Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuletea mafuriko katika Wilaya ya Kilwa na familia au kaya 4,000 hazina mahali pa kulala, kaya 4,000 hazina chakula, kaya 4,000, Allahu Akbar!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu na nawapa pole wahanga wote wa mafuriko Mkoa wa Lindi. Ninaomba wasamaria wema wote wa Tanzania pamoja na Bunge lako tukufu mtusaidie katika mchango.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Wabunge wote tuwasaidie wananchi waliopata mafuriko, tunaomba sana. Hili liangalie sana, hali siyo nzuri. Mimi nimekwenda Kilwa, nimekaa siku nne, lakini wananchi hali siyo nzuri.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba tufanye mchango tuwasaidie watu hawa. Hata ukisema aaah, lakini tulipata tetemeko la ardhi Bukoba Wabunge tulichanga.

MBUNGE FULANI: Aaah!

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Sasa wewe unayesema, aah, kwa kuwa tumepata mafuriko sisi watu wa Kilwa, sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa mujibu wa Katiba, inasema wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Kama kweli nchi yetu tumejenga misingi ya udugu na watu wa Kilwa na Lindi wamepata mafuriko, wewe unasema aah! Basi ile misingi ambayo tumejiwekea kwa mujibu wa Katiba na sisi tumeapa kwa mujibu wa Katiba tumeishika Biblia, na Misahafu, halafu unasema aah, basi Inshaallah.

Mheshimiwa Spika, nasema tena, angalia sana, hali siyo nzuri Kilwa.

SPIKA: Mheshimiwa, si utoe hoja basi uone wangapi wanakuunga mkono?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, nachangia, nitatoa hoja baadaye.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa misingi hiyo ya uhuru, haki, udugu na amani itatekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambapo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye Wajumbe waliochaguliwa na wananchi, pia yenye Mahakama huru zenye wajibu wa kutoa haki bila uoga wala upendeleo wowote, hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa, kulindwa kwa wajibu wa mtu anayetekelezwa kwa uaminifu;

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, Katiba hii imetungwa na Bunge Maalum la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi. Unajua nchi yetu, sisi tumeapa. Mimi sikuapa kuilinda Katiba ya CUF, sikuapa hivyo! Wala mtu wa CCM hajaapa kuilinda Katiba ya CCM, hatukuapa hivyo. Sisi tumeapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ndani ya mijadala yetu hii sasa hivi hapa ni kwa uchama tu, sijui CCM itashinda! Nyote ndani mtakuwa CCM, CUF mtashindwa!

Mheshimiwa Spika, huko Zanzibar hakuna CUF hata mmoja, hakuna CHADEMA hata mmoja? Mko CCM watupu! Kinachofanyika kitu gani? Haya, mwakani muwe ninyi nyote CCM, Bunge lenu, maana mnasema mtashinda, mtashinda; haya, wote muwe CCM watupu, sisi wengine tusiwepo ndani. Jambo lenu mtasimamia Katiba tu, wala hamsimamii CCM. Tena mtapata taabu sana kwa sababu wa kuwasokola mtakuwa hamna ndani. Mtasokolana wenyewe kwa wenyewe. Badala ya kutushambulia sisi, mtashambuliana wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana, tuache mambo ya uchama. CCM imeundwa; imeanza kuundwa Tanzania halafu ndiyo CCM; imeanza kuundwa Tanzania halafu ndiyo CUF. Naomba sana tuache mambo ya uchama. Wangapi walikuwepo humu? Wako wapi sasa hivi? Wangapi? Mtu unakuja ndani humu, Bwege utakuwa sio Mbunge. Kwani mwanzo nilikuwa Mbunge? Hata kama nikikosa Ubunge! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba usalama wa nchi yetu, amani ya nchi yetu na amani haipatikani bila haki. Leo tunaongea hapa, tunasema hapa Serikali inajifanya haisikii. Ndiyo maana pia wameenda kumsema Marekani huko, ninyi hamsikii hapa. Mtu akipambana anapambana kwa njia yoyote ile, ndani ya nchi na nje ya nchi. Akienda nje ya nchi, oh msaliti! Usaliti gani wakati ninyi hamsikii hapa!

Mheshimiwa Spika, mimi niliwaambia Waislamu kule wamepigwa risasi, wameuliwa, Serikali iko kimyaa! Msaliti nani? Tukiwaambia hamsikii. Mnaangalia nani kasema? Hamwangalii kasema nini. Tunaitaka Serikali ijue nini inasema?

SPIKA: Mheshimiwa Bungara nilitaka tu kukukumbusha neno moja…

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Inshaalah. Nikae!

SPIKA: Hapana usikae. Kwa suti uliyopiga leo, blue bahari inataka leo upige taratibu taratibu, maana yaani leo uko vizuri. (Kicheko)

Endelea Mheshimiwa. (Kicheko/Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, leo tunasimama hapa, Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sio Mbunge wa CCM wewe, wewe ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi yako ni kuisimamia Serikali. Siyo kila kitu Serikali ikisema baya, ndiyo! Zuri, ndiyo! Why? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Wabunge sasa hivi mmekuwa kama mbumbumbu; umeshiba? Eeh! Una njaa? Eeh! Why? Unachokisimamia hukijui! (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Jamani Wabunge wote wa CCM mmepigwa ganzi? Hakuna hata Taarifa? (Kicheko/Makofi)

MHE. RICHARD P. MBOGO: Taarifa ipo.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, unanichanganya bwana! SPIKA: Mheshimiwa Bungara unapewa taarifa bwana, tafadhali. (Kicheko) MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Ananipa nani taarifa? Haya.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimesimama kwa mujibu wa Kanuni ya 68(8) ambayo inaniongoza niweze kutoa taarifa.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa kwamba Wabunge wa CCM kwa wingi wao wamekuwa wakitoa ushauri ndani ya Bunge hili ndani ya Kamati za Kudumu za Bunge na wamekuwa pia wakitoa ushauri kwenye mabadiliko mbalimbali ya sheria kwa kuleta schedule of amendments ambazo zimekuwa zikichangiwa humu ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimpe taarifa kwamba tuko vizuri na tuko imara na tunafahamu kazi vizuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bwege, pokea taarifa hiyo, halafu endelea.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, nimemwelewa sana, lakini nataka nimwulize swali moja halafu ukatoe ushauri. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sisi ni nchi ya kidemokrasia ya vyama vingi vya siasa. Sasa katoe ushauri kuzuia mikutano ya siasa, kuzuia Bunge Live! Sasa katoe ushauri huko kwamba ndiyo sheria? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Katiba inasema katika Ibara ya 9 kwamba Sheria za nchi zilindwe na zitekelezwe. Sasa kwa kuwa wewe unasimamia sheria za nchi na zilindwe na kutekelezwa, Sheria ya Mfumo wa Vyama Vingi inavyosema ni kwamba mikutano ya hadhara na maandamano ni haki, wewe unaizuia; kaishauri Serikali yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria inasema lazima isimamiwe na itekelezwe. Sasa kwa kuwa wewe unajua kushauri sana na kuisimamia sana Serikali, sisi vyama vingi tunaambiwa mikutano ya hadhara hakuna, Wabunge tunazuiwa; wewe unasemaje kuhusu hilo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemjibu taarifa yake, akaishauri vizuri Serikali waifuate Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba sana, nawasifia kidogo kuhusu mambo ya umeme. Aaah, kwa umeme Alhamdullilah! Kwa umeme aah, mnatufikisha mahali pazuri! Kama mtaendelea hivi kuhusu umeme na mkafanya speed katika maji, mkawalipa wakandarasi wa umeme hela zao vizuri, mkawalipa wakulima wa korosho hela zao wote, mkawaongeza mishahara kwa wafanyakazi, kukawa hakuna kesi za kubambikia, kukawa maandamani yapo, aaah, CCM itashinda! Mashehe wale waliokuwa ndani kwa miaka minane mkiwaachia, aaah CCM dole! Ikiwa wenyewe tunalia umeme, Mashehe hawatoki, mishahara hamwongezi, wakulima hamwalipi na kadhalika, aaah, hesabuni kuumia tu 2020. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bungara, sijui; ninyi Makatibu mbona hamwangalii muda? (Kicheko)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninawaomba Wabunge wote mtuchangie watu wa Kilwa, natoa hoja Waheshimiwa mniunge mkono.

SPIKA: Hoja haijaungwa mkono bado. Jamani Mheshimiwa ametoa hoja, mnasemaje?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MBUNGE FULANI: Tunaomba Mkoa mzima wa Lindi, kama tunachangia Mkoa mzima wa Lindi.

SPIKA: Hilo tutalifanyia maamuzi baadaye Mheshimiwa Bungara.