Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukutu tena kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Maziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga pamoja na Manaibu Mawaziri wake; Mheshimiwa Mgumba na Mheshimiwa Bashe.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Luhaga Mpina na Naibu wake, Mheshimiwa Abdallah Ulega. Naomba nichukue fursa hii tena kumpongeza Mheshimiwa Profesa Mbarawa Makame, pamoja na Naibu wake Jumaa Aweso kwa ushirikiano wanaotupatia kama Kamati na kazi nzuri wanazofanya katika kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kutekeleza baadhi ya maazimio ya Bunge lililopita. Naomba nichukue fursa hii tena kuiomba Serikali iendelee kutekeleza maazimio ya Bunge lililopita yale ambayo bado hawajayafanyia kazi. Nawapongeza wote waliochangia katika ripoti yetu. Katika wachangiaji 21, 20 wamechangia katika hii Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, nawapongezeni sana.
Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Kilimo hoja ambayo imechangiwa na Wabunge wengi ni suala la bajeti ndogo. Kila Mbunge alipokuwa anasimama hapa, ukiyasikiliza maelezo yake kwa kina alikuwa anazungumzia udogo wa bajeti; na siyo udogo wa bajeti tu; na kiwango cha pesa kinachokwenda katika utekelezaji wa hiyo bajeti.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati tuliliona hili, ndiyo maana katika miongoni mwa maombi yetu tumekuomba Wizara hii ya Kilimo iingie kwenye Wizara za vipaumbele kwa sababu ndiyo Wizara ambayo inaajiri Watanzania walio wengo na ndiyo Wizara inayotoa malighafi ya kutosha. Asilimia 80 ya malighafi hapa nchini yanapatikana katika Wizara hii ya Kilimo. Kwa hiyo, tunkuomba sana hii Wizara ya Kilimo iingie kwenye Wizara za vipaumbele.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Tanzania tuliingia kwenye Azimio Malabo au Maputo Declaration. Azimio hili linasema Serikali inatakiwa itenge asilimia 10 ya bajeti kuu kwa ajili ya Sekta ya Kilimo. Tunaiomba tena Serikali iliangalie jambo hili kwa sababu hata 4% katika bajeti kuu ambayo inakwenda kwenye maeneo ya kilimo haiendi. Eneo hili ni very sensitive na tunahitaji kuona viwanda vyetu vinafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, kama tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda, hatuna sababu yakutokuboresha katika sekta hii ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo lilichangia na baadhi ya Wajumbe wengi ni suala la horticulture; kilimo cha mboga mboga pamoja na kilimo cha matunda. Kilimo cha mboga mboga na matunda kitatusaidia kupata fedha nyingi za kigeni, lakini kuna tatizo katika eneo hili. Kuna takribani kodi zaidi ya 45 ambazo zinawakwaza kwa njia moja wakulima katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ifike wakati Serikali ilitambue jambo hili kusudi tuendelee kupata mapato ya kutosha tuangalie mchakato huu ambao uko kwenye blueprint, ifanyike mapema iwezekanavyo kusudi tuweze kuondokana na hii adha wanayoipata wakulima wetu. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amejitahidi kuzungumzia suala la mbegu, lakini katika suala la mbegu tatizo kubwa lipo, bado kuna tatizo la bajeti.
Mheshimiwa Spika, ili tupate mbegu bora na za uhakika, lazima tujielekeze katika kuwekeza kwenye eneo la utafiti. Hata hivyo, tuna shida kwenye eneo hili la utafiti. Mara nyingi tunazungumza kwamba Serikali imetenga asilimia moja kwenye bajeti kuu kwa ajili ya eneo hili la utafiti, lakini ni shilingi ngapi linakwenda kwenda kwenye eneo hili la utafiti? Kwa hiyo, ifike wakati Serikali ijiekeleze kwenye eneo hili kuongeza kwenye bajeti eneo la utafiki kusudi tuweze kupata mbegu za uhakika na nyingi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati tuliiomba Wizara ya Kilimo ifanye marekebisho ya Sera na Sheria ya Kilimo na iletwe Bungeni mapema ili kuondoa ukakasi uliopo. Mabadiliko haya yatawasaidia wakulima. Kwa mfano, mkulima wa mahindi wa Mufindi anapoanza kulima mahindi yake hakuna sehemu yoyote Serikali ina-interfere. Anaingia shambani, analima, anapanda, anaweka mbolea, anavuna. Anapoanza kuvuna tu, akitaka kuanza kuuza Serikali inaingia kati, inaanza kusema kwamba sasa hivi mahindi yasiuzwe. Kwa hiyo, ifike wakati tuwekewe Sera na Sheria iliyokuwa bora ambao itaondoa ukakasi uliokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo wamechangia wachangiaji wengi ni eneo la mifugo. Hili ni eneo muhimu na kama tulivyozungumza kwenye ripoti yetu kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi katika bara la Afrika, lakini je, kuwa wa pili katika Bara ya Afrika na kuwa na mifugo mingi inaleta tija? Hilo ndilo suala la kujiuliza.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya vizuri kupitia Wizara yetu ya mifugo kwa kupitisha chanjo nyingi kwa mifugo yetu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amelitekeleza zoezi hili vizuri, lakini bado kuna shida kwenye eneo hili. Kuna baadhi ya magonjwa ambayo yanatakiwa yaangaliwe kwa kina kusudi tupate ng‟ombe walio bora wenye quality bora kusudi tuweze kupata soko zuri katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi sisi kama Watanzania tuna soko la uhakika Dubai na Oman, lakini hatuna soko la uhakika nchi za SADC na Ulaya. Kwa nini hatuna soko la uhakika? Ni kwa sababu quality ya ng‟ombe wetu haijafikia hadhi ya nyama ambayo inaweza kuuzwa kwenye Soko la Dunia. Sisi kama Kamati tunaendelea kuishauri Serikali iangalie kwa kina kwenye eneo hili kusudi tupate ng‟ombe waliokuwa bora na tuweze kupata soko la uhakika katika nchi za Ulaya na SADC.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uvuvi ni muhimu sana kwa mustakabali wa uchumi wa nchi yetu. Kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa wavuvi wetu, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa uvuvi tena, alianza mchakato wa kuhakikisha tunafanya mabadiliko ya Sheria ya Uvuvi. Mchakato huu umechukua muda mrefu. Tunaomba mchakato huu uje Bungeni kwa sababu tunaamini kabisa mchakato huu ndiyo mwarobaini ya malalamiko ya wavuvi katika nchi yetu. Kwahiyo, miongoni mwa maazimio yetu, tunaomba Serikali iharakishe kuleta mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni eneo la maji. Katika wachangiaji wetu akiwemo Mheshimiwa Jitu Soni, amezungumzia kodi ya mitambo ya kuchimba visima iangaliwe. Ni kweli kuna haja ya kuangalia kwa sabbau Watanzania wana matatizo mengi ya maji. Kwa hiyo, Serikali iangalie zile kodi ambazo siyo za lazima kwenye eneo hili zipunguzwe kusudi watu wengi waweze kupata maji.
Mheshimiwa Spika, kuna shida nyingine, kuna watu wengi katika nchi hii wamejitolea kuisaidia nchi yetu katika Sekta ya Maji, lakini kuna tatizo. Wanapoanza kufanya kazi za kusaidia katika Sekta ya Maji kuna shida, wanapoagiza vifaa kutoka nje, Serikali inaendelea kuwatoza kodi nyingi ikiwemo VAT. Ifike wakati wale wote ambao wanasaidia nchi yetu kupata maji, Serikali isamehe kodi za VAT pamoja na kodi mbalimbali kusudi wale wafadhili wetu waweze kujielekeza zaidi katika maeneo makubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine la mwisho ambalo nataka kuchangia hapa ni eneo la force account. Wizara ya Maji imeamua kabisa kujielekeza katika kuhakikisha miradi yake inatatuliwa kwa utaratibu wa force account. Force account inapunguza gharama, inaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na inapunguza ubadhirifu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na faida hizi tatu tulizoiona hapo juu, lazima tuweke angalizo. Tunaweza kuwa tuna faida hizi za msingi hapa tatu, lakini je, ubora wa miradi uko sawa? Kwa hiyo, tujiangalie, tunapokwenda kwenye force account tuhakikishe na miradi yetu inakuwa bora.
Mheshimiwa Spika, la pili, tunawaondolea ajira Watanzania wengi wenye makampuni ya maji. Kwa hiyo, kwenye eneo hili lazima tuhakikishe Serikali inafanya kazi yake kuhakikisha na watu wengi ambao wamesajili makampuni ya kutekeleza miradi ya maji wanapata fursa ya kufanya hiyo. Kwa sababu kwa kuziondoa hizi kampuni za maji kunakosesha kodi kwenye Serikali na kunaondolea ajira vijana wetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, la mwisho wataalam wa kutosha kwa kutekeleza hiyo miradi ya force account hatuna. Wengi wamesimama kulizungumzia suala la force account, lakini kwa nini Wizara ya Maji imeamua kujielekeza kwenye force account kuna shida sehemu.
Mheshimiwa Spika, BOQ za miradi ya maji zinaandaliwa na wataalam wa Wizara ya Maji. Ifike sehemu Serikali iangalie wataalam wake wanavyoandaa hizo BOQ wanaandaa kwa uhalisia? Kama hawaandai kwa uhalisia Serikali iwachukulie hatua waandaji wote BOQ ambao wanafanya ulaghai katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, sasa naomba Bunge lako Tukufu lipitishe Maazimio tuliyoleta pamoja na marekebisho ya takwimu yaliyoletwa na Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi na Mifugo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, naafiki.