Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo imewekwa hapo mezani. Katika taarifa zote nilizosoma hakuna mahali katika Taarifa ya Utawala Bora na Utumishi ambayo imezungumzia group kubwa ambalo ni muhimu sana la watumishi wa Serikali, rasilimaliwatu. Kwa miaka mingi, minne sasa hawajawahi kuongezewa mshahara, na hili jambo nimeshalisema sijui mara ngapi katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa Serikali ikaweka katika bajeti ijayo mishahara kwa ajili ya kuwaongezea watumishi ambao hali zao ni mbaya na wanahitaji kuboresha maisha yao na kuendesha familia zao. Itengwe bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya watumishi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia suala la uhuru wa kutoa maoni. Awamu hii uhuru wa kutoa maoni umeminywa sana, ukitoa maoni yoyote ya kuikosoa Serikali, unatekwa au unapotezwa au unauawa au unafunguliwa kesi ya uchochezi. Wengine wamenyang‟anywa passports zao. Mfano mzuri ni yule Chief Executive wa TWAWEZA alinyang‟anywa passport, Mheshimiwa baba Askofu wa Kagera Niwemugizi, yeye pia alizungumza tu kuhusu Katiba mpya akanyang‟anywa passport yake na mpaka leo ninapozungumza hajarudishiwa passport yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ni pamoja na kumwambia huyu Askofu kama passport yake hairudishwi kwa sababu gani na lini atarudishiwa passport yake maana ni kama sasa yupo kwenye house arrest. Hawezi kutoka nje ya nchi kwenda kwenye shughuli zake, hawezi kufanya chochote. Kwa hiyo ninaomba Serikali imueleze yule Bishop kama yeye si raia arudishwe kule alikotoka au arejeshewe pasi yake ya kusafiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye eneo lingine la utakatishaji fedha. hii dhana ya utakatishaji fedha imekuwa ni ngumu sana na imekuwa na uonevu mkubwa sana. Watu wanawekwa ndani kwa money laundering, wanakaa miaka, upelelezi unaendelea. Ni kwa nini TAKUKURU inapeleka hizi kesi kwa DPP ilhali haijamaliza upelelezi? Mimi naishauri Serikali, upelelezi ukamilike kabla ya kupeleka hizi kesi kwa DPP badala ya kuwanyima watu haki zao na kuwaweka rumande mwaka nenda mwaka rudi. Hii ni sawa na kuwa kama kifungo kwa saabu hakuna kitu chochote unachoweza kufanya ila ni kukaa ndani. Kwa hiyo upelelezi ukamilike ndipo watu wapelekwe Mahakamani, kesi zao ziende vizuri, kama ni kuhukumiwa wahukumiwe, kama hawana makosa warudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunao mfano mzuri Zanzibar, wenzetu ukienda kesi zote zinadhaminika, ukienda unawekwa ndani, ikifika miezi tisa upelelezi haujakamilika, unapata dhamana unatoka na kesi inaendelea. Kama una kosa unafungwa na kama huna kosa unaachiwa. Kwa hiyo tuna mfano mzuri ambao tunaweza kuiga kwa wenzetu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninazungumzia suala la mahusiano. Suala la mahusiano ni kama hii issue iliyotokea Mambo ya Ndani; tunaona Waziri Lugola ametumbuliwa lakini ninajiuliza mimi kama Katibu Mkuu Mstaafu inawezekanaje Waziri atuhumiwe lakini Katibu Mkuu ambaye ndiye Afisa Masuhuli, yeye ndiye anasimamia mikataba, yeye ndiye anayesimamia kila kitu katika Wizara, inakuwaje? Ikanipa tafakari kubwa sana. Kwamba inawezekana Makatibu Wakuu na Mawaziri pengine hawapati semina ya kutosha kujua majukumu yao, majukumu ya Waziri ni yapi, majukumu ya Katibu Mkuu ni yapi; na inawezekana pia, naona Waziri wa Utumishi hayupo; kwamba je, Mawaziri wanapewa ile red book waweze kuzisoma na kuzielewa? Mimi sina hakika kama Mawaziri wote wamepewa ile red book, Mheshimiwa Jenista, wapewe red book wajue majukumu yao.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ruth Mollel subiri kuna taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimpe Taarifa Mheshimiwa Ruth Mollel. Kwanza taratibu zote za utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba, kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, zote zimefuatwa na kila instrument imeeleza kazi za Mheshimiwa Waziri na kila jambo ambalo Mheshimiwa Waziri anatakiwa kuwa nalo katika kutekeleza wajibu wake, vifaa, documents na zana zote za kiutendaji kila Waziri anazo, tuko full nondo hapa na kila mtu ana kila kitu!. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile tu naomba niendelee kumwambia dada Ruth, yeye aendelee kutushauri katika muundo wa utendaji kazi wetu na namna ya kufanya kazi lakini asiwe na mashaka. Rais wetu anatusimamia vizuri na sisi tunatekeleza wajibu wetu kama inavyotakiwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ruth Mollel nafikiri umeelewa hayo ambayo ulikuwa unamuambia Mheshimiwa Jenista. Endelea Mheshimiwa Ruth.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama anavyosema Mheshimiwa Jenista ni sahihi basi liko tatizo; na kama liko tatizo litafutwe ni tatizo gani linalosababisha huu mtafaruku katika Wizara. Kwa sababu haiwezekani kuwe na mtafuruku kati ya Waziri na Katibu Mkuu kama hizo instrument zote zipo, basi iko shida na hiyo shida itafutwe ili itafutiwe dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala pia ambalo linahusu TAMISEMI na ul mradi wa DART. Ule mradi wa DART ofisi zile kila mara kunapokuwa na mafuriko maji yanajaa, na unajiuliza ingekuwa ni nyumba za watu binafsi sasahivi zingebomolewa na zikaondolewa; na hali hii inahatarisha usalama wa raia na pia usalama wa nchi yenyewe. Ni kwa nini sasa katika bajeti ijayo hizi ofisi za DART pale Jangwani zisiondolewe kwa sababu zipo katika mkondo wa maji na kila mara kumekuwa maji yanajaa mabasi yanasimama hayawezi kuyahudumia wananchi wakati wananchi wanahitaji huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho mimi nasema hivi kwamba Serikali iliyopo madarakani ni ya wananchi, ni wananchi ndio tumeiweka Serikali madarakani. Kwa hiyo Serikali inawajibika kwa wannachi, maana sisi ndio tumeiweka madarakani. Kwa hiyo tunapotoa maoni yetu. Tunapoikosoa Serikali, tunaisaidia Serikali iweze kwenda katika namna inayopaswa na kuboresha huduma na kutuhudumia inavyopaswa kwa kodi zetu ambazo zinakatwa kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo muhimu sana, tujue kwamba hata Serikali inapofanya kazi vizuri inatimiza wajibu wake kwa wananchi na kwamba hawatupi msaada, sio msaada ni wajibu wa Serikali. na hiyo inatumika kwa kutumia kodi zetu sisi wenyewe. (Makofi)

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi/Vigelegele)