Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa nafasi hii, na mimi niweze kutoa mchango wangu katika kamati zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze Wenyeviti wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Kipekee kabisa nianze na Kamati ya UKIMWI; na niwapongeze sana wewe pamoja Mheshimiwa Spika kwa ubunifu mkubwa wa kamati hii ambayo hapo mwanzoni Kamati hii wajumbe walikuwa wanaikimbia. Sasa hivi imekuwa ni kamati moja muhimu sana, tumepata semina za kutosha. Ni kamati ambayo imetoa madarasa mengi na imefanya mambo makubwa na kwa kweli Mwenyekiti wake Mheshimiwa Oscar Mukasa anahitaji pongezi za ziada kabisa katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo kamati zimeeleza kwenye eneo hili la Kamati ya UKIMWI pamoja na madawa ya kulevya bado kuna changamoto hasa katika eneo zima la udhibiti wa madawa ya kulevya lakini pia tumeona katika kifua kikuu bado nguvu si kubwa kama ambavyo tunaiona katika UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu isaidie katika eneo hili, na haswa katika suala lile la Tume ya Madawa ya Kulevya, ili kuhakikisha kabisa kwamba tunaongeza ufanisi ili katika hali ambayo tumeona sasa hivi kwamba kumekuwa na udhibiti mkubwa wa madawa basi taifa letu liendelee kunusurika na hii hali ambayo tunaiona.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningetamani nilichangie ni katika eneo hili la elimu haswa kwa kupitia Kamati ya Huduma za Jamii. Suala la elimu ni suala ambalo linahitaji tafakuri mpya kama taifa. Tumeona maoni na ushauri umekuwa ukitolewa, na mara ya mwisho Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu naye alitoa wazo hili la kupitia mfumo wetu wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wetu wa elimu bado unazalisha watu ambao wanashindwa kushindana katika dunia hii ambayo artificial intelligence imechukua nafasi kubwa. Kwa hiyo, sisi kama taifa tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba tunaitizama upya elimu yetu. Na tunaposema hapa maana yake tuanzie katika Sera lakini pia katika sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo bado hatufanyi vizuri katika elimu na mara nyingi tunajificha katika kichaka cha Sera na sheria. Kwa mfano, hivi ninavyozungumza wanafunzi ambao wapo darasa la saba mwaka huu, Sera ya Elimu ilikuwa inatuelekeza vitabu mwisho ni darasa la sita lakini wapo darasa la saba; ina maana hakuna vitabu, sasa tunaweza tukaona kwamba wanapoteza mwaka mzima bure shuleni kwa kitu ambacho walishakisoma wakiwa katika darasa la sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni uzalishaji wa mitaala; Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala kwamba mitaala yetu sasa tuiboreshe zaidi ili iweze kuendana na dunia ya sasa. Kama ambavyo tumeona kupitia SADC tumepata fursa ya Kiswahili kuwa bidhaa katika nchi 16 za SADC. Ili Kiswahili kiwe bidhaa ni lazima sasa mitaala na yenyewe ilitamaze eneo hili; kwa maana huwezi ukaenda kufundisha nchi ambazo zinazungumza Kireno kama lugha ya asili bila hawa tunaowategemea wakafundishe Kiswahili katika nchi hizo bila kujua lugha ya Kireno ama lugha nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nata anitoe rai kwamba kwa kuwa ndio tunaelekea katika maandalizi ya bajeti basi eneo hili lionekane ni mahususi kabisa katika bajeti ili Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala iweze kuendana na soko hili la SADC ambalo tunakusudia kwenda kulifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni uhaba wa watumishi hasa katika kada ya elimu. Katika Halmashauri ya Lushoto tuna uhaba wa walimu 1,200. Utaona kabisa kwamba kule Lushoto mwalimu mmoja anafundisha vipindi 40 hadi 46 kwa wiki, tofauti kabisa na mapendekezo ambayo ni vipindi 24 hadi 26 kwa wiki. Kwa hiyo, utaona ni tatizo kubwa sana; lakini wakati Taasisi ya Mitihani inapotangaza matokeo huwa haiangalii maeneo ambayo hayana walimu, inatangazwa kwa usawa nchi nzima; wenye walimu na wasio na walimu wote mnawekwa katika kapu moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningetaka pia tuangalie kwamba wakati wa kutangaza matokeo ya mitihani mbalimbali kuanzia shule za msingi, sekondari za kawaida na high school basi wazingatie pia kwamba kuna Halmashauri hazina walimu wa kutosha. Kama ambavyo umeona hapa kwamba kwa wiki moja mwalimu anafundisha vipindi 40 hadi 46 maana yake ni kwamba hapa huwezi ukatarajia kwamba utapata ufanisi wa kutosha sawa na shule za seminari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili ni muhimu sana tunapoelekea katika bajeti na Wizara ya Utumishi, na wametuahidi kwamba wanakusudia kuajiri watumishi wengi, basi eneo la elimu liwe ni eneo mahususi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine pia ni katika usimamizi katika elimu. Nitatoa mfano wa Halmashauri ya Lushoto ina shule za msingi 169, ni Halmashauri ya nne kwa kuwa na shule nyingi za msingi hapa nchini. Halmashauri inayoongoza ni ya Moshi Vijiji, hii pamoja na kwamba inaitwa vijijini lakini ipo mjini, zinazofuata ni Ubungo na Kinondoni, hizi zipo mijini; utaona hata miundombinu yake ya kufikia shule ni rahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza Halmashauri ya Lushoto jiografia yake ya milima, mabonde, maporomoko na majabali ni ngumu sana kufikika kiasi kwamba hata ukaguzi hauwezi ukafanyika vile inavyopaswa, vilevile pia ndiyo maana unakuta hata upungufu huo wa walimu unachangiwa na kutokuwepo na miundombinu wezeshi ikiwemo ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe rai tu kwamba Wizara pamoja na TAMISEMI kuangalia maeneo fulani fulani ikiwezeka pia tutengenezewe kanda maalumu. Zisiwe tu zinatengenezwa kanda maalum za mambo ya uharifu lakini hata mambo haya ya elimu; kwa sababu Halmashauri yenye shule 169 maana yake ni kwamba kuna mwamko mkubwa sana wa kujenga hizi shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sitaki kuamini kwamba kwa mwamko huo wa kujenga shule kusiwe na mwamko wa kupata faida inayotokana na elimu. kwa hiyo, sisi kwetu shida sio vyumba madarasa, kwetu shida sisi ni ubora wa elimu ambayo inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala zima la TBC. TBC wanafanya kazi nzuri, tumeona maboresho mbalimbali yanaendelea upatikana lakini bado usikivu na upatikanaji wa TBC ni katika maeneo ya mjini; kiasi kwamba sasa TBC sasa hivi inashindana na redio hizi za kawaida. Kwa hiyo, tungetamani kuiona TBC ikienea nchi nzima hasa katika maeneo ya pembezoni. Hii itasaidia sana haswa katika vipindi vile ambavyo vinatoa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kipindi kile cha lishe; sasa hivi vipindi vizuri kama hiki wananchi hawapati faida ya kuvisikia kwa sababu TBC haisikiki. Naamini kwa namna ambavyo Tanzania tunazalisha na vyakula vilivyo vingi, wananchi wakipata elimu hizi za lishe na mambo mengineyo kupitia TBC itasaidia sana kuhakikisha kwamba hata huu udumavu ambao tunausema utapungua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, pamoja na kazi kubwa ambayo anaifanya pale TBC, lakini tunaomba shirika letu hili lipate uboreshaji mkubwa. Tunaomba sana kuwa na Televisheni ya Taifa ambayo ndiyo msingi wa kulinda maadili, mila na desturi za Kitanzania, aweze kusaidia katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)