Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia. Nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za pekee kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli aliyoitoa kwamba uchaguzi mwaka huu utakuwa ni wa huru na haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuzungumza hilo, naomba pia nikumbushe kwamba Mheshimiwa Rais huyo aliyetoa kauli hiyo ndio Mheshimiwa Rais pia liyesema kwamba atamshangaa Mkurugenzi ambaye amemchagua yeye atakayetangaza mtu wa Upinzani kwamba ameshinda kwenye eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kauli hizi; hiyo ya kwanza kuhusu Wakurugenzi aliitamka zamani kidogo na hii ametamka siku za hivi karibuni. Nategemea kwamba inawezekana kuna badiliko kidogo Mungu ametusaidia. Kama hivyo ndivyo, basi tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tufanye mabadiliko kwenye Sheria ya Tume ya Uchaguzi ili kuwaondoa Wakurugenzi hawa ambazo alishawaambia kauli ya kwanza, maana yake itakuwa ni mchanganyiko kidogo. Ulishamwambia mara ya kwana asitangaze, halafu sasa hivi ukimwambia ni huru na haki inaweza isieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukabadilisha sheria hizi tuweze kuwaondoa na hatimaye tupate wasimamizi wa uchaguzi ambao watu wa Upinzani na wa Chama Tawala watakuwa huru na itaweza kutusaidia kutoka pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili pia linawaathiri wananchi, kwa sababu kama Mbunge wa CCM ana uhakika kwamba kwa vyovyote vile atatangazwa, kuna maana gani hata kurudi kwa wananchi kufanya kazi? Kikubwa zaidi utakuwa unaenda kwenye Chama chako kujitahidi kutengeneza mambo vizuri, basi. Kwamba nikishashinda kwenye kura za maoni, imetosha huku kwingine nitaibiwa halafu mambo yataenda. Hakuna maana kupinga ufisadi kama unahimiza wizi wa kura. Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba hilo liweze kuzingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala zima la suala la Daftari la Wapiga Kura. Daftari hili limeanza kuandikisha na muda umeenda kidogo. Katika maeneo mengi ambayo uandikishaji umefanyika, imekuwa ni zoezi ambalo siyo rafiki, limekuwa ni zoezi ambalo Serikali haitumii muda kuhimiza wananchi kwenda kujiandikisha na taarifa kutoka kwa wakati. Pia vingine ni kwamba daftari limekuwa likigongana na uandikishaji wakati wa Serikali za Mitaa. Daftari limekuwa likigongana pamoja na uandikishaji wa NIDA. Kwa hiyo, unakuta wananchi wamekuwa wakipata mgongano katika kujiandikisha kwenye daftari hilo la wapiga kura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji sasa, sheria inasema kwamba uandikishwaji ufanyike mara mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hii imefanyika mara moja na leo ni mwezi wa pili sasa. Tunajiangalia: Je, nchi nzima na ukubwa wake tutafanikiwa kuweza kuandikisha kwa ukubwa huo ambao tunahitaji ili kutimiza matakwa ya kisheria ya kuandikisha mara mbili kabla ya kufika kwenye Uchaguzi Mkuu ili wananchi wote wapate fursa ya kuweza kujiandikisha na kuweza kupigia kura viongozi wao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho lazima tuone ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni uchaguzi ambao umefanya dhuluma kubwa sana. Tuna Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao hawahitajiki. Hata hivyo, hili suala limetoa funzo tena kubwa sana. Mkurugenzi anafanya wizi; hapokei fomu za watu, anachafua fomu za Wagombea katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, somo ambalo limepatikana ni kwamba tunapoenda kwenye uchaguzi Mkuu, pamoja na kutafuta hela za kampeni, sasa tunamdhibiti vipi Mkurugenzi? Suala sasa ni kwamba tunamdhibiti vipi Mkurugenzi? Fomu zipokelewe, zibandikwe kama inavyohitajika na uchaguzi uweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali inavyoenda ni fujo kubwa itakayotokea ndani ya nchi hii, ni mauaji makubwa ambayo yatatokea nchi hii, watu hawatakubali haki yao iendelee kunyang‟anywa mwaka hadi mwaka. Kwa sababu hiyo basi, Mheshimiwa Mbowe ametumia busara sana, ni Mwenyekiti wangu wa Chama, namheshimu na pia Mungu amembariki hekima ya ajabu sana. Alipokuwa kwenye Mkutano wa Uhuru Mwanza tarehe 9 Desemba alisema kwamba ifike mahali nchi tufikie maridhiano, tuzungumze, tuondoe changamoto tulizonazo ili kuepusha maafa makubwa ambayo yanaweza kutokea ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana ameweka msisitizo kwamba anamaanisha ombi la maridhiano. Jana ametoa press conference ambayo imeandika barua na vitu gani ambavyo tunahitaji kubadilisha. Sasa mara nyingi katika nchi nyingine maridhiano yanafanyika baada ya watu kuuana, baada ya watu kukatana mapanga ndiyo watu wanakaa kwenye meza kuzungumza kwamba kila mtu ameshaonesha ubabe wake, sasa watu wanazidi kufa, sasa tukae chini tuzungumze mambo yaende. Sasa yeye ametumia busara kwamba tuzungumze kwanza kabla maafa hayajatokea. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa busara hiyo basi, ninaomba Mheshimiwa Rais atumie busara aliyonayo tukae chini tuzungumze, tubadilishe yanayowezekana, twende mbele…

MBUNGE FULANI: Kaa chini kelele wewe!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Upendo malizia.

MHE. UPENDO F. PENEZA: …na tufanye uchaguzi wa haki ili hii amani tunayohitaji ndani ya nchi hii iweze kudumu.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kitendo cha uzalendo zaidi ya kuitakia nchi yako amani na maridhiano na kuomba maridhiano ni kitendo cha uzalendo mkubwa sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Upendo muda wako umeisha.

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/Vigelegele)