Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kupata fursa hii japokuwa muda ni mchache. Napenda kuchangia zaidi, eneo la kwanza ni eneo la mbegu. Bado nchi yetu na Wizara hasa hatujawa serious kwenye mbegu. Nchi inapoteza fedha nyingi kwa ajili ya uagizaji mbegu.
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo sasa hivi, tulitarajia na Waziri alikuja kutuambia hapa tunategemea kwamba tungeweza kujitosheleza kwa mbegu kwa asilimia 20 mpaka 30, lakini hali ilivyo kwa nchi yetu tumeweza kutoa mbegu siyo zaidi ya asilimia 19. Hivyo nchi imetumia zaidi ya trilioni 1.8 kuagiza mbegu kutoka nje. Maeneo tunayo, watafiti wapo, vituo vipo, tatizo hatujaamua kuwekeza katika eneo hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla iangalie katika eneo ambalo tunapoteza pesa nyingi wakati uwezo wa kuzikabili hizo changamoto upo.
Mheshimiwa Spika, kingine katika eneo hilo, kuna tafiti ambazo zinahitajika ziweze kuendelea. Ile mbegu ya pamba tunayoendelea nayo mwaka huu ni wa mwisho, tunatakiwa tuwe tumetoa mbegu nyingine ambayo itachukua mbadala wake, kwa sababu ikiendelea kuzalishwa ile, huko mbele haitakuwa na mavuno yoyote, itakuwa imeshamaliza muda wake wa uzalishaji. Sasa sijui Wizara na Bodi ya Pamba ina mkakati gani katika eneo hilo. Naiomba Wizara tuangalie zaidi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala zima la pareto. Hapa kuna changamto hasa kwenye Bodi ya Pareto. Viongozi ni tatizo kubwa na ndiyo maana Sekta ile haiendi mbele. Bado tumewaruhusu baadhi ya watu ambao wananunua zile pareto zinakwenda kuchakatwa nje ya nchi, wakati mikataba ya kununua pareto tunataka kuiona ile crude oil inatoka hapa na kunufaisha watu wetu ndnai ya nchi wapate ajira lakini tupate raw material ambayo tunaweza kuitumia kwa uzalishaji wa vitu mbalimbali. Sasa leo mchakato wa umalizaji wa pareto unaenda kufanywa Kenya kwa sababu ipi?
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri hapa aje na majibu, atueleze sababu ni zipi wakati mikataba haiko hivyo? Ni kiwanda kimoja tu ambacho kinachakata hiyo crude oil na inapatikana hapa na tunauza na kuweza kupata faida na kodi zinatozwa. Kwa hiyo, tunaona tatizo ni Bodi ya Pareto na usimamizi wake bado umekuwa ni tatio kubwa.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa sababu ya muda, bado tunarudia tena kwenye Sekta ya Uvuvi, hatunufaiki. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuifanyia kazi 0.4, kule Zanzibar imeanza kuleta matunda. Juzi tu baada ya mwezi mmoja na nusu baada ya kuruhusu ile 0.4 ambayo ni probation period, zaidi ya meli 27 zimeshasajiliwa na tunatarajia meli nyingine zaidi ya 60 zitaweza kusajiliwa, hivyo kuifanya ile Mamlaka ya Uvuvi iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi lililokuwepo, kuna akiba kubwa ya samaki ambao sasa hivi wanahitaji kuvuliwa. Ni eneo la buffer zone ambalo lipo baina ya Msumbiji na Mtwara. Eneo lile lina samaki wasiopungua zaidi ya milioni 50 wa tuna wazee walioko kwa miaka zaidi ya minne, mitano, wanahitaji kuvuliwa kwa percent maalum ambazo sisi kama nchi tungeingiza pesa nyingi tukaingia udau na wale ambao watavua kwa sababu sisi hatuna vyombo vya kuvulia. Samaki wale sasa hivi wanakula samaki wadogo wanaozaliwa katika eneo lile. Tunahitaji tuweze kujiwekeza katika eneo hilo, tuwavue.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ni ombi. Wenye meli kubwa wakitaka kuleta ombi hilo kwa kuvua, tuwaruhusu kwa sababu akiba tuliyokuwa nayo katika eneo letu hilo la mazalio ya samaki kutoka Kizimkazi, Kitutio Mafia mpaka Mtwara ni zaidi ya milioni 70 ya samaki wako katika eneo lile, wanatosheleza kabisa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Rehani.