Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuhitimisha hoja ya Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Kamati yetu imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wanane. Pia nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wote; Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, nikianza na Mheshimiwa Jitu Soni, amezungumzia suala la miundombinu mibovu katika hifadhi zetu za Taifa. Hili suala ni kweli, nasi kama Kamati ya Maliasili tumelizungumzia kwenye Kamati yetu na tukatoa mapendekezo kwa Serikali ifanye utaratibu wa haraka kushughulikia miundombinu yote ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu Wizara ya Maliasili ina mchango mkubwa sana wa pato la Taifa katika nchi yetu. Kwa hiyo, kuboresha miundombinu hii kutawezesha watalii wetu wa nje na ndani kufika kwenye hifadhi zetu kiurahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jitu Soni pia alizungumzia miradi ya ujirani mwema ya TANAPA. Mawazo yake ni mazuri na nina imani Wizara imechukua maoni yake na itayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mchangiaji wa pili alikuwa Mheshimiwa Mch. Msigwa ambaye alizungumzia masuala ya utalii kuhusu Wizara kutofanya jukumu la kutangaza watalii kutoka nje kwa sehemu kubwa linalofanywa na makampuni ya utalii. Nianze kwa kuonyesha kwanza masikitiko makubwa kwamba Mheshimiwa Msigwa ndio Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii na jitihada zote zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii hazioni.

Mheshimiwa Spika, kazi inayofanywa na Wizara ni kubwa, watalii wameongezeka Mheshimiwa Waziri ametuambia kutoka milioni moja mwaka 2015, mpaka milioni 1.5 mwaka 2020 ambayo tupo. Suala lingine ambalo Mheshimiwa Msigwa alizungumzia ni kuhusu wasanii wetu wa ndani. Napenda nimwambie Mheshimiwa Mch. Msigwa, utalii ni two way traffic; tunahitaji watalii wa nje na vilevile tunahitaji sana watalii wa ndani. Tanzania ina watu zaidi ya milioni 50 na mpaka sasa tunavyozungumza ni watalii 600,000 tu wa ndani ambao ni Watanzania kwa takwimu za mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ni jukumu letu sote kama Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi wa wananchi wa Tanzania ambao tumo humu ndani kulisemea na kufanyia kampeni nchi yetu. Wote tuendelee kusema na tuwashawishi Watanzania wenzetu waende kutembelea hifadhi zetu kwa sababu pia tunahitaji sana watalii wa ndani ambao wanatokana na sisi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mch. Msigwa vilevile amezungumzia masuala ya wasanii wetu wa ndani na akatoea mfano wa Steve Nyerere. Mheshimiwa Waziri amelizungumzia hili vizuri, lakini kwa kuongezea tu, huyu Steve Nyerere ana segment ya watu ambao wanamfuata na ni muhimu pia kwa hao watu. Kwa hiyo, ni vizuri tusiwabeze wasanii wetu wa ndani kwa sababu wanakubalika ndani na vilevile na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Getere amezungumzia kuhusu utalii wa ndani, nadhani nimeshalizungumzia hilo. Pia ameongelea suala la TANAPA ambalo tumeshalileta kwenye Bunge lake Tukufu. Ni katika miaka minne yote ambayo nimekuwa kwenye hiyo Kamati, tumelizungumzia mara kadhaa, tumeomba TANAPA wapunguziwe tozo kwa sababu hifadhi zimeongezeka kutoka hifadhi 15 zilizokuwepo mpaka 22 sasa hivi tunavyozungumza na hifadhi tano tu ndizo ambazo zinaweza kujiendesha na hifadhi mbili ya Serengeti na Kilimanjaro ndizo ambazo zinachangia kuendesha hifadhi nyingine ambazo haziwezi kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mzigo walionao ni mkubwa. Ni vyema kabisa Bunge lako Tukufu tukaishauri Serikali kutafuta namna bora ambayo itaiwezesha TANAPA kuweza kukidhi mahitaji waliyonayo. Kwa mfano, mdogo tu ambao tunaweza kuutoa, watu hawa wa TANAPA wanafanya SCR (Social and Cooperate Responsibilities) lakini katika kazi ambazo wanazifanya za kijamii kwa mfano wakijenga shule au wakifanya shughuli yoyote ya kijamii bado wanatozwa kodi kwenye kazi ambazo wamezifanya; na kazi hiyo wanazozifanya ni kubwa na ni nyingi. Kwa hiyo, kwa kuwapunguzia tu hata hiyo, tutakuwa tumepunguza mzigo ambao utawawezesha kwenda kufanya mambo mengine na kwenye hifadhi nyingine kuziboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchangiaji mwingine anayefuata ni Dkt. Kiruswa, amepongeza Wizara na Serikali kwa kazi inayofanya. Mheshimiwa Kiruswa pia amezungumzia suala upimaji wa ardhi ambayo napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza, kazi ya kupima na kupanga ardhi ya nchi hii imepewa mamlaka hiyo. Siku zote traditionally imekuwa kazi ya TAMISEMI, lakini ukweli ni kwamba mpaka leo ardhi ambayo imepimwa ya nchi hii ni chini ya asilimia 20 ambayo kwa kweli siyo kitu kizuri. Ndiyo maana tumekuwa na migogoro mingi ya ardhi, wafugaji na wakulima. Kwa sababu ardhi kubwa ya nchi hii haijapimwa na kupangwa.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha nyingi sana na kuwapa Wizara ya Ardhi ambayo kuna miradi mikubwa miwili ambayo itakwenda kupima, kupanga maeneo yote ya Tanzania. Ardhi yote ya Tanzania itapimwa na kupangwa. Hili siyo tu kwamba litaongeza mapato kwa sababu ya kulipia hati ambazo wananchi watakuwa wamepata, lakini vilevile itapunguza migogoro mingi sana ya ardhi ambayo inaendelea katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, maendeleo hayana chama, wote tunafahamu. Naomba kuchukua fursa hii kukuomba kushauri Wabunge wote tuliomo humu ndani ya Bunge hili Tukufu, tuchukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kumpigia makofi mengi sana san asana kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya kupima na kupanga maeneo yote ya ardhi nchini mwetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mchangiaji mwingine alikuwa Mheshimiwa Rhoda ambaye amezungumzia suala la vijiji 920 ambalo Mheshimiwa Waziri amelitolea maelezo vizuri kabisa, nadhani amelielewa, nasi kama Kamati tunaunga mkono, lakini ripoti hiyo haijaja rasmi kwenye Kamati yetu na itakapokuja tutaiwasilisha Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maftaha amezungumzia suala la TAWA. Sisi kama Kamati kweli tunamuunga mkono na tumeliongelea kwenye ripoti yetu, TAWA tangu imeanzishwa bado haijapa sheria na haijajitegemea. Kwa hiyo, kuna mambo mengi ambayo inashindwa kufanya kama mamlaka kwa sababu hawana maamuzi ya kuweza kufanya kama mamlaka kamili. Kwa hiyo, tunaisihi Serikali, tunaiomba Wizara ifanye huu mchakato kwa haraka ili TAWA iweze kupata sheria yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dau amezungumzia suala la viboko wa Mafia; watu wamefariki, hili suala siyo kwa Mheshimiwa Dau peke yake, limejitokeza kwa Waheshimiwa Wabunge wengi, Mheshimiwa Gekul ameshalizungumzia hilo suala Bungeni hapa, Mheshimiwa Mulugo ameshatuambia wazazi wake wote wawili walifariki kwa sababu ya viboko huko Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, hili suala ni muhimu, nami na Kamati yetu tunaomba sana hili suala la viboko lifanyiwe utaratibu wa haraka ili tuweze kutatua changamoto hii ambayo inaleteleza vifo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba Bunge lako Tukufu lipitishe maazimio tuliyoleta mbele ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naafiki.