Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia. Kwanza kabisa nawapa pongezi Wenyeviti wote wawili wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Kamati ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimimwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri hasa kwa upande wa Kilimo, Maji pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nawapa pongezi sana hasa kwa upande wa mifugo, kwa kweli mambo waliyoyafanya yote yanaonekana ni mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kilimo, naomba nichangie kuwa wote tunajua kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo. Pia kilimo kinachangia kwa asilimia 30 ya pato la Taifa na asilimia 95 ya chakula kinatokana na kilimo, asilimia 30 ya mauzo ni ya nje na asilimia 70 malighafi inachangia malighafi ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, nikisema hivyo, naomba na ninashauri kuwa kilimo kipewe kipaumbele na hasa kwenye bajeti tunayokuja kutunga hapo baadaye kuwa asilimia 10 ya bajeti nzima iweze kwenda upande wa kilimo ili kuweza kutekeleza Azimio la Abuja pamoja na Malabo.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na ninaipongeza Serikali kuona Tume ya Umwagiliaji imerudishwa Wizara ya kilimo kutoka Wizara ya Maji kwa sababu tangu wameingia huko kwenye Wizara ya Kilimo, ndiyo wenyewe tunategemea sana kilimo cha umwagiliaji. Huwezi kuongea kilimo cha umwagiliaji bila ya kuongea kilimo. Kilimo cha umwagiliaji ndicho tunachotegemea sana kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Umwagiliaji tangu wamehamia Wizara ya Kilimo, nawapongeza Serikali pamoja na Benki ya Dunia kwa kuweza kukamilisha vizuri mradi wa kuongeza mpunga unaotekelezwa huko Mkoani Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Tume ya Umwagiliaji imeweza pia kukamilisha miradi mingine, pamoja na skimu 10 kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo alivyoisema kwenye Kamati yetu ambayo tumeiorodhesha. Ila tatizo lililopo ni kuwa walikuwa watekeleze tena miradi mingine mitano lakini hawakuweza kuitekeleza kwa sababu ya tatizo la fedha. Ninaloshauri na tunaloshauri ni kuwa fedha za maendeleo na hasa zinazotoka kwenye nchi yetu naomba ziwe zinatengwa za kutosha na ziwe zinatolewa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, wote tunaelewa kuwa mboga mboga na matunda ni muhimu sana kwa afya ya binadamu na hasa kwa upande wa lishe ya binadamu kutoka kwa mtu mzima mpaka kwa mtoto, tunahitaji kupata matunda pamoja na mboga mboga pamoja na vyakula vingine. Kwa hiyo, kilimo cha mboga mboga na matunda kinaajiri watu zaidi ya 8%.
Mheshimiwa Spika, ninachoshauri hapa ni kuwa soko lipo ila uzalishaji bado haujawekwa sawa sawa. Kwa hiyo, nilichokuwa nashauri, uzalishaji kwa wingi uweze kuangaliwa, pia na soko la uhakika liweze kuonekana vizuri sana kwa sababu kilimo cha mboga mboga na matunda unakuta ni vijana wengi na akina mama ndiyo wanaolima kilimo hiki.
Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa lililopo ni tozo na kodi ambapo Kamati imeona kuwa ni zaidi ya 45 hivi. Hii tuliongea na TAHA ambao ndiyo sana sana wanaoshughulika na mambo ya kilimo cha mboga mboga na matunda.
Mheshimiwa Spika, kilimo mseto wote tunakijua. Kilimo mseto ni kuchanganya changanya mazao mbalimbali, hasa ndiyo kilimo mseto ambapo wakulima wadogo wadogo Tanzania tumekizoea sana. Kilimo hifadhi ni ile unalima mazao yanafunika udongo, unyevunyevu unabaki, halafu unaweza ukafanya kilimo cha kubadilisha badilisha kiasi rutuba inabaki kwenye udongo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri kuwa kilimo mseto pamoja na kilimo hifadhi viweze kuhimizwa kwa wananchi kwa sababu kama unatumia kilimo mseto na unatumia unachanganya kwa mfano mahindi pamoja na karanga au pamoja na maharage, zile nodules mizizi yake inatengeneza nitrogen. Kwa hiyo, kama inatengeneza nitrogen unaweza ukapunguza matumizi ya mbolea ya kemikali na ukatumia hiyo mbolea ya asili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nawapongeza sana kwa upande wa mifugo. Mmefanya vizuri, mmepunguza mambo mengi, samaki wameongezeka kwenye mifugo, lakini soko bado samaki bei iko juu. Kwa hiyo, tunaomba sana kuhusu hilo. Pia nawapongeza kwa sababu ya kutoa 0.4 mrabaha ambao inaweza ikachangia kuleta mapato mengi kwa muda hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bandari, nilikuwa nashauri tena, najua Serikali iko kwenye mkakati wa ujenzi wa bandari, lakini mpaka sasa hivi bado hawajaamua ni wapi itajengwa hii bandari. Hapo naongelea uvuvi wa bahari kuu. Kwa hiyo, naomba ili tuweze kuongeza kipato cha nchi yetu lazima tuangalie uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kingine ni ufugaji wa viumbe kwenye maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na Mwenyezi Mungu akubariki zaidi na zaidi. Ahsante.