilaya kwenda moja kwa moja mpaka kaskazini kule kwenye light house ni kama kilometa 55 na ndiyo kabarabara kenyewe kamoja hakohako tu kama roho. Mheshimiwa Waziri Kwandikwa, mjukuu wangu, hebu kwanza watusaidie pale Mafia watumalizie hizi kilometa 55, sisi tena tunakuwa tumeshaagana na wao, tukiomba tutaomba mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kwa namna ya kipekee sana, tukimaliza ujenzi wa barabara hii ya kilometa 55, tutafungua na fursa za kiutalii upande wa kaskazini mwa Mafia ambapo nako pia kuna fukwe nzuri na kuna maeneo mengi sana ambapo mahoteli na ma-lodge yanaweza yakajengwa na kuweza kupata watalii wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la mawasiliano; namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Engineer Nditiye, alishafika pale Mafia na akaona changamoto zetu. Sisi kule zao letu kubwa ni zao la nazi, kwa hiyo minara ya simu inapata kidogo obstacles kwenye kurusha signals zake kwa sababu kunahitaji minara mingi zaidi kutokana na uwepo wa minazi mingi. Sasa maeneo mengi ya vijiji vya Mafia yanakosa mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Mawasiliano tuangalie kwa sababu eneo linapokuwa tena la kitalii na watalii siku hizi dunia imekuwa ndogo, imekuwa kijiji, wanataka zaidi kufanya mawasiliano ya intaneti, ya simu na vitu vingine, ingependeza zaidi tukawa na mawasiliano ya uhakika zaidi. Najua hilo lipo katika mikono salama kwa sababu watu wa Mfuko ule wa Mawasiliano kwa Wote na Mheshimiwa Naibu Waziri alinihakikishia kwamba watalifanyia kazi hilo ili kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri pale Kisiwani Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa harakaharaka tu nizungumzie kidogo na Wizara…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau kwa mchango wako mzuri sana na ushauri, kwa hiyo muda wetu ndiyo huo, tunakushukuru sana.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)