Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja za kamati zote tatu. Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati zao walitushauri kama Serikali, tumechukua hatua kwa mambo ambayo walielekeza na tunaendelea kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye hoja zilizozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya elimu, na Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumzia maboma. Niwaambie tu kwamba, tulitoa fedha hapa shilingi bilioni 29.9 ya kupeleka kwenye maboma mbalimbali yakaleta mabadiliko makubwa, lakini pia hapa tulipo tupo kwenye mkakati wakupeleka fedha zaidi ya shilingi bilioni 200, ili kuongeza miundombinu ya elimu. Pia tumetenga fedha zaidi ya bilioni 200 kwa ajili ya kwenda kuimarisha elimu ya shule za msingi, na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu watu wakaelewa kwamba kila mtu akisimama anazungumza miundombinu hapa. Juzi tulizungumza mjadala wa fedha hapa tunatarajia kupata, zingesaidia sana. Tunatafuta vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu yetu. Ufaulu umeongezeka sana. Kwa kauli ya Mheshimiwa Rais na maelekezo yake ni kwamba elimu bure ipatikane kwa watoto wengi wa Tanzania ambao walikosa fursa hiyo imesaidia sana kuwa na watoto wengi shuleni; kwahiyo tunahitaji kuboresha huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ambzo zinazungumzwsa trilioni 1.5 zingeweza kujenga mabweni zaidi ya 300 Tanzania nzima, madarasa 800 ya sekondari, madarasa 1,200 ya shule za msingi, tungejenga shule 26 mpya za wasichana, tungejenga mabweni maalum mahsusi na shule za msingi, ni mambo makubwa sana. Ukitaka kujua hili tafuta taarifa hizi ili tuweze kuzungumza kwa pamoja, kwamba tunapokuwa tunapanga mipango kuboresha elimu yetu tushirikiane kwa pamoja bila kuleta ubaguzi na ubinafsi uliopitiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hoja hapa zimezungumzwa; kwa mfano kuna hoja ya Serikali za mitaa. Uchaguzi huu uliashaisha na wenzetu walisusa wenyewe na maelekezo na msimamo wa Serikali ni kwamba uchaguzi umekwisha. Kama kuna mtu anampinga Mwenyekiti wa Mtaa afuate utaratibu, asipofuata mtakuja hapa tena kulialia na kulalamika. Sheria ndogo zipo kwenye vijiji, kamati za ulinzi na usalama zipo pale watafanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na si kweli kwamba ukienda kwenye ngazi za vijiji na vitongoji eti wanachama wa upinzani ni wengi kuliko wa CCM, sijapata kuona hali hiyo. Kwa hiyo, ukitaka kuleta, haiwezekani, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni wengi kuliko wa upinzani; na ndiyo maana hata huko mtaani wala hakuna kelele. Kwa hiyo kama kuna mtu anahamasisha na kutisha watu Wenyeviti waliochaguliwa halali kisheria na kikatiba wafanye kazi zao kama kuna mtu anawabughudhi sheria lazima ichukue mkondo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja hapa ambayo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge wa Tanga Mjini. Mheshimiwa Mbaruku amekuja kutoa hoja kwamba kuna Madiwani wamerudi kutoka CUF wameingia CCM na wamehudhuria vikao vya Halmashauri kule. Nimeongea na Mkurugenzi wa Jiji, Mheshimiwa Mbunge amekaa hapa wiki mbili za kamati hakuleta hoja, hakupiga simu, hakuja Wizarani, hajalalamika na hana barua yoyote ile. Hii wiki ya kwanza ya Bunge imeisha. Kwa hiyo natoa hoja ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Tanga hawezi kufanyia kazi mambo ya mtaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ni kwamba, barua ilipaswa kuandikwa ya kuonesha kama kweli CUF hao madiwani wamehama. Yeye ameona watu wanasema Katibu Mkuu wa CCM ameenda kwenye mkutano, wamevutiwa na mambo yake mazuri na utekelezaji wa ilani, wakaenda kumsalimia, huenda walikuwa wanaweka booking kwamba, hivi karibuni watarudi CCM. Sasa kama CUF wanasema madiwani wamehama…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …wampelekee barua Mkurugenzi ili aweze kuchukua hatua hiyo. Kwa hiyo, utaratibu uliopo kama barua haijaenda wale wataenda kupata stahiki zao na huu ndio utaratibu wa kawaida…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kama kuna mambo yanatolewa ya mlalamiko ndiyo maana tuko hapa kwenye corridor, tunakunywa pale chai canteen tunazungumza tunawasiliana tunapeana taarifa. Ukileta hapa kama taarifa rasmi tutaku-crush kwa sababu ni taarifa ya uongo; tuwasilisne kama una taarifa za kutosha, barua iandikwe ifanyiwe kazi, haijaandikwa wakurugenzi watafanya kazi na watawatambua hao madiwani wataendelea kuwapa stahiki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, imezungumzwa hapa uchaguzi wa 2020. Niseme tu vizuri bahati nzuri nina uzoefu wa ile kambi na nina uzoefu wa hapa. Waheshimiwa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi naomba niwaambie ukweli hawa wanaweweseka hali ni mbaya kwelikweli huko majimboni. Hali ni mbaya kwelikweli! Kwa sababu katika awamu za nchi hii, hii ndio awamu pekee kila Mbunge iwe kisirisiri, iwe chumbani kwake akisimama lazima amtaje Rais John Pombe Magufuli kwa kazi aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna jimbo la uchaguzi halina mkono wa Rais Magufuli. Hakuna mkoa hauna mkono wa Waziri, hakuna maeneo hakuna jiwe ambalo limeacha kuguswa. Kwa mazingira hayo Watanzania hawakutaka upinzani walitaka kazi na …
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): ..kiongozi mwenye msimamo, kuondoa rushwa. Upele wa Tanzania umepata mkunaji na 2020 wanatoa zawadi na kura za asante kwa Rais Magufuli ili aweze kusonga mbele na kazi lazima iendelee…
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni muhimu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …Kwa hiyo, wasiwasi wao ni faida kwetu kamba, mchezo umewashinda kabla ya kuingia uwanjani. Asante.
(Hapa, baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waitara.