Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kushukuru kunipa nafasi kwanza nieleze naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nichukue nafasi hii kukupongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Wajumbe wa Kamati kwa jinsi wanavyotuongoza vizuri yale mazuri mliyoyaona katika taarifa tumeyatekeleza kutokana na mwongozo na maelekezo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekuwa mchache nitagusia mambo matatu manne kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza limezungumzwa humu ndani nadhani katika Kamati zote nyingi suala la uhaba wa Watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba Serikali tumejipanga mwaka huu tunaajiri Watumishi 43,000 wa Kada mbalimbali lakini niungane na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndugu yangu Kandege kuungana naye nami niwahakikishie Watanzania wote ambao wameshiriki kwa mikono yao kujenga Hospitali 67, Vituo vya Afya 350, Zahanati kemkem kwamba hayatakuwa majengo ya maonesho tutaajiri Watumishi na tumekaa pamoja na Wizara ya Afya tumekaa na wataalam mbalimbali kuhusu suala la kuagiza vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishieni kwamba watumishi wataajiriwa na kama mlivyosikia wengine wamekwisha anza kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo limezungumzwa humu ndani kwa kirefu ni Mradi wa kunusuru Kaya maskini TASAF, TASAF tulikuwa tuna tatizo moja kwamba katika Vijiji tulivyokwenda tumefikia asilimia 70 ya walengwa katika vijiji vyote nchini tulifikia vijiji asilimia 70 na shehia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tulikuwa tuna changamoto ya kumaliza walengwa waliobaki ambao hatujawafikia, nataka niwaambie Watanzania kwamba Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya maandalizi tumepata fedha za kutosha mwisho wa mwezi huu tutafanya maandalizi kabambe ya kuzindua TASAF Awamu nyingine ambayo tutamaliza thelathini wote waliobaki tutafika Vijiji vyote asilimia 100 tutafika walengwa wote asilimia 100 ili kuweza kuwahudumia wale ambao bado hawajafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Watanzania wenzangu kwamba sisi katika kijiji wasimamizi wa TASAF hatuendi na orodha ya walengwa. Walengwa wanapatikana pale kijijini ninawaomba tu wanakijiji wote tushirikiane katika kuwatambua walengwa wale ambao kwa uhakika tunajua huyu anahitaji msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye Kijiji tukaambiwa kuna walengwa ambao hawakustahili kuwemo kwa kweli wa kulaumiwa ni Wanakijiji wenyewe kwa sababu wao ndiyo wanaoandaa orodha ya walengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeshauriwa hapa tufanye malipo ki-electronic, tumejaribu kufanya majaribio mahali. Nataka niseme kwamba tutafika mahala tutafanya malipo kwa mtandao, lakini itawezekana tu kwa wale ambao wana simu na wanajua kusoma na kuandika. Kwa wale ambao itashinikana hivyo, sisi tutaendelea kuwafuata na kuwagawia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililozungumzwa hapa ndani ni suala la MKURABITA, naungana na Kamati. Kamati inasema tuwawezeshe zaidi, sisi tunakubali kwamba tuwawezeshe zaidi. Tukiwawezesha, naamini watafanya kazi nzuri zaidi. Ilitolewa hoja kwa baadhi ya Wabunge kwamba pengine mabenki yanakataa. Juzi kama alivyosema somo yangu Mheshimiwa George pale, nilikuwa Mpwapwa, tumekwenda kugawa vyeti. Bahati nzuri walialikwa mabenki yote pale, yapo manne pale Mpwapwa. Benki zote nne pale Mpwapwa zimetoa mikopo kwa watu waliokuwa wanamiliki hati za kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mabenki hayana matatizo. Nataka niseme, mahali popote ambapo mabenki yatawaletea matatizo labda hawawakopeshi kupitia MKURABITA, basi tupate taarifa katika Wizara na sisi tutachukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, hapa ndani asubuhi, mchana huu naona kumetulia kidogo, limezungumzwa sana suala la utawala bora. Nitakuwa sifanyi haki kama ni Waziri wa Utawala Bora halafu nisiseme jambo, tena kwa takwimu ili wale waliosema uongo waone haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora katika nchi, maana yake ni watu kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ambazo zimepitishwa democratically. Democratically maana yake sheria imepitishwa na watu walio wengi. Humu ndani hata kama jambo hulitaki, lakini walio wengi wamelipitisha, hiyo ni sheria halali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia nzima kwa watu walioenda shule wanajua kwamba katika demokrasia walio wengi wape, lakini wale wachache uwasikilize. Kusikilizwa mnasikilizwa, si ndiyo maana mpo humu ndani! Si mpo wachache! (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tusioenda shule tunalitambua hilo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mtu mzima, naona aibu kusimama mwongozo, mwongozo! Hivi mtu anachangia, alikuwa anachangia mtu fulani asubuhi, hoja inapigwa pale, wanapiga kelele wee, mtu asisikilizwe. Kupiga kelele humu ndani wakati mwenzio anaongea huo ni ushamba. Huo ni ushamba! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Watanzania wenzangu, nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni na imemweka Waziri maalum wa kusimamia utawala bora.

MBUNGE FULANI: Ambaye ni wewe.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Ambaye ni mimi. Kumbe unajua eeh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niteo mifano hapa. Unajua Baba wa Taifa alipokuwepo aliruhusu column moja katika gazeti la Daily News ilikuwa inasema: “What They Say About Us?” Wanatusemaje walio nje kule? Kwa sababu wengine humu ndani mnapenda sana ku-quote mambo ya nje, sasa nami mzee nataka ku-quote huko huko mlikoenda nyie, niwaonyesheni kwamba ninyi hayo mnayoyasema siyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika kuhitimisha Hoja ya Kamati iliyowekwa Mezani nimeeleza suala utawala bora, nataka nieleze jinsi tulivyo, tunavyopiga hatua katika utawala bora. (Makofi)

(i) Kutokana na takwimu zinazotokana na tafiti, Tanzania imeonekana kuongeza kiwango cha utawala bora na hasa eneo la mapambano dhidi ya rushwa na hasa eneo la kutumia vizuri rasilimali za wananchi, na kodi ya wananchi. Sasa watu wamelipa kodi, hela inatumika vizuri wewe unataka nini zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanywa Transparency International; hawa wanazungumza mambo ya uwazi Kimataifa, wanaheshimika Afrika nzima, siyo Tanzania, hapana dunia nzima. Wanasema, 2019 kwa taarifa iliyotolewa na Transparency International, Global Corruption Parameter Africa 2016: “Tanzania imefanya vizuri zaidi kwa kupata alama 37 na kushika nafasi ya 96 katika nchi 180 duniani.” Lililopimwa ikiwa ni ongozeko la nafasi 21. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Mheshimiwa Dkt. Magufuli baada ya kuingia madarakani, tunavyofanya vizuri katika utawala bora, Transparency International wamempandisha nafasi 21. Tumsikilize nani, Transparency International au wewe uliyefanya utafiti kwenye kijiji? (Makofi/Kicheko/Vigelele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuendelee. Kwa matokeo ya takwimu za utafiti wa kila mwaka, Tanzania imekuwa inapanda nafasi tangu mwaka 2015 Mheshimiwa Dkt. Magufuli anapoingia madarakani. Mwaka 2018 Tanzania ilipata alama 36 na kushika nafasi ya 99 ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo ilipata alama 36 na kushika nafasi ya 103. Kila mwaka tunapanda, tunapanda, tunapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Utawala Bora anawaahidi kwamba tunataka siku moja Tanzania tuwe na digit moja tu, siyo kumi na ngapi, hapana. Kumi kushuka chini. Hivi mnayoyaona tunayoyafanya, mwendo ni huo wa kufika huko kwenye digit moja, hiyo ndiyo Tanzania ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Hiyo ndiyo Tanzania inayopendwa na watu wa nchi wa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende na matokeo ya kitakwimu hayo hayo na kama mtu anabisha aje nimwoneshe. Katika matokeo, takwimu hizo kwa upande wa Afrika Mashariki, Tanzania ni ya pili kwa Utawala Bora. Tunachuana sisi na Rwanda. Hivyo ndivyo wanavyosema wasomi na watu wenye authority katika mambo haya. Wewe unatuletea figure za ajabu ajabu hapa, ulifanyia wapi utafiti? Mao Tse Tung anasema: “no research, no right to speak. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya shirikisho Shirika la Mo Ibrahim Award, yule anayetoa zawadi kwa Marais katika masuala ya utawala bora, ambapo hutolewa ripoti yake kuhusu utawala bora kwa nchi za Afrika; mwaka 2018 Tanzania ilipata alama 58.5 kwa 100. Amevuka huyo! Ilikuwa nchi ya 14 katika Bara la Afrika katika suala la utawala bora ambapo ukilinganisha na huko nyuma tulikuwa na alama 57. Hao ndio wasomi, authority katika mambo ya utawala bora, nami wananisomesha wao. Kama mimi wananisomesha wao; je, wewe! (Makofi/Vigelele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende sasa; mimi nitakwenda nje na ndani, lakini nazungumza na watu wenye authority tu, wale ambao hawana authority sikuwa-quote hapa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti mwingine wa taasisi ya ndani ya nchi wanaita Repoa. Mwaka 2017 imeonyesha wananchi saba kati 10 ya waliohojiwa walisema ushiriki wa Serikali katika mapambano dhini ya rushwa ni mzuri sana. Imani hiyo imeongezeka imetoka sasa 37% kwenye matokeo yaliyotolewa ukilinganisha 2018. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameulizwa wenye nchi yao, mnasemaje kuhusu habari ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Serikali yake na kwa habari ya utawala bora? Wakasema Serikali yake inafanya vizuri sana, sana. Wameulizwa mmoja mmoja; matajiri wameulizwa, masikini wameulizwa, CHADEMA wameulizwa, CUF wameulizwa, sembuse CCM; nao wameulizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukija hapa, tunapongea watoto wetu wanatusikiliza huko nje; na watoto wa siku hizi shomile, wamesoma, analinganisha alichosoma yeye kwenye kitabu cha watu wenye authority anakulinganisa na unayosema wewe. Hivi ukifika nyumbani siyo ajabu akakwambia eeh, baba, mama ulisoma kitabu gani? Kitabu hiki hapa, kisome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu kubwa ya mafanikio ya haya ni utashi wa kisiasa (political will). Ili nchi ipambane na rushwa, lazima kuwe na ipambane na political will. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Magufuli ana political will ya kupambana na ufisadi. Alisema ataanzisha Mahakama ya Mafisadi na ameianzisha. (Makofi)

Mheshiiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimalizie point moja, mbili za mwisho, maana darasa hili huwa linawapotea, hamlipati kila siku. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utashi huo, imani ya wananchi imeongezeka, nidhamu ya watumishi wa Umma ninaowaongoza mimi Serikalini imeongezeka, imeimarika. Matumizi mabovu ya fedha za ndani, ndani ya Serikali yamedhibitiwa. Kwa sababu tunakusanya vizuri mapato, tunadhibiti matumizi mazuri na watalaam wanasema tunazitumia fedha zetu, ndiyo maana tukienda huku ndege huuuuu, mpaka Songea kwa watani zangu amalo ilikuwa ndege hazitui, zinaenda. Mtwara huko sisemi, Mwanza na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namsikiliza Rais wangu, amewaulizeni wala hamjamjibu bado. Kwa nini Mheshimiwa Dkt. Magufuli unanunua ndege kwa fedha taslimu? Akawaambieni kama hela ninayo mfukoni kwa nini nikope? Hivi mtu anayekopa si hana kitu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Tusikilizane. Mifumo ya utendaji kazi imeimarishwa ikiwa ni pamoja na kuziimalisha taasisi simamizi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Tulikuwa na Wilaya…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ndivyo walivyo, wala hatuwashangai, ndivyo walivyo. Mimi Waziri nimepewa muda wa kutosha.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mkuchika, naomba umalizie endelea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa hilo neno la mwisho “endelea”, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema hivi, tumepandisha vyombo vya kupambana na rushwa. Tulikuwa na Wilaya 21 hazina ofisi, tumefungua ofisi, tumewapa na magari. Mwaka huu Wilaya zote nchi hii kila Wilaya ina Ofisi ya TAKUKURU. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimewasikiliza sana asubuhi. Vyama vingi tangu vimeanza nchi hii, hoja ni Katiba mpya, Katiba mpya. CCM tukasema haya, tukaja humu ndani kutengeneza Katiba mpya. Tulipopiga kura Serikali tatu au ziwe mbili? Walio wengi wakasema ziwe mbili. Kitu gani kingine? Hawakupata walichotoka. Hivi humu ndani aliyechukua mpira akaweka kwapani tukasababisha Katiba mpya isipatikane, ni CCM au nani? Sasa leo bila aibu mnasimama hapa, tunataka Katiba mpya, Katiba mpya, aliyekimbia na mpira, mpira ukavunjika alikuwa nani? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naona ndugu zangu wamefurahi, wameelewa. Wale ambao hawakuelewa, wameelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko/Vigelele)