Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutujalia afya njema na kuweza kuendelea na shughuli zetu za Bunge. Vilevile nitoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Kamati kwa taarifa zao walizowasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hii Wizara ni nyeti na imebeba au imeshikilia maisha ya Watanzania, lakini ukiangalia changamoto zilizokuwemo katika Wizara hii ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mzungumzaji aliyepita hapa amezungumza kwamba gharama za matibabu zimekuwa juu sana. Huu ni ukweli usiofichika. Ushahidi wa hili ni pale Mtanzania anapokuwa na maradhi kwa sababu ya ukali wa maisha, kwa sababu ya umasikini anakwenda katika vyombo vya habari kama ITV Television au Channel Ten anakwenda kujidharirisha kuomba, kwamba naomba wasamaria wema wanichangie. Mimi hili jambo linaniuma kweli kweli, kwa sababu huyu ni Mtanzania, tunajifaragua na kujidai kwamba tunakusanya 1.9 trillion kwa mwezi, lakini kwa nini Mtanzania aende akajioneshe pengine ana maradhi ya aibu, anachukuliwa na moving camera anaonyeshwa namna hii yale maradhi yake. Huu ni udhalilishaji! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetembea katika baadhi ya nchi, najua hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge humu mmetembea, Naibu Spika, umetembea. Kwa mfano, nchi kama Qatar au Saudia, Denimak, Norway, Finland, kwa wenzetu matibabu hakuna mtu anayekufa kwa sababu hana fedha ya matibabu. Serikali imeweka utaratibu kwamba elimu ni bure na matibabu ni bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtanzania, hata mtoto mchanga, watoto waliozaliwa wameungana, bila aibu tunaenda kuwaonyesha kwenye television kwamba watoto hawa wanahitaji wasamaria wema wawachangie. Hili pato la Taifa tunalokusanya kupitia mamlaka ya mapato, shughuli yake ni ipi? Kazi yake ni kununua silaha peke yake? Kazi yake ni kutulipa mishahara sisi Wabunge na Watumishi wa Serikali peke yake? Hawa Watanzania wakimbilie wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali mambo mengine ni aibu!

MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: …na kwa bahati mbaya sana, vyombo vyetu vya habari sasa hivi vinaonekana Kimataifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, kuna taarifa. Mheshimiwa Amina Mollel.

T A A R I F A

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kumpa taarifa Mheshimiwa Mbarouk kwamba moja ya kazi za vyombo vya habari ni pamoja na kuihabarisha jamii. Katika kuihabarisha jamii ni pamoja na kuishirikisha katika mambo mbalimbali ikiwemo pia matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni utaratibu wa kawaida kabisa unaotumika na vyombo vya habari, anapokwenda mtu mwenye tatizo kuweza kutaka kuwasilisha tatizo lake kwa jamii na kwa sababu kwenye jamii wapo watu ambao wanaguswa na kuweza kusadia. Kwa hiyo, asione kwamba ni aibu bali ni utaratibu uliopo katika vyombo vya habari. Ndiyo maana katika vipindi mbalimbali pia watu wanaweza kwenda na kushiriki katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa siipokei. Namwomba Amina Mollel aichukue mwenyewe taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia aibu maana yake, kwa mfano tangu majuzi inarushwa clip, kuna mtoto ana matatizo ya figo, tumbo lake limekuwa kubwa kabisa. Ukimtazama mama yake yupo kwenye television analia, maana yake hana uwezo wa kwenda kumtibu yule mtoto wake India. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine labda niutoe, mimi na Waziri wangu wa Afya pale Mheshimiwa Ummy Mwalimu, sote ni watu wa Tanga, yupo dada mmoja wa Kwanjeka, ana maradhi ya mguu kama tende hivi. Tumejitahidi tukampatia Bima ya Afya, lakini Bima ya Afya kumbe nayo kuna baadhi ya package hazihusiki kwamba labda mtu kupelekwa nje. Sasa mtu anadhalilika na maradhi mpaka anakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ndugu yenu mnamwangalia huyu ndio anakwenda zake sasa, lakini hamna cha kumfanya. Mbona kwenye Serikali za wenzetu wanaweza? Kutibiwa na masuala ya elimu ni bure. Kwa nini sisi inashindikana wakati sisi Mwenyezi Mungu ametujalia rasilimali bila ya kumpa rushwa? Ametujalia madini, ametujalia bahari, ametujalia mazao, ametujalia wanyama, vyote hivyo Serikali inapata pesa, lakini inashindwa kuwatibu wananchi wake. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mashimba Ndaki.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Hizi taarifa zinakula muda…

T A A R I F A

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa msemaji ayezungumza kwamba yeye ni Mbunge. Kipindi cha kupitisha bajeti hapa mwezi Juni alikuwepo. Mambo anayoyazungumza alikuwa anayajua, lakini hajayaleta mbele ya Bunge lako ili kwamba bajeti iweze ku-consider jambo hilo. Sasa anakuja kusema kipindi hiki ambacho hata hatupangi mipango kama hiyo anayosema, sasa anayewahurumia watu hao ni yeye au anapenda tu kujisemea? Ahsante. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, jitahidi utumie lugha ya Kibunge maana hapo umezungumza mambo mengine. Kwanza umemwambia Mheshimiwa Amina Mollel aichukue mwenyewe taarifa, hairuhusiwi kikanuni. Wewe unajibu kama unaipokea ama huipokei, unaendelea na utaratibu.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, basi taarifa siipokei.

NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, hii pia siipokei. Labda niseme, Mheshimiwa aliyesema kwamba eti tunapitisha bajeti; bajeti ndiyo tunapitisha, lakini kwa mfano jana mchangiaji mmoja alizungumza hapa, nami niliwahi kuzungumza huko nyuma, tunapitisha bajeti labda ya Wizara ya Kilimo kwamba wapewe asilimia 100 ya fedha, wanapewa asilimia 11, ni bajeti isiyotekelezeka. Hata mimi najua dada yangu Mheshimiwa Ummy hiyo bajeti tunayompelekea pia haimtoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naizungumzia Serikali kwa ujumla wake sasa kwa sababu ndiyo inayokusanya mapato yote ya Serikali. Ni wajibu wa Serikali kuwatibu wananchi wake hasa pale wanapokuwa katika maradhi ambayo hawayamudu kugharamia kwa matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niseme, kwa mfano Sera ya Taifa ni kwamba Wazee, Watoto na Akinamama Wajawazito Watibiwe Bure, lakini ukienda katika hospitali zetu hawa akina mama kwenye hizo delivery kit pia unakuta katika baadhi ya maeneo wanachangishwa, wanaambiwa walipie, siyo kwamba ni bure. Mtu anaambiwa alipie hiyo delivery kit, lakini pia kuna vitu vingine ambavyo anatakiwa alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akina mama Wabunge humu ni mashahidi, labda kama watakuwa wanapendelewa kwa upendelo kwa hadhi waliyokuwa nayo, lakini akina mama wengi hususan maeneo ya vijijini, akienda kujifungua lazima delivery kit alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kusema, hata watoto ndiyo huo mfano ninaoutoa kwamba watoto chini ya umri wa miaka mitano wameambiwa watibiwe bure, sasa huyu mtoto ambaye anapelekwa kwenye television wakaombwa wasamaria wema, matibabu bure yako wapi hapo? Huyu ni Mtanzania, tena ni mtoto mchanga, malaika wa Mungu, basi sisi hata hatumwonei huruma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tunaposema matibabu yawe bure, basi yawe bure; akina mama wapate delivery kits zile free no charge, wazee watibiwe bure. Tena kwa bahati mbaya, anakwenda mzee labda kutaka matibabu, anaambiwa wewe si una watoto? Sera ya Taifa haikusema kwamba mtu akiwa na watoto asitibiwe bure. Imesema “mzee.” Au anafika hospitalini au Kituo cha Afya mzee anaambiwa, lete kitambulisho cha uzee. Sura yake ukimtazama, si unamwona ni mzee huyu, kitambulisho cha nini? Mtu unamwona kabisa huyu ni mzee, lakini anaambiwa atoe kitambulisho cha uzee.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naona huku ni kuwanyanyasa. Kama tumeshindwa kuwatibu bure watu wetu, naomba tuwaambie basi hakuna matibabu bure, kuliko tunawapa moyo, mtu anajua anaumwa anakwenda kutibiwa bure halafu akifika kule anakatishwa tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua umenilindia muda wangu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni watoto wa mitaani. Wizara inazungumza kwamba itahudumia maendeleo ya jamii, lakini watoto wa mitaani wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kwa sababu hatushughuliki nao, hatuna center tunazowaweka tukawapatia labda elimu, tukawapa mafunzo; matokeo yake wale wale ndio wanaogeuka kuja kuwa vibaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tukiachilia mbali watoto wa mitaani, hata vichaa; unakuta kichaa anatembea uchi sokoni au anapita maeneo ya shule; yaani watoto wadogo wanajua kumbe mtu akishakuwa mtu mzima, ana vitu hivi na hivi! Kichaa hana mtu wa
kumwangalia, hana hata nguo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikari iweke vituo maalum kama baadhi ya nchi za wenzetu. Watu wenye kichaa tunawachukua, tuhakikishe na wao wanaoga, wanabadilishwa nguo na wanapewa chakula. Wengine wanakufa kwa njaa tu. Mtu ni kichaa, amekaa sehemu hana akili hata ya kujua kwamba muda huu natawakiwa nile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, watoto wa mitaani na vichaa lazima tuwawekee utaratibu, tuhakikishe kwamba kwanza watoto wa mitaani wanapata elimu, lakini hata hawa vichaa isiwe ni aibu sasa mitaani. Wawekewe maeneo maalum. Hebu fikiria wewe usipooga kwa muda wa siku moja tu unajisikiaje? Sasa kichaa miezi tisa hajaoga, unafikiri anajisikia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, hawa nao ni Watanzania, wanahusika kabisa na pato la Taifa au keki ya Taifa ambayo inakusanywa na Serikali nao iwahudumie kwenye mavazi, chakula na hata hali ya kimazingira ya afya zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho labda nizungumzie kwenye masuala ya huduma; huduma ziko katika maeneo mengi sana. Sasa hivi tuzungumze hata kwenye huduma hizi kama za maji, labda na umeme, tunashukuru kwenye umeme wamejitahidi, lakini kwenye masuala ya maji bado wenzetu wa vijijini wana matatizo makubwa ya huduma hii ya maji. Maji wanayotumia kwa kweli yanawasababishia maradhi kwa sababu siyo safi na salama. Tuishauri Serikali sasa, katika ile miradi ya vijiji kumi kila Halmashauri, wahakikishe wananchi wa Vijijini nao wanapata maji kwa usalama wa afya zao, lakini kwa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuzungumzia ni suala la maiti. Kumekuwa na tabia sasa maiti imekuwa ni dili au nacho ni chanzo cha mapato ya Serikali. Huyu mtu ameshatangulia mbele ya Mungu, amesamehewa. Kwa mfano sisi Waislamu, mtu akishakufa, amesamehewa kuswali, amesamehewa kufunga, maana yake huyu amerudi mikononi mwa Mwenyezi Mungu, lakini Serikali yetu ya Tanzania, maiti anachajiwa akikaa mortuary. Hii mimi nasema ni aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuhakikishe kwamba sasa hawa maiti isiwe dili, wasamehewe kama walivyosamehewa na Mwenyezi Mungu. Kuna baadhi ya familia hazina uwezo; mtu anaambiwa shilingi milioni tano, ndiyo hayo sasa aliyosema Mheshimiwa Sugu hapa, kwamba mtu anajitokeza mbele ya Mkutano wa Rais anaomba shilingi milioni tano akakomboe maiti. Hivi Rais huyu kwa nini tunamlundikia mizigo ya kazi nyingine ambazo hata hazimuhusu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tena, maiti kwenye nchi yetu ya Tanzania wasichajiwe. Wakiwekwa mortuary, siku hizi kuna mawasiliano mengi tu, ifahamishwe familia yake waje wachukue maiti yao wakazike, lakini kumdhalisha maiti kumweka katika mortuary kwa muda mrefu, hilo nalo pia sio haki. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda tayari.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)