Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami naunga mkono Taarifa ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo mimi ni member. Tuko vizuri chini ya Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Serukamba, ingawa kuna muda anakuwa very partisan badala ya kuwa bipartisan tunapokuwa kwenye vikao, anakuwa na mambo ya uchama sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitagusia kwenye afya na habari. Kwenye afya tunajisifu kwa kujenga majengo mengi ya Zahanati, Vituo vya Afya na hata Hospitali. Hii lazima tuelewane, hata mimi najenga kupitia Mfuko wa Jimbo, na kadhalika; najenga Zahanati, natoa bati kwenye Vituo vya Afya na kadhalika, lakini tuna tatizo la madawa na vifaa tiba kwenye maboma tunayojenga. Kwa hiyo, yale maboma maana yake bila vifaa vya matibabu yanaweza yakawa hata guest house. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajisifu kujenga majengo lakini hatuna watumishi wa kutosha wa afya. Kwa mujibu wa study pungufu ni takribani asilimia 52; tuna asilimia 48 tu ya Watumishi wa Afya wakiwemo Madaktari, kwa sababu hatuajiri kabisa. Kinachoshangaza, graduates wapo wengi sana kwenye kada ya afya wakiwemo Madaktari ambao wako mitaani hawana kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, yupo kijana mmoja Daktari, amemaliza Udaktari, amesajiliwa na Baraza la Madaktari, lakini yuko pale Uyole mpigakura wangu anauza vocha za kurusha. Daktari ambaye ame-graduate, amesajiliwa na Baraza yuko mtaani anauza vocha kwa sababu hakuna ajira. Kwa hiyo, hili ni tatizo sana. Inabidi tuangalie namna gani tunaongeza nguvu ya kuajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya sasa hata wale wachache waliopo, hiyo asilimia 48, maslahi yao ni duni sana bado, kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Serikali au wa Umma. Sasa hivi kwa takribani miaka mitano Madaktari na Watumishi wengine wa Umma hawajaongezewa mshahara hata shilingi mia ndani ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari walikuwa vocal, wanaongea na kugoma, sasa hivi hamsikii wanagoma mnafikiri kwamba wameridhika; sisi tunakutana nao kwenye Kamati, hawajaridhika. Ni kwamba sasa hivi kidogo mambo yako chini ya iron fist, hard kidogo! Hawawezi, wanaogopa kuishia kule ambako tunaishia wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu yote hawajaongezwa mshahara hata shilingi mia, hali inayosababisha tudhani labda hawa watu wanafanya kazi chini ya mgomo baridi. Kwa sababu haiwezekani, hata hili suala la kwenda kutibiwa nje, nafikiri hili suala tunasema kwamba hatuendi tena nje kisiasa, lakini kiuhalisia (practically) bado tunahitaji kupeleka baadhi ya wagonjwa nje kwa ajili ya matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni Mheshimiwa Lwakatare, my brother hapa, amekaa Hospitali ya Muhimbili, hospitali kuu kabisa ya Tanzania takribani miezi mitatu hajanyanyuka. Amepelekwa India, amekaa siku tano, siku ya sita amerudi, siku ya saba tuko naye Bungeni. Huu ni ushahidi kwamba bado kuna vitu tuna-miss; kama siyo vifaa, basi wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la matibabu kwa wananchi masikini ni gharama mno. Ni gharama sana! Sasa nashauri, wakati tunajipanga vyema na masuala ya Bima ya Afya na kadhalika, tusiache watu wafe, tuwatibu. Uzuri ni kwamba ninyi mnajipambanua kama ni wajamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuko mlengo wa kati, huku ubepari huku nini, soko huria ndiyo msimamo wetu. Ninyi mnasema ni wajamaa; wajamaa gani mnaacha kutibu watu? Kwa sababu hata Uingereza ambao ni mabepari wanatibu watu bure chini ya mfumo wa NHS (National Health Services). Nashangaa sana, hivi mnawezaje kutoa elimu bure mshindwe kutoa matibabu bure? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi subiri kidogo. Mheshimiwa Ummy, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji. Kwanza Sera ya Serikali, lakini pia ndiyo uhalisia, hakuna Mtanzania anyehitaji matibabu ambaye amekosa kupata matibabu. Ndiyo maana taarifa ya Kamati imeonesha, tukichukua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kipindi
cha Julai hadi Desemba, zaidi ya shilingi milioni 800 zimetumika kuwalipia wagonjwa wasio na uwezo wa kulipia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Sugu anapotosha, hatujasema hatupeleki kabisa wagonjwa nje. Ninyi ni mashahidi, watu wa mafua, Malaria na magonjwa madogo madogo wote walikuwa wanakwenda nje. Tumewapunguza kutoka 600 mpaka 53. Kwa hiyo, ni kweli hatupeleki nje kwa magonjwa ambayo tuna uwezo wa kuyatibu ndani ya nchi na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumefanya vizuri. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana. Halafu asimwingize Rais, hapa tunaongea na ninyi ambao mmetumwa na Rais kufanya hizi kazi. Kwa hiyo, msimwingize Rais kwenye mijadala yetu humu, maana yake mnajificha kwenye kichaka cha Rais. Nini watu!
Wewe Mheshimiwa Waziri, ninyi mnasema kwamba hamjakosa fedha za kutibu Mtanzania, ninyi mnashikilia maiti za Watanzania kwa sababu wamekosa fedha za matibabu! Eeh! (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hawalipi!

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Watanzania; nenda Muhimbili, nenda Hospitali zote za Serikali, Mtanzania mwalimu mshahara wake shilingi 300,000/= au shilingi 400,000/=, anaumwa ugonjwa serious, analazwa miezi mitatu, minne, bili inakuja shilingi milioni saba, shilingi milioni nane, shilingi milioni tisa; anafariki dunia, hawa wanashikilia maiti. Mnashikilia maiti za Watanzania ninyi. Wanawanyima fursa Watanzania ya kwenda kufanya ibada za maziko. Wanawanyima Watanzania fursa...(Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi, kuna taarifa nyingine. Mheshimiwa Kandege.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naheshimu sana mchango wa Mheshimiwa Mbunge, lakini siyo vizuri akapotosha. Kwa sababu hakuna mtumishi wa Serikali hata mmoja ambaye hayuko kwenye insurance. Sasa anasema mwalimu ambaye ana mshahara wa shilingi 300,000/= anashindwa kutibiwa wakati yuko fully covered na insurance! Siyo sahihi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, haya basi, tufanye siyo walimu, tufanye Watanzania wa kawaida kama yule ambaye alimwomba Mheshimiwa Rais shilingi milioni tano ili agomboe maiti yake. Sasa ni wangapi ambao wanamwona Rais mpaka wapate huo msaada? Mpaka Watanzania wengine wachangie ili kumfanya Mheshimiwa Rais afanye shughuli zake. Ninyi, msimwingize Rais kwenye haya mambo ya humu Bungeni. Tukae na ninyi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hiyo itakuwa taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Mbilinyi. Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namheshimu sana Mheshimiwa Mbilinyi, ni rafiki yangu sana, lakini kwa kweli kile anachokisema hapa ni upotoshaji wa hali ya juu sana na akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ndani ya Wizara na kupitia hospitali zetu tumeweka utaratibu mzuri sana; na ni fursa hii ya kuwaelekeza Waheshimiwa Wabunge. Tuna Dawati la Social Welfare ambalo kama kuna mwananchi ambaye amepata matibabu ya aina yoyote ile na akashindwa kugharamia aidha amepona au mgonjwa wake amefariki anakwenda katika Dawati hili la Social Welfare pale, watamfanyia assessment.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi hatuna maiti ambayo tunaishikilia kama Serikali. Ndiyo maana lile ambalo alikuwa anasema Mheshimiwa Waziri hapa, tunatumia fedha nyingi sana, zaidi ya shilingi milioni 800 katika hospitali zetu nyingi kwa ajili ya kugharamia haya matibabu mengine ya watu ambao hawana uwezo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana. Ndiyo tunachosema, kwa sababu kama dawati lipo, halafu wananchi hawalijui na ninyi mpo, mpaka mwananchi anakurupuka kwenda kumwomba Mheshimiwa Rais shilingi milioni tano, tuna tatizo! Ndiyo maana tunasema hapa kuna tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu ni gharama sana kwenye kila eneo. Twende kwa akina mama kwenye huduma za uzazi, kujifungua; hospitali za Serikali sasa gharama ni balaa. Ni gharama kubwa mno! Hospitali ya Wazazi Meta Mbeya kujifungua ni mpaka shilingi 300,000/= kwa operation, kujifungua kawaida mpaka shilingi 150,000/=, shilingi 200,000/=. Hii ni Hospitali ya Rufaa ya Wazazi Meta, Maternity Hospital pale Mbeya Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najiuliza, wakati wa Mheshimiwa Dkt. Kikwete na Mheshimiwa Mkapa huko nyuma wazazi walikuwa wanaambiwa waende hospitali na kanga, pamba, nyembe, sijui sindano na vitu vidogo vidogo, mambo mengine yote wanayakuta huko huko; inakuwaje? Ni nini kimesababisha Sera ile ya Afya Bure, Matibabu Bure kwa Wazazi Wajawazito Pamoja na Watoto Mpaka Miaka Mitano, ile sera imekwenda wapi? Au kama ndiyo matokeo ya sanctions ambazo tumeanza kuwekewa, basi mtuambie ili tufunge mkanda na tujiandae kwamba tuko katika stage gani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi kengele ya pili imeshagonga.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Kweli!

NAIBU SPIKA: Sina saa mimi jamani, Makatibu wananiongoza hapa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, wamekula sana dakika zangu!