Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu ya Taarifa za Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Taarifa ya Ukimwi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Maoni ambayo ametoa Mwenyekiti wetu ndiyo tumeyafanyiakazi na nina hoja zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitazungumzia katika sekta ya afya pamoja na elimu. Katika sekta ya afya, ninapozunguma sasa, kwa takwimu za UNICEF tuna watoto chini ya miaka mitano ambao wanafariki kila siku kwa idadi ya watoto 312 kwa siku. Ninapozungumza hapa, watoto 312 kila siku wanafariki. Hii ina maana gani? Tukiona kuna ajali inatokea ya basi kwa mfano lenye abiria 65 na tunasikitika watu hawa wamefariki basi moja, kwa watoto 312 ambayo yanaangusha abiria kila siku. Kwa hiyo watoto hawa wanapoteza uhai, na hii ni kwa sababu ya changamoto kubwa tunazozipata katika utoaji wa huduma na ukosefu wa huduma za afya zikiwemo huduma za dharura za upasuaji kwa wakina mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya ni masuala ambayo tunapaswa tuyaone na tuyaangalie kwa mapana kwa sababu tunapoteza watoto wengi wakati huo huo sisi tunasema kwamba tuna makusanyo makubwa ya fedha; haya makusanyo makubwa yanakwenda wapi? Hatuna watumishi wa kutosha takribani asilimia zaidi ya 50, hawapo. Sasa kama Serikali hatuna watumishi zaidi ya asilimia 50 kwa Sekta ya afya tunatarajia nini? Hawa Watanzania wengi tunaowapoteza matarajio ni yapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali lazima ijipime, ijiangalie, wapi ambako wanatakiwa waweke mkazo tumesema tunakusanya fedha nyingi za mafisadi sawa japokuwa mimi sijaona hao mafisadi wameweza kuhukumiwa wapi tukapata hizo pesa, lakini hatujaajiri wafanyakazi ni miaka mwaka wa nne unakwenda wa sekta ya afya hawapo, hii inaleta adha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda katika sekta hiyo ya afya watumishi wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Sekta hii ni muhimu, ndiyo kinga. Tunapata semina mbalimbali hapa Wabunge viribatumbo, sijui kuna hiki, kuna kile; yote haya ni kwa sababu sekta hii hajaajiri, tuna upungufu takribani asilimia 95 ya watumishi wa maendeleo ya jamii katika sehemu zetu kwenye kata na vijiji ambao walikuwa wakipita zamani wakielimisha jamii, kuleni kuku, mayai, mboga, samaki, maziwa havipo tena sasa hivi ambao walikuwa wanaelimisha, wanawaelekeza wakina mama na wananchi kwa ujumla wapate hiyo elimu, haipo. Sasa kama hatuwezi kuwekeza kwa watumishi hawa ambao ndio kinga matarajio yetu ndio hii kuongeza bajeti ya dawa ambayo inatu-cost kama Serikali. Kwa hiyo Serikali lazima iangalie, kinga ni bora kuliko tiba; tuwekeze kwenye sekta hii na tupeleke wafanyakazi ili waweze kuhudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za wenzetu unakuta watu wana-volunteer, wanajitolea. Serikali haiamasishi hicho, hamasisheni wananchi wajitolee wakiwa shuleni, wanapotoka shuleni waende wajitolee. Tunaona volunteers wengi wanatoka nje wanakuja hapa sisi wa kwetu tunapelekea wapi? Hatuna huo mkakati, Serikali iweke mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika sekta ya elimu, ninapozungumza ratio ya mwalimu wa elimu ya awali ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 146; inayotakiwa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25, na pale ndipo tunapojenga msingi wa elimu, tunapowakuza watoto wetu wakuzwe vipi, wawe na study zipi , wafanye nini, baadae waweje hapa ndio tunapokuza. Lakini sasa tuna uhaba wa walimu 44,273, ni zaidi ya mara nne ya walimu tulionao, miaka 50; miaka 50. Ina maana tutatumia zaidi ya miaka 200 kupata walimu ambao watatosheleza katika nchi yetu, halafu mnasema mtaendelea kuchaguliwa katika awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye suala la wasichana kurudi shuleni wapatapo ujauzito; hiyo ni haki yao ya kielimu. Katika Ilani yenu ya Chama Cha Mapinduzi Kifungu 52 ukurasa 99 kipengele cha elimu (i) roman(ii), naomba ninukuuu, kinasema;
“Wasichana wote wa elimu ya msingi wanaoacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito wataendelea na masomo”
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo imenukuliwa, na hii mliipeleka kwenye mpango na ikawa mpango mzima wa utekelezaji; hata tunavyotafuta fedha kwa wafadhili tunatumia kifungu hicho. Niwaulize imetekelezwa wapi? Hawa wanafunzi wengi; mimi siwezi kutetea kwamba mwanafunzi apate ujauzito lakini wale kwa bahati mbaya ambao wanapata ujauzito hakuna mkakati mzima wa kutengenezea utaratibu wa kwenda kwenye masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Zambia wameweka utaratibu, huyu mtoto anatokaje shule, atafanyaje, ataendelezwaje mpaka atarudije shule kuwa-formal education; sisi tunataka tumpeleke kwa upeo mwingine aende akatengeneze sijui vitambaa, kufanya hivi. Huyu alikuwa na ndoto zake pengine awe Pilot, awe engineer, awe mtu ambaye ana mtazamo wake alikuwa anautaka sisi….(Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
T A A R I F A
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Grace Tendega kuna taarifa Mheshimiwa Ally Keissy.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa mzungumzaji kama alikuwa na ndoto zake kwa nini alipata mimba ungemzuia asipate mimba.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Grace Tendega endelea na mchango wako.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei ninasema hivi kama tendo hilo hilo ambalo linafanya watoto wapate ujauzito na tendo hilo hilo linafanya watu wapate UKIMWI mbona kwenye UKIMWI hatusemi chochote na tunapeleka fedha wanahudumiwa? Kwa nini kwa upande huu tunasema haipo? Ama kwa sababu kwenye UKIMWI na wanaume wanakuwemo? Lazima tuliangalie hili na tupigie kelele hawa watoto wa kike wapate elimu, wapate ndoto zao ambazo wanazitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za Afrika Mashariki wameweza kuingiza hilo ukiangalia Kenya, ukiangalia Uganda na soko la ajira ni moja. Sisi tunapokuja kuwa hatuna soko la pamoja tunasema tuko nyuma ni kwa sababu hatuweki mkakati madhubuti watoto wa kike kwenda shule na kuendelea na shule zao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha ahsante sana.