Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima nikaweza kuwepo mbele ya Bunge lako. Nikushukuru wewe binafsi kwa mambo mawili; moja umefanya kazi yangu au ya Wabunge wengine iwe rafiki kwa kuleta hii Bunge Mtandao, yaani unasoma bila matatizo na mambo yana-flow yenywe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia sekta za leo, hizi sekta mbili ndizo sekta mhimili za uchumi jumuishi. Yapo maswali, ziko hoja nyingi za kwamba uchumi unakua, watu wako vipi, ukitaka watu na uchumi ukue lazima uguse hizi sekta hizi, zinaitwa sekta za uchumi jumuishi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufikisha pongezi zangu mezani kwako, nichukue fursa hii kumshukuru Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Luhaga Mpina. Watu wa Rutoro na vijiji vyake na watu wa Misenyi wanamshukuru kwa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. Tumekuwa na migogoro muda mrefu kati ya NARCO na wananchi lakini kwa kauli yake ambayo ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais migogoro ile ameimaliza. Nachoomba kwa Serikali Mheshimiwa Mpina sasa toa maelekezo wa watekelezaji wako ili washirikiane na Serikali ya Mkoa wa Kagera waweze kuonesha wananchi watakuwa wapi wakifanya shughuli zao na NARCO watakuwa wapi wakiendelea na shughuli za mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichangie mchango wangu katika taarifa hizi za Kamati. Niwapongeze Wenyeviti wote na Kamati zao zote mbili. Napenda nizungumze kidogo kuhusu suala la mifugo. Katika mchango wa Kamati, imeelezea vizuri sana Tanzania ni namba mbili kwa idadi ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, napenda nizungumze kwa masikitiko kwamba tuna idadi ya mifugo, hawa ng‟ombe tulionao huwezi kuwapeleka sokoni na Kamati imezungumza tatizo la masoko. Nyama yetu haiwezi kuuzwa kwa sababu tuna idadi ya ng‟ombe kinachotakiwa katika soko la dunia ni nyama quality, kuna watu ambao wanajali afya zao. Kwa hiyo, niungane na Kamati kusema kwamba Serikali inapojenga uchumi jumuishi lazima iwekeze katika mifugo. Wizara hii lazima isaidiwe kama Kamati inavyosema, kusudi tuweze kutengeneza malisho na kuzalisha mifugo yenye tija.
Mheshimiwa Spika, taarifa nilizonazo Tanzania ina fursa ya kuzalisha lita milioni nne za maziwa kwa siku lakini tunazalisha lita laki moja au laki moja na nusu. Tukizalisha lita milioni nne kwa siku maana yake tutaongeza afya ya Watanzania, tunaweza kufikia hatua hata ya kugawa maziwa bure kwa watoto wa shule. Taarifa nilizonazo ni kwamba huu ukanda wa Dodoma, Iringa na Mbeya mnaweza kuchakata zaidi ya lita milioni moja kwa siku, lakini ukanda wa Tanga kwenda mpaka Moshi kuna opportunity ya kuchakata lita milioni moja kwa siku, ukanda wa Kagera kwenda kwenye hizi hifadhi tunazogombania kuna uwezo wa kuchakata lita zaidi ya milioni moja. Ina maana lita milioni nne kwa siku wananchi wote watajumuishwa. Kwa hiyo, hakuna atakayelalamika kwamba uchumi wa vitu unapanda wa watu unadhoofu. Ni kwa sababu, watu moja kwa moja watakaokwenda kuuza maziwa wataweza kuhusishwa katika mchakato huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Kamati ya Bajeti ambalo linahusiana na hapa, suala la mazao. Iko Tume ya Serikali wanasema ilichunguza bei ya ngozi kwamba ngozi zetu haziuzwi. Napenda nichangie katika Kamati hii na Kamati ya Bajeti, ngozi ni bidhaa ya kigolobali, it is a global product, huwezi kuichunguza hapa. Unapochunguza soko la ngozi lazima uangalie Pakistan anafanya nini kwenye sekta ya ngozi na wewe Tanzania unafanya nini? Huwezi kujaza kodi kwenye sekta ya ngozi Tanzania au kwenye industrial sector ya ngozi Tanzania wakati Pakistan anaiacha ngozi iende ishindane duniani ukaweza kushindana naye. Nilipaswa nilizungumze hilo tuweze kulielewa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye sekta ya uvuvi, mimi nusu ya Jimbo langu ni maji, ninavyo visiwa tunafanya shughuli ya uvuvi. Nikubaliane na Mheshimiwa Waziri na Serikali namna mlivyodhibiti uvuvi haramu, nakubaliananalo, nawapa mapendekezo. Njia mnayotumia sasa haiwezi kuwa endelevu, ili kuleta udhibiti ulioendelevu nashauri muwashirikishe wananchi wa sehemu husika. Kabla wavuvi wengi hawajaja, hawa wanaofanya samaki wapotee, katika maeneo ya kwetu walikuwepo wavuvi, kwetu Bumbire, Goziba, Kelebe, Bakibwe wavuvi walikuwepo, sasa huwezi kuja na mapolisi kuzuia uvuvi haramu bila kumhusisha mzee wa mahalia. Huyu mzee wa mahalia pale lazima umuhusishe akuambie mwenye kokoro ni nani, aweze kutoa taarifa. Wewe katika mapato makubwa unayompa lazima urudishe kwa mtu wa pale ili aweze kuona shughuli zinazofanyika na yeye ana manufaa, nilitaka nilizungumze hilo.
Mheshimiwa Spika, lakini tumezungumza katika Kamati ya Kilimo sikuona suala la soko. Tunalo tatizo la soko la mazao, ni kipaumbele na ni kikwazo kikubwa. Nipenda kuzungumzia mahindi na nafaka. Ili tuweze kutafuta soko la uhakika la mazao yetu, hasa nafaka, lazima Taifa lijikite kwenye kujenga storage capacity, hizi silos, ma-godown. Kenya yuko mtu mmoja anao uwezo wa kutunza tani laki saba. Sasa Serikali iige mfumo wa sekta ya mafuta ihamasishe sekta binafsi tuwe na uwezo mkubwa wa kuhifadhi.
Mheshimiwa Spika, jambo lililo wazi katika ukanda wetu wa Afrika haiwezi kupita miaka mitatu hatujapata shida ya chakula, Mungu atunusuru. Haya mafuriko na wale nzige tutapata shida ya chakula hata tufanyeje. Sasa kama tungekuwa na storage capacity kubwa ya kutunza tani milioni nne na Serikali katafuta mfumo mzuri wa ku-finance watu wanaleta mazao yanakuwa managed, halafu benki zinatoa mikopo. Ina maana mazao yangenunuliwa, mkulima kaondoka, halafu kile chakula kikabaki kwenye silos. Haiwezekani, lazima tutapata jirani yetu mwenye shida ya chakula na sisi kwa sababu tuna faida ya uoto tungeweza kuwa-supply hawa wenzetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Kamati na Serikali kwamba tuwekeze kwenye silos. Kasi ya Serikali kuwekeza kwenye storage ni ndogo sana. Tuongeze kasi ya kuweza kuongeza storage capacity kusudi tutumie hizo finance modalities tuweze kuwa na chakula cha kutosha.
Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo mazingira ya biashara na nimshukuru Mheshimiwa Jitu umenikumbusha Blue Print Regulatory Reform. Nimesikitika tunapokwenda kwenye kuuza mbogamboga, tunapozungumzia avocado, kwenda kuuza avocado Ulaya ukiangalia tozo zinazotozwa inaonekana kama mkulima labda anapewa adhabu. Ni vilevile hata kwenye samaki, mmezungumza samaki hawana soko lakini linganisha tozo na kodi tunazotoza sisi upande wa Tanzania na wanazotoza wenzetu wa Kenya na Uganda, landing fee ya ndege Mwanza na landing fee ya Entebe ni tofauti, lakini kontena la minofu ya samaki linapotoka kwenye kiwanda Mwanza linatozwa kiasi gani na wenzetu wa upande wa Uganda wanatoza kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, tunapokuwa tunazungumzia bidhaa zetuna nizungumze hili, ili tuweze kujenga uchumi na shilingi iliyo imara lazima tu-export zaidi. Hatuwezi kulenga kujitosheleza hapa, tulianguka zamani kwa sababu tulilenga kujitosheleza, we must invest in import substitution come export promotion. Kwa hiyo, kujitosheleza-kujitosheleza hakutatusaidia, lazima uuze nje na lazima tuuze nje kwa mazao haya niliyoyasema kwamba ndio yanashikilia uchumi jumuishi. Uchumi jumuishi uko kwenye kilimo, mifugo na kwenye utalii kwa sababu wananchi wazawa wa Tanzania wataweza kuhusika moja kwa moja na kuweza kupata kipato. Kwa hiyo, uchumi wa vitu na wa wananchi utaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache nawapongeza Wenyeviti wa Kamati hizi mbili. Naipongeza Serikali, tuongeze nguvu, mwelekeo wetu ni mzuri.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)