Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa asubuhi ya leo kuweza kuchangia bajeti ya Wizara yetu hii ya Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi. Nianze moja kwa moja, kwanza kuwapongeza Walimu wote nchini Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya. Kipekee niwashukuru Walimu hao kuanzia Shule ya Msingi, Sekondari Mtwara Girls na Ndanda High School, Chuoni IFM, Mzumbe University na Walimu wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kwa namna ambavyo wamenisaidia, nimepata fursa ya kusimama ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo, kabla hata sijachangia niliwasiliana na wanafunzi niliosoma nao ambao pia ni Walimu ambapo, changamoto nitakazozichangia hapa na ni maombi yao, ni maombi yaliyotokana na Walimu wenyewe baada ya kuwasiliana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi vizuri; hatua alizochukua dhidi ya Bodi ya Mikopo, hatua alizozichukua dhidi ya TCU, binafsi naziunga mkono. Pia, nampa pole sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufiwa na mama yake mzazi, Mwenyezi Mungu ampe subira na wepesi katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nina matumaini sana ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuwa, naamini inaongozwa na Rais wetu aliyepata kuwa Mwalimu, Waziri Mkuu aliyepata kuwa Mwalimu, First Lady aliyepata kuwa Mwalimu, Walimu wana matumaini makubwa sana katika Awamu hii kwamba, jitihada zilizoanzishwa katika Awamu mbalimbali changamoto zao nyingi zitapata fursa ya kutatuliwa katika Awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nipongeze kwa utekelezaji wa suala zima la Waraka Namba Tano (5) wa Elimu Bure ambao umeanza mwaka jana Disemba, 2015 mpaka sasa. Nipongeze dhamira ya Serikali ya kutenga kiasi cha bilioni 18 kila mwezi kukabiliana na majukumu mazima ya kutoa elimu kwa Shule za Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Pwani suala hili limetusaidia, ongezeko la uandikishaji kwa ngazi ya mkoa limefikia 150%. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile 50% ya watoto walioongezeka katika Elimu ya Awali na Msingi ni wazi kuwa kuna wazazi ambao ilikuwa inashindikana kabisa kupeleka watoto wao kutokana na changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwanzo wa hesabu moja. Natambua Roma haikujengwa kwa siku moja. Katika utaratibu mzima wa utoaji wa elimu bure, naiomba Wizara iangalie, isije ikawa utekelezaji wa elimu bure imewapa Walimu Wakuu mzigo mkubwa na Walimu wenyewe bado wanalalamika mishahara bado ni midogo na marupurupu yao mengine; kwa nini nasema hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji huu wa elimu bure, kuna kipengele cha utawala. Utakuta shule inawezekana ina wanafunzi wachache, lakini gharama za utawala ni moja; kama ni bei ya shajara ni moja, masuala ya mitihani ni mamoja, lakini utakuta ile 10% hasa kwa shule ambazo zina mazingira magumu, mfano shule za Kata ya Kibindu Wilaya ya Bagamoyo, Shule za Delta, Kiongoroni, Mbuchi, Msala, Maparoni Wilaya ya Rufiji! Shule za Wilaya ya Kisarawe zilizopo Vikumburu, Dololo, Kimaramisale, Mafia, Visiwa vya Jibondo, Chole, Mkuranga, Visiwa vya Kwale, Koma, mazingira yao ni magumu kiasi kwa mfano Visiwa vya Rufiji, kuja Makao Makuu ya Wilaya Utete, Mwalimu anatumia 50,000/= nauli. Zilikuwepo boti kwa ajili ya kuwasaidia walimu hawa, lakini zile boti zimeharibika, lakini anaenda kufuatilia cheque kwa ajili ya masuala ya utawala. Kwa mfano kuna shule iko Msala na inapokea 40,000/= asilimia 10 ni 4,000/=, lakini afuatilie hiyo hela mpaka Utete ni 40,000!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iangalie mazingira haya magumu na iwatendee haki Walimu, wamelalamika! Walimu sasa wanatumia pesa zao mifukoni kwa ajili ya uendeshaji wa shule. Vile vile suala hili limeathiri masuala ya mitihani; kifungu cha mitihani hakitoshelezi, kwa hiyo, baadhi ya mitihani imepunguzwa! Labda shule zilipanga utaratibu mock ya Kikata, mock ya Wilaya, mitihani ya kila mwezi, ya kila wiki na mitihani hii ilikuwa inasaidia ufaulu. Kwa hiyo, nadhani Wizara iangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Walimu niliowasiliana nao wameomba hiki Chama cha Walimu Tanzania, wamesema chama hiki kimeshasimama, kina miliki jengo, kinafungua benki! Masuala ya kuwakata asilimia ya mishahara yao kwa ajili ya kuchangia chama ambacho kimeshasimama, kina uwezo, naomba Wizara mfuatilie, Walimu wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini chama hiki hakipo wazi! Sisi tumekaa Wilayani, hatuoni msaada mkubwa kwa Walimu wetu, lakini mara nyingi utakuta kwenye masuala ya michakato ya kisiasa kiko mbele, lakini siyo katika kuwasaidia Walimu! Nadhani michango waliyochangia Walimu ingewezekana Chama cha Walimu kingethubutu, sasa hivi kinamiliki benki, kinamiliki jengo kubwa Dar-es-Salaam, kingethubutu hata kuwapunguzia makali ya maisha walimu ambao ni wanachama wao. Kwa hiyo, hilo nalo walimu waliniomba, lakini wamesema sasa hivi chama kimesimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Walimu wameiomba jitihada za kuimarisha miundombinu. Bajeti ya miaka iliyopita, hususan mwaka jana, kulikuwa na kifungu waziwazi cha ujenzi wa nyumba zao kama 500 kila mwaka.
Nimejaribu sana kuangalia kwenye bajeti ya mwaka huu sioni vizuri, hakionekani waziwazi, lakini bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Walimu wameniomba, kuna Walimu waliajiriwa Juni, 2015 mpaka leo bado hawajalipwa pesa zao za kujikimu na pesa zao za nauli, inawakatisha tamaa. Walimu pia, wameniomba Serikali iendelee na jitihada za kulipa madeni yao; wanatambua hata mwaka jana mwezi wa 10 baadhi ya madeni yao yamelipwa, lakini kwa kuwa yanajilimbikiza kwa muda mrefu, Walimu wameomba pia suala hili litekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu pia wameniomba niwasilishe, utekelezaji wa Waraka wa Posho za Viongozi, sijaliona waziwazi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri! Walimu Waratibu wa Elimu Kata walipangiwa sh. 250,000/=, Wakuu wa Shule walipangiwa sh. 200,000/=, hizi zinaweza zikawasaidia, naomba hilo nalo litazamwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Pwani tunalo tatizo, baadhi ya shule zetu zina Walimu mmoja mmoja. Mfano Shule ya Gundumu Kata ya Talawanda, Shule ya Kwa Ikonji, Pera, Kata ya Kibindu ina Mwalimu mmoja, lakini shule hizi zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba. Kwa mfano kwenye Shule ya Gundumu kuna Walimu wawili wanajitolea kwa sh. 50,000/= lakini tangu Disemba hawajalipwa! Kwa hiyo, mimi binafsi kama Mbunge wao nimeona niwasaidie, nilichukue jukumu hilo ili niweze kuona jinsi Serikali itakavyotusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la Bodi ya Elimu. Kwanza nakubaliana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya TCU, lakini pia nasikitika hela zaidi ya milioni 700 zilizotumika kwa vijana wale na mimi binafsi siyo Mwalimu, lakini nikiangalia maelezo ya Mheshimiwa Waziri na vigezo walivyovitumia kuwadahili wale na nikirejea maelezo ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii, ukurasa wa 11 kwamba, Kamati imebaini kuwa, vijana wengi wenye alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya elimu ya juu wameshindwa kuendelea kutokana na hela hizi za mikopo kuwa si nyingi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kama wapo vijana wenye elimu, wenye vigezo, wako mitaani wanakosa fursa ya mikopo, tufike hatua ya kuwadahili wanafunzi wenye Arts kusoma masomo ya sayansi kwa ajili ya kuja kutufundishia watoto wetu! Kwenye suala hili kwa kweli, naunga mkono. Nimesema mimi siyo Mwalimu, lakini naamini Profesa Ndalichako amejiridhisha, naamini na Tume aliyoiunda itafanya kazi nzuri, lakini hatua lazima zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nimalizie kwa kuomba huu ujenzi wa miundombinu, hasa kwenye shule ambazo, kwa mfano tuna Shule ya Mlegele Kisarawe, tuna Shule ya Kidugalo, Tondoroni, Sofu na Kola; shule hizi zina vyumba viwili viwili vya madarasa, lakini zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba! Kwa hiyo, utakuta changamoto katika miundombinu ya elimu, bado ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niiombe Serikali, maoni ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii ni mazuri sana, hasa uwekezaji kwenye Sekta ya Elimu. Tunapoliandaa Taifa letu kuwa Taifa la kipato cha kati na Taifa la viwanda, tunatarajia kufufua Viwanda vya Nguo, Viwanda vya Kusindika Korosho, tusipoandaa wataalam na tukawekeza zaidi katika Wizara hii, hasa miundombinu yake. Tunaweza tukawa na kila kitu, lakini Taifa litakalokosa wafanyakazi wenye elimu inawezekana hata hii azma nzima tusiitimize. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante sana.