Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wa Kamati kwa mawasilisho mazuri, lakini pia nawapongeza baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri wanaoshughulika na hizi Kamati za Kisekta.
Mheshimiwa Spika, nitazungumza kwa haraka haraka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, nitajikita sana kwenye Sekta hii ya Utalii. Kumekuwa na mpango wa kuboresha utalii Tanzania nzima na hasa ukanda ule wa Kusini; na Serikali imejikita kwenye kukopa fedha Benki ya Dunia. Hizi fedha tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili, huu ni mwaka wa tatu hivi sasa, zililetwa fedha za regrow kwa ajili ya kukuza utalii maeneo ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hizi fedha mpaka leo hazieleweki kwamba zinapelekwa wapi? Taarifa zinaeleza kwamba wanapeleka mikoa ya kule Iringa na Mkoa wa Morogoro. Wameacha mikoa ya Kusini halisi ambayo ni Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, tunaomba Wenyeviti watakapokuja kuhitimisha hizi hoja, hili suala watueleze kinagaubaga kwamba kwa nini mkakati wa fedha za regrow ambazo ni fedha za mkopo wa Serikali na kazi yake ni kuboresha utalii Southern Circuit, tukimaanisha Mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara na Lindi kwa kiasi kikubwa, bado hakuna mpango wa kuboresha miundombinu ya barabara kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo barabara ya Selous kule kutoka Nachingwea kuelekea Liwale na mvua hizi, haipitiki kabisa, lakini hizi fedha zipo, Waziri anashindwa kuzileta kwa ajili ya kuboresha miundombinu ile ili watalii waweze kupita kuanzia pale Lindi Nachingwea mpaka kule Liwale. Hizo ni fedha za regrow ambazo ni mkopo wa kuboresha miundombinu ya mikoa ya kusini katika Sekta ya Utalii, tunaomba zifike Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kuna suala hili la utalii wa mambo kale tunaona kama limesahaulika hivi. Pale Mikindani tuna majengo ya mambo kale kule Mtwara ambayo hayapo Tanzania yote hii, yapo Mikoa ya Mtwara hasa hasa Mikindani, Mtwara na Lindi. Pia kuna ule ufukwe wa bahari ambao unaanzia kule Msimbati mpaka kule Kilwa Kisiwani. Tunaomba Serikali itupe mpango maalum wa kuuboresha na kutangaza yale maeneo ili tuweze kuleta watalii wengi kwa ajili ya kuliingizia Taifa hili Pato.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tuna taasisi ile inaitwa TAWA ambayo iko affiliated katika Wizara. Tulikuwa tunaomba sana, wakati fulani tuliwasikia kwenye Kamati yetu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wakaeleza changamoto zao ni nyingi sana, lakini changamoto kubwa ni kwamba ile Taasisi ya TAWA ambayo imepewa mamlaka ya kuweza kutangaza vivutio mbalimbali vya maeneo ya Pwani, kwa mfano ule Kilwa Kisiwani, yale majengo ya kale tunaomba ipewe mamlaka kamili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la ajabu kwenye hii Taasisi ya TAWA, kuna wafanyakazi ambao walipewa training kwa miaka mitatu hivi sasa, wale wafanyakazi ambao walipaswa kuibeba ile Taasisi ili iweze kufanya kazi sawasawa na kuwa na mamlaka kamili, wale wafanyakazi wamehamishiwa Wizarani. Sasa sijui mkakati wa Serikali ukoje wa kuhakikisha ya kwamba TAWA inapewa meno ya kutosha, inakuwa ni taasisi ambayo imesimama yenyewe kama ilivyo Ngorongoro na TANAPA ili iweze kujitangaza na kutangaza maeneo ya kiutalii.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu TAWA imepewa maeneo ya Pwani, sisi tunaamini kwamba ingekuwa na mamlaka kamili, ingeweza kusaidia kutangaza utalii maeneo yale yote ya bahari na fukwe zote na mambo kale. Ilishawahi kusemwa hapo nyuma kwamba wanyama hawa wanaenda wanakufa, mabadiliko ya hali ya nchi, hawa wanyama watapotea, utalii utakaobaki ni utalii wa mambo kale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali isidharau mambo kale. Tunahitaji miji hii ambayo duniani yamaingiza fedha nyingi sana. Kwa mfano, kuanzia pale Mikindani kwenda kule Kilwa Kisiwani na maeneo yote ya Zanzibar, Serikali iweze kuboresha, tuhakikishe kwamba inaboresha miji hii na inaitangaza ili tuweze kuingia fedha nyingi za utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, tunaomba sana kwenye Sekta ile ya Uvuvi, basi tumekuwa tunazungumza kwenye Bunge hili kwa muda mrefu iweze kutengwa bahari ya uvuvi. Sasa imekuwa ni historia tu kila siku inazungumzwa kwamba ile bandari ya uvuvi haijengwi. Wizara haitengi fedha, Waziri hatengi fedha.
Mheshimiwa Spika, Tanzania tumebarikiwa, Wazungu wanasema Tanzania ina virgin sea (bahari bikira), ina samaki wengi sana, kuanzia ile strip ya Kusini kule mpaka Zanzibar, hakuna bahari ya uvuvi. Tunaomba Serikali mwaka huu ije na mkakati maalum kuweza kutenga bandari ya uvuvi ili wavuvi wetu waweze kuvua na kuwa na masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika za nyongeza. (Makofi)